Oct 3, 2019
Fedha Hutupa Furaha Tunapokuwa ‘Vijogoo’ Tu.
Je, kuwa au kupata fedha nyingi ndiko kunakoweza kumfanya mtu awe na furaha ya kweli? Hili ni swali ambalo huenda kwa sasa, idadi ya watakaojibu kwa ndiyo, inaweza kuwa ya chini kuliko miaka kadhaa iliyopita.
Kwa kiasi fulani, watu
wanaoamini kwamba, fedha ni kila kitu imepungua. Sababu ni nyingi, lakini
ugunduzi wa matumizi ya akili ya kawaida umekuwa ukijitokeza siku hadi siku. Nchi
zilizoendelea kwa fedha, watu wake wamekuwa wakiingia kwenye kukosa furaha kwa
mapana makubwa zaidi.
Wamerekani, wajapani,
waingereza na wengine wamekuwa wakisongeka na kujiua na kukata tamaa, zaidi
kuliko muda mwingine wowote huko nyuma, kwa sababu ya pesa tu.
Watafiti wamebaini hivi
karibuni kwamba, fedha huweza kuongeza furaha kwa aliyenazo kama yeye ndiye ‘kijogoo’
kwenye eneo analoishi, ofisini au pale ambapo mtu huweza kubainishwa na wengine
kuwa ndiyo ‘kijogoo’ kwa fedha nyingi kuliko wenzake. Lakini inayopatikana ni
furaha kidogo na ya muda mfupi.
Wanasema, hapo suala siyo
mtu ana kiasi gani, bali zaidi anamzidi nani. Kama mtu ana fedha, lakini
akabaini kwamba, hapo mtaani kuna wanaomzidi, ni wazi hatafurahia kuwa na fedha
hizo. Kwa nini hatafurahia?
Wamebaini watafiti hao
kwamba, fedha huwa zina tatizo la kutafuta ushindi. Kama mtu hujui saikolojia
ya fedha, ni dhahiri atajibainisha nazo. Akishafanya kosa hilo la kujibainisha
nazo atataka au kujikuta akitaka awe ndiye mwenye nyingi zaidi. Katika kutafuta
yeye awe ‘kijogoo’ ndipo furaha inapoondoka. Siku zote tunaposhindana maishani,
furaha nayo hukimbia.
Furaha ya kweli kutoka
kwenye fedha haiji kwa mtu kutaka kuwafikia wengine, hapana. Furaha ya kweli
huja pale ambapo mtu yuko juu ya wengine na hao wengine wanajitahidi kupigana
vikumbo kutaka kumfikia.
Kwa mfano, watafiti
wamegundua kuwa, mtu analipwa au pato lake ni kiasi gani, siyo suala la maana
sana, bali wenzake wanalipwa au pato lao ni kiasi gani, ndilo jambo la maana. Hii
ina maana kwamba, kama mtu anapata 500,000 kwa mwezi na wenzake, wale wakaribu
yake ambao ndiyo kipimo chake, wanapata kila mmoja kiasi kisichozidi 400,000,
huyu mtu ni lazima atakuwa na furaha tu. Hata kama fedha hizo hazitoshi
matumizi, ili mradi yeye ndiye mwenye kufukuzwa ili akutwe, atakuwa na furaha
zaidi.
Umri unatajwa pia na
wataalamu hawa. Wanasema, watu wakiwa kwenye umri unaolingana au kukaribiana,
mwingine anapokuwa na fedha zaidi, hawa wanaomfukuza au wanaojilinganisha naye,
hutaka kumpita, kukosa furaha zaidi, hata kama wana mamilioni zaidi.
Kwa hiyo, kinachowakosesha
wengi furaha katika suala la pesa, siyo fedha yenyewe, hapana. Kinachowakosesha
furaha ni kutaka kufika mahali ambapo wao ndiyo watakuwa kipimo cha juu cha
wenye fedha zaidi. Bado hata hivyo furaha hiyo itakuwa siyo ya muda mrefu
mwingine atakapoonesha dalili za kutaka kumfikia, kiwango cha furaha ni lazima
kitapungua au kwisha.
Kwa kuwa kila siku watu
wanapitana kwa kipato, kutegemea furaha kupitia fedha ni upotezaji wa muda kwa
sababu, furaha hiyo ni bandia sana na inakuwa siyo ya kudumu kwako.
