Jan 21, 2015
Tabia 8 Muhimu Unazotakiwa Kuwa Nazo, Ili Kujenga Maisha Ya Mafanikio Makubwa.
Ni ukweli usiofichika ili
uweze kubadili maisha yako na kuwa ya mafanikio ya kiwango cha juu ni lazima
ubadili tabia zako ulizonazo sasa na kuwa na tabia ambazo zitakuongoza kufikia
mafanikio mkubwa zaidi. Unaweza usilione hili mapema lakini huu ndio ukweli,
linapokuja suala la kutafuta mafanikio vipo vitu vingi unavyotakiwa kuvifanya
na kubadili kama vile matumizi mabaya ya muda na pesa, lakini likiwemo na suala
la kubadili tabia ulizonazo ambazo zimekufikisha hapo ulipo. (Unaweza ukasoma pia Kama Unataka Kufanikiwa Na Kuwa Tajiri, Acha Tabia Hizi)
Unapobadili baadhi ya tabia
zako unakuwa unajiweka kwenye mstari wa kufikia mafanikio yako uliyojiwekea.
Kumbuka, mafanikio yanajegwa na na tabia ulizonazo, kwa kadri unavyokuwa na
tabia za aina fulani, ndivyo mafanikio yanakuwa upande wako na kwa jinsi
unavyokuwa na tabia za aina fulani pia utajikuta ndivyo unavyofukuza mafanikio
katika maisha yako bila ya wewe kujijua. Ili kujenga maisha ya mafanikio
makubwa unayohitaji, hakikisha unakuwa na tabia hizi katika masha yako.
1. Tabia
ya kuamka asubuhi na mapema.
Unapoamka asubuhi na mapema
kabla ya muda uliojiwekea, kabla ya watu
wengine, unakuwa unapata muda wa kutuliza akili yako, kujisikiliza wewe
mwenyewe na kupata nafasi ya kutafakari juu ya maisha yako kwa ujumla. Pia kwa kuamka asubuhi na mapema sio tu
itakusaidia kukupa muda wa ziada wa kutafakari juu ya maisha, hiyo itakusaidia
pia kukujengea tabia muhimu ya kupangilia siku yako mapema, wapi uanzie na wapi
uishie, ambapo tabia hii itakuongoza kwenye mafanikio. Watu wengi wenye
mafanikio wana tabia hii muhimu ambayo inawafanya wazidi kufanikiwa. Ni tabia
ambayo unaweza hata wewe kuwa nayo ili ikuletee mafanikio mkubwa.
2.
Tabia ya kuilisha akili yako kila mara.
Mara nyingi maisha yetu kwa
wengi huwa yametawaliwa na kula vyakula vya kila aina, hilo unalijua. Lakini
kuna kitu muhimu ambacho huwa haukilishi na kukisahau mara kwa mara. Kitu hiki
sio kingine ni akili yako. Kama ambavyo mwili wako unahitaji kula kila siku pia hata akili yako inahitaji kulishwa tena sana
kila siku. Unahitaji kuilisha akili yako kwa kujisomea kila siku na hili ndilo
hitaji la msingi unalotakiwa kuwa nalo ili uweze kufanikiwa. Usiache siku
ikapita bila kwako kujifunza kitu kitakachobadili maisha yako. Tumia muda wako
vizuri jifunze hata kwa dakika 20 au 30 kwa siku, baada ya muda utaona
mabadiliko makubwa katika maisha yako. Hii ni tabia muhimu sana kwako ambayo
hutakiwi kuiacha ili kujenga mafanikio ya kudumu.
3.
Tabia ya kufanya mazoezi kila siku.
Hata kama ni kwa dakika kumi
na tano tu, unahitajika kujiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi kila siku. Ili
uweze kufikia mafanikio makubwa unayotaka, kumbuka unatakiwa kuwa na akili safi
ndani ya mwili wenye afya ya kutosha. Unapojenga tabia ya kufanya mazoezi
unakuwa unaifanya akili yako iwe nzuri kiafya na kujikuta ukifikiri vizuri
zaidi. Isitoshe mazoezi yanakusaidia
wewe kupunguza magonjwa hususani ya moyo na mengineyo mengi ambayo
ungeyaweza kuyapata kizembe, kama ungekaa tu bila kufanya mazoezi ya aina
yoyote ile, hivyo ni kitu kizuri kwa mafanikio yako unayoyahitaji.
4.
Tabia ya kutekeleza mipango yako mapema.
