Oct 2, 2019
Hawa Ndio Watu Hatari Usiowajua, Wanaonyonya Nguvu Za Wengine.
Inaweza kuonekana kama
ni kitu cha kushangaza lakini huu ndio ukweli wapo watu wanaonyonya nguvu za
watu. Watu hawa wana uwezo wa kumwandama mtu hadi anakufa bila kujua. Watu hawa
hawajafa,wako hai na tunaishi nao, wengine wakiwa ni watu wetu wa karibu sana,
kama wazazi, wapenzi, watoto, jirani, marafiki au mabosi wetu. Hufanya vipi
kunyonya nguvu zetu? Hutumia njia za aina mbalimbali, ambazo huzaa matunda
kweli.
Mtu anaweza kuuliza,
inawezekana vipi mwingine anyonye nguvu zangu na hizo nguvu ni zipi? Kwa mfano,
mimi ninapo kuwa nakukera kila siku, ninakugusa kihisia. Ninapokugusa kihisia,
unaumia kihisia na kimwili. Baada ya muda Fulani wa kero zangu, nakuwa nimekupa
athari kubwa kimwili na kiakili bila mwenyewe kujua na kama imeshawahi
kukutokea umekerwa na mtu huwa inapelekea hata unapokutana na mtu huyu
anayekukera unakuwa unajisikia vibaya.
Hebu pia tuchukue mfano
wa bosi na mtumishi wake. Kama bosi ni mtu wa maringo, dharau, kulaumu bila
kujali nini kimefanyika, mkandamizaji na asiyejali kuhusu madhila ya wengine,
ni wazi aliye chini yake ataumia tu,
kwanza, kihisia, halafu kimwili. Ataichukia kazi yake na hatimaye anaweza
kufika mahali akaona maisha haya maana aliyoitarajia.
Ni vigumu kubaini mtu
ambaye ni mnyonya nguvu mapema, lakini kwa kuelekezwa, mtu anaweza kuwa makini
na kuwabaini watu wa aina hiyo popote walipo au watakapokuwa. Nimeamua
nikuelekeze au kukutajia sifa za watu wanaoweza kuwanyonya wengine na kuwaacha
wakiwa maganda matupu, huku wakiwaacha wakiwa wanyonge hawajui ni kipi cha
kufanya.
Hizi
ndizo sifa za watu wanaoweza kuwanyonya wengine:-
1. Kuna
watu ambao tunanaweza kuwaita, “miye maskini.”
Hawa ni watu ambao muda
wote unapokutana nao, wanalalamika tu. Hakuna siku ambayo utakutana nao ukute
wanazungumzia mambo mazuri au wanafurahia hali. Kila siku wao ni walalamikaji,
wanaoamini kwamba, wanaonewa na kuteswa. Unaweza kukuta ni watu wa kulalamika au
kukosoa tu, lakini bila kutoa pendekezo au kuonesha ni njia zipi zingepaswa kufuatwa au njia zipi
zingetatua tatizo.
Wao wanaona kwamba,
wanaonewa, wananyimwa nafasi, wanatafutwa na kuchukiwa. Hawa kwa kawaida hawana
uwezo wa kusema lao, kusema wanachofikiria au walichobuni, hapana. Hata kama
wanatakiwa kusema kuhusu jambo fulani maalumu, ambalo halihusiani na kuonewa na
mtu, watajikuta wakiingia kwenye kulaumu au kukosoa kwanza, ndipo waweze
kujibu, kama basi watakuwa na uwezo wa kujibu.
Hawa ni wanyonya nguvu
za wengine. Hawa ni watu wa kuepukwa sana. Kama mtu wa aina hii anakujia na
kutaka mjadili jambo, ambapo anaanza malalamiko au kukosoa kwake, huna budi
kutafuta sababu ya kukataa kuwa karibu naye. Ni lazima ufanye hivyo, kwani
akikuzoea ni lazima atakunyonya nguvu zako zote.
2. Kuna
watu ambao wao ni wakuzaji wa mambo.
Hawa ni wanyonya nguvu
pia ambao wao kitu au jambo dogo hufanywa kubwa hadi mtu anaweza kuamini kwamba
ni jambo kubwa kweli, ingawa awali alijua ni jambo dogo. Hawa wako maofisini na
majumbani. Mtu anaumwa na mafua, lakini atalalamika, atagumia na kuaga kabisa
na kuacha kabisa wosia, kwamba anakufa.
Yeye mwenyewe huyu
anayefanya visa hivyo anaamini kwamba, kwa kufanya hivyo, atapata huruma zaidi,
ataona watu wanavyohangaika kuonesha wanavyomjali na kutaka kupima umuhimu
wake. Kwa kawaida kukuza kwao mambo kunaweza hata kusababisha hata wengine
wakaugua zaidi au hata kupoteza maisha kabisa, kutokana na kuongeza chumvi sana
kwenye maneno yao.
