Feb 9, 2015
Maisha Ni Vitendo Na Si Ndoto Pekee, Ndoto Ni Mwanzo Tu Wa Maisha…
Kwa kawaida, binadamu ana mambo matatu muhimu ambayo anaweza
kuyaendesha au yakamwendesha kichwani kwake, moja ni fikra zake au mtazamo (thoughts
you think), mbili ni taswira anazozijenga kichwani kwake (image you visualize)
na tatu ni vitendo vyake (the actions you take). Sisi binadamu tunawajibu
wakuhakikisha tunaleta maendeleo katika maeneo tunayoishi kwa juhudi zetu
binafsi. Ni kweli tumesikia na kujifunza mengi katika dunia lakini maana ya
maisha iliyo halisi na ya kweli ya mwanadamu mhusika hutoka ndani ya binadamu
mwenyewe.
Kila mwanadamu anao ukweli wa maisha yake ndani yake. Mambo yote
tunayoyaona duniani, ugunduzi, vitabu, miziki, filamu na kila kitu kilichopo
duniani kilichosababishwa na mwanadamu asili yake ni ndani ya binadamu na si
nje. Ndani yako mwanadamu kuna maajabu, ndani yako kuna hazina ya maisha,
vipaji, talanta na habari njema ya maisha yako. Kutokana na upekee ulionao
duniani, huna mshindani, mshindani wako ni wewe mwenyewe. Historia ya dunia
inaonyesha kuwa wanadamu walio wengi duniani wanafichwa mambo ya ukweli na
makubwa kuhusu uwezo wao.
Toka enzi za wajasiriamali tunaowasoma katika historia akina
Adam Smith, kipindi cha viwanda na utumwa wanadamu wengi, waliishi chini ya
viwango kwa kutumika kama mashine zinazoweza kubadilishwa wakati wowote, hii
imekuwa sababu kubwa ya binadamu wengi kutokujua ukweli wa vipawa ndani yao na
hata kutojiamini kabisa. Vilevile Kutokana na mabadiliko ya maisha, karne hii
ya 21 inatabiriwa kuwa karne ya vipawa na maajabu ya ndani ya mwanadamu kwani
imedhihirishwa na baadhi ya watu wa kawaida sana ambao wameweza kugundua mambo
mengi kwa kutumia vipawa vyao.
Tunaishi katika dunia ambayo ni rahisi kubebwa na misukumo ya
nje na wengi hawaamini ukweli huu kuwa kila mtu ana kipaji, kila mtu ana habari
njema ya ndani yake hii ni kwasababu wengi wameshawishiwa na mifumo ya dunia na
maisha ya wanadamu wengine na kujikuta kuwa wanaishi si kama wao bali kama
nakala. Watu wote wenye mafanikio duniani, ambao huonekana kana kwamba
wamebarikiwa hutafuta maana ya wao kuwa wao, uwezo wao wa kipekee na kutumia
upekee walionao na kuishi maisha yao kimafanikio watakavyo wao.
Dunia hii inayo nafasi kwa mwanadamu ambaye anatafuta maana ya
maisha yake mwenyewe, haijalishi umezaliwa katika familia ya aina gani bali
ukikubali ukweli kuwa unayo hazina ya maisha ndani yako basi maisha yako
yatapata maana. Unacho kipaji ndani yako. Hakuna mwanadamu ambaye hakuumbwa na
kitu ndani yake, Mungu hakuumba takataka duniani, Mungu aliumba mwanadamu
mwenye hazina ndani yake. Kila mwanadamu anao uwezo wa kipekee na kiasili
aliojaliwa na Mungu ambao bila yeye hakuna ukamilifu. Uliletwa duniani ili
ukamilishe upekee wako. Wewe ni ukamilifu wa dunia, kuishi kama nakala haina
tofauti na kuishi kama marehemu anayetembea.
Unaweza usiwe na uwezo kuanzisha biashara ya mgahawa au ya
daladala lakini ukawa na uwezo wa kuimba na kutunga nyimbo za kila aina hivyo
ukawa mjasiriamali katika kanda ya mziki
iwapo una uwezo wa kuchekesha basi fanya ujasiriamali katika kipengele cha
ucheshi kama jamaa wa futuhi. Wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia
icheke, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia icheze,wapo walioletwa
duniani ili kuifanya dunia itembee, wapo
walioletwa duniani ili kuifanya dunia ifikiri, wapo walioletwa duniani ili
kuifanya dunia isikilize radio,TVs na muziki, wapo walioletwa duniani ili
kuifanya dunia ing'are na mengine mengi unayoyajua na ambayo mpaka sasa
hatujayajua bado lakini yamo ndani yako. Aidha wapo walioletwa duniani ili kuifanya
dunia iwe na mitandao tunayoiona sasa hivi.
Dunia hii inakuhitaji wewe kama wewe, na mafanikio yako duniani
yanakutegemea wewe kama wewe. Hata kama usipokubali ukweli wa uwezo wako wa
ndani, haitaondoa maana ya ukweli ulio ndani yako. Kumbuka kuwa utamu wa maisha
duniani ni matumizi ya kipaji chako na kusikiliza sauti ya ndani.Ulipewa vipaji
ili uvitumie duniani katika biashara,kazi,sanaa,uongozi,ujuzi,masomo na
mengine. Bila kujionea aibu mwenyewe, na kujitafuta na kujiuliza kasoro zako
ulizonazo na jinsi ya kuzizuia au kuzipunguza, tafuta kujua mazuri ya kwako
huku ukitafuta kuongeza mengine.
Ukiona Kama kuna kitu kinakufurahisha duniani, usiogope
kujaribu, jaribu, jaribu tena ipo siku utagundua wewe ni mzuri wapi. Sikiliza
sauti za dunia lakini sikiliza sana sana sauti yako ya ndani kwani ndiko
kutokako chemchem ya uhai wa maisha yako. Jifunze kujiuliza, wewe ni nani?
Umetoka wapi? Una nini cha kujivunia duniani? Unataka dunia ikukumbuke vipi? Je
uko tayari kuja duniani kama moshi na kuondoka kama moshi, usikumbukwe? Nini
unaweza zaidi ya mwingine? Ni nini madhumuni yako duniani?
Kumbuka kuwa wewe ndiye mkurugenzi mtendaji wa maisha yako,
mazingira, mifumo, familia na vikwazo vyovyote duniani visiwe sababu ya
kuutuliza utu wako. Unazo nguvu zaidi ya nguvu zilizo nje yako za kuwa
unavyotaka, kulingana na jinsi ulivyojaliwa. Vipo vitu vinavyoweza kukuzuia
hata kukumaliza lakini ni uamuzi wako kusimama kidete kwaajili ya maisha yako
na kuonyesha nguvu zilizo ndani yako au kukubali kumalizwa bila ubishi wowote. Vipo
vitu vingi vinavyoweza kukuchanganya. Lakini ni uamuzi wako kukubali
kuchanganywa na kuishi maisha ya bora liende au ili mradi kumekucha mpaka
unakufa bila maana au kuamua maisha yako na kusema ama zangu ama zao nitakuwa
vile ninavyotaka maishani.
Kumbuka kuwa dunia haina huruma kwa mwanadamu aliyekubali
kumalizwa, vumilia, jiamini, Jipende, jiendeleze, jikaze, jionyeshe, jitafute
mwenyewe, jikubali na mwisho wa siku dunia itakukubali tu hata kama kuwe na
nguvu zozote mbele yako. Kumbuka kuwa dunia hii itaendelea kuendeshwa na hata
kutengenezwa na binadamu wenye uelewa mpana wa nguvu iliyo ndani yao na si
wababaishaji na wenye maisha ya maridadi.Wanadamu wote walioweza kufanikiwa.
Kuna wakati tumekuwa tukilaumu watu wasiohusika katika maisha
yetu magumu, kuwa wanaharakati wa mambo yasiyotuhusu, kutoa maoni yasiyo na
maoni na kuchambua timu za ulaya na kuelezea mchezaji fulani analipwa kiasi
gani cha mshahara. Ni lini umewahi kaa nyumbani kwako au kwenu na ukatumia muda
wako kuchambua vipaji vyako? Ambavyo ungevitumia katika maisha yako na jamii
inayokuzunguka?Kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale ambao
wametambua sababu ya wao kuwa wao, wanajijua ni nini wanakitaka na wanajua kuwa
ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe.
Maisha ya mafanikio duniani ni haki ya kila mwanadamu. Hakuna
binadamu aliyeletwa duniani kuja kushuhudia wengine wakifanikiwa huku yeye
akiwa katika umaskini siku zote. Kila mwanadamu mwenye pumzi anayo haki,
nafasi, uwezo na uchaguzi wa kuwa anavyotaka kulingana na maana ya mafanikio
atakayotengeneza na mwenyewe. Ni kweli tunaishi katika dunia yenye utofauti
kimafanikio wapo wenye mafanikio makubwa, wapo maskini na wale wenye maisha ya
kawaida. Lakini kwa pamoja yatupasa tufahamu kuwa, kila mwanadamu anao uwezo wa
kufanikiwa. Na zaidi ni kuwa kila mtu anao uchaguzi wa kuamua maisha yake,
lakini angalizo ni kuwa mtu yeyote aliyeweza kufanikiwa ametambua kuwa , kuna
vichangizi vya mafanikio / success ingredients.
Unachopaswa kutambua ni kuwa, hali ya maisha uliyonayo sasa si
kipimo cha mafanikio yako ya baadaye, unaweza kuwa vyovyote kimafanikio
kulingana na utakavyochagua mwenyewe. Ni muhimu kuyajua maisha Kwa kujua vipaji
na vichagizi hivyo ni kama vifuatavyo: Mwanadamu anayejua dhumuni lake duniani
huishi maisha ya maana. Hatukuja duniani kuwepo tu bali kuishi kimafanikio huku
tukijua kwanini tunaishi. Ukijua ni kwanini unaishi hutakubali kuishi
kiholelaholela huku ukisubiri muda wako wa kuishi duniani kuisha.
Dhumuni la wewe kuwepo duniani ni kuishi maisha yenye madhumuni,
maisha yenye mafanikio na maisha yanayonufaisha wengine. Wanadamu wote
walioweza kufanikiwa kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale
ambao wametambua sababu ya wao kuwa wao, wananjua ni nini wanakitaka na wanajua
kuwa ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe katika hilo. Ukitaka
kutengeneza maisha yenye mafanikio duniani, tafuta kujua dhumuni lako hapa
duniani.
Wanadamu wote waliofanikiwa duniani waliamini kuwa wanaweza
kuibadili dunia. Mwanadamu anayeyarudisha maisha yako nyuma ni wewe mwenyewe,
ukitaka kufanikiwa katika lolote utakalochagua jiamini na amini kuwa unaweza.
Hakuna kitu chochote kilichowahi kutokea duniani bila kujiamini. Kila mwanadamu
anayo zawadi ndani yake, zawadi hii huja kama kitu anachokipenda na kukiweza.
Ndani ya mwanadamu vipo vipawa na uwezo wa ajabu wa kuishi maisha ya mafanikio.
Kila mtu ana kitu anachopenda, kinachoweza kutumika na kuendelezwa na kuleta
mafanikio.
Dunia ya sasa ni dunia ya wanadamu wanaojua ni kitu gani
wanaweza. Wapo wanaopenda kuwa madaktari, wapo wanaopenda kuwa waimbaji nk.
Kila mtu ana kitu anachopenda kinachomfanya acheke akiwa duniani. Tafuta kitu
unachokipenda na kiendeleze, kitakuletea mafanikio. Maisha ni vitendo na si
ndoto pekee, ndoto ni mwanzo tu wa maisha. Maisha ni kuchukua hatua na si
kufikiri pekee. Maisha ya kijasiriamali ni kusonga mbele na si kupanga peke
yake. Katika yote uliyochagua maishani kuwa mtendaji, usikubali kuyaishi maneno
ishi matendo.
Maisha bila maarifa ni sawa na gari lisilo na mafuta. Ukitaka
kutembea na kuishi kimafanikio kuwa na njaa ya maarifa kila siku. Binadamu wote
wenye mafanikio duniani hawachoki kutafuta maarifa kwa kusoma vitabu, kuuliza
na kujifunaza, na hata kuhudhuria mafunzo ya kuwaendeleza mara kwa mara. Maisha
bila maarifa hayatembei. Maisha yana mengi, muda mwingine yale tunayapanga
hayaji kama tulivyopanga lakini yote hutokea kwasababu.
Mambo yote tunayapitia katika maisha huwa ni hatua ya ukuaji
kimaisha. Ukiona biashara yako inafanya vizuri tambua kuwa ni kweli biashara
yako inakua, lakini ukiona biashara yako inafanya vibaya tambua kuwa uwezo wako
unakua zaidi. Nahitimisha kwa kusema kila mtu ana uwezo wa kuchagua kuwa
mjasiriamali wa kipekee na yale ayatakayo maishani, Dunia ina mengi ya
kuyafanya na kuna kila nafasi kwa mwanadamu yeyote anayechagua kuwa anavyotaka
maishani. Chagua maisha unayotaka kuyaishi na uyaishi kweli.
Usiogope kujaribu kitu, maisha ya kuogopa kufanya kitu ni maisha
yasiyo na maana. Usikubali maisha ya ukawaida na yenye usalama ambayo
yatakufanya usiishi maisha makubwa unayostahili. Siri kubwa ya watu wenye
mafanikio duniani, ni kuwa hawaogopi maisha, wapo tayari kuumia kwa kuchagua
maisha wayatakayo. Chagua kipengele mojawapo cha kijasiriamali unachotaka
kukifanya na ukifanye kweli kwa moyo wote. Jiendeleze kila siku katika
ulilochagua kiasi ambacho utavunja mipaka na kuweka rekodi yako. Chagua
kufanikiwa.
·
MAKALA
HII IMEANDIKWA NA MESHACK MAGANGA – IRINGA
·
MASALIANO
- 0713486636
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.