Kuweza kuifanya siku yako
iwe ya mafanikio, ni muhimu sana kwako kujiwekea utaratibu wa kupanga mambo
yako mapema ikiwezekana siku moja kabla ili kuepuka kuingiliana kwa mambo
ambako kunaweza kukwamisha katika mipango yako uliyojiwekea. Utaweza kufanya hivi
kwa kuwa na ratiba yako ndogo ambayo itakuonyesha kwa uzuri ni nini ufanye
katika siku husika inayofuata. Kuwa na utaratibu huu wa kujipangia mambo yako
mapema utakusaidia wewe kufanya mambo yako kwa ufanisi na utalaam zaidi. Ukiwa
na tabia hii, itakusaidia sana kufanikisha mipango yako mingi uliyojiwekea.
5.
Tabia ya kuzingatia mambo.
Haijalishi unakumbana na
changamoto za aina gani sasa, kitu kikubwa unachotakiwa nacho wewe ni kujifunza
kutenda kwa uzingativu mkubwa unapotenda mambo yako. Acha tabia ya kuairisha na
kusema ngoja nitafanya kesho, hii ni tabia ambayo itakukwamisha na kukurudisha
nyuma kila siku. Kama kuna jambo au kitu ambacho ulitakiwa kukamilisha leo leo
hata kama ni kidogo ni vizuri ukakamilisha leo ili kesho uingie kwenye jukumu
lingine tofauti. Ili uweze kujenga mafanikio, ni muhimu kwako kuwa na tabia ya
kuzingatia kila jambo unalolifanya na unatakiwa ulifanye kwa ufanisi mkubwa.
6.
Tabia ya kuangalia malengo yako upya.
Ni kweli unaweza ukawa una
mipango na malengo mazuri uliyojiwekea, lakini ni muhimu sana kwako kuwa na
tabia ya kuangalia au kukagua malengo yako mara kwa mara. Unapokuwa na tabia ya
kukagua malengo yako mara kwa mara, nakuyapitia tena tena na kuangalia wapi
ulipokosea na wapi ulipofikia inakuwa inakusaidia wewe kusonga mbele na kuyafanya malengo yako yazidi kuwa hai.
Hakikisha kila siku unatenga muda kidogo wa kuyapitia malengo yako upya. Hii ni
tabia muhimu sana mbayo unatakiwa kujijngea ili kuweza kufikia mafanikio
makubwa yaliyoko mbele yako.
7.
Tabia ya kujiamini zaidi.
Hii ni tabia ambayo muhimu
pia unayotakiwa kuwa nayo ili kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako. Kwa
kawaida linapokuja suala zima la kujiamini kwa wengine huwa ni shida kidogo.
Unaposhindwa kujiamini elewa kabisa kwako itakuwa ni ngumu kuweza kufikia
kiwango cha mafanikio unachotaka. Kwa nini inakuwa ngumu kufikia mafanikio
unayotaka? Hii ni kwa sababu kila kitu ambacho utakuwa unataka kufanya utakuwa unahisi
au unajiona kama vile huwezi, matokeo yake utajikuta utakuwa ni mtu wa
kushindwa katika mambo mengi hata kwa yale ambayo hukustahili.
8.Tabia
ya kufanya kazi kwa bidii.
Kufanya kazi kwa bidii, kuwa
king’ang’azi katika malengo yako ni nguzo muhimu sana ya kukufikisha kwenye
mafanikio makubwa katika maisha yako.
Ikiwa utaamua kujitoa mhanga na kufanya kazi zako kwa bidii zote na kujifunza
vitu muhimu kwa kile unachokifanya, elewa kabisa mafanikio makubwa ni yako.
Kama una nia ya kweli ya kutaka mafanikio makubwa, chukua jukumu la
kujibidiisha kwa shughuli zako zote unazozifanya. Matokeo na matunda makubwa
utayaona upande wako kadiri siku zitakavyokuwa zinaenda mbele. Hata ikifika
wakati huoni matokeo mazuri wewe weka bidii hupotezi kitu.
Kwa kawaida tabia zetu ndizo
zina nguvu ya kujenga ama kubomoa maisha yetu ya kila siku. Kama unataka maisha
ya mafanikio, hakikisha unajifunza kujenga tabia zitakazo kuongoza kwenye
mafanikio ya kweli na sio kukwamisha. Chukua hatua muhimu za kubadili na
kuboresha maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika
safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na
kuhamasika kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 035/dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.