DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, July 28, 2017

Wakati Bora Wa Kufikia Mafanikio Yako Ni Huu…

No comments :


Leo nimejikuta namkumbuka sana mwalimu wangu wa somo la Kiswahili, moja kati ya vitu ambavyo vimenifanya niweze kumkumbuka ni vile ambavyo alikuwa anajitoa kwa hali na mali katika kuhakikisha tunaelewa somo la Kiswahili. Ni siku nyingi kidogo zimepita lakini kile ambacho alinifundisha bado hakijafutika  akili mwangu, na sina uhakika kama kitakuja kufutika.

Mwalimu wangu huyu  sitachoka kumuombea kwa mwenyezi  Mungu kwa kila jambo ambalo analifanya aweze kufanikiwa Zaidi. Namkumbuka kwa sababu kuna somo ambalo alitufundisha kwa kutumia nguvu zote, somo hili ni somo la nyakati.

Na katika somo hili alisema zipo nyakati mbalimbali ambazo ni wakati uliopita, wakati uliopo na wakati ujao. Pia alieleza ya kwamba nyakati hizi zote humuhusu mwanadamu, katika kufanya na kusimulia mambo mbalimbali ambayo yalikwisha fanyika au ambayo yatafanyika.

Na miongoni mwa vitu ambavyo nakumbuka aliweza kutushauri kuhusu nyakati hizi alisema ya kwamba,  mwanadamu yeyote yule ili aweze kufanikiwa katika maisha yake ni lazima aweze kutambua ya kwamba katika nyakati hizo ni nyakati moja tu ndiyo muhimu kwake.

Na nyakati hiyo ni wakati uliopo na si vinginevyo, kwani wakati uliopita na wakati ujao si rafiki kwa mwadamu hata kidogo katika kutenda mambo ya msingi, kwani watu wengi wamekufa na ndoto zao kwa sababu waliamini Zaidi nyakati zijazo, wao pamoja na kuwa na mambo mazuri walijifariji na kusema nitafanya kesho, kesho hiyo ikawa kesho mpaka siku wakazikwa na neno lao nitafanya kesho.

Kwa maneno mengine kusema nitafanya kesho, kwa neno moja lenye kujifariji tunasema“nimeahirisha”. Neno hili ni baya sana kwani wale wote waliofanya kitendo hiki hawakuweza kufikia lengo lao kwa asilimia zote. Kuahirisha kufanya jambo la msingi ni kutafuta visingizio.

Hivyo kama wewe ni mtu wa kuahirisha sana mambo, hasa kwa kile kitu unachokifanya, elewa kabisa unapanda mbegu au unajitengenezea mazingira ya kushindwa kwako. Kama kuna jambo ambalo unataka kulifanya leo, hebu lifanye bila kusita sita au bila kuwa na shaka ya kitu chochote.

Hivyo kama kweli unataka mafanikio ya kweli jifunze kufanya mambo kwa wakati, huku ukikimbia visingizio visivyokuwa vya msingi. Daima ikumbukwe  ya kwamba ni heri upate ugonjwa wa malaria, kwani ugonjwa  huu utatibika,Ila ukipata ugonjwa wa kuahirisha mambo ya msingi basi jiandae kufa maskini.

Mwisho nikuache na nukuu isemayo; Kumbuka ukianza leo si sawa na kuanza kesho.

Imeandikwa na uongozi wa mtandao huu wa dira ya mafanikio,
Imani Ngwangwalu & Benson Chonya,


Thursday, July 27, 2017

Hatua Hizi Ni Msingi Wa Mafanikio Yako.