Tunakutakia mafanikio mema
endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com
Oct 2, 2019
Hawa Ndio Watu Hatari Usiowajua, Wanaonyonya Nguvu Za Wengine.
Inaweza kuonekana kama
ni kitu cha kushangaza lakini huu ndio ukweli wapo watu wanaonyonya nguvu za
watu. Watu hawa wana uwezo wa kumwandama mtu hadi anakufa bila kujua. Watu hawa
hawajafa,wako hai na tunaishi nao, wengine wakiwa ni watu wetu wa karibu sana,
kama wazazi, wapenzi, watoto, jirani, marafiki au mabosi wetu. Hufanya vipi
kunyonya nguvu zetu? Hutumia njia za aina mbalimbali, ambazo huzaa matunda
kweli.
Mtu anaweza kuuliza,
inawezekana vipi mwingine anyonye nguvu zangu na hizo nguvu ni zipi? Kwa mfano,
mimi ninapo kuwa nakukera kila siku, ninakugusa kihisia. Ninapokugusa kihisia,
unaumia kihisia na kimwili. Baada ya muda Fulani wa kero zangu, nakuwa nimekupa
athari kubwa kimwili na kiakili bila mwenyewe kujua na kama imeshawahi
kukutokea umekerwa na mtu huwa inapelekea hata unapokutana na mtu huyu
anayekukera unakuwa unajisikia vibaya.
Hebu pia tuchukue mfano
wa bosi na mtumishi wake. Kama bosi ni mtu wa maringo, dharau, kulaumu bila
kujali nini kimefanyika, mkandamizaji na asiyejali kuhusu madhila ya wengine,
ni wazi aliye chini yake ataumia tu,
kwanza, kihisia, halafu kimwili. Ataichukia kazi yake na hatimaye anaweza
kufika mahali akaona maisha haya maana aliyoitarajia.
Ni vigumu kubaini mtu
ambaye ni mnyonya nguvu mapema, lakini kwa kuelekezwa, mtu anaweza kuwa makini
na kuwabaini watu wa aina hiyo popote walipo au watakapokuwa. Nimeamua
nikuelekeze au kukutajia sifa za watu wanaoweza kuwanyonya wengine na kuwaacha
wakiwa maganda matupu, huku wakiwaacha wakiwa wanyonge hawajui ni kipi cha
kufanya.
Hizi
ndizo sifa za watu wanaoweza kuwanyonya wengine:-
1. Kuna
watu ambao tunanaweza kuwaita, “miye maskini.”
Hawa ni watu ambao muda
wote unapokutana nao, wanalalamika tu. Hakuna siku ambayo utakutana nao ukute
wanazungumzia mambo mazuri au wanafurahia hali. Kila siku wao ni walalamikaji,
wanaoamini kwamba, wanaonewa na kuteswa. Unaweza kukuta ni watu wa kulalamika au
kukosoa tu, lakini bila kutoa pendekezo au kuonesha ni njia zipi zingepaswa kufuatwa au njia zipi
zingetatua tatizo.
Wao wanaona kwamba,
wanaonewa, wananyimwa nafasi, wanatafutwa na kuchukiwa. Hawa kwa kawaida hawana
uwezo wa kusema lao, kusema wanachofikiria au walichobuni, hapana. Hata kama
wanatakiwa kusema kuhusu jambo fulani maalumu, ambalo halihusiani na kuonewa na
mtu, watajikuta wakiingia kwenye kulaumu au kukosoa kwanza, ndipo waweze
kujibu, kama basi watakuwa na uwezo wa kujibu.
Hawa ni wanyonya nguvu
za wengine. Hawa ni watu wa kuepukwa sana. Kama mtu wa aina hii anakujia na
kutaka mjadili jambo, ambapo anaanza malalamiko au kukosoa kwake, huna budi
kutafuta sababu ya kukataa kuwa karibu naye. Ni lazima ufanye hivyo, kwani
akikuzoea ni lazima atakunyonya nguvu zako zote.
2. Kuna
watu ambao wao ni wakuzaji wa mambo.
Hawa ni wanyonya nguvu
pia ambao wao kitu au jambo dogo hufanywa kubwa hadi mtu anaweza kuamini kwamba
ni jambo kubwa kweli, ingawa awali alijua ni jambo dogo. Hawa wako maofisini na
majumbani. Mtu anaumwa na mafua, lakini atalalamika, atagumia na kuaga kabisa
na kuacha kabisa wosia, kwamba anakufa.
Yeye mwenyewe huyu
anayefanya visa hivyo anaamini kwamba, kwa kufanya hivyo, atapata huruma zaidi,
ataona watu wanavyohangaika kuonesha wanavyomjali na kutaka kupima umuhimu
wake. Kwa kawaida kukuza kwao mambo kunaweza hata kusababisha hata wengine
wakaugua zaidi au hata kupoteza maisha kabisa, kutokana na kuongeza chumvi sana
kwenye maneno yao.
3. Kuna
wale ambao kwa lugha ya mtaani tunawaita wameza kaseti.
Hawa ni wale ambao wanataka waongee wao tu, wanataka wao ndiyo wasikilizwe na mwingine anapotaka hata kusema moja hapewi
nafasi. Mtu atazungumza yeye kuanzia mwanzo hadi mwisho, hata kama ni kwa saa
tatu mfululizo. Mwingine anapotaka kuongea, yeye ameshamkatisha na kuzungumza
yeye. Hataki kuona mtu mwigine akizungumza kama yeye yupo. Hata kama ni mgeni
mahali, akishapewa nafasi ya kuzungumza, huzungumza kweli.
Hajali kama kuna mtu
ambaye anataka aseme hisia zake, hapana. Inafika mahali, kama unamsikiliza
unachoka kabisa. Hatajali, hata kama utamwonesha kutokujali. Kama ni nyumbani
au ofisini, hatajali kukupotezea muda wako kwa vyovyote vile. Kama ni ushauri
aliomba kwako, yeye ndiye atakupa ushauri kwa sababu, hatakupa nafasi ya
kuzungumza katika kumshauri. Hawa ni wanyonya nguvu ambao tunao kila siku.
4. Kuna
wanyonya nguvu ambao kazi yao ni kuwafanya wengine washitakiwe na dhamira.
Kila wakati linapotoea
jambo , juhudi yao kubwa ipo kwenye kutafuta njia ya kulaumu ili wengine
washitakiwe na dhamira. Wakati mwingine jambo liko wazi kabisa kwamba, hao
anaowalaumu hawahusiki, lakini ni lazima atalaumu tu. Hata kama atafafanuliwa
na kuona kwamba, anaowalaumu hawana tatizo, bado atasema, ‘hata kama hamtaki anahusika kidogo’Wanyonya nguvu hawa wanatafuta
kasoro ili walaumu, ili mtu mwingine ajisikie kukosa, ashitakiwe na dhamira.
Anaweza kuangalia mtu
anavyofanya kazi Fulani na kuona ni nzuri sana. Lakini atajaribu kwa kadiri
awezavyo kumkosoa mtu huyo kwa kitu ambacho wala wakati mwingine hakihusiani
moja kwa moja na kazi ile. Anaweza kusema ‘ile
kazi ya mwaka jana angefanya hivi tusingekosa tenda’ lengo ni kumfanya mtu
ashitakiwe na dhamira. Hataki kusifia hii kazi nzuri ya sasa, anataka kukosoa
ya zamani ambayo iliharibika.Dawa ya hawa ni kuwapuuzia.
5. Kuna
wanyonya nguvu wengine ambao ni wale wasioisha kuwa na matatizo yanayohitaji
ushauri.
Asubuhi atakuja
kukuomba ushauri unaohusu jambo Fulani, mchana atakuja na jioni atakutafuta.
Wakati mwingine ushauri anaoomba ni wa kawaida tu. Ni vizuri kumwonesha kwamba,
unajali anachosema, lakini ni vema kila wakati kumwonesha kwamba, huna jibu,
siyo huna nia ya kumsaidia kwenye tatizo lake. Ajue kwamba, huna jibu kwa sababu
hujui. Ukikosa njia au jibu mara kadhaa, atakata tamaa na kukuacha. Usimwoneshe
jeuri au dharau ama kisirani.
6. Kuna
wanyonya nguvu ambao kazi yao ni kuudhi kwa maneno ya kushushua na kushushua.
Badala ya kunyamaza,
akikuona na nguo ya aina Fulani, atakwambia, ‘bwana mzee huwezi kuvaa nguo za mtumba kwa hadhi yako vipi’ Ni
wakati ambao kila mkikutana , watatafuta namna ya kukera kihisia zako na
kujaribu kukushushua. Anaweza mtu kusema ‘ mbona afya yako inazidi kuwa mbaya’
bila hata sababu ya msingi. Ni watu ambao muda wote wanataka kuumiza hisia za
mwingine.
