Oct 17, 2018
Hivi Ndivyo Jinsi Unavyopanga Kuwa Maskini.
Katika hali ya kawaida,
kila binadamu anaishi kwa kupanga vitu vya kufanya. Katika zoezi zima la mpango,
kuna makundi mawili ya watu. Kundi la kwanza ni watu waliopanga kutokuwa na
mpango wowote wa maisha yao na kundi la pili ni watu waliopanga
kuwa na mpango wa maisha yao.
Kundi la watu waliopanga
kutokuwa na mpango, maisha yao yanategemea zaidi imani na matumaini. Kwa
kawaida watu hawa wanaamini mambo yote yanapangwa na Mungu, na kwa hiyo, wao ni
kufanya yale tu yanayowajia vichwani mwao kila waamkapo asubuhi.
Imekuwa ni kitu cha
kawaida kusikia wengi wa kundi hili wakinena “Hata ufanyeje, Mungu kama
hajapanga unajisumbua bure! huwezi kufanikiwa”. Kauli za namna hii ni za
kukata tamaa ya maisha na pia yule anayeambiwa anakatishwa tamaa pia—anza kukaa
mbali na wenye kutoa kauli hizi ni hatari kwa mafanikio yako.
Tabia hii ya kutokupanga
aina ya matokeo unayoyataka ndiyo inayopelekea watu kuishi maisha ya kufuata
upepo kama siyo mkumbo. Pia ni tabia hii inayowafanya watu kuwa na mipango ya
muda mfupi na kupenda matokeo ya haraka.
Kwanini
tunasema ni lazima kuwa na mpango? Kwasababu
kuna vitu vikubwa viwili ambavyo vina nguvu sana katika maisha yako; navyo ni
MUDA na MABADILIKO. Muda una nguvu kwasababu, utake usitake lazima muda uende
na mabadiliko ni hivyo hivyo, lazima yaje utake usitake .
Njia pekee ya kuweza kuwa
na mamlaka juu ya muda na mabadiliko ni wewe kuwa na mpango. Binadamu wote
tumepewa uwezo wa kuweza kupanga nini cha kufanya hata kama hakijatokea.
Tofauti na wanyama
wengine, wao huweza kuishi kwa kufuata matukio au hali ya wakati huo. Wanyama
hawana kabisa mpango unaoweza kuwaongoza kwenda kwenye mwelekeo wa maisha
wanayoyataka.
Ikitokea malisho yameisha
wao uhamia sehemu nyingine na hiyo sehemu nyingine wakikuta wanyama
wanaowawinda watarudi huko ambako walihama mwanzoni.
Ajabu na kweli ni kwamba
watu wengi wanaishi kwa kufuata mabadiliko yanayojitokeza kwenye mazingira yao.
Kikubwa hapa ni wewe kubadilika na siyo kubadilishwa na mabadiliko. Ukisubili
kubadilishwa na mabadiliko maana yake mabadiliko yatakubadilisha jinsi
yanavyotaka.
Yawezekana wewe unajiona
uko sawa na mambo yako yanaenda vizuri, lakini ujue kuwa ukiwa na maisha ambayo
huna mpango ulio katika maadishi, hapo ujue kuwa lazima ufuate kile ambacho
mabadiliko yatakuletea na siyo wewe unavyotaka mabadiliko yawe. Ndiyo maana
tunaambiwa kwamba ufunguo pekee wa mtu kuweza kudhibiti MUDA na MABADILIKO ni
kuandika “mpango”.
Mpango
maana yake ni kwamba wewe mwenyewe unapanga aina ya mafanikio unayoyataka
kabla ya kuanza kuyatafuta. Mafanikio yoyote makubwa lazima upange kuyapata.
Kwahiyo, tuseme kuwa mafanikio yako yapo tayari, kinachosubiliwa sasa hivi ni
mpango kazi wako. Kama umepanga kutokuwa na mpango—tambua kuwa “Usipopanga
kupata mafanikio, basi ujue unapanga kimya kimya kuwa masikini”.
Mpango
ndio unakupa mwelekeo mzuri wa unakotakiwa kwenda. Kama wewe ndiye
unayeshika upinde na mshale basi “Mpango” ndio unasaidia kuelekeza wapi mshale
uende—wewe unachagua upande gani mshale upige. Athari za kutokuwa na mpango
ambao unatuongoza juu ya nini cha kufanya ni pale tunapojikuta tunadhibitiwa na
maisha badala ya sisi kuyadhibiti maisha.
Mpango
unakupa nguvu na uwezo wa kuuamrisha muda ukufanyie nini. Ikiwa
umepanga kutokuwa na mpango, basi ujue muda ndio utakupangia nini cha kufanya.
Inafika kipindi fulani muda wenyewe unakulazimisha kufanya vitu ambavyo hupendi
kuvifanya. Ulikuwa na nafasi ya kuamrisha muda, lakini hukuitumia, sasa ni zamu
ya muda wenyewe kukuamrisha cha kufanya.
Ukiwa huna mpango unakuwa
ni mtu wa kuishi kwa matumaini. Lakini kumbuka kuwa watu wengi wanaoishi kwa
matumaini mara nyingi ni maskini. Kwahiyo, unahitaji mpango ambao ndio
utakujengea imani ya kufanikiwa.
“Imani ni bora zaidi
kuliko matumaini” jitahidi kuwa na imani juu ya mpango wako,
huku ukizidi kuutekeleza kwa nguvu zako zote—hakika mafanikio uliyolenga kupata
lazima yatokee tu!
Habari njema ni kwamba
Mungu yupo anasubiri mpango wako ili aubariki. Mafanikio yako makubwa yapo,
lakini utayapata tu endapo utaandika leo mpango wako. Ukishindwa kupanga
unapanga kuwa maskini—habari ndio hiyo!.
Kuendelea kupata maarifa
mengi jiunge na kundi la Whats app kwa
ajili ya kujifunza zaidi. Kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S kwenda 0713 04 80 35 ili kuunganishwa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.