Feb 27, 2015
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutumia Muda Wako Vizuri Na Kukuletea Mafanikio Makubwa.
Muda ni mali! Huu
ni usemi maarufu sana kwa vijana na wazee. Unaonekana ni usemi wa kawaida na
uliozoeleka kwa watu wengi, maskini na matajiri, wanawake na wanaume. Japokuwa watu
wengi tunautumia usemi huu, lakini baadhi yetu hatuelewi maana yake na wengi
wetu hatuutumii katika maisha yetu.
Muda ni mali
maana yake kila kitu, vitu vyote vinavyoonekana vidogo na vikubwa ni matokeo ya
matumizi ya muda. Hata mimi na wewe ni matokeo ya matumizi mazuri ya muda. Kila
mafanikio yaliyowahi kutokea na yanayoendelea kutokea ni matokeo ya matumizi
mazuri ya muda. Kwa hiyo kuna uhusiano mkubwa sana kati ya mafanikio na
matumizi ya muda,yaani muda ukitumika vizuri mafanikio yanapatikana na muda huo
huo usipotumika vizuri hakuna mafanikio.
Hakuna haja ya
kueleza na kufafanua maana ya muda, ila nataka ujue kuwa kuna aina za muda, ndiyo
zipo aina mbili za muda. Aina ya kwanza ya muda ni MUDA WA SAA. Muda huu
unaanzia sekunde hadi mwaka. Katika muda wa saa, tunaposema miaka miwili ni
miaka miwili, haizidi wala haipungui.Tunaposema huyu ana miaka hamsini ina
maana mtu ameishi vipindi hamsini ambapo kila kipindi kina jumla ya miezi kumi
na mbili, haizidi wala haipungui.
Aina ya aili ya
muda ni MUDA HALISI. Muda halisi unaundwa na muda wa saa na matukio. Katika
aina hii ya muda tunaangalia matukio yaliyotokea katika muda wa saa
husika.Tunalinganisha idadi ya miaka na miezi na matukio au mafanikio
yaliyopatikana katika kipindi husika. Watu wanaweza kuwa sawa katika muda wa
saa lakini wakawa tofauti katika muda halisi. Mtu anaweza kuwa na umri wa miaka
sitini(katika muda wa saa) lakini akawa kwa mafanikio ni kama mtu aliyeishi
miaka thelathini tu.
Na pia mtu
mwingine anaweza kuwa na umri wa miaka thelathini, lakini akawa na mafanikio
makubwa sana kimaisha kama mtu aliyeishi miaka mingi sana duniani, yawezekana
hata miaka sabini. Usichanganyikiwe, nalinganisha muda wa saa na mafanikio. Muda
halisi unatuambia kwamba kuna kuchelewa katika maisha. Muda halisi
unatukumbusha kuwa kuna wakati tunaweza kupoteza miaka yetu bila kujua. Unatukumbusha
kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi.
Tumejifunza aina za muda na tofauti
zake, sasa tuangalie matumizi ya muda wa
saa.Tunatumia muda huu kufanya mambo
matatu ambayo yanatuleta kwenye muda halisi, tukiwa tumewahi au
tumechelewa tunatumia muda katika kufikiri, kusema au kuzungumza na kufanya
mambo mbalimbali katika maisha yetu.
Baada ya
kuangalia matumizi ya muda wa saa, tumegundua kuwa tunautumia muda kama chombo
kutusafirisha kutoka katika ulimwengu wa namba na mahesabu kwenda kwenye
ulimwengu wa halisi,ulimwengu wa vitendo ambapo tunaweza kufanya tathmini na
kuona kuwa tumewahi au tumechelewa, tuko nyuma au tuko
mahali sahihi.
Sasa tuangalie
mambo ya kufanya ili tuweze kuutumia muda wa saa na kufikia mafanikio ambayo yataweka
uwiano sawa kati ya muda wa saa na muda halisi katika maisha yetu.Yapo mambo
mengi ambayo unapaswa kuyafanya ili uweze kutumia muda wako vizuri, baadhi ya mambo hayo ni haya yafuatayo:-
1. Weka kumbukumbu ya mambo unayofikiria, unayoyasema na kutenda.
Kumbukumbu ni
muhimu sana katika maisha ya binadamu kwa sababu ndizo zinazotusaidia kufanya
tathmini. Jitahidi kuweka kumbukumbu za mambo unayofikiri, unayosema na kutenda
japo kwa siku moja. Mwisho wa siku jitahidi kukukumbuka mambo uliyofikiria, uliyosema
na kutenda yawe mazuri au Mabaya. Hii itakusaidia kufanya tathmini ya matumizi
ya muda kwa siku hiyo.
Tathmini hiyo
itakusaidia pia kujua umetumia muda vizuri au vibaya. Mara nyingi sana siyo
rahisi kukukumbuka mambo yote uliyofikiria na kusema lakini ni rahisi
kukukumbuka matukio na mara nyingi matukio hutokana na kufikiri na kusema,kwa
hiyo kukumbuka matukio ni njia rahisi zaidi yakukuwezesha kufanya tathmini ya
siku nzima.