Bila shaka umeshawahi
kukutana na mmoja kati ya wanyonya nguvu hawa. Jitahidi wakati wote kuwa makini
wasije wakafanikiwa kukuweka chini ya himaya zao. Jitahidi kuwabaini na kujua
namna ya kuwaondolea mbali kwenye maisha yako.
Nakutakia mafanikio
mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza zaidi na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 0345/dirayamafanikio@gmail.com
Oct 1, 2019
Kama Una Tabia Hizi, Mafanikio Kwako Yatabaki Kuwa Ndoto.
Adui wa kwanza wa mafanikio
katika maisha yako ni wewe mwenyewe. Wewe
ndiye unayeamua,ufanikiwe au usifanikiwe. Ninaposema hivi nina maana kwamba ziko
tabia ambazo ukiwa nazo unafanikiwa na zipo tabia mbazo ukiwa nazo utaishia kuona wenzako
wanafanikiwa wewe unabaki palepale.Tabia hizi ni adui mkubwa wa mafanikio yako. Kwa hiyo usianze kutafuta mchawi wa mafanikio yako,mchawi wa kwanza ni wewe. Wewe ndiye mwenye maamuzi ya
mwisho juu ya maisha yako unataka yaweje.
Hizi ni tabia ambazo umekuwa
nazo kwa muda mrefu na hutaki kuziachia. Kwa jinsi unavyoendelea kuwa nazo
ndivyo ambapo unajikuta maisha yako yanazidi kuwa magumu na wakati huo huo mafanikio
kwako yataishia kuwa ndoto ya saa sita mchana, ndoto ya alinacha na mara nyingi
utajikuta ukiishi maisha ya wasiwasi huku ukiwa hauna uhuru katika maisha yako.
Unapojifunza tabia hizi fanya mabadiliko, chukua hatua sahihi za kubadili
maisha yako na utafanikiwa.
Hizi
ndizo tabia ambazo ukiwa nazo, mafanikio kwako yataishia kuwa ndoto za mchana:-
1.Kutokuwa na malengo.
Ili mtu afanikiwe lazima awe na malengo.
Malengo ndio chanzo cha mafanikio, mafanikio
hayaji kwa bahatí mbaya. Watu wote waliofankiwa unaowafahamu na
usiowafahamu walikuwa na malengo, wakayaweka katika vitendo na kufanikiwa. Kama
wewe ni mwanafunzi weka lengo unataka kuwa nani baadaye, vinginevyo utaishia
kusoma na kubaki huna kazi ya kufanya; unakuwa umepoteza muda bure katika
maisha yako.
Kama wewe ni mfanyabiashara weka lengo la kuwa mfanyabiashara mkubwa. Zingatia
kwamba malengo ndiyo yanakupa dira na muelekeo katika maisha yako. Kupitia malengo
unajua unatakiwa uanzie wapi na uishie wapi kulingana na lengo ulilojiwekea kwa
wakati huo. Kutokuwa na malengo katika maisha ni sawa sawa na kusafiri bila
kujua unaenda wapi. Hii ni hatari sana kwako.
2 .Kutokuwa na malengo
maalum yanayoeleweka.
Kuwa na malengo haitoshi, ni lazima uwe na malengo yanayoeleweka na
kufikika. Ni kosa Kubwa kuwa na malengo mengi Ambayo hayafikiki na kutaka kuyatekeleza
kwa wakati mmoja. Kuwa na malengo mengi
humfanya mtu achanganyikiwe. Mtu mwenye malengo mengi ana hatari ya; Kuchanganyikiwa na kushindwa kuamua
aanze na lipi, amalize na lipi,pia ana hatari ya kutekeleza mambo nusunusu
na hatimaye kushindwa kuendelea kabisa na mipango hiyo.
Weka malengo machache ambayo una uwezo wa kuyatekeleza kwa muda uliopanga
kisha anza kutekeleza mpango mmoja hadi mwingine. Ukishafanikiwa kutekeleza
mipango hiyo weka lengo lingine na utazidi kupiga hatua moja hadi nyingine na
kuzidi kufanikiwa siku hadi siku.
