google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jul 23, 2015

Nguvu Kubwa 5 Za Mafanikio Ulizonazo Ndani Mwako.

No comments :
Habari za siku rafiki na mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO Kwa nguvu zake Mungu naamini umzima na unaendelea na harakati nzima za kuhakikisha maisha yako yanakuwa imara kufikia viwango vya juu vya mafanikio.
Karibu tena katika siku nyingi nzuri ambapo tunakuwa katika darasa huru la kuweza kujadili mambo muhimu ya kimafanikio. Leo katika makala yetu ya leo tutaangalia nguvu kubwa za kimafanikio ambazo binadamu kama binadamu huwa anazo ndani yake na zinapotumiwa kikamilifu huwa zinaleta matokeo makubwa ya kimafanikio kwa maisha ya mtu.
Hizi ni nguvu ambazo kila binadamu aliye chini ya jua huwa anazo ingawa kwa wengi inakuwa ni ngumu kuweza kuzijua. Ni nguvu hizihizi ambazo zinapotumika katika maisha ya wengine huweza kuleta maajabu na kuonekana maisha yao kama vile ya ajabu hivi kumbe ni matokeo ya nguvu ambazo hata wewe unaweza ukazitumia na kufanikiwa.
Ni nguvu ambazo huwa ni zaidi ya bomu la nyukilia zinapotumika kikamilifu. Na ni nguvu ambazo nataka hata wewe uweze kuzijua ili kuweza kujiweka katika nafasi nzuri yamafanikio. Ikumbukwe kuwa mara nyingi binadamu anapoambiwa kuwa ana nguvu nyingi za ziada kwa wengi huonekana ni kichekesho na huwa hawaamini kitu kama hicho.
Kwa pamoja napenda nikushirikishe nguvu hizi muhimu kwako ambazo ukizitumia kwa namna yoyote ile lazima uwe mshindi na uachane na maisha ya kulalamika ambayo umekuwa nayo sasa kwa muda mrefu. Je, unajua ni nguvu zipi hasa ambazo unazo ndani yako zenye uwezo wa kukufikisha kwenye mafanikio makubwa?
1. Nguvu ya Uzingativu.
Hii ni moja kati ya nguvu kubwa sana uliyonayo ndani mwako lakini inapotumiwa huwa ina uwezo mkubwa wa kukupa mafanikio unayoyataka. Mara nyingi unapokuwa unaweka nguvu kubwa ya mawazo katika kitu kimoja na kuamua kuachana na vitu vingine kabisa visivyoendana na kile unachokitafuta hapo ndipo unapokuwa unatumia nguvu ya uzingativu kwa usahihi zaidi.
Nguvu hizi za uzingativu unapozidi kuziweka katika jambo moja iwe malengo yako au kitu chochote kile ni lazima uweze kufanikisha jambo hilo hata iweje. Itakuwa ni ngumu sana kwako kuweza kushindwa kutokufanikiwa kama kweli utakuwa umeweka nguvu yako ya uzingativu  sehemu moja tu na kutoisambaza sehemu nyingine. Hii ni siri mojawapo nzuri ya kimafanikio kama utaitumia.
Unaweza ukalijua hili zaidi kwa kuangalia mfano wa kioo ambacho kisayansi kinafahamika kama lensi. Hiki ni kioo ambacho wengi tumewahi kukutana nacho tukiwa shuleni. Kioo hiki huwa kinatabia na sifa moja kubwa ya kuweza kukusanya mwanga au miale ya jua na kuweza kuiweka sehemu moja. Kama ilivyo kwa kioo hicho ndivyo ambavyo nguvu ya uzingativu inavyofanya kazi kwetu na kuleta matokeo chanya ikiwa itatumiwa vizuri.

2. Nguvu ya maamuzi.
Hii pia ni moja kati ya nguvu kubwa iliyondani mwako lakini kwa wengi pia huwa haijulikani. Kama ilivyo kwa nguvu ya uzingativu na jinsi ambavyo inavyofanya kazi, nayo pia nguvu hii huwa ina matokeo yake ambayo yanaweza kuwa hasi ama chanya kulingana na jinsi ambavyo ilivyotumika kila siku katika maisha yako.
Kumbuka maisha yako, yapo hivyo kutokana na nguvu ya mamuzi ambayo uliweza kuifanya katika kipindi cha nyuma. Kama uliweza kufanya maamuzi sahihi basi upo kwenye njia sahihi ya kuelekea mafanikio, lakini kama maamuzi yako yalikuwa mabovu ndivyo ambavyo na maisha yako yalivyo kutokana na maamuzi uliyofanya.
Haijalishi unapitia kwenye utata au ugumu wa maamuzi kiasi gani, lakini kitu kikubwa ambacho unatakiwa kukijua ni lazima uwe na maamuzi sahihi ambayo yatakusaidia kukupa mafanikio unayoyahitaji katika maisha yako. Kinyume cha hapo utakuwa ni mtu wa kupoteza muda wako bure kwani hutoweza kufikia mafanikio makubwa unayoyahitaji katika maisha.
3. Nguvu ya ung’ang’anizi.
Katika maisha yetu kuna wakati huwa tunakutana na vikwazo vingi sana ambavyo huwa vina uwezo mkubwa wa kuturudisha nyuma. Vikwazo hivi huwa tunauwezo wa kuviweza kuviepuka kwa kufanya kitu kimoja ambacho nacho ni kuweza kung’ang’ania mpaka kuhakikisha kuona matokeo tunayoyataka katika maisha yetu.
Kwa kung’angania jambo ambalo tunataka kulifanya ndivyo ambavyo huwa  tunajikuta tunatumia nguvu hii ambayo huwa tunayo ndani mwetu. Kumbuka huwezi kung’ang’ania kitu mpaka kuweza kuwa na msukumo fulani ndani yako. Msukumo huo ambao unakuwa unauhisi unachemka ndani mwako huo ndio nguvu mojawapo ya kimafanikio ambayo unakuwa nayo bila kujua.
Watu wengi ambao unaweza ukawaona wanashindwa katika maisha yao kwa namna moja au nyingine huwa ni watu ambao mara nyingi wameshindwa kutumia nguvu hii ambayo ipo ndani mwao. Kwa kawaida unaposhindwa kutumia nguvu hii ya kung’ang’ania changamoto kidogo tu ikijitokeza katika maisha ni lazima kwako uweze kushindwa hata ufanyanye nini.
4. Nguvu ya kufikiri kile unachokitaka.
Ili uweze kupata kile unachokihitaji hii ndiyo nguvu pekee unayotakiwa kuitumia. Nguvu hii ni nguvu ambayo huweza kufanya kazi kwa kuweka picha kwenye ubongo au akili yako yale mambo unayoyata tu. Kwa mfano kama unataka kujenga nyumba nzuri, picha ipi inayokujia kichwani mwako? bila shaka ni aina ya nyumba tofauti tofauti zinakuja kichwani mwako.
Picha hizo unazoziona hizo ndizo nguvu ya kufikiri kile unachokitaka. Nguvu hii wakati mwingine kitaalamu hufahamika kama ‘Power of imagination’. Hivyo unaona kabisa hata wewe unaposema nataka gari nzuri, kichwani mwako hayaji maneno G-A-R-I N-Z-U-R-I. kinachokuja ni picha za hizo gari za aina tofauti.
Kufikiri kile unachokitaka ni nguvu mojawapo muhimu ambayo binadamu anayo ndani yake na inauwezo mkubwa wa kumsaidia kufikia mafanikio yoyote anayotaka. Kwa vyovyote vile iwavyo katika maisha yako, jizoeze kuujaza ubongo wako picha ambazo unataka zikutokee. Kwa kufanya hivyo ni lazima uweze kