Mar 4, 2015
Acha kutumia Njia Hii Kutafuta Mafanikio, Itakukwamisha Tu.
Kuwa na mafanikio makubwa ni
ndoto ambayo karibu kila mmoja wetu anayo katika maisha yake. Umuhimu huu wa
kutafuta mafanikio unakuja, kutokana na wengi wetu kuwa wamechoshwa na maisha
ya kubahatisha ambayo wanayo kila siku. Hivyo, kwa sababu hiyo wengi hujikuta
wakifanya kila linalowezekana ili kufikia mafanikio hayo wanayoyahitaji ili
mradi tu wafanikiwe.
Hata hivyo wengi wengi wetu
huamua kusaka mafanikio kwa kutumia njia tunazojua na kuziamini sisi kuwa
zitatufikisha katika kilele cha mafanikio. Kwa bahati mbaya, wapo ambao hutumia
njia ambazo siyo sahihi kutafuta mafanikio na siku ya mwisho hujikuta wamekwama
na kuanza kulaumu. Kwa leo nataka nikuonyeshe njia moja tu, ambayo wengi wamekuwa
wakiiamini kwamba wakiitumia watapata mafanikio kwa urahisi.
Hii ni njia ambayo hata wewe
unaijua na pengine umeshawahi kuitumia, lakini ukiendelea kuing’angania ipo
siku itakurudisha nyuma sana mpaka utashangaa. Njia hii ni njia ya mkato, ni
njia ambayo inapendwa na wengi katika kutafuta mafanikio. Hapa wengi sana
wanaamini kupata mafanikio kwa njia rahisi na za mkato na mwisho wa siku
huishia wakipoteza hata kile kidogo walichonacho kwa sababu ya kutumia njia hii
kutafuta mafanikio.
Mara nyingi nchini kumewahi
kutokea michezo inayohusisha pesa ama upatu, ambapo watu walichukuliwa fedha
kiujanja ujanja kwa mamilioni. Ingekuwa
ni mara moja, mtu angeweza kusema jambo hilo lilikuwa ni bahati mbaya. Lakini
kutokea zaidi ya mara moja na katika mazingira ya wazi kabisa kwamba, ni wizi
wa mchana na bado watu wakashiriki, inaonesha ni kwa kiasi gani, watu wengi
wanapenda njia za mkato kufikia mafanikio.
Hii inaonekana kwenye Nyanja
zote za maisha, kuanzia kusoma, ajira, biashara, malezi, michezo na hata uongozi.
Mtu au watu wanatarajia mambo yaende na kujitengeneza yenyewe bila juhudi zao.
Kila mmoja anatarajia alale na kuamka asubuhi, mambo yakiwa yamebadilika
yenyewe na kuwa safi. Kitu ambacho ni ndoto na hakita kuja kutokea, ingawa ndio
wengi wanataka maisha yawe hivyo, hata kama hawasemi vitendo vinasema.
Ndiyo maana waganga wengi wa
asili ambao wanadai wanaweza kumfanya mtu kupendwa bila yeye kupenda, kupata
pesa bila kazi, kupanda cheo bila juhudi, kufaulu mtihani bila kusoma, wamejaa
na wanapata fedha nyingi sana kutokana na wajinga hawa wanaoamini katika njia
za mkato. Waganga hawa wamebaini kuwa kuna kufikiri kulikopogoka ambapo wengi
hawajiamini katika kujiletea mafanikio halisi.
Bila shaka, ipo idadi kubwa
ya watu wanaomini sana kutafuta mafanikio kwa njia ya mkato. Ni watu wanaoamini
hadi sasa kwamba, mafanikio yanaweza kuja bila ya mtu kufanyia kazi. Umefika
wakati sasa wa wewe kufundishwa, kubadilika na kujua kwamba, ni kwa juhudi na
maarifa yako pekee, utaweza kujinasua kutoka kwenye ujinga, umaskini na vikwazo
vingine vya kimaisha.
Ni vigumu sana kung’oa au
hata kukwangua ukoko ulio vichwani mwa watu wengi, kwamba yapo mafanikio bila
ya njia za mkato na pia zipo njia zinazoweza kuwatajirisha kuliko wanavyofikiri
sasa. Ni vigumu kwa sababu ukoko huo sio wa jana au juzi, bali ni wa miaka
mingi sana vichwani mwao, ambao unawakwamisha na wakati mwingine huweza kujiona
kama vile wanamikosi kumbe siyo.
Lakini kwa juhudi za pamoja
na hasa kutoka kwa wale ambao wanaamini katika nguvu alizonazo binadamu katika
kujikomboa kutoka kwenye lindi la umaskini, hilo linawezekana. Wenye ufahamu
huu wanapaswa kujua kwamba, wakimsaidia mtu mmoja kujua hilo hasa, yapo
mafanikio bila njia za mkato, watakuwa wamesaidia lundo la watu kujua ukweli
huu ambao utaleta mafanikio kwa jamii.
Ili kufanikisha hilo, bila
shaka utahitaji mambo ambayo yatakufundisha kitu kipya kuhusu maisha yako ya
kipato, misukosuko ya maisha, imani na mikabala mingine mingi ya kimaisha
ambayo itakupa nguvu ya kujiamini na kujua kuwa hata wewe unaweza kufanikiwa
bila kutumia mkato wala kubahatisha. Ni wazi unahitaji kuyajua haya yote kwa
uchambuzi wa kina, kutoka kwenye watu wenye ufahamu usio na shaka ndani.
Unatakiwa ukisoma jambo
likujenge siku hadi siku na sio likubomoe, hivyo, unahitaji vilivyo bora zaidi.
Sasa una nafasi ya kufanya hivyo kwa kuboresha maisha yako na wengine ikiwa tu
kila siku utatembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza. Mtandao huu upo kwa
ajili yako, na washirikishe wengine kujifunza Mambo mazuri yanayoendelea.
Nakutakia mafanikio mema,
endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 0345
- dirayamafanikio@gmail.com
- dirayamafanikio.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.