2. Weka ratiba ya siku nzima.
Ratiba ni muhimu
sana katika maisha ya kila siku.Usianze siku bila kujua utafanya nini siku
hiyo. Unaweza kuweka na kupanga ratiba ya siku inayofuata kabla ya kulala au
asubuhi kabla hujaanza jambo lolote. Watu wote waliofanikiwa, wamefanikiwa kwa
sababu ya matumizi mazuri ya muda, wanafanya kazi zao kwa ratiba na wana
nidhamu linapokuja swala la matumizi ya muda. Bila kuwa na ratiba muda hutumika
bila mpangilio na wakati mwingine muda hupotea bure. Unapoweka ratiba hakikisha
kila kitu ulichokiweka kina wakati na muda wake. Kinaanza saa ngapi na kuisha saa ngapi. Ni
vyema ratiba hii iwe na mambo ya msingi tu. Usisahau mapumziko. Mapumziko ni
muhimu kwa utendajibora wa akili na mwili.
3. Epuka kuwa na mipango mingi.
Katika ratiba
yako usiweke mambo mengi sana ambayo utekelezaji wake ni mgumu au
yanachosha.Weka mambo machache ambayo
yanakupa nafasi ya kupumzika na kutafakari namna ya kuianza siku inayofuata. Ukiweka
mambo mengi kuna hatari ya kuyatekeleza nusunusu na mengine yanaweza yasitekelezwe
kabisa.
4. Usiruhusu mambo yasiyo ya msingi kuingilia ratiba
yako.
Mara unapoanza
kutekeleza mipango ambayo iko kwenye ratiba yako, usiruhusu mambo yasiyo ya
msingi kuingilia na kuvuruga ratiba yako. Kuwa na nidhamu na heshimu ratiba
yako. Zipo dharura lakini si dharura zote
zinahitaji kushughulikiwa papo .Kama dharura ni ya msingi na inahitaji
kushughulikiwa papo hapo hamna tatizo.Jifunze kutambua na kutofautisha dharura
zinazohitaji kushughulikiwa papo hapo na zile zinazoweza kushughulikiwa baada
ya ratiba kukamilika.
Kuna watu ambao
wako tayari kuvuruga ratiba zao na kuacha shughuli zao kwa sababu ya mambo
yasiyo ya msingi kwa mfano kuangalia mechi na burudani zingine ambazo
haziwasaidii katika maisha yao. Narudia tena,uwe na nidhamu heshimu ratiba
yako.
5. Epuka kutumia muda mwingi kufanya mambo yasiyo ya
lazima na yasiyo na faida.
Epuka kutumia
muda mrefu kufanya mambo yasiyo ya msingi na yasiyo na faida kwa mfano kuchati
kwenye mitandao ya kijamii, kuangalia mechi na burudani zingine wakati ambapo
unatakiwa kufanya mambo ya msingi kwa ajili yako na jamii inayokuzunguka. Sina
maana mitandao ya kijamii mibaya ila nasisitiza kuwa na kiasi na kuipa nafasi
ndogo katika maisha ya kila siku. Kama
utakuwa unawasiliana kwenye mtandao
wa kijamii basi iwe kwa faida na si kupoteza muda.
Ninasema hivi kwa
sababu hili limekuwa tatizo Kubwa sana
kwa kizazi cha sasa hasa vijana, tena wanafunzi ambao wanatakiwa wasome kwa
bidii wasipoteze muda hata kidogo. Muda wa kufanya mambo ya msingi utumike
kufanya mambo ya msingi na mambo mengine yapewe nafasi ya pili au ya mwisho.
5. Tumia sehemu Kubwa ya muda wako kufanya mambo ya
msingi.
Unashauriwa
kutumia 75% hadi 80% ya muda wako kufanya mambo yenye tija kwako na kwa
wanaokutegemea.Tumia sehemu Kubwa ya muda wako kufanya mambo yatakayokujenga na
kukuimarisha kiakili,kijamii na kiuchumi. Fanya kazi za kukuingizia kipato, soma
vitabu, magazeti, na majarida yatakayokuongezea
maarifa na kupanua ufahamu wako.Ukiingia kwenye Internet soma vitu
vinavyokujenga na siyo kufuatilia habari za watu maarufu huku hakuna cha maana
unachopata.
Wengine wanaingia
kwenye Internet kuangalia ili kuangalia
picha za ngono na utupu. Watanzania wengi watu wazima ukiwauliza walisoma
vitabu lini, hawakumbuki, wengine wanakwambia shule ya msingi na wengine
sekondari, inasikitisha. Wengine
hata wanaponunua simu, hawasomi vile vitabu vinavyoelekeza namna ya kutumia
hiyo simu. Watu walio wengi sana kama ni kusoma wanapenda kusoma vitu ambavyo
haviwasaidii sana katika maisha yao kama magazeti ya udaku.
Nakutakia kila la
kheri, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora
yatakayoboresha maisha yako.
- Makala hii imeandikwa na Deogratius Harold wa Mbeya- Tanzania.
- Mawasiliano 0718 610 022
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.