Apr 1, 2015
Hawa Ndio Watu 5 Hatari Wanaoweza kuharibu Maisha Yako.
Ni ukweli na imedhibitishwa katika taaluma mbalimbali ikiwemo ya malezi na dini zetu, kwamba huwa tunaambukizwa tabia nzuri au mbaya na wale watu ambao kwa muda mrefu tuko nao na tunawaamini kwa kiasi fulani. Watu hao wanaweza kuwa wazazi, marafiki, wafanyakazi wenzetu, wanafunzi wenzetu, jirani zetu na wengine.
Nimeona siyo vibaya kwa hali
hiyo, kukushauri kwamba, unapaswa kuwa makini sana na watu ambao kwa namna moja
ama nyingine wanaweza kuharibu maisha yako kwa sehemu kubwa hata kama
tunawapenda vipi. Hili si jambo la mzaha
kama unavyoweza kulitazama kijuu-juu. Ni jambo la dhati. Kwa haraka haraka
naomba nikutajie watu hawa, wanaoweza kuharibu maisha yako.
1.
Watu wanaofikiri, kusema na kutenda hasi.
Hawa ni watu ambao siku zote
huwa hawaoni suluhu ya jambo, bali kuona matatizo tu. Ni watu ambao huzingatia
zaidi mambo yasiyopendeza na siyo yale yanayopendeza. Mtu anaweza kufanikiwa
kupata zabuni ya shilingi milioni 20 na kukosa ile ya milioni 100. Badala ya
kushukuru na kuangalia ile zabuni aliyoipata, atazingatia na kuumizwa kichwa na
kile alichokikosa.
Hawa huwa ni watu ambao hata
wakifanikiwa kivipi kimapato,bado maisha yao yanakuwa yamezingwa na hofu
zisizoisha, kutoridhika na kutamani tena na tena bila ukomo. Kwao kushindwa
kupata wakitakacho, bila kujali ni kitu gani, ndilo jambo linalopewa uzito
badala ya kile walichokipata.
Lakini kwa bahati mbaya,
watu wa aina hii huwa ni vigumu pia kufanikiwa kimapato katika Nyanja
waitakayo. Ni kwa sababu, kwao matatizo madogo kuyaongeza chumvi nyingi na
kuonekana kuwa makubwa sana. Kwao kushindwa jambo wanakutazama kama msiba
mkubwa ajabu. Hukata tamaa haraka kwenye matatizo na hivyo hawapati nafasi ya
kujifunza kupitia katika matatizo yao.
Ukiwa karibu na watu wa
namna hii, ni wazi utadhani maisha ni tahadhari na mashindano ambayo mshindwa
hapaswi kuishi. Lakini hata kama nawe uko hivyo, inabidi ujue kwamba, una
safari ndefu kuelekea kwenye mafanikio kama kweli unayataka. Watu wa aina hii
wana nguvu hasi za kuweza kuambukiza maradhi yao kirahisi kwa wengine.
2.
Watu ambao ni wafujaji wa mali.
Bila shaka umewahi kusikia
watu wakisema ‘ponda mali kufa kwaja’. Sina uhakika watu wanaoamini katika
usemi huu wana maana gani? Inawezekana ukawa na ukweli kama mtu anaamini kwamba
yeye ni huo mwili wake na maisha yake huisha pale mwili wake unapoachana na
mawazo au roho yake. Lakini hata kama mtu anaamini hivyo, bado kuna swali la
msingi kwamba, maisha ni yeye peke yake?
Kuna wengine wanaoamini
hivyo ambao wamesomeshwa kwa fedha za mifuko ambayo waanzilishi wake
walishakufa zamani. Ni watu waliohangaika kutafuta, wakapata na kuweka ili
wateja waje wawasaidie wengine. Sasa unashindwa kujua inakuaje mtu huyu
anayeamini katika kuponda mali kufa kwaja asijiulize mchango wake kwa wengine
ambao atawaachia nyuma.
Hatukuletwa duniani ili kula
na kuvaa vizuri na kufanya mapenzi sana, halafu tufe. Tuliletwa kwa kusudi
maalumu na kusudi hilo kwa sehemu kubwa ni mchango wetu kwetu na kwa wengine
hapa duniani. Elewa tu, unapaswa kuwaepuka watu ambao hawaamini kwamba
wanapaswa kuweka akiba ili kufanya mambo ambayo yatawasaidia wengine baadaye.
Wengine wao wanaweza kuwa ni familia zao, ndugu au jamaa zao, ama jamii nzima
kwa ujumla. Bila shaka huko ndiko kufanikiwa kwa juu kabisa, tunapokuzungumzia
kufanikiwa kwa upana wake.
3.
Watu wasiojua cha kufanya baadaye.
Kuna watu ambao ukweli ni
kwamba hawajui cha kufanya muda ujao. Watu hawa hula chakula tu, kunywa pombe
tu, kucheza bao au karata tu, lakini wafanye jambo gani la kuwasaidia wao au
wengine inawawia vigumu. Ni afadhali mtu ambaye hana malengo lakini kuna jambo
au mambo anafanya, hawa hawana wanachofanya kabisa.
Kazi yao ni kutafuta mtu wa
kumlaumu kwa kushindwa kwao kuwajibika. Hata wakipewa shughuli, watashindwa na
kurejea kwenye kuishi kama mawe au kuku wa kufugwa bandani. Wanajua sana watu
hawa kusingizia serikali au viongozi wa nchi. ‘wanaiba sana, ndiyo maana
wengine hatuna cha kufanya’. Ni hodari sana kulaumu ndugu, ama jamaa zao.
Hawa ni watu ambao kwa
kawaida ukiwaendekeza wanakufikisha mahali ambapo unaweza kuamini kwamba maisha
yana kasoro na wanaweza kukufanya uamini kwamba hata wewe hutendi mema kufanya
shughuli na kuingiza kipato kingi. Dawa ni kuwakwepa kwa mbali na wala
usikubali ‘kuwafuga’, watakuharibia sana maisha yako.
4.
Watu wanaoharibu majina ya wengine.
Siyo rahisi kwa mtu
kufanikiwa kama ana kijicho, dhidi ya watu waliofanikiwa. Kuna watu ambao ni
maadui wa watu wote wanaofanya vizuri. Hutumia kila wanaloweza kuwaharibu ama
kuwazuia ili wasiende mbali. Wanaweza kukuza majungu au sifa mbaya kwa watu
ambao wanaonyesha kuelekea kwenye mafanikio au hata kufanya njama tu ili
waanguke. Badala ya kuwa karibu na hao wanaoelekea kwenye mafanikio ili
wajifunze kitu, hutaka kuwaona wameanguka, hivyo muda wao mwingi huupoteza
katika kutafuta na kumharibia yule au huyu na sio katika kutafuta mafanikio.
Kufuatana au kuwa karibu na
watu hawa ni sawa na kutaka kuambukizwa bure nguvu hizi hasi ambazo zinadhuru
sana bila mhusika kujua. Kwa nini tusijaribu kuiga na kujifunza kupitia
mafanikio ya wengine katika kutafuta mafanikio yetu, badala ya kuwachukia? Kwa
nini tusiamini kwamba wengine wakifanikiwa, nasi bila kujua tumefanikiwa pia?
Kama kweli tunataka mafanikio ni lazima tuwaepuke watu hawa wenye kijicho na
chuki.
5.
Watu wasipenda shida wala usumbufu.
Hawa huwa ni watu ambao
idadi yao inazidi kuwa kubwa kila kuchao. Ni watu ambao mara nyingi wakishasoma
basi kila kitu huishia hapo na hutamani ama hupenda zaidi kila kitu kiletwe
miguuni mwao. Ni watu ambao hawana juhudi wala ubunifu kwa kile wanachokifanya
katika maisha yao. Watu hawa huwa ni watu wa jua kucha, jua kuzama siyo zaidi
ya hapo. Matokeo yake ni kupata shida katika maisha. Pia hawa ni watu hatari
sana kwako unaotakiwa kuwaepuka sana.
Hao ndio watu hatari ambao
usipokuwa nao makini wanaweza kuharibu maisha yako kwa sehemu kubwa sana.
Tunakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza
kila siku.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com
.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.