google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

May 16, 2016

Tabia Zinazoua Ndoto Na Mafanikio Ya Wengi.

No comments :
Kimsingi, tabia ni nguzo kubwa ya mafanikio katika maisha yako ikiwa lakini utazitumia tabia hizo vizuri. Mafanikio yote uliyonayo na yale unayoyategemea kuyapata, siku zote yanategemea sana tabia ulizonazo. Kwa maana hiyo, kabla hujaamua kuibeba tabia ya aina fulani, ni vyema ukajiuliza kwanza kwa tabia hii itanisaidia kunifanikisha au itanirudisha nyuma?
Maswali hayo ni muhimu kujiuliza ili yakusaidie kuchagua tabia zinazokupa mafanikio. Kwa sababu tunaambiwa mafanikio ni tabia. Kama mafanikio ni tabia usibishe na wala hutakiwi kujiandaa kubisha, ni lazima kwako uwe na tabia za mafanikio ili ufanikiwe. Ni tabia za mafanikio ambazo utakuwa unazitumia kila siku, ndizo zitakazo kufanikisha na si vinginevyo.
Lakini, hata hivyo katika hali ya kushangaza watu wengi bado wana tabia nyingi hasi zinazowafanya wasifanikiwe. Kwa kifupi, ni watu wanaotumia sana tabia zisizo za mafanikio kuendesha maisha yao. Kutokana na kuwa na tabia hizi kwa muda mrefu, zimekuwa zikipelekea wao kuua ndoto na mafanikio yao kwa ujumla katika maisha.
Ni tabia hizi hizi ambazo hata wewe unatakiwa kuzijua ama kuziepuka kabisa ili usiweze kuua ndoto na mafanikio yako. Naamini una hamu ya kutaka kujua ni tabia zipi ambazo ukiwa nazo huwezi kufanikiwa. Kwa sasa, tuliza akili yako na fuatana nami katika makala haya kujua tabia zenye uwezo wa kuua ndoto na mafanikio yako kabisa.
1) Kuahirisha.
Kama unataka kuokoa ndoto na mafanikio yako kwa ujumla, kuahirisha mambo ni tabia ya kwanza ambayo unatakiwa kuachana nayo mara moja. Wengi wamekuwa ni watu wa tabia hii ya kuahirisha mambo na kuona ni kitu cha kawaida.
Kwa mfano, utakuta mtu anataka kuanzisha jambo fulani lakini katika hali ya kushangaza analiacha jambo lile na kudai kwamba atalifanya muda mwingine. Kuahirisha mambo kwa namna hiyo kunavyoendelea kwa muda ndivyo ambavyo hujikuta ndoto na mafanikio ya wengi hufia hapo.

