May 22, 2015
Unahitaji Kitu Hiki Cha Ziada Ili Uwe Na Mafanikio Makubwa Unayohitaji.
Daktari mmoja maarufu
sana duniani na hasa kwa nchi za joto kama kwetu, anaitwa Ronald Rose. Daktari huyu
alifanya utafiti mkubwa na wa miaka mingi kule nchini India kuhusiana na
malaria. Wakati anafanya utafiti huu mgumu, bila shaka kulikuwa hakujagunduliwa
hasa chanzo cha malaria. Kwa hiyo, unaweza kufikiria kuhusu mtu, ambaye anaanza
kutafuta chanzo cha tatizo akiwa hana msaada wa tafiti za kutosha za kabla. Bila
shaka ilikuwa ni kazi ngumu sana kwake.
Daktari huyu alifanyia
utafiti huu kwenye mazingira magumu sana ya kimaskini. Alikuwa akifanyia kazi
yake kwenye maabara ambayo mchana ilimlazimu lazima atumia pangaboi ili kujinga
na joto kali sana la India. Lakini pangaboi hilohilo likawa linapeperusha mbu
ambao alikuwa akiwatafiti. Basi, ikawa ni shida kubwa sana ya afanye kipi na
aache kipi. Hiyo haitoshi usiku kulikuwa na baridi sana na usumbufu mkubwa wa
mbu.
Najua utasema,
angejikinga kwa mbu kwa kufanya hivi au vile ni sawa. Utakuwa unasema hivyo kwa
kuzingatia zaidi mazingira ya siku hizi. Kwa wakati ule, mbu alikuwa
hajabainika kuwa adui wa maradhi na hivyo hakukuwa na njia rasmi za kujikinga
naye. Akiwa na matumaini ya kugundua na kuthibitisha kwamba, mbu ndiye
anayeeneza malaria, alifanya kazi kwa nguvu zake zote. Lakini hata baaada ya
kuwafanyia utafiti mbu kwa maelfu, alikuwa hajahisi hata kwamba, angeweza
kupata jibu.
Kila mbu alikuwa
anachukua zaidi ya saa mbili kufanyiwa utafiti. Kwa maelfu ya mbu, ilikuwa na
maana ya siku nyingi za kazi ngumu isiyolipa. Bado, alikuwa na haja ya kujaribu
tena na tena na siyo kwa sababu analipwa chochote, hapana. Alikuwa anafanya kwa
sababu, alitaka kufanya kilichomleta duniani, kugundua kitu kitakachosaidia
wengine. Kumbuka muda wowote kwake ungeonekana mrefu sana , kwa sababu ya shida
mbalimbali kama zilizotajwa.
Pamoja na shida zote
hizo, mbaya zaidi wahindi ambao ndiyo waliokuwa wanaathiriwa sana na mbu kuliko
watu wengine wowote duniani wakati ule, hawakuwa wema kwake. Walikuwa wakijazana
kumwangalia wakati akiwanyia utafiti mbu hao na walimbeza sana. Walikuwa wanamcheka,
wanamwita kichaa na wengine walisema ni mchawi. Hivyo, hata maisha yake
yalikuwa hatarini pia kutokana na mazingira ya kigeni aliyokuwa akifanyia kazi
hayakuwa rafiki kwake.
Hapa angeweza kusema, ‘nimtoka kwetu kuja kuchunguza kinachouwa watu
hawa, halafu wao wananibeza,’ halafu angenawa mikono nakurudi kwao ulaya. Hakufanya
hivyo, badala yake, aliwapuuza na kuendelea na utafiti wake. Lengo lake
halikuwa sifa, bali kuchangia kwenye maisha ya binadamu wengine. Aliendelea na
hatimaye alihisi kuanza kukata tamaa. Alifikia hatua hiyo, baada ya siku moja
kukamata aina mpya ya mbu nakujiambia, ‘huyu
atatoa jibu.’ Lakini kwa bahati mbaya, wala hakutoa kitu hata kinachokaribia
jibu.
Alipokosa kupata kile
alichotarajia kwenye mbu huyu, alijiinamia na kujiuliza, ni kwa nini
imeshindikana? Wakati anajiuliza hivyo, msaidizi wake alikuja na aina nyingine
ya mbu wapya. Dk. Ronald alitaka kumwambia msaidizi wake Yule awaachie mbu hao
waende zao, kwa sababu alijua mbu wote wapya wasingempa jibu, hakukuwa na jibu.
Lakini alibadili mawazo yake ghafla na kumwambia msaidizi wake ampe mbu wale.
Akiwa amechoka na kazi
nzito ya siku nyingi isiyo na majibu anayoyataka alianza kuwafanyia utafiti mbu
wale mmoja baada ya mwingine. Akiwa amebaki mbu mmoja, alikuwa hajapata jibu na
alijua angelazimika kufunga virago kurudi kwao, baada ya miaka mingi ya ‘kusota’.
Alimchukua mbu wa mwisho na kuanza kumfanyia utafiti. Halafu alishindwa
kuamini, mbu yule alitoa jibu alilokuwa amelitafuta kwa miaka mingi kwa shida
na mateso. Aligundua chanzo cha ugonjwa
wa malaria. Alimgundua maikrobu,
aliye mwenezi wa malaria.
Kupenda tunachofanya ni
sifa muhimu sana kwetu, kuliko ujuzi wetu au fedha zetu tulizonazo. Dk. Ronald alidhamiria na akasema, kuna siku
nitagundua, kuna siku nitapata jibu ninalotafuta. Alifanikiwa kupata jibu
kweli. Ndani ya kero, shida, kebehi na dharau, hatimaye ikawezekana. Lakini kubwa
la kujifunza ni hili. Mtu anapofika mahali anajikuta anaanza kukata tamaa kwenye
kile anachokifanya, inabidi ujue kwamba, huenda upo karibu kufikia mafanikio
unayoyataka.
Ni kama Dk. Ronald
alipokuwa amefikia mahali ambapo alikuwa amejiandaa kusema, ‘sasa kinachofuata ni kufunga virago.’ Lakini
kabla hajaweka chini vifaa jibu likaja. Hii yote inaonyesha ni kwa jinsi gani
hatutakiwi kukata tamaa hata mambo yawe magumu vipi kwetu, tunatakiwa kuwa
wavumilivu. Unaweza ukajikuta biashara uliyokuwa ukiitegemea kuwa italipa sana
haikupi faida uliyokuwa ukitaka hicho nacho ni kipindi cha kutokata tama kama
ambavyo Dk. Ronald hakuweza kukata tamaa.
Kwa kuwa umeamua kuwa
mjasiriamali kuwa na roho ya paka usikubali kufa au kushindwa kiurahisi, hata
watu wakutukane ama wakupigie kelele vipi, wewe ziba masikio kisha songa mbele
na amini kile unachofanya ndio kipo sahihi. Acha kuyumbishwa na kitu chochote
katika maisha yako kuwa na msimamo wako utakaousimamia. Kumbuka, usipokuwa na
msimamo juu ya maisha yako huwezi kufanikisha kitu utakuwa unayumbishwa tu kama
bendera.
Uwezo wa kutoka hapo
ulipo unao, jipe moyo, kuwa na subira na mvumilivu katika kipindi unachotafuta
mafanikio, zaidi penda kile unachokifanya hapo utakuwa upo kwenye mstari sahihi
wa mafanikio.
Nakutakia mafanikio
mema, karibu katika mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO uendelee kupata maarifa
bora yatakayokutoa kwenye umaskini, kwa pamoja tunaweza.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 0345/dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.