Apr 14, 2015
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuondokana Na Msongo Wa Mawazo.
Je, huwa unaingia kwenye
msongo wa mawazo haraka au kirahisi? Kama jibu ni ndiyo, kwa nini usijiulize ni
kwa vipi unaingia kwenye kusongeka? Kitu ninachoamini kwa kujiuliza ni kwa nini
mtu anasongeka, kunakuwa kuna mengi ya kujifunza, lakini wakati mwingine, mengi
ya kushangaza pia.
Kusongeka humfanya mtu kuona
kwamba, kila kitu kinakwenda hovyo, kila kitu kiko shaghalaghabala, kila kitu
kiko hovyo. Wanaoingia kwenye kusongeka kiakili hujiambia siku zote kwamba,
kila kitu hakina maana, yakiwemo maisha yao pia.
Je, kitu cha kujiuliza hapa
kama itatokea nikaingia kwenye kusongeka kiakili nitakuwa nazungumza vipi,
yaani kwa sauti namna gani? Bila shaka nitakuwa nazungumza kwa sauti ya chini
na pia ya kuburuza. Siyo kuzungumza tu, bali hata kusimama au kutembea kwangu
kutakuwa ni kwa kujiinamia na kuona kila kitu kwangu kimeharibika.
Hivi ndivyo wengi
wanavyojiona wanapokuwa wamesongeka kimawazo, ingawa kuna wakati mwingine
huweza hata kuonyesha nyuso za huzuni na simanzi, hiyo yote huweza kutusaidia
sisi kubaini na kutambua wazi kinachoendelea kwenye akili zao kuwa wana mawazo
mengi au kusongeka sana ndiko kunakowasumbua.
Kama upo kwenye kusongeka na unaendeleza mawazo hayohayo kila mara ambayo yanakupekea wewe kusongeka hiyo inakuwa sawa na wewe kuamua kujichanganya kwenye maisha yako. Na unapoamua kujichanganya mwenyewe kwenye maisha yako, tambua kabisa hakuna utakachoweza kufanikisha, zaidi ya kuharibu maisha yako tu.
Ni vizuri kwako kujua kuwa
unaouwezo wa kuweza kubadili kusongeka kwako kimawazo na kuishi huru kabisa.
Najua inaweza ikawa kwako sio rahisi kuelewa, lakini ninachotaka kukwambia kuwa
unaweza kuondokana na kusongeka kwako, ikiwa tu utaweza kubadili namna ya
kuyatazama mambo au matukio katika maisha yako.
Ni kweli kwamba, kusongeka
kiakili husababishwa na mambo mbalimbali, lakini sisi huweza kufanya kusongeka
huko kushika mizizi kwa namna tunavyokaa, kusimama au hata kwa namna yetu
tunavyofikiri na kutafsiri mambo. Tunapokaa au kufikiri kwa namna ya kinyonge,
tunafanya mawazo yanayotupitia kuwa ya kinyonge pia.
Kwa kuhakikisha hili zaidi,
hebu jaribu kumuuliza au kumchunguza mtu anayetembea huku akiwa ameinama na Yule
anayejiinamia kama atakwambia kuwa anafikiria mambo mazuri. Ni wazi kabisa mtu
kama huyu ni lazima atakuwa anafikiria mambo mabaya yanayopelekea kusongeka
kwake kimawazo.
Kufikiri kwetu kukiwa nako
ni kule kunakotutia hofu, mashaka na kutuingiza kwenye kijicho, ni lazima
tutajikuta tukianza kusimama au kutembea kwa njia yenye kuonesha kukata tamaa,
wanyonge na hata tusiojiweza. Kwa nini tusibadili mambo hayo ili tuweze
kuondoka kwenye huzuni kali au kusongeka? Kwa kujiambia mambo yenye kutia
huzuni na simanzi tunajiingiza kwenye huzuni bila kujua.
Lakini kumbuka kuwa kwa
kujiambia mambo mazuri na yenye kutia moyo ndivyo tunajikuta ambavyo tunaingia
mahali ambapo tunayaona au kuyatazama maisha katika mwanga mkubwa zaidi. Na
hivi ndivyo tunavyoweza kuondokana na msongo wa mawazo kwa kujiambia mambo mazuri
kila mara katika maisha yetu na si vinginevyo.
Kwa kuwa tunaweza kufikiri
kwa namna isiyoumiza, tunaweza kwa hali hiyo kujitoa kwenye kusongeka. Kuna wakati
mtu mwenye msongo wa mawazo anahitaji tabasamu tu au kujiambia kimoyomoyo
kwamba, kila kitu kiko sahihi na kinakwenda kama kilivyotarajiwa. Halafu, ni
kweli, ataanza kuhisi tofauti, kuhisi ukamilifu na uwezo zaidi katika maisha
yake na kuondokana na kusongeka ambako kunaweza kuwa kunamtesa.
Ninaomba nikutakie mafanikio
mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza zaidi.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA DEVOTA KAUKI WA MANYONI, SINGIDA.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA DEVOTA KAUKI WA MANYONI, SINGIDA.
Kama una maoni au ushauri
unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa email truesuccess89@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.