No comments :

Kuna yale mambo ambayo kwenye maisha huwa yanaonekana ni rahisi kabisa kufanyika na pengine kukupa mafanikio. Hata hivyo kitu cha kushangaza mambo hayo pamoja na urahisi wake wengi huwa hawayafanyi.
Hali hiyo huwa inatokea kwako kwa sababu ya kujikuta upo katika hali ya ‘easy to do…also easy not do,’ yaani urahisi kwa hali ya kawaida unauona, Lakini ndani yake kuna ugumu fulani hivi ambao unakuzuia kufanikiwa.
Ukweli wa mambo ulivyo kwenye maisha yako, iwe afya, furaha au utajiri unaweza kuvipata ikiwa utachukua hatua ndogo ndogo kila siku zile zinazowezekana ambazo zitakusogeza kwenye lengo lako bila kudharau hatua yoyote ile.
Kama ni rahisi hivyo, kwa nini watu wengi wanashindwa kufikia malengo yao? Hiyo yote ni kwa sababu ‘easy to do…also easy not do,’ kama tulivyosema. Hatua ndogo ndogo zinakuwa ni ngumu sana kuweza kutekelezwa na wengi wetu.
Jiulize ni mambo mangapi katika maisha yako ulipoambiwa fanya kitu hiki, ulisema kwamba, ‘aaah kitu hiki ni rahisi, nitakifanya tu’. Lakini mwisho wa siku unajikuta unashindwa kuchukua hatua kabisa.
Kuanzia sasa, acha kuwa mtumwa wa ‘easy to do…also not easy to do.’ Chukua hatua ndogo ndogo bila kudharau udogo wa hatua hiyo. Ukifanya hivyo utaweza kufanikiwa na kutimiza ndoto zako.

Wednesday, July 26, 2017

Kama Unashindwa Kufanya Mabadiliko Kwenye Maisha Yako, Basi Tatizo Ni Hili…

No comments :
Kuna wakati unaweza ukajikuta unataka kufanya mabadiliko kwenye maisha yako, lakini unashindwa. Je, umeshawahi kujiuliza kushindwa huko kunatokana hasa na nini au kitu gani. Najua hili linaweza likawa limekotekea.
Ikiwa kila wakati unajaribu kufanya mabadiliko ya kitu fulani na unashindwa kuleta mabadiliko hayo, basi tambua maumivu ya kushindwa hayajawa makubwa sana ndani yako hadi uweze kuleta mabadiliko hayo.
Kwa mfano, unataka kuwa na mtaji na unashindwa kila mara, basi elewa kabisa maumivu ya kushindwa kupata mtaji hayajawa makubwa vya kutosha. Tuchukulie leo hii, ukaambiwa usipokuwa na mtaji hadi mwaka huu unaisha, utapigwa risasi.
Jiulize utakubali kufa kwa sababu ya kukosa mtaji huo unaoutaka? Bila shaka haitawezekana, utafanya kila linalowezekana kufanikisha hilo. Hivyo, wakati mwingine mabadiliko yanakuja kwenye maisha yako kwa sababu ya kule kuumia sana.
Wakati ulipokuwa shule ulisoma sana na kuhakikisha unafaulu ili kukwepa maumivu ya kufeli. Pia kuna wakati umeweka juhudi nyingi sana ili kukwepa maumivu ya aina fulani na kutafuta mahala sahihi kwako.    
Tunaambiwa kitu chenye nguvu ya kubadili tabia yako na mafanikio ni maumivu. Waulize wote ambao wamefanikiwa na ambao wanafikiri chanya kuhusu mafanikio, watakwambia maumivu yamewasaidia sana kubadilika na kuweza kufika hapo walipo mpaka leo.
Hivyo basi, kila wakati tambua hasira ya kushindwa kupata kile unachokita, maumivu ya kushindwa kupata kile unachotaka kukibadili, yatumie maumivu hayo ili yaweze kukusaidia kuweza kufanikiwa.

Tuesday, July 25, 2017

Kitu Pekee Cha Kukiogopa Pale Unapohitaji Mafanikio Ya Kweli.

