Dec 23, 2014
Linalokuhuzunisha Si Tatizo Kubwa Sana, Unajitesa Bure.
Nafahamu kwamba katika
maisha ya kila siku hayakosekani mambo ya kuumiza. Sina shaka kuugua, kufiwa,
kukosa chakula, kusalitiwa katika mapenzi, kudhurumiwa, kufilisika, kutotimiza
malengo tuliyojiwekea na pengine kufutwa kazi ni mambo ambayo huzaa huzuni na
machozi miongoni mwa watu wengi. Lakini jambo la kujiuliza ni kwamba tunalia au
kuhuzunika kwa sababu matatizo yetu ni makubwa au ni kwa sababu yametuumiza
sana na tumejikuta tukiwa ni watu ambao hatujui nini cha kufanya?
Hebu tujiulize ni
wangapi tunahuzunikia mishahara midogo tunayolipwa makazini mwetu? Je katika huzuni
hizo tulishawahi kuwaza kwamba kuna binadamu wengine hawana kazi na
wanahangaika kutafuta shilingi mia tano kwa kuuza mihogo na karanga kwenye kona
za mitaa huku wakiwa juani?. Kama hao wapo ukubwa wa tatizo la mshahara kidogo
unaotuliza kila siku uko wapi? Uko wapi ukubwa wa tatizo la kutokuzaa wakati
kuna waliozaa na watoto wote wakafa.
Kimsingi uwiano wa
shida na uhimili wake unaopatikana baina ya mtu na mtu, kamwe sifa ya huzuni
hailetwi na ukubwa wa tatizo, isipokuwa ni kukosekana kwa sanaa ya kuishi,
yenye maono na hisia za kupunguza mambo makubwa kuwa madogo. Katika hisia,
mwanadamu hawezi kuzuia machozi ya furaha au huzuni yasitoke, ni kitu ambacho
hakiwezekani kabisa. Ifahamike kwamba kila mwanadamu ana uwezo wake wa kufanya,
zaidi ya tatizo analokutana nalo.
Bila shaka umewahi
kuona au kuwasikia watu wanalia kila siku kwa kuhitaji utajiri, lakini
hawafikii malengo kwa sababu wanaona umasikini ni jambo kubwa na kuufikia
utajiri ni jambo kubwa pia. Kitakachotokea hapo kama mambo yote ni magumu ni
huzuni ndani mwao. Unaweza pia ukajiuliza mwenyewe ni kitu gani kinakuliza?
Fahamu kwamba hulii au kuhuzunika kwa sababu matatizo ni makubwa, bali umekosa
ufahamu wa maono.
Hebu chukua jukumu la
kudharau shida zako kwa kujilinganisha na wengine ambao ambao wana matatizo
makubwa kuliko yako. Fanya hivyo kila unapokabiliwa na tatizo, usilione tatizo
ni kubwa kwa takwimu, lichukulie kuwa ni dogo kisha uanze kulishughulikia,
utaona linamalizika kwa ushindi mkubwa. Kamwe usijaribu kulitatua kwa kulikuza
sana, hutapata matokeo mazuri. Kuwa na mtizamo chanya kwenye tatizo lako,
itakusaidia kukabiliana nalo vizuri.
Ya nini ulie na
kuhuzunika kila siku? Ukiwa ni umasikini, kutokuzaa, kukosa kazi, kuteswa na
mume na matatizo yote yatakayokukuta katika maisha yako yaone ni madogo kisha
tumia nguvu zako zote kuyakabili nina hakika utayashinda kirahisi. Jaribu
kupunguza matatizo, badala ya kuyakuza kwa kuona hayawezekani kutatuliwa,
utaona majibu yake. Tambua kuwa tatizo lako si kubwa bali unalikuza katika
mawazo yako, kwa kuwa wapo wenye matatizo makubwa zaidi yako na hawalii kama
wewe.
Ili uweze kuwa mshindi
na usihuzunike tena kumbuka hili siku zote ‘nyakati
ngumu katika maisha hazitaisha, ni jukumu lako kukabiliana nazo tu.’
Jiulize tena mwenyewe, kama ni kulia utalia kwa mangapi? Dunia haina usawa,
jifunze kuyakabili matatizo yako kwa mtazamo chanya hapo utakuwa mshindi. Acha
kuwa na huzuni na simanzi kupitiliza linalokuhuzunisha siyo tatizo kubwa sana.
Wapo watu ambao walishashavuka tatizo kama lako jifunze kwao, kisha songa
mbele.
Nakutakia maisha mema
yawe na amani na furaha, ansante kwa kutembelea DIRA YA MAFANIKIO endelea kujifunza
na kuhamasika zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 0345/dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.