Jun 6, 2015
Mambo 12 Ya Kuzingatia Kama Unataka Kujiajiri.
Ulishawahi kufikiria kujiajiri wewe
mwenyewe katika maisha yako? Hili
ni swali ambalo litakuwa linakuja kwako kila utakapokuwa unalalamika kukosa
kazi uliyoisomea. Kila mmoja wetu amezaliwa na uwezo huu wa kujiajiri, ingawa
wengi wetu huwa siyo rahisi kutambua uwezo huo na kujikuta ni watu wa
kukimbilia kazi za wengine.
Ikumbukwe kuwa tumezaliwa na shauku, kiu, kufanya mambo ya hatari,
uvumbuzi, akili na vitu vingine vingi ambavyo huonyesha wazi kuwa mtu hawezi
kufundishwa ujasiliamali bali uko ndani yake kiasili, kinachohitajika ni
yeye tu kujiweka katika mazingira ya kuruhusu akili yake kutatua
tatizo lililojitokeza sehemu husika.
Kwa kadiri jinsi mtu anavyoifikirisha akili yake katika kutaka
kujiajiri, ndivyo anavyapata majibu na mafanikio zaidi. Kwa nini uteseke kwa
kujiajiri wakati uwezo wakujiajiri unao na unaweza kufanikiwa sana. Hapa katika
makala hii utajifunza mfululizo wa mambo unayotakiwa kuyazingatia kama kweli
una nia ya kujiajiri na kuiamsha hamasa ya ujasiriamali iliyo ndani yako:-
1. Jenga nidhamu:
Unapotaka kuwa mjasiriamali ni lazima utengeneze nidhamu yako ya
kazi.
Kabla hujaanza kuingia katika hatua ya kujiajiri ili uepuke hatari
ya kupoteza kila kitu jiulize kama una nidhamu ya kutosha kuingia katika hiyo
shughuli. Huwezi ukawa mjasiriamali ambaye hauheshimu hata muda wako wa kazi.
Hii itakuwa ngumu sana kwako kufanikiwa. Kujenga nidhamu, hili ndilo jambo la
kwanza la kuzingatia kama unataka kujiajiri.
2. Tambua jamii inahitaji nini.
Kama unataka kuwa mjasiriamali ni lazima uwe na uwezo wa kuchemsha
akili yako katika kuyasoma mazingira uliyopo yanahitaji kitu gani na wewe ili
uje na utatuzi wake. Lenga eneo moja ambalo unaona kweli lina uhitaji na
unaweza ukaja na utatuzi wake. Toa huduma ile muhimu ambayo jamii yako
inaihitaji na siyo kinyume chake. Kwa kufanya hivyo utakuwa unajitengenezea
sifa halisi ambayo mjasiriamali wa kweli anatakiwa kuwa nayo.
3. Tengeneza lengo
Kutengeneza lengo la biashara ni hatua muhimu katika hatua za kuwa
mjasiriamali. Lengo hili uliweke katika maandishi na litakusaidia katika
kuwashawishi watu kukusaidia mtaji. Mara utakapokuwa umeandika lengo la
biashara unayotaka kufanya usiweke maandishi hayo kabatini, anza
kuyatafutia njia ya kuwa kitu halisi kutokana na hayo maandishi.Na pia lengo
hili litakusaidia wewe usiyumbe na kutoka katika mstari wa lengo ulilojiwekea
na litakuwa ni muongozo wako.
4. Jiunge na wajasiriamali.
Ikiwa unataka kuwa mjasiliamali ni muhimu kutafuta eneo ambalo
wajasiriamali wengi wanakutana kujadiliana.Katika mazingira kama haya utakuwa
kama yai linaloatamiwa na kuku ili lije kutoa kifaranga. Wengi wao huwa
wamepitia magumu kufika walipofika na hivyo wakiwa wanasimulia habari zao
watakufanya ujiamini kuwa na wewe unaweza.
5.Hojiana na wajasiriamali waliokutangulia.