No comments :

Kuna wakati mwingine inabidi ujutie katika hali ambayo upo hivi sasa, nasema hivyo kwa sababu moja kati ya mambo ambayo inakubidi ujutie katika maisha yako ni kwa sababu umekuwa ni mtu wa kushangaa kuliko kutenda mambo ya msingi.
Tabia hii ya kushangaa kila kitu pasipo wewe kuchukua hatua ndiyo ambayo kiukweli inakufanya uje kujuta hapo baadae, na pia ikumbukwe wakati wewe unazidi kushangaa wapo wengine ambao wanazidi kusonga mbele katika utendaji.
Tabia hii ya kushanga ni mbaya sana katika safari ya mafanikio, kwa mfano, Utakuta wao ni watu wa kushangaa na kuhamasika sana na miradi wanayofanya watu wengine, ukija upande wao hakuna hata kitu kimoja wanachofanya.
Vilevile utakuta watu hawa kazi yao ni  kuingia kundi moja, wanashangaa kinachoendelea humo na kutoka na kuingia tena kundi lingine wanashangaa wee na kutoka tena, pia bila kuchukua hatua, endapo utachukua jukumu la kuwauliza watu hawa watakwambia wanashangaa mataa.
Tabia hii kama unayo ni vyema ukaamua kuiacha mara moja kwani dunia ya sasa hivi ni ya mwendo kasi Zaidi ya kasi ya 4G hivyo kila wakati ni lazima uweze kufanya kazi. Kama kuna fursa hata kama ni ndogo kiasi gani, itumie ikusaidie kufanikiwa na acha kubaki tu kuwa mtu wa kushangaa.  Kama ni kujifunza, jifunze kweli.
Uzuri au ubaya wa maisha hakuna ubabaishaji, ukileta ubabaishaji wa aina yoyote ile, utaumbuka tu na ni lazima utajibiwa na maisha kama vile wewe unavyobabaisha. Badilika rafiki na achana na biashara ya kushangaa, kuwa mtendaji na aamua kufanya kazi.
Hivyo amua sasa kuwa ni mtu wa kuchua hatua kuliko kubaki kushangaa, kwani kufanya hivyo ni kujichelewesha mwenyewe kumbuka ya kwamba kuendelea kushangaa ni kupoteza muda na kupoteza muda ni sawa na kuacha pesa zipite machoni mwako.
Mpaka kufikia hapo hatuna la ziada tukutakie siku njema na mafaniko mema, Mwenyezi Mungu akubariki sana kwa kusoma Makala haya.
Imeandikwa na uongozi wa mtandao blog ya dira ya mafanikio,
Imani Ngwangwalu & Benson Chonya,


Monday, July 24, 2017

Utajiri Au Umaskini Wako, Unatokana Sana Na Maamuzi Haya.

No comments :
Maisha unayoishi sasa, kwa sehemu kubwa, yanatokana na maamuzi uliyoyafanya kipindi cha nyuma na maisha utakayoishi kesho pia yanategemea sana maamuzi unayoyafanya leo kwenye maisha yako.
Unauwezo wa kuboresha maisha yako kwa kufanya uchaguzi sahihi wa hatua unazozichukua kila siku. Moja ya kitu unachotakiwa uanze nacho ili uweze kuchukua hatua sahihi ni kujifunza juu ya kutawala pesa zako.
Hivi pengine nikuulize, umeshawahi kujiuliza katika maisha yako pesa ngapi zimepita mikononi mwako? Ukiangalia, ni pesa nyingi sana, lakini cha ajabu kwa wengi zimewaacha jinsi walivyo wakiwa hawana kitu.
Sasa basi, ili kuendelea kukosa pesa kusitokee kwako, unahitajika sana kujifunza juu ya kuwa na maamuzi sahihi ya kutawala pesa zako. Ukiipata elimu hii na ukaielewa vizuri, utakuwa umefanya maamuzi sahihi ya kukupeleka kwenye utajiri wako moja kwa moja.
Kwa mujibu wa uchunguzi mdogo uliofanyika unaonyesha hivi, asilimia kubwa ya watu  waliomaskini wanaweka akiba chini ya asilimi 2 na wengine hawaweki kabisa. Hiyo ikiwa na maana kipato chote kinachobakia kinaingizwa kwenye matumizi.
Mpaka hapo kwenye maamuzi hayo, ni moja ya maamuzi mabaya yanayowapeleka wengi kwenye umaskini.  Akiba au kujilipa mwenyewe kiasi kidogo cha kila pesa unayopata ni kitu cha msingi sana kama unataka kesho yako iwe ya mafanikio.
Ni kweli swala la matumizi ya pesa zako liko mikononi mwako, lakini ili uwe tajiri ni lazima ujue namna ya kutawala pesa zako. Sio kwa sababu una pesa unanunua vitu hovyo na kujikuta hakuna hata kiasi kidogo cha pesa ulichobaki nacho.
Angalia usije ukajikuta ukajuta kesho kutokana na maamuzi mabovu unayoyafanya leo juu ya pesa zako.  Fanya maamuzi leo bora yatakayokufanya kesho ukajiona shujaa mkubwa kwa kujiona ulifanya kitu cha maana kwa sababu ya pesa zako.
Ikiwa unataka kuendelea kimaisha na hata kuwa tajiri elewa vizuri juu ya kutawala pesa, yote haya unatakiwa ujifunze ukiwa bado kijana, kama hautafanya maamuzi hayo sahihi, ni wazi hautafanikiwa.
Utajiri au umaskini wako, siku zote upo mikononi mwako kutokana na maamuzi unayoyafanya juu ya pesa. Leo jiwekee kiapo kwamba, kwa pesa yoyote unayoipata ni lazima uweke kidogo kwa ajili yako.
Kwa kuanzia, anza hata na asilimia kumi ya kile unachokipata, umeshindwa kabisa, anza na kiasi chochote. Pesa hiyo kumbuka ni yako, unakuwa haujapoteza popote, hivyo usiwe na wasiwasi, chukua maamuzi sahihi leo yatakaokupa utajiri.
Endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kwa ajili ya kujifunza na kuhamasika kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com.

