Jan 1, 2015
Kama Unataka Mafanikio Makubwa Mwaka 2015, Acha Kukata Tamaa Tena Katika Mambo Haya.
Mara nyingi wengi wetu
huwa ni watu wa kufikiria kukata tamaa hasa pale tunapokutana na magumu katika
maisha yetu. Kukata tamaa huwa kuna kuja
pale ambapo mambo huwa hayajaenda sawa kama tulivyopanga, na wakati mwingine
huwa tunakatishwa tamaa na mazingira ambayo huwa tuna uhakika nayo hayawezi
kutufanikisha katika kile tunachokitaka katika maisha yetu.
Kabla hujakata tamaa
kwa kile unachokifanya, elewa kabisa kukata tamaa ni moja ya sababu inayowafanya
watu wengi sana washindwe kufikia malengo yao waliyojiwekea. Katika maisha yako
acha kufikiria kwanza kukata tamaa pale unapokumbana na magumu. Hakuna
utakalopanga kulipata ukalipata kirahisi rahisi kama wengi wetu tunavyotamani
iwe. Maisha ni changamoto.
Inawezekana ni kweli
malengo na mipango yako mikubwa uliyojiwekea mwaka huu unaoisha leo,
hayajakuendea vizuri kama ulivyokuwa ukitaka. Hilo lisikutishe unayonafasi ya
kujipanga upya kwa mwaka 2015 na kufanya mambo makubwa. Hata kama kuna mambo
yalikukatisha tamaa sana na ukajiona umeshindwa, ninachotaka kukuwambia huo sio
mwisho wa safari yako ya mafanikio.
Kumbuka, tunaishi
katika dunia ambayo ina njia nyingi za kutufanikisha kwa yale tunayofanya. Acha
kujidanganya na kuamini kuwa umeshindwa na huwezi tena kusonga mbele kutokana
na mambo yaliyokukatisha tamaa. wewe sio mtu wa kushindwa kama unavyofikiri,
unayo nafasi kubwa ya kufanya mabadiliko na kuufanya mwaka 2015 uwe wa historia
kwako kama ukiamua.
Kama
Unataka Mafanikio Makubwa Mwaka 2015, Acha Kukata Tamaa Tena Katika Mambo
Haya:-
1. Acha
kukata tamaa kujiwekea mipango na
malengo yako upya.
Ni kweli mambo yako
yanaweza yakawa yameharibika kiasi cha kwamba kwako unaona kama inakuwa ngumu
kusonga mbele. Huo sasa ndio wakati wako wa kutulia na kuweka malengo yako
upya. Acha kukaa chini na kusikilizia maumivu ya kushindwa huku ukiwa upo hapo
hufanyi kitu. Chukua hatua ya kuendelea mbele kwa kuweka malengo yako upya.
Usikatishwe tamaa wewe ndio mwamuzi wa mwisho wa maisha yako, weka mikakati
upya ya kufanikiwa.
2. Acha kukata tamaa kushughulikia matatizo yako.
Kuna wakati katika
maisha yetu mambo yanaweza kuwa magumu kiasi cha kwamba unaweza ukaanza kukata
tamaa. Na ugumu huu huwa wakati mwingine unakuja pale ambapo unajikuta wewe
binafsi unapokuwa unakabiliana na tatizo zaidi ya moja. Usipokuwa makini hapa,
huwa ni rahisi kwako kukata tamaa na kuacha kabisa kushughulikia hayo matatizo
yako. Ili ufanikiwe hutakiwi kukata tamaa, matatizo
hayawezi kuondoka mpaka wewe mwenyewe uyakabili. Fanya jitihada zako zote pale
unapoweza halafu jipongeze kwa hatua utakayopiga.
3. Acha kukata tamaa
kuweka wazi wazo na ndoto zako.
Utaweza kuweka wazi wazo
na ndoto zako kama utajijengea utaratibu wa kuwa na kijitabu kidogo ambacho
utakuwa unaweka malengo yako, hiyo itakupa nguvu ya kufatilia malengo yako kwa
ukaribu kabisa. Ukifanya hivyo hapo utakuwa unaweka wazi wazo na ndoto zako
kutekelezwa, hata kama ulifanya hivi mambo hayakukaa sawa, acha kukata tamaa
hii ni muhimu sana kwako. Ukifanya hivi katika maisha yako hii itakuwa na sawa
na kuzifuata fursa huko ziliko nazo zitakupokea kwa mikono miwili.