Kama unataka kuwa mjasiriamali utapata faida kubwa sana kuzungumza
na watu ambao tayari wanafanya ujasiriamali. Ukiwa na bahati kumpata mwenye
moyo wa dhati wa ujasiliamali hatokuficha kitu ili kukusaidia ufikie ndoto
yako. Kwani kiasili mjasiriamali huwa anajitoa kuisadia jamii yake na hana haja
ya kuwa mchoyo wa maarifa.
6. Tengeneza marafiki.
Yeyote anayetaka kuwa mjasiriamali ni lazima atengeneze marafiki
wengi wenye mtazamo chanya kama yeye. Usiwe na marafiki ambao
unatofautiana nao mtazamo, watakuwa wanakukatisha tamaa kwani kwao hilo wazo
wanaona haliwezekani na watakwambia huwezi. Kauli kama hizo zitakukatisha tamaa
na ukizingatia wazo lolote mwanzo huwa gumu na haliwezekani mpaka uanze
kulifanyia kazi. Ndio ule msemo wa ukitembea na mwizi na wewe utakuwa mwizi
unaingia hapa.
7. Tengeneza wazo rahisi kutekelezeka.
Kama unataka kuwa mjasiliamali ni vyema ukawa umechagua eneo moja
maalumu la kulitafutia ufumbuzi na ambalo rahisi kutekelezeka na pia kuwa
makini na hilo jambo unalotaka kulifanyia kazi uwe na uzoefu nalo japo
kidogo, kwani huwezi kutibu ugonjwa usijua hata unakaa wapi.
8. Fanya bidii kuliko wengine.
Hapa lazima utambue kuwa kila mtu anaweza kuwa mjasiriamali, lakini
tofauti huja katika bidii wanayoweka katika shughuli waliyochagua. Kama
umejitolea kuwa mjasiriamali ni lazima ujitoe kufanya kazi kwa bidii kuliko mtu
yeyote yule.
9. Tafuta mshauri.
Ukitaka kuwa mjasiriamali ni vizuri ukawa na mtu anayekuongoza kwa
mawazo kwani si kila wakati utakuwa unawazo sahihi. Si kwamba yeye ndio awe
anakutengenezea wazo bali anaweza akawa anapitia wazo lako na kukushauri
kama uboreshe au kuna vitu uondoe. Ikiwa utampata mshauri mzuri itakusaidia
kupunguza hatari ya kuumia mapema. Kuwa makini na mtu utakayemchagua, uwe
unamuamini na awe hana ushindani na wewe.
10. Hakikisha unafurahia:
Hapa ni lazima ujue, kama unataka kuwa mjasiriamali mzuri na
utakayefanikiwa ni lazima ufanye kitu unachokipenda. Unapokuwa unafanya kitu
unachokipenda unajitengenezea mazingira ya kuwa na furaha muda mwingi.
11. Fanyia kazi hatari unayoifahamu.
Sifa ya mjasiriamali wa kweli, ni yule asiyeingia kichwa kichwa
kutaka kutatua tatizo pasipo kupiga hesabu za kutosha za hatari iliyopo. Mjasiriamali,
kweli huwa anachukua hatari za jamii na kujibebesha yeye lakini anapaswa
achukue hatari ambayo hesabu zake anazifahamu.
12. Hudhuria semina na makongamano
Wewe kama unataka kuwa mjasiriamali ni lazima utenge muda wako
kuhudhuria semina mbali mbali, zinazohusiana na shughuli unazotaka kuja
kufanya. Unapohudhuria maeneo kama hayo itakusaidia kutengeneza mtandao na watu
wengine na hata kukutana na watu wanaoweza kukusaidia kufika unapotaka.
Kwa wale wote
wenye mawazo ya kutaka kujiajiri, hizo ni baadhi ya hatua ambazo unaweza
kuzitumia katika kufikia ndoto yako. Unaweza kuvitumia vidokezo hivyo
kukusaidia kutimiza ndoto zako.
Tunakutakia
kila la kheri katika safari yako ya mafanikio ya kibiashara iwe ya ushindi
kwako, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO
PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
MAKALA HII IMEANDIKWA NA FRANK VICTOR
WA LISHA UBONGO.
.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.