Sunday, July 23, 2017

KITABU; The Success System That Never Fails (Mfumo Wa Mafanikio Ambao Haushindwi)

No comments :

Kwenye  kitabu hiki mwandishi W. Clement Stone anaeleza upo mfumo katika maisha , ambapo ukiutumia mfumo huo vizuri, utayafanya maisha yako yasiwe ya kushindwa kamwe, bali yawe ya mafanikio siku zote.
Katika mfumo huo mwandishi ameongelea mfumo usioshindwa katika maisha jinsi ulivyokuwa wa muhimu katika maisha yako. Na mfumo huo umebebwa sana na mambo makubwa matatu ambayo ni;-
Hatua/vitendo (Action)
Hapa inakubidi kuchukua vitendo kwa kitu unachotakiwa kufanya. Unatakiwa kuchukua vitendo bila kujali kitu. Kitu unachokifanya kama umeamua kukifanya, kifanye. Acha kupoteza muda chochote unachokiamini, hebu kifanye bila woga.
Kujua namna ya kufanya (Know-how)
Kuchukua hatua kwenye jambo lolote yenyewe haitoshi peke yake, unatakiwa sasa kujua namna ya kufanya kitu hicho tena. Unatakiwa kujua namna ya kufanya katika hali ambayo itakupa matokeo sahihi.
Maarifa (Knowledge)
Maarifa ni kitu cha msingi katika kufanikisha jambo lolote lile. Lazima uwe umeiva kwa maarifa ya kutosha ili yakusaidie kufanya mambo yako kwa usanifu wa hali juu na kukupa mafanikio. Ukikosa maarifa ya msingi kwa jambo lolote utashindwa.
Hayo ndiyo mambo matatu ya msingi sana ambayo mwandishi ameyasititiza na kuyatilia mkazo karibu katika kitabu chake chote. Mambo mengine ya kujifunza kwenye kitabu hiki ni kama haya yafuatayo;-
1. Maamuzi mazuri katika maisha yanaendana na kuchukua hatua. Kama huchukui hatua, halafu ukasema eti una maamuzi mazuri, basi elewa unajidanganya na  maamuzi hayo hayana maana yoyote kwako kwa sababu hayawezi kukusaidia.
2. Kama umeamua kufanya kitu fulani, iwe ni biashara , masomo au kitu chochote ambacho kipo kwenye malengo yako, usirudi nyuma hadi umefanikisha kitu hicho. Haijalishi njiani umekutana na changamoto nyingi kiasi gani, pambana mpaka upate kile kitu ambacho ulikuwa umelenga kukifanikisha.
3. Unaweza ukaongeza uwezo mkubwa wa kufanikiwa ikiwa utatumia kanuni za mafanikio na kuzifanyia kazi kila siku. Unaweza pia ukapunguza hali ya kushindwa sana kwenye maisha yako, ikiwa kama utaendelea kutumia kanuni hizo hizo za mafanikio. Kama utafanya kinyume na hapo jiandae na anguko kubwa la maisha yako.
4. Mafanikio yanakuja kwa wale wote wanaojaribu hiki au kile mara kwa mara bila kujali wanashindwa kwa kiasi gani. Huwezi kuwa mshindi kama umekaa tu. Jaribu kwa jinsi unavyoweza ili kujenga mafanikio yako.
5. Kila wakati hakikisha unayatawala mazingira yako na sio mazingira yakutawale. Epuka kila hali iwe mazingira au watu wakutawale. Hakikisha unatawala mazingira yako vizuri ili yakupe nguvu ya kushinda.