4. Acha kukata tamaa kujifunza kutokana na makosa.
Kama ulikuwa ukifanya hivi na umesahau na kukumbusha anza kujifunza tena
kutokana na makosa uliyoyafanya. Kama uliwahi kukosea na ukapata funzo fulani anza kulithamini
hilo funzo kwa kuchukua mafundisho yake na kuyafanyia kazi. Na ukiweza
kufanya hilo, utaona kumbe kukosea ni hatua moja wapo katika kupata mafanikio. Kwani
kuna uwezekano mkubwa kabisa kama usipotaka kujifunza kutokana na hilo
basi utakuwa unalikwepa daraja ambalo lingekuunganisha na mafanikio.
5. Acha kukata tamaa kuwekeza kwako mwenyewe.
Mara nyingi tumekuwa
tukitumia pesa kuwekeza katika miradi yetu, lakini tumekuwa tukisahasahau
kujiwekeza sisi wenyewe katika maisha yetu. Ili uwe na mafanikio makubwa ni
muhimu kwako kujiwekeza wewe kwa kujisomea kila siku. Unapochukua jukumu la
kujifunza kila siku kwa kujisomea vitabu na vitu vya mafanikio hapo unakuwa
unafanya uwekezaji mkubwa kwako mwenyewe. Pengine mwaka huu ilikuwa tabu kidogo
kwako kijisomea, mwaka 2015 fanya mabadiliko makubwa sana kwa kujisomea vitu
vingi vitakavyobadili maisha yako.
6. Acha kukata tamaa kuwa na watu sahihi.
Hawa ni watu ambao wewe
unapokuwa nao unafurahia, wanaokupenda, kukuthamini, na wanaokutia
moyo wa kutokata tamaa katika mambo yako. Hawa ni wale watu ambao ukikaa nao
wanakufanya ujihisi uko hai, ambao wanaokukumbatia wewe wa sasa hivi na
wanaotamani kumkumbatia yule unayetamani kuwa, bila masharti yoyote. Ni watu
ambao wanapenda kuona ndoto zako zikitimia, hivyo ni muhimu kuwa nao ili
kutimiza malengo yako.
7. Acha kukataa kuomba msaada wa kimawazo.
Kuna uwezekano mkubwa
ukawa umekatishwa tamaa na watu ambao umekuwa ukiwaomba msaada wa kimawazo,
pengine pale mambo yako yalipokuwa yakikwama. Na inawezekana walikushauri
vibaya na kukatisha tamaa na wewe ukafikiri kuwa kuomba ushauri kwa mtu kama ni
aina fulani ya udhaifu. Acha kukata tamaa kwa hili, kwa kawaida binadamu huwa
hatujui kila kitu, tafuta watu sahihi watakaokushauri katika mambo yako na hii
itakusaidia wewe kukupa nguvu kusonga
mbele hata kama kuna sehemu ulikuwa unahisi umekata tamaa.
8. Acha kukata tamaa kusamehe.
Migongano katika maisha
ya kila siku ni kitu ambacho mara nyingi huwa hakikwepeki. Na kila mmoja wetu
kwa sehemu amewahi kukosewa na mtu kwa namna yoyote ile. Kama hili limekutokea
katika maisha yako, jifunze kusamehe. Acha kujenga chuki, kisirani moyoni na
kuona kuwa haiwezekani kumsamehe. Hata kama mtu kakukosea mara ngapi acha
kukata tamaa kwake, msamehe na kisha chukua jukumu la kufanya mambo mengine.
Unaposamehe hii inakusaidia wewe kuishi maisha ya amani na utulivu ndani mwako.
Kwa kuchukua jukumu hilo la kutokukata tamaa kwa mambo hayo, mwaka 2015
utakuwa na mafanikio makubwa kwako na wala hutajuta. Chukua hatua muhimu kwa
kutafakari haya unapoenda kuanza mwaka mpya kwa siku ya kesho.
DIRA YA MAFANIKIO
inakutakia mafanikio mema na kheri ya mwaka mpya uwe wa Baraka na mafanikio
makubwa kwako, ansante kwa kuwa pamoja nasi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 0345/dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.