Feb 20, 2015
Haya Ndiyo Maradhi Ya Utajiri Wa Ghafla. Soma Hapa Kujua Zaidi.
Siku hizi mazungumzo yanayohusu pesa, mali na utajiri kwa ujumla, yamekuwa ni jambo la msingi linalopewa kipaumbele na kila mtu katika jamii yetu. Ingawa, tamaa ya kutaka kujitajirisha kwa vyovyote vile, imejengeka na kujizatiti ndani ya mioyo ya watu kiasi cha kutufanya kuwa kama watumwa vile. Mwelekeo huu wa kupenda na kutamani sana utajiri, umewafanya baadhi ya watu wavuke mipaka ya maadili mema na kuutafuta utajiri huo kwa njia za mkato, zisizo halali.
Nakumbuka kuna jamaa yangu
mmoja kipindi cha nyuma kidogo, baada ya kumaliza shahada yake ya kwanza ya
biashara katika chuo kimojawapo hapa nchini, aliweza kubahatika kuajiriwa na
serikali katika idara moja iliyokuwa ikijihusisha na maduhuri ya serikali
kutoka kwa wafanyabishara wadogo na hata kwa wale wakubwa. Katika muda wa miaka
tu tokea aajiriwe, jamaa huyu aliweza kujitajirisha kwa kiwango kikubwa na cha kutisha sana.
Njia alizotumia katika
kujitajirisha kwake bado inabaki kuwa siri yake. Lakini kwawatu wenye kujua
kiwango chake cha mshahara na muda aliofanya kazi, hawakusita kusema kwamba,
utajiri huo ulipatikana kwa njia za mkato mkato, ikiwa ni pamoja na kuibia
serikali. Mara baada ya kuona kwamba ametajirika kiasi cha kuogofya, akawa sasa
hata mwenyewe anaonekana kutokuamini, kutokana na wingi wa pesa alizokuwa nazo.
Hivyo kutokana na hali hiyo, alianza kushitakiwa na dhamira yake.
Matokeo yake ni kwamba ,
alianza kuingiwa na hofu ya kuja kukamatwa na mwajiri wake. Hali hiyo iliendelea
kumsumbua kwa muda mrefu. Katika hali kama hii aliendelea kusumbuliwa na
maumivu makubwa ya kiakili na kihisia. Hivyo, ikawa kwamba, katika harakati za
jamaa huyu kuondokana na maumivu hayo, aliamua kutafuta mwavuli wa kumpa nafuu.
Ilibidi aanze ufujaji wa pesa hizo kwa kulewa kupita kiasi na ngono za hovyo.
Ilifika hatua ambapo jamaa
huyu akawa anashindana na mkewe katika kuzichota fedha hizo kutoka sehemu
walikokuwa wakizihifadhi ndani ya nyumba yao. Migogoro ya ugomvi kwenye ndoa
yake likawa ni jambo la kawaida. Vilevile jamaa huyu akawa anawaalika jamaa
zake aliomaliza nao masomo ya chuo kikuu, wakanywa na kufurahia maisha.
Alifanya hivyo, bila yeye
mwenyewe kujua kwamba, ilikuwa ni jitihada yake ya kutibu majeraha ya hisia
zake, kutokana na kushtakiwa na dhamira zake, kwa vitendo vyake vya ubadhirifu, rushwa na wizi wa
fedhaza ofisi yake. Hata hivyo, tiba hiyo haikufua dafu kwani hatimaye jamaa
huyu aliamua kuacha kazi yeye mwenyewe kwa hofu ya kudakwa na mwajiri wake.
Wataalamu wengi wa afya ya akili
wanadai kwamba mtu anapopata utajiri wa ghafla huwa ni ngumu sana kwake kuweza
kukabiliana nao huo utajiri wa ghafla. Wataalamu huweza kuongeza kuwa utajiri
huo huweza kusababisha familia kuvunjika na kuharibu kabisa maisha yao. Na
kwamba fedha hizo, zinakuwa haziwaletei tena amani, uraha na hata kuridhika
kama walivyokuwa wakifikiri mwanzo.
Vilevile kulingana na maoni
ya wataalamu mbalimbali wa masuala yahusuyo afya ya akili, wanaendelea kudai
kuwa watu wengi ambao hupata utajiri huu wa ghafla na wa kupindukia mara nyingi
huwa ni watu wa kuugua maradhi ambayo yamepewa jina la maradhi ya utajiri wa
ghafla, ambayo huwa yana dalili kama hizi:-
Kushtuka moyo sana, hofu za
ghafla na ya mara kwa mara, kukosa usingizi, kukosa amani na kuhisi kuwa na
hatia kwa sababu ya kuwa na pesa nyingi kupindukia ambazo tena ukiangalia sio
za halali. Pia, kuhisi kwamba hawastahili kuwa na pesa au utajiri mkubwa wa
kiasi hicho. Watu wengi wenye utajiri mkubwa na wa ghafla ndivyo walivyo na
wanaishi na maradhi ya utajiri wa ghafla, ingawa sio rahisi sana kubaini na
hawawezi pia kukwambia.
Hivyo, ni vizuri tukawa na
mtazamo chanya na unaofaa kuelekea kwenye utajiri tunaoutaka na kuumiliki baada ya kufanya kazi halali
tena pengine muda mrefu, ni sehemu tu ya jitihada za kujipatia mafanikio ya
kweli. Kwani mafanikio haya yanatutaka tuutumie utajiri huo vizuri. Kutumia
utajiri huo vizuri ni pamoja na kuutumia katika kuwatendea mema watu wengine,
kuutumia katika kazi na miradi mbalimbali ya kijamii.
Kwa kufanya hivyo, ni wazi
kabisa tutakuwa tumeigundua na kuipata siri au tiba itakayoweza kutusaidia
katika kuepukana na mashtaka hata hukumu itokanayo na utajiri wa haraka haraka.
Nakutakia kila la kheri,
endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kupata maarifa bora yatakayobadili maisha
yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com
- dirayamafanikio.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.