Jul 7, 2020
Hii Ndiyo Silaha Kubwa Ya Mjasiriamali Katika Kufikia Mafanikio Makubwa.
Wahenga walisema:
“Maisha ni kuona mbele.” Huu ni usemi unaompa mjasiriamali matumaini ya kusonga
mbele pasipo kutumia muda mwingi kuwaza yale aliyokwishafanya.
Katika maisha ya kila
siku kwenye ujasiriamali, wajasiriamali wanakumbana na changamoto nyingi.
Changamoto hizi wakati mwingine huwasaidia kuona mbele na hatimaye kuwa watu
wenye mafanikio.
Kwa mfano, kama mtu
anajishughulisha na ujasiriamali halafu akawa anasumbuliwa na mamlaka
zinazohusika na urasimishaji wa biashara kwa sababu za kutorasimisha shughuli
zake, akiamua kurasimisha biashara yake atafanya shughuli zake bila
kubughudhiwa.
Mwisho wa siku atakua
kibiashara, hivyo kuchangia maendeleo ya nchi yake kwa kulipa kodi na kuajiri
watu. Kwa mjasiriamali wa aina hii hatakuwa na muda tena wa kuanza kuwaza yale
yaliyotokea bali atakuwa anaiona dunia yenye matumaini kesho yake.
Atakuwa anafikiria
zaidi juu ya siku za baadaye. Atakuwa na malengo ya kuhakikisha anaibadili
dunia na wala siyo kusubiri dunia imbadilishe. Ni kwa sababu, akisubiri dunia
imbadili, atakuwa miongoni mwa watu wanaosubiri kutupwa kwenye shimo la sahau.
Hii ina maana kuwa,
mjasiriamali hatakiwi kukumbuka changamoto za jana kwa lengo la kumpa huzuni na
machungu yatakayomsababisha ashindwe kupiga hatua. Bali anatakiwa kuchukulia
changamoto hizo kama somo, ambalo litamwezesha kufika anakoelekea pasipo kurudi
katika hali yake ya jana, ambayo siyo taswira nzuri katika kichwa chake.
Kama nilivyowahi
kusema katika makala zangu za mwaka jana, mwanzo ni mgumu. Leo narudia tena
kusema kuwa mwanzo ni mgumu. Mwanzo wa shughuli za ujasiriamali, wakati
mwingine utaona kama hakuna anayekujali.
Unaweza kuhangaika
siku nzima na hata zaidi ya miezi kadhaa pasipo kupata kile ulichokusudia. Wakati
mwingine unaweza kuwa unatafuta msaada fulani ili kukamilisha kile
ulichokianzisha ukaambulia patupu! Unaweza kuchekwa na baadhi ya watu, wakiwamo
wale uliowategemea kuwa wangekuunga mkono. Pia, unaweza kukutana na upinzani
mkubwa kutoka kwa wajasiriamali wenzako, hata kwa wivu wake kana kwamba
unapigana vita.
Hata hivyo, ukiamua
kuona mbele utavuka vikwazo hivi vyote na kupata kile ulichokusudia. Kuona
mbele ni pamoja na kuwa na dira au mweleko wa wapi unataka kuwa. Mjasiriamali
mwenye dira huwa hakati tamaa na haogopi vita kutoka kwa wenzake au kwa baadhi
ya watu. Ni mtu mwenye kuangalia ni njia zipi azitumie kufika pale anapotaka
kufika.
Ikumbukwe kuwa
ushindi huja kwa mtu mwenye kupambana kwa malengo ya kuiona kesho yenye nuru ya
mafanikio.
Ushindi hupatikana na
kujifunza kila hatua na njia anayoipita mjasiriamali ili kufika kwa mafanikio
pale anapopata. Ili kufanikisha hili, mbali ya kuwa na maono, mjasiriamali
anatakiwa kuwa mvumilivu na mwenye kuthubutu.
Uvumilivu na uthubutu
ni miongoni mwa vitu muhimu sana kwa mjasiriamali. Ni vitu vinavyochangia suala
zima la utekelezaji wa dira ya mjasiriamali, ambayo siku zote huwa ni kuona
mbele. Kwa hiyo utakuja kutambua kuwa uvumilivu na uthubutu ndiyo silaha ya
mjasiriamali kufikia kwenye mafanikio.
Watu wengi
wameshindwa kufika popote kwa sababu ya kukosa uthubutu na uvumilivu wa kufanya
yale wanayofikiria.
Kwa mjasiriamali
anayethubutu na kuvumilia, ataiona kesho yake yenye neema na ambayo
itamfaidisha yeye, jamii yake na Taifa kwa ujumla kwani mwendapole hajikwai,
akijikwaa hataanguka wala kushindwa kuendelea na safari yake.
Makala hii imeandikwa na Chiraka Muhura
wa Gazeti la Mwanachi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Asante kwa somo zuri
ReplyDelete