Jan 24, 2015
Hiki Ndicho Kitu Kinachokufanya Ushindwe Mara Kwa Mara Katika Maisha Yako.
Habari za leo ndugu msomaji
wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO, naamini umzima na unaendelea na jitihada
za kuboresha maisha yako. Nakukaribisha tena kwa moyo mkunjufu katika makala
hii ya leo ambayo ipo kwenye mfumo wa simulizi ambapo kupitia simulizi hii
utajifunza vitu vya muhimu vinavyohusiana na maisha yetu kwa ujumla ya mafanikio
tunayotafuta kila siku. Kupitia simulizi hii utajifunza na kutambua mambo
muhimu ambayo unatakiwa uyafanye na yatakayokuletea mabadiliko makubwa sana
katika maisha yako.
Wakati fulani, mtu mmoja
alinisimulia kisa ambacho kilinifundisha ukweli mkubwa zaidi kuhusu maisha. Mtu
Yule alinisimulia kuwa kulikuwa na bwana mmoja ambaye alienda kwa kinyozi.
Wakati anaendelea kunyolewa kulizuka mjadala wa masuala mbalimbali . Mjadala
huo, hatimaye ulifika mahali ambapo kinyozi na mteja walijikuta wakijadili
masuala ya Mungu. Kinyozi alisema, ‘mimi
naamini kabisa hakuna Mungu.’ Yule mteja( Yaani Yule bwana anayenyolewa)
alimuuliza, ‘ni kwa nini unaamini kwamba,
hakuna Mungu?’
Kinyozi kwa kujiamini kabisa
alisema, ‘naamini hivyo kwa sababu, ukienda hapo mtaani hata sasa hivi
utathibitisha. Kuna mateso kibao utayaona. Naamini, kama Mungu angekuwepo
kusingekuwa na watu wanaoumwa, watu maskini kila mahali, watu wanaouawa bila
sababu na uovu ambao umejaa hivi sasa duniani.’ Yule mteja hakuwa anataka
kubishana kuhusu masuala ya Mungu, hivyo aliamua kunyamaza. Kinyozi alimnyoa na
kumaliza kazi yake, ambapo mteja alitoka nje.
Yule mteja alipofika nje
alimwona mtu mmoja ambaye alikuwa na nywele chafu na ndevu nyingi zinazofanana
na ukoka kwa uchafu. Kuona vile, Yule mteja alirudi hadi pale kwa kinyozi na
alipoingia tu ndani alimwambia, ‘ naamini hakuna vinyozi’. Yule kinyozi
alimtazama mteja wake kwa wasiwasi, kabla hajamwambia, ‘hakuna vinyozi wakati
mimi unaniona hapa, na nimemaliza mara hii tu kukunyoa?’ Yule mteja alimwambia,
‘kama ingekuwa kuna vinyozi, kusingekuwa na watu wenye nywele ndefu na chafu
huko mtaani.’
Yule kinyozi kwa kujiamini
kabisa kwamba, ameshinda, alisema, ‘ sasa kama ni kunyolewa si hadi waje hapa
ofisini, wanifuate, ndiyo watahudumiwa….’ Yule mteja alimwambia, ‘basi Mungu
pia yupo, bali ni hadi wenye shida na matatizo wamfuate na kumjua na kumkubali,
ndipo ambapo watapata ahueni kupitia kwake.’ Halafu alitoka nje na kuendelea na
shughuli zake.
Ndivyo ilivyo, watu wengi
huwa wanadhani kitu au jambo fulani halipo kwa sababu tu hawajui jambo au kitu
hicho kinavyofanya kazi. Siyo lazima Mungu, kila kitu kina kanuni ya namna
kinavyoweza kujidhihirisha katika hali halisi. Utakuta mtu anakwambia,
haiwezekani kufanikiwa kama hujasoma, haiwezekani kufanikiwa kama huna refa,
haiwezekani kufanikiwa kama huna au hujafanya kile na kile. Lakini, kati ya hao
wanaosema, hakuna hata mmoja ambaye amefanya au amethibitisha nadharia yake.
Ni kwa kuona tu watu wakiwa
na shida njiani, wanaamini kwamba ni majibu kwamba Mungu hayupo. Kwa kuona
maskini wengi hawana hela wala mali, wanaamini kwamba, hiyo ni dalili ya
kutokuwezekana. Kama ilivyo kwa Mungu, hata mafanikio yoyote yale ni lazima mtu
ayafuate kule yaliko. Kwa kuyafuata mtu atakutana nayo, kwa kunyoosha miguu tu,
ni kweli hatayapata. Kila kitu hapa chini ya jua kinakwenda kwa kanuni, tofauti
na watu wengi wanavyofikiri na kudhani.
Kwa hiyo, kama mtu
anataka kujua kitu fulani kipo au hapana, inabidi ajifunze kanuni zake. Ni
hatari sana kusema haiwezekani kufanikiwa kwa kuwa wewe u maskini au umeshindwa
kuyafikia mafanikio unayoyataka, haiwezekani kwa sababu njia zimezibwa. Ni
hatari kwa sababu, anachokiona mtu mara nyingi ni umbumbumbu wake au udhaifu
wake. Fumbua macho sasa! Ubadili maisha yako kabisa. Achana na fikra za kudhani
haiwezekani, tafuta njia kwanini hufanikiwi na kisha songa mbele. Kama utakuwa
mtu wa hivi tu, mtu wa kufikiria hufanikiwi kwa sababu zako binafsi zisizo na
maana, basi utakuwa umeng’ang’ania kitu kinachozuia mafanikio yako na hiki
ndicho kitu kinachokufanya ushindwe mara kwa mara katika maisha yako.
Nakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa
kupata maarifa bora, yakayokuwa msaada mkubwa kwa maisha yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 035/dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.