Acha kukata tamaa mapema.
2) Uvivu.
Huwezi kufanikiwa katika maisha yako kama kazi zako unazifanya kwa uvivu. Kwa bahati mbaya wengi wetu ni watu wa kufanya kazi kivivu na kutegemea kupata matokeo makubwa kitu ambacho hakiwezekani. Ni watu wa kupenda starehe na kutaka kuona mafanikio yanatokea kirahisi rahisi bila kujituma sana.
Ukweli wa mambo ulivyo hakuna mafanikio rahisi. Hakuna mafanikio ya muujiza ya kulala maskini na kuamka tajiri. Ili uweze kufanikiwa unatakiwa kujituma sana na kuacha kila aina ya uvivu pembeni. Ila uking’ang’ania uvivu elewa kabisa unaua ndoto na mafanikio yako na sahau kufanikiwa.
3) Kukata tamaa mapema.
Hakuna ubishi wowote, ikiwa una tabia ya kukata tamaa mapema ni wazi huwezi kufanikiwa. Kutokufanikiwa kwako kutakuja si kwa sababu huna uwezo wa kufanikiwa, bali ni kwa sababu unakuwa umeacha kile unachokifanya kabla ya kufikia mwisho wa mafanikio yalipo.
Kwa mfano, ili kuku aweze kutotoa kifaranga ni lazima aatamie kwa siku ishirini na moja. Ikiwa kuku huyo ataatamia yai lake kwa siku ishirini na kuliacha, ni wazi vifaranga wa kuku hao hawawezi kutoka kwa sababu siku za kuatamia hazijafika. Halikadhalika na mafanikio yako hivyohivyo. Upo muda wa kufikia mafanikio yako. Ukikata tamaa mapema kabla ya kufikia muda wako wa mafanikio, hautaweza kufanikiwa.
4) Visingizio.
Mara nyingi  zipo sababu nyingi sana ambazo watu wanajiambia karibu kila siku kwa nini wanashindwa kufikia mafanikio ya aina fulani. Kati ya sababu hizo ambazo zinatolewa ukiziangalia hakuna sababu mbaya za wao kushindwa kufanikiwa, sababu zote ni nzuri na zinafaa. Lakini, linapokuja suala la mafanikio kwa bahati mbaya sana huwa hakuna sababu.
Kwa mfano, tuchukulie umepanga kufanya jambo fulani baada ya mwezi mmoja. Inapofika ule mwezi ukashindwa kulifanya jambo hilo kutokana na sababu zako ambazo unazijua, basi umeshindwa. Hakuna kutoa sababu. Hata kama sababu zako ukatoa zikawa za kweli, haziwezi kusaidia kufanikisha jambo lako tena. Dunia haitaki sababu zako, inachotaka ni matokeo ya kile unachokifanya. Ukikumbatia sana visingizio hutaweza kufanikiwa.
5) Mawazo hasi.
Tabia kubwa ambayo watu wengi wanayo na inaua ndoto za wengi ni mawazo hasi. Mara nyingi wengi wetu ni watu wa mawazo hasi sana. Mawazo haya hasi huwa yapo kwetu sisi na hata kwa wale wanaotuzunguka. Ni kitu ambacho watu huwa wanakichulia kwa kawaida iwe kwa kujua au kutokujua lakini kwa kifupi mawazo hasi yanaua ndoto na mafanikio kwa ujumla. 
Kwa mfano, kama unaamini una mkosi, laana au unaona huna uwezo wa kufanikiwa, tambua hayo ni moja ya mawazo hasi ambayo unayo na ni hatari sana kwa mafanikio yako. Ili kufanikiwa ni vizuri ukajijengea tabia ya kuwa na mawazo chanya. Bila kuwa na mawazo chanya ya kuamini kuna ushindi na mafanikio yapo, hakika huwezi kufanikiwa hata ufanyaje.
6) Matumizi mabaya ya pesa.
Ili ndoto zako ziweze kutumia zinahitaji pesa. Bila kuwa na pesa malengo na mipango yako haiwezi kutumia kwa uhakika kama unavyotaka. Sasa kama unapata pesa halafu ukawa una matumizi mabovu, hiyo ni moja ya tabia ambayo inaua ndoto na mafanikio yako kwa kiasi kikubwa.
Pesa yoyote inayopatikana inatakiwa kutunzwa tena sana kwa ajili ya uwekezaji. Kwa hiyo kabla hujatumia pesa yako ni vyema ukajiuliza mara mbilimbili, kwamba je, fedha hii inakwenda kwa matumizi sahihi? Ukiwa na matumizi mabovu ya pesa hakuna utakachokifanikisha kikubwa kwenye safari yako ya mafanikio.
7) Kuridhika.
Kati ya kitu ambacho hakifahamiki sana, lakini kinaua mafanikio makubwa ya wengi ni kuridhika. Kama ndani yako una tabia ukipata mafanikio kidogo ndio umeridhika basi elewa hutaweza kufanikiwa sana. Hautafanikiwa kwa sababu tena utakuwa hauna kitu chenye nguvu au uwezo wa kukusukuma na kukutoa hapo ulipo.
Kama unafikiria natania waangalie watu ambao baada ya kupata mafanikio kidogo wakaridhika maisha yao yakoje. Bila shaka yoyote utagundua maisha yao yameshuka si ya viwango vile vya kipindi kile. Kwa kawaida unaporidhika unakuwa unakosa ubunifu na matokeo yake kujikuta siku hadi siku unakuwa unarudi nyuma badala ya kufanikiwa.
8) Ulevi kwenye mitandao ya kijamii.
Changamoto kubwa inayowakabili vijana wa sasa ni matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii. Vijana wengi badala ya kutumia mitandao ya kijamii kwa faida huitumia kwa hasara. Wengi hutumia mitandao hiyo kama ‘kuchati’ na kutuma picha ambazo hazina mbele wala nyuma.
Kama unatumia mitandao ya kijamii kwa namna hii, ujue kabisa unaua mafanikio yako bila wewe kujua. Hiyo yote kwa sababu unakuwa unapoteza muda na nguvu nyingi kwa vitu ambavyo vilitakiwa kukusaidia. Kama unataka kufanikiwa badilisha matumizi ya mitandao ya kijamii yawe kwa faida kwako.
Kwa leo tutaishia hapa, lakini hizo ndizo tabia ambazo unatakiwa kuwa nazo makini ili kuepuka kuua ndoto na mafanikio katika maisha yako.
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 04 80 35,








No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.