Sep 2, 2018
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuondokana Na Majuto Uliyonayo Na Kuishi Maisha Ya Amani Na Furaha.
Wengi wetu huwa tunajuta sana. Mara nyingi tunapokumbana na kushindwa kwetu au mambo yetu kukataa kwenda kama tulivyotarajia, huwa tunajuta sana. Nini yaweza kuwa hasa sababu ya kujuta kwako sana na pengine huweza kupelekea wewe mwenyewe kuanza kujiona kama hufai vile.
Kujuta huweza kujitokeza pale ambapo hukutenda itakiwavyo kwa kile
ulichokuwa ukikifanya. Kujuta sio kubaya kama ni kwa ajili ya kurekebisha
makosa. Kuyajua makosa hayo ina faida kwa maana kwamba sasa unaweza kubadilika
na kuwa tayari kwa ajili ya maendeleo au kufanya vizuri zaidi.
Huku ni kujuta kwenye kujenga na kwa hali hiyo hatupaswi kuita hali hii
kujuta. Kama tutajilaumu kwa kushindwa, bila kujali kama ni kosa letu au
hapana, hapo ndipo tunapoita kujuta. Kujuta siyo kule kujua kwamba, tumekosea
na pengine ni uzembe, lakini tukawa tayari kujifunza.
Kihoro cha mawazo kina uhusiano na mambo yaliyopita. Ili mawazo hayo yaweze
kudumu hayana budi kubaki ndani ya moyo wako. Kila siku unayoishi, yaani leo,
ndiyo siku yako kubwa ya kujisahihisha. Ukiruhusu mawazo yako yakutawale, basi
utakuwa umejilimbikizia kikwazo kikubwa dhidi ya maendeleo yako.
Kwa kadiri utakavyoendelea kujuta sana bila kujifunza kitu, ndivyo
utakavyojikuta maisha yako unazidi kuyaharibu. Hii inatokea kwa sababu unakuwa
hufanyi kitu kipya, unakuwa umeganda kwenye kujuta tu. Unawezaje kupambana na
majuto haya unayokutana nayo mara kwa mara katika maisha yako na ili
yasikuumize tena?
1. Kuwa na muda wa maamuzi.
Kufikia sasa utakuwa umeshajielewa wewe ni nani na unataka kuzoea nini
badala ya kile ulichokuwa umekizoea. Ukishajua unachokitaka fanya kile ambacho
unapaswa kufanya kama vile, kubadilisha imani. Njia yenye nguvu ni kuvifanya vitu
ambavyo una uwezo wa kuvifanya. Unachokifanya leo kinaathiri maisha yako ya
baadae na kitakusaidia usijute baadae.
2. Jiulize sana maswali.
Kile ukifanyacho ni kupambana kwa ajili ya kubadili unavyojisikia. Unataka
kujisikia vizuri kwa nini uhisi majuto ndani yako na kufadhaika. Kama una
utashi wa kweli wa kutaka kuondokana na kujilaumu, lazima upitie zoezi zima la
kujiuliza maswali mazito.
Hii ni aina mojawapo ya kubadili mwelekeo wa ubongo wako. Kwa yale yote
unayoyajua unaweza kuwa unayaalewa mambo pengine kimakosa. Endelea kujiuliza
maswali ili kuweza kugundua mambo ambayo ulikuwa hujayaona na ambayo
yanakufanya uumie na kujuta.
3. Badilisha picha katika mawazo
yako.
Mawazo kuhusu mwenendo wako mbaya au upumbavu wako husababishwa na picha
ambazo uliziunda ndani ya akili yako.
Unaendelea kujiadhibu, kwa kila wakati kwa kuziona taswira na
kukurudisha nyuma ulikotoka. Unavyozidi kukumbuka ya kale, ndivyo unavyozidi
kuleta majuto.
Una udhibiti juu ya yale tu yanayojionyesha kwenye fikira zako. Unaweza kufanya
hivyo kwa kupandikiza mawazo mapya na mazito juu ya yale ya zamani, ambayo
umeyagandisha kwenye ubongo wako. Inahitaji nidhamu na kujitoa mhanga, tena ni
jambo la maana ili kujiondoa kutokana na uozo uliopita.
4. Geuka na fanya mabadiliko.
Kama ulichokuwa umekifanya kilikuwa kibaya achana nacho. Badilisha
mwelekeo. Jipe ahadi mwenyewe kwamba hutarudia tena. Jisamehe kwa ujinga wako.
Kama umewakosea wengine au umewaumiza waombe msamaha, kisha songa mbele.
Fanya kazi na fanya vitu ambavyo vitakufanya ujisikie vizuri na kurudisha
kujiamini kulikokuwa kumepotea. Hujacheleweshwa kuanza upya wala usijali kuhusu
umri wako. Daima kuna kitu ambacho unaweza kukifanya ili kuyaweka maisha yako
na ya wengine sawa.
Kumbuka, ni lazima wote tuathiriwe na aina mbili za maumivu, maumivu ya
nidhamu na maumivu ya kujuta. Tofauti ni kwamba nidhamu ina uzito kidogo na
majuto yana uzito mkubwa. Hivyo, ndivyo unavyoweza kuondokana na majuto
uliyonayo na kuishi maisha ya amani na furaha.
Nakutakia mafanikio mema katika maisha yako, karibu sana na endelea
kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza mambo mazuri yatakayokuwa
yanakujia.
TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.