7. Kufikiri peke yake hakuwezi kukafanya wewe ukashinda uoga ulionao. Kitu kitakachoweza kukufanya ukashinda uoga ulionao ni zile hatua unazochukua. Hatua au vitendo ni dawa pekee ya kuondoa hofu au woga wowote ule kwako.
8. Kama hujiwekei akiba yoyote, elewa kabisa ndani yako umekosa mbegu ya mafanikio. Wanaojiwekea akiba hata kama ni pesa kidogo sana, hiyo inawasaidia kuweza kukuza mbengu ya mafanikio iliyo ndani mwao. Angalia watu wengi ambao hawaweki akiba, maisha yao sio mazuri na kufanikiwa inakuwa ni ngumu.
9. Moja ya sifa kubwa ya mafanikio unayotakiwa kuwa nayo na kuiendeleza ni TABIA zako ulizonazo. Ukiwa na tabia sahihi, uwe na uhakika zitakuongoza hadi kuweza kufikia mafanikio yako.
10. Ukishakijua vizuri kile unachokitaka kwenye maisha yako, tafuta maarifa na mbinu za kukichimba kitu hicho ndani, nje mpaka ukielewe vizuri. Kukijua vizuri kitu hicho ndani, nje itakupa wewe uwezo wa kukifanya kwa ufasaha sana na kupata matokeo chanya.
11. Nguvu ya kuendelea kufanya jambo lolote itazidi kuchochewa ndani yako kama moto, ikiwa ndani yako pia una hasira, imani ya kufanikiwa na pengine maumivu ya kuumizwa na wengine. Kama ndani yako unavitu hivyo, itachochea nguvu kubwa iliyoko ndani yako ya kufanikiwa na utafanya kila linawezekana kuhakikisha unafanikiwa.
12. Unapokuwa una hamu na hamasa ya kufikia malengo yako, ni lazima kutafuta njia na kila aina ya maarifa yatakayokusaidia kufikia malengo yako. Maarifa hayo utayapata kutoka kwa watu ambao tayari wameshafanikisha hicho unachokitaka au hata kwenye vitabu mbalimbali vya kimafanikio.
13. Ili ukijue vizuri hicho unachotaka kukifanya ni lazima uchuke hatua. Huwezi kukijua kitu hicho kwa kusoma peke yake ni muhimu kuchukua hatua zitakazo kupa uzoefu ambao uzoefu huo utapelekea wewe kujua namna ya kufanya kwa ubora wa hali ya juu.
14. Kama kuna jambo ambalo umelianzisha hata kama linakuletea utata endelea kulifanya. Ikiwa kama utasimama inachukua muda mrefu tena kulianza jambo hilo na kuwa kwenye mwendo sahihi kuliko ungeendelea na safari. Siri ya kuendelea ipo kwenye kufanya sasa hicho unachotaka kukifanya. Acha kujisemea kuwa utafanya kesho au lini, fanya sasa.
15. Siku zote mafanikio ya mtu yanaanzia kwenye akili yake. Unachotakiwa kufanya ni kuangalia fursa zinazokuzunguka au changamoto zinazoizunguka jamii yako na kisha baada ya hapo tafutia majibu yake na utafanikiwa.
.16. Maadili bora ni msingi mkubwa wa mafanikio yoyote. Kushindwa kwingi kunaanza pale mtu anapokosa maadili na kujiingiza kwenye tabia za hovyo kama ulevi, zinaa na hata wizi. Mafanikio hayajengwi kwenye misingi kama hiyo hata siku moja.
Chukua hatua kila siku kujifunza haya muhimu uliyojifunza kwenye kitabu hiki.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com