3. Kuna
wale ambao kwa lugha ya mtaani tunawaita wameza kaseti.
Hawa ni wale ambao wanataka waongee wao tu, wanataka wao ndiyo wasikilizwe na mwingine anapotaka hata kusema moja hapewi
nafasi. Mtu atazungumza yeye kuanzia mwanzo hadi mwisho, hata kama ni kwa saa
tatu mfululizo. Mwingine anapotaka kuongea, yeye ameshamkatisha na kuzungumza
yeye. Hataki kuona mtu mwigine akizungumza kama yeye yupo. Hata kama ni mgeni
mahali, akishapewa nafasi ya kuzungumza, huzungumza kweli.
Hajali kama kuna mtu
ambaye anataka aseme hisia zake, hapana. Inafika mahali, kama unamsikiliza
unachoka kabisa. Hatajali, hata kama utamwonesha kutokujali. Kama ni nyumbani
au ofisini, hatajali kukupotezea muda wako kwa vyovyote vile. Kama ni ushauri
aliomba kwako, yeye ndiye atakupa ushauri kwa sababu, hatakupa nafasi ya
kuzungumza katika kumshauri. Hawa ni wanyonya nguvu ambao tunao kila siku.
4. Kuna
wanyonya nguvu ambao kazi yao ni kuwafanya wengine washitakiwe na dhamira.
Kila wakati linapotoea
jambo , juhudi yao kubwa ipo kwenye kutafuta njia ya kulaumu ili wengine
washitakiwe na dhamira. Wakati mwingine jambo liko wazi kabisa kwamba, hao
anaowalaumu hawahusiki, lakini ni lazima atalaumu tu. Hata kama atafafanuliwa
na kuona kwamba, anaowalaumu hawana tatizo, bado atasema, ‘hata kama hamtaki anahusika kidogo’Wanyonya nguvu hawa wanatafuta
kasoro ili walaumu, ili mtu mwingine ajisikie kukosa, ashitakiwe na dhamira.
Anaweza kuangalia mtu
anavyofanya kazi Fulani na kuona ni nzuri sana. Lakini atajaribu kwa kadiri
awezavyo kumkosoa mtu huyo kwa kitu ambacho wala wakati mwingine hakihusiani
moja kwa moja na kazi ile. Anaweza kusema ‘ile
kazi ya mwaka jana angefanya hivi tusingekosa tenda’ lengo ni kumfanya mtu
ashitakiwe na dhamira. Hataki kusifia hii kazi nzuri ya sasa, anataka kukosoa
ya zamani ambayo iliharibika.Dawa ya hawa ni kuwapuuzia.
5. Kuna
wanyonya nguvu wengine ambao ni wale wasioisha kuwa na matatizo yanayohitaji
ushauri.
Asubuhi atakuja
kukuomba ushauri unaohusu jambo Fulani, mchana atakuja na jioni atakutafuta.
Wakati mwingine ushauri anaoomba ni wa kawaida tu. Ni vizuri kumwonesha kwamba,
unajali anachosema, lakini ni vema kila wakati kumwonesha kwamba, huna jibu,
siyo huna nia ya kumsaidia kwenye tatizo lake. Ajue kwamba, huna jibu kwa sababu
hujui. Ukikosa njia au jibu mara kadhaa, atakata tamaa na kukuacha. Usimwoneshe
jeuri au dharau ama kisirani.
6. Kuna
wanyonya nguvu ambao kazi yao ni kuudhi kwa maneno ya kushushua na kushushua.
Badala ya kunyamaza,
akikuona na nguo ya aina Fulani, atakwambia, ‘bwana mzee huwezi kuvaa nguo za mtumba kwa hadhi yako vipi’ Ni
wakati ambao kila mkikutana , watatafuta namna ya kukera kihisia zako na
kujaribu kukushushua. Anaweza mtu kusema ‘ mbona afya yako inazidi kuwa mbaya’
bila hata sababu ya msingi. Ni watu ambao muda wote wanataka kuumiza hisia za
mwingine.
Bila shaka umeshawahi
kukutana na mmoja kati ya wanyonya nguvu hawa. Jitahidi wakati wote kuwa makini
wasije wakafanikiwa kukuweka chini ya himaya zao. Jitahidi kuwabaini na kujua
namna ya kuwaondolea mbali kwenye maisha yako.
Nakutakia mafanikio
mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza zaidi na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 0345/dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Thanks bro!
ReplyDeleteAsante Sana mkuu
ReplyDeleteElectrotza
Nikwer mana limekuwa nitatizo San ktk jamii zetu hasa jeshi LA uswazi%
ReplyDelete