Jan 31, 2017
Kilimo Cha Maharage Ya Njano.
Kilimo cha maharage ni rahisi na
kinalipa sana kikifanyika kwa utaalamu. Gharama nafuu na ushindani wa soko sio
mkubwa sana. Huhitaji kusafiri, kinachofanyika ni kuwaita wateja waje shambani
kwako na kuchukua mzigo.
Ekari moja ya maharage ya njano kwa
maeneo mengi unaweza pata gunia kati ya 8 – 12 au zaidi ila inategemea na eneo
unalolimia.
Shamba la maharage kama unalima kwa
kumwagilia unaweza lima mara tatu kwa mwaka . Hii ina maana ukilima ekari moja
tu utakua na uhakika wa kipato cha uhakika na kikubwa kila baada ya miezi
minne.
Upandaji wa Maharage
1.Mbegu.
Upandaji wa maharage unatakiwa
ufanyike katika muda muafaka kutokana na eneo ili kuweza kupata maji ya
kutosha (mvua) na wakati wa mavuno kunatakiwa kuwe na ukavu ili maharage
yasiharibikie shambani.
Maji mengi yaliyotuama na ukame
siyo nzuri kwa maharage na husababishia mmea magonjwa na kuoza au kukauka.
Kuna aina nyingi za maharage ambazo
zinaweza kupandwa kwa mfano (Rojo, Mshindi, Pesa, SUA 90 na Canadian wonder)
ambazo ni mbegu zilizoboreshwa, lakini pia kuna mbegu za kawaida zilizopo kwa
wakulima ambazo huhimili
baadhi ya magonjwa na wadudu.
Inashauriwa kupanda maharage katika
umbali wa (50×20) sentimita 50 (mstari kwa mstari) na sentimita 20 (mmea
kwa mmea), panda mbegu mbili za maharage katika shimo moja, mbegu zinaweza
kupandwa katika umbali wa sentimita 3-6 kwenda chini.
Kama mbegu moja moja katika kila
shimo, nafasi itapungua. Kwa maharage yaliyokuwa vizuri kunatakiwa kuwe na
idadi ya mimea 150,000-200,000 kwa hekta (maharage mafupi), maharage yatambaayo
idadi yake ni nusu ya
maharage mafupi kwa hecta. Hekta 1 =
ekari 2.471.
2.Mbolea.
Mimea huhitaji virutubisho kutoka
kwenye udongo ili kuweza kukua na kuzalisha matunda yenye afya. Maharage
huhitaji madini ya ‘phosphorous’
na ‘potassium’ ambayo hupatikana
kutoka kwenye mbolea hai kama vile samadi, mboji, majivu, mkojo wa mifugo
na mabaki ya mimea.
Ni muhimu kufahamu udongo ambao
unatarajia kupanda mimea yako ili
kutathmini viwango vya madini
yaliyopungua ili kufanya juhudi za kuongeza.
Zaidi ya yote ni vizuri kutumia
mbolea hai ambazo zinasaidia viumbe hai huweza kukua na kuendeleza
kurutubisha udongo, kwa mfano mizizi ya maharage husaidiana na viumbe hai
(nitrogen fixing bacteria) waishio kwenye udongo kutengeneza nitrogen.
Mbolea za chumvichumvi huharibu na kufukuza viumbe hai kutoka kwenye
udongo.
3.Magugu.
Inashauriwa kupalilia mimea kabla
haijatoa maua. Shughuli hii inatakiwa ifanywe kwa uangalifu ili kukinga
mimea isiharibike kwenye mizizi kwani uharibifu wa aina yoyote huweza
kusababisha magonjwa kwa mmea.
Inashauriwa kupanda mimea kwa
kuzunguka (crop rotation) ili kupunguza uwezekano wa magugu na maradhi kuweza
kushambulia
mimea.
4.Wadudu na magonjwa.
Maharage hushambuliwa na wadudu na
magonjwa. Miongoni mwa njia
za kuzuia, kukinga na kufukuza wadudu
ni kuhakikisha kuwa mimea
ipo katika hali nzuri (imepaliliwa,
nafasi ya kutosha na haijaharibika).
Pia kubadilisha aina ya mimea
inayopandwa kwenye shamba moja mara
kwa mara husaidia kupunguza uwezekano
wa wadudu kuongezeka.
Kwa baadhi ya wadudu kama vile viwavi
(African Ballworm) huweza
kufukuzwa kwa kutumia muarobaini au
vitunguu saumu.
Maji ya muarobaini ni dawa nzuri
sana kwaajili ya kufukuzia wadudu na haina madhara yoyote kwa
binadamu.
5.Kukomaa na Kuvuna.
Maharage ya kijani yanatakiwa yavunwe
kabla punje za maharage hazijakuwa sana. Hii ni kati ya wiki 7-8 baada ya kupanda.
Maharage makavu huvunwa mara tu kiasi cha kuridhisha cha kukomaa na kukauka
kinapokuwa kimefikiwa.
Kwa mfano asilimia 80 ya maharage
yakishakomaa na kuanza kubadilika rangi (kukauka) au kwa aina nyingine
kusinyaa yanakuwa tayari kwa mavuno.
Kwa kawaida mmea wote hung’olewa na
kuwekwa juani ili uendelee kukauka kisha maharage hutolewa kutoka kwenye mmea
na kuendelea kukaushwa ili kupunguza matatizo wakati wa kuhifadhi.
Baada ya kukauka hadi kufikia
angalaua asilimia 12 ya unyevu, maharage yanatakiwa yahifadhiwe kwenye
chombo chenye mfuniko kama vile ndoo ya plastiki au pipa na kuendelea
kuyaangalia mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa wadudu hawajaingia na kisha
kuyafunika tena.
6. Kilimo mchanganyiko.
Ni vizuri sana na inashauriwa kupanda
maharage pamoja na mimea ya jamii nyingine kama vile mahindi kwani
husaidia katika kusambaza madini ya nitrogen na kwa maharage yenye
kutambaa, hupata sehemu ya kujishikilia au kutambalia.
Maharage yanaweza yakapandwa katikati
ya mistari ya mahindi. Pia viazi huweza kupandwa pamoja na maharage. Inashauriwa
kutokupanda maharage pamoja na mimea mingine ya jamii ya maharage (leguminous)
kwani husababisha mimea isiweze kukua vizuri kwasababu ya kutokupata
virutubisho vya kutosha na huweza kusababisha matatizo kama ya wadudu kama nzi
weupe.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
ngwangwaruu ankooo, mbona hujaeleza unavuna kiasi gani na mbegu bora wanapata waapiii
ReplyDeletegoood nimeona aina ya mbegu
ReplyDelete