Saturday, July 22, 2017

Watu Wenye Sifa Hii…Ndiyo Wanaofanikiwa.

No comments :
Linapokuja swala la mafanikio zipo sifa na mambo mengi ambayo yanakuwa yanatajwa katika kumfikisha mtu ili aweze kufanikiwa. Mambo au sifa  hizo huwa ni za msingi sana kwa kila mtu ili kufikia mafanikio.
Hata hivyo pamoja na sifa hizo,  ipo sifa moja muhimu sana ambayo kwa mtafuta mafanikio kama unayo ni lazima utafanikiwa. Sifa hii  muhimu ya kimafanikio ambayo nataka kuiongelea hapa ni uvumilivu wako katika kuelekea mafanikio.
Unaweza ukawa unajituma kweli, una nidhamu binafsi na unafanya juhudi za kuwekeza kila wakati, lakini ukikosa uvumilivu hasa pale unapokutana na changamoto au pale unaposubiri mafanikio yako makubwa huwezi kufanikiwa.
Uvumilivu ni kitu cha muhimu sana kama umeamua kuishi maisha ya ndoto zako. Inabidi uvumilie  hali ngumu unazokutana nazo, inabidi uvumilie kuishi wakati mwingine chini ya kipato ili kutimiza malengo ya ndoto zako.
Kuna kitu najua unataka kujiuliza nitavumilia mpaka lini, mbona maisha yangu naona kama magumu, hayaeleweki na hii biashara italeta mafanikio lini? Ndio, najua yote hayo unapitia, hakuna namna zaidi ya wewe kukomaa na kukubali kuvumilia.
Sikiliza, kiuhalisia mara nyingi inachukua miaka 3 hadi 5, ili kuweza kupata mafanikio ya uhakika kwa kile ambacho umekianzisha leo. Huo sio muda mrefu sana kama unavyofikiri. Unachotakiwa kufanya ni kuwa na subira na kuweka juhudi sana kila siku.
Hebu jiulize kuna yale mambo ambayo uliyaanza miaka mitatu iliyopita, yanaonekana kama yalianza jana tu. Kama hiyo iko hivyo hata maisha yako unaweza kuyabadili. Kwa  nini usikubali kuvumulia ili kutengeneza ndoto zako za kimafanikio.
Hata kila unayemwona amefanikiwa, au kila unayemwona yupo ngazi fulani ya kimafanikio kuna mengi ambayo amepitia na kuvumulia hadi akavuna hicho alichokivuna. Kama hutaki kuwa na uvumilivu, utajiweka pembeni kwenye njia ya mafanikio wewe mwenyewe.
Huna haja ya kujiona unachelewa, hebu jipe muda wa kubadili ndoto zako. Uwe na uhakika hilo litafanikiwa na utajenga maisha ya mafanikio unayoyataka wewe. Watu wenye sifa ya kuvumilia magumu mengi na kuweka juhudi hao ndio wanaofanikiwa.
Hakuna hata siku moja mtu ambaye akipata hasara kidogo anaacha biashara eti akafanikiwa, mtu hayupo. Uvumilvu wako ni muhimu sana katika safari ya mafanikio uliyoichagua. Ukiona huna uvumilivu wa kutosha, SAHAU MAFANIKIO.
Tunakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kwa ajili ya kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com