Jan 30, 2015
Kama Unataka Kuwa Mtaalamu Katika Shughuli Unayofanya? Soma Hapa.
Si kila anayefanya shughuli fulani huwa na utaalamu nayo, wengine
wanaifanya kwa kuwa tu nafasi ilitokea ya kuifanya. Na hautachukua muda kumgundua
mtu anayefanya kazi zake kwa utaalamu, na yule anayebangaiza njaa tu, kwa
jinsi wanavyoenenda na tabia zao. Mara nyingi
waajiri na wateja hulalamika kuwa anayewafanyia
kazi hana utaalamu.
Yawezekana humalizi kazi vizuri, umemcheleweshea au hata
kumzungusha kwa muda mrefu bila taarifa sahihi. Si mara moja tunasikia
ni jinsi gani tunatakiwa kuwa wataalamu katika shughuli
tunazofanya. Kama unataka kupata mafanikio, kuchukuliwa kama mtu
makini, kuonekana una mchango kwa unaofanya nao shuguli zako, kuzifanya
kitaalamu ndio njia pekee ya kukufikisha huko.
Lakini tujiulize waajiri ama wateja
wanatafsiri gani juu ya utaalamu? Wengi wao watakuona mtaalamu ikiwa wewe: Unafika eneo la kazi
katika muda unaotakiwa; Unaifanya kazi uliyopewa vizuri; Unamaliza kazi kwa
wakati.
Unadhani kuna matukio mengine ambayo
unahisi ukiyafanya yatakuonyesha wewe si mtaalamu? Kuna matukio ukiwa
unayafanya yanakutafsiri moja kwa moja kuwa wewe si mtaalamu wa shughuli
unayofanya.
Kwa mfano ukiwa:- Unachelewesha kazi za watu, unahudhuria vikao
ukiwa haujajiandaa, unatumia muda mwingi kuongea umbea muda wa kazi, kuwavunjia
heshima wenzako, kuwasubirisha wateja
muda mrefu bila sababu za msingi, kuiba mawazo ya watu wengine kufanyia
shughuli zako bila kuwahusisha, na kuvunja ahadi zako mara kwa mara.
Hebu leo tuangalie njia kumi utakazoweza kutumia kuwa mtaalamu
katika shughuli yoyote unayofanya. Jitahidi kufanya shughuli zako kitaalamu na
watu waweze kukuamini, kukuheshimu, na kukuona una uwezo wa kipekee. Japo
mazingira ya kila kazi yanatofautiana lakini linapokuja suala la
utaalamu huwa na tafsiri moja dunia nzima.
Hebu tuangalie sifa za kuwa mtaalamu ni zipi:-
1. Umahiri.
Lazima uwe mahiri katika kile unachofanya, ukitumia ujuzi na
maarifa ya kutosha katika kazi yako ni lazima utaonekana mtaalamu na
watu. Ni muhimu kwako kujifunza hili ili kuweza kujenga uwezo mkubwa wa kufanya
kazi kwa ufanisi ambapo itakupelekea wewe moja kwa moja kuwa mtaalamu katika
kile unachokifanya. Na utakuwa mtaalamu kutokana kujifunza kwako mara kwa mara,
hivyo ni muhimu kuwa mahiri.
2. Zingatia muda:
Watu watakuwa wanakutegemea wewe ufike katika muda
unaotakiwa ili shughuli ziende na umalize kwa wakati. Sio kuendelea
kufanya shughuli zako kwa mazoea tu bila kujali muda, kwani hakuna anayependa
kumuamini na kumpa kazi mtu asiyemaliza kwa wakati. Kama utaendelea kuwa mtu
ambaye sio wa kutunza muda na unajidanganya kuwa eti unataka kuwa mahiri kwa kile
unachokifanya sahau katika maisha yako.
3. Uaminifu.
Unatakiwa kuwa muwazi wa shughuli zako, na wale
unaofanya ama unaowafanyia kazi nao wajue nini kinachoendelea. Ukianza
kujifanya mjanja mjanja, katika
shughuli unayofanya huku huwaweki wazi watu wengine hakuna
atakayekuona mtaalamu hata kidogo. Matokeo yake utajishushia heshima hasa pale
itakapobainika kuwa mambo yako hayaendi sawa kiaminifu zaidi.
4. Uadilifu.
Utaonekana mtaalamu ikiwa utakuwa unasimamia kanuni
za shughuli yako. Hakuna anayependa kumpa kazi mtu asiyejua kufuata kanuni
za kazi yake. Jifunze kufuata kanuni za kazi yako ili uwe mtaalamu uliyebobea
vinginevyo utajikuta unakuwa ni mtu wa kubabaisha katika eneo ulilopo. Zingatia
pia misingi ya maadili kati yako na wafanyakazi wenzako hilo ni jambo la
msingi.
5. Heshima.
Kama huna heshima kwa watu wengine unaofanya nao au
unaowafanyia shughuli basi hautaonekana mtaalamu hata kidogo. Ni muhimu
sana kwako kuchunga heshima kwa wafanyakazi wenzako hata kama umewazidi cheo ni
lazima uwe na heshima kwao. Kuwa na heshima tambua kuwa hiyo ni nguzo kubwa
wewe ya kuweza kukutambulisha kuwa wewe umebobea na ni mtaalamu katika kazi
yako na wala si mbabaishaji.
6. Ongeza ujuzi.
Tafuta ujuzi wa ziada, usiendelee kung'ang'ania ujuzi ule
ule kila siku. Toka nje ya yale unayoyafahamu ili kupata mengine
mapya kuongezea katika yale unayayafahamu ili kuboresha zaidi
utendaji. Kama utaendelea kung’ang’ania kuwa na ujuzi ule ule bila ya wewe
kutaka kubadilika na kujifunza kitu
kipya, elewa kabisa utakuwa unajipunguzia sifa za kuwa mtaalamu kwa kile
unachokifanya.
7. Mtazamo chanya.
Kama wewe kila siku unaangalia makosa tu bila kuwa na mtazamo
chanya juu ya shughuli unayofanya kuwa mtaalamu itakuwa ndoto kwako. Ni lazima
uwe na mtazamo chanya ili ujue nini cha kufanya kuliko kuangalia makosa tu kila
wakati ambapo hayo makosa yanaweza yakakupunguzia na kasi ya kufanya vitu
vingine vitakavyoweza kubadili mwelekeo wako na pengine kukufanya kuwa mtaalamu
zaidi.
8. Toa msaada:
Wasaidie wenzako unaofanya nao shughuli sio kwa kuwa wewe
unafahamu kitu fulani basi hutaki wenzako wafahamu. Waonyeshe jinsi
ya kufanya kazi vizuri pale unapoweza na wasikilize pale
wanapokuuliza maswali. Unapowasaidia wenzako ambao unakuwa unafanya nao
kazi hii inakufanya kila siku utajikuta unaongeza utaalamu wako katika maisha
yako.
9. Tenganisha matukio.
Usihusishe matukio ya nyumbani au mtaani na kazi, ukiwa
katika shughuli zako weka mawazo yako yote hapo. Utakuwa mtu wa ajabu
kufika eneo la kazi na kuanza kushughulikia masuala ya nyumbani huku
ukiacha kazi haziendi. Jifunze kufanya kazi
kwa uangalifu ili usije ukajikuta unaupoteza muda wako mwingi pasipo
kujijua hiyo inaweza ikawa ni hatari sana na itapunguza utaalamu wako.
10. Kuwa msikivu.
Kila mtu ana hitaji la kusikilizwa pale anapokuwa
na jambo la kusema,
Kwa hiyo wape watu nafasi ya kukuelezea yale wanayodhani
yatasaidia katika utendaji wa kazi. Acha kuwa king’ang’azi wa kutaka
mipango yako au mambo yako ndiyo yatekelezwe na kusahau usikivu unaotakiwa kuwa
nao hata wewe ili kuleta ushirikiano utakaoleta ufanisi hata kwako na kukufanya
kuwa mtaalamu zaidi.
Kila mmoja
wetu anapenda kupata mafanikio katika shuguhuli ile anayofanya, basi tuanze sasa kufanya kazi kitaalamu ili
tuweze kufikia yale tunayoyataka. Nakutakia mafanikio mema, karibu DIRA YA MAFANIKIO uendelee kujifunza na kuhamasika kila siku.
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 035/dirayamafanikio@gmail.com.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.