3. Kukosa uvumilivu.
Mafanikio ni safari ndefu sana katika maisha ya binadamu. Mafanikio ya
kweli yanachukua muda mrefu kupatikana, hayachukui muda mfupi kama wengi
tunavyotaka. Kutaka mafanikio kwa muda mfupi ni tatizo ambalo limetukumba wengi
katika dunia ya leo yenye changamoto nyingi za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Watu
wengi tunaiogopa safari ndefu ya mafanikio, tunataka mafanikio ya muda mfupi.
WatuWengi wanakata tamaa mapema kwa
kwa sababu wanataka mafanikio kwa mnuda mfupi jambo ambalo haliwezekani. Matokeo
yake wanaamua kupita njia za mkato ili kufikia malengo wanayojiwekea. Usiogope kuchukua muda mrefu hadi
kufanikiwa,hayo ndiyo mafanikio ya kweli. Ikiwa unataka kufikia mafanikio, usiogope kupita jangwani.
4. Kukosa nidhamu.
Nidhamu ndicho chanzo cha mafanikio. Ukitaka kufanikiwa ni lazima ujitambue
wewe ni nani una lengo gani na unapaswa kufanya nini ili kufanikisha lengo
lako. Si hivyo tu unapaswa kuwa na mipaka katika utendaji wako. Unapaswa kujua
lipi la kufanya na lipi si la kufanya, LAZIMA
UWE NA NIDHAMU. Nidhamu ni uwezo wa kujitawala na kujizuia, kujiwekea mipaka ya utendaji wewe mwenyewe bila
kusimamiwa.
Unaweza kuiga na kufanya karibú kila kitu unachokiona na kukisikia, lakini
si lazima uige na kufanya, mambo mengine siyo ya kuiga. Jiheshimu mwenyewe, pia
heshimu na kazi yako.Usiache kazi
na kufanya mambo mengine yasiyo ya
msingi ambayo hayakusaidii kufikia lengo lako.
5. Kukosa shukurani.
Hakuna mtu anayefanikiwa katika maisha yake kwa juhudi zake mwenyewe bila
kuwategemea wengine kwa namana yeyote ile, hayupo dunia hii. Tambua mchango wa
wengine katika mafanikio yako. Kuna njia
nyingi za kuonyesha kwamba unatambua mchango wa jamii inayokuzunguka
katika mafanikio yako. Baadhi ya mashirika na taasisi huamua kuchangia huduma
za jamii kama elimu na afya kwa kutoa vitendea kazi kwa shule au hospitali.
Baadhi ya watu huamua kuwasaidia wengine katika shughuli zao kiuchumi.
Yapomambo mengi unayoweza kufanya ili kuonyesha kwamba unatambua mchango wa
wengine katika mafanikio yako. Si vyema kutokufanya jambo kwa ajili ya wengine
ikiwa wapo ambao walifanya kitu fulani na wengine wanaendelea kufanya kwa ajili
ya mafanikio yako. Kwa hakika kuna watu wamefanya kitu fulani kuchangia
mafanikio yako, wewe unafanya nini kwa ajili ya wengine?
6. Kuwa na hofu sana.
Watu wengi huwa wanaogopa kujaribu
kufanya kazi fulani kwa sababu watachekwa au kujishushia hadhi mbele ya jamii. Baadhi
ya watu wanaogopa kujaribu kwa sababu
wakishindwa watachekwa na kujisikia vibaya. Wengine wanaogopa kupoteza fedha
baada ya kupata hasara. Ni bora kujaribu ukashindwa kuliko kutokujaribu kabisa.
Mafanikio huja kwa kujaribu na kushindwa bila kukata tamaa. Katika ugunduzi
wa gropu,Thomas Edison alishindwa zaidi ya mara elfu moja, hatimaye alifanikiwa
mpaka leo hii tunasimulia habarí zake na kujifunza kutoka kwake.
Thomas Edison anasema,Udhaifu wetu mkubwa upo kwenye kukata tamaa. Njia ya
hakika ya kuweza kufanikiwa ni kujaribu mara nyingine tena. Kupata matokeo Ambayo hukuyatarajia na
huyataki katika jambo ulilolifanya, haina maana kwamba matokeo hayo hayana
faida.Wakati umejaribu njia zote na kushindwa, kumbuka hili-HUJASHINDWA. Kumbuka,
kujaribu na kushindwa ni sehemu ya mafanikio.
Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku, karibu sana.
- Makala hii imeandikwa na DEOGRATIUS GUNJU WA MBEYA TANZANIA
- Mawasiliano 0718 610022
Subscribe to:
Posts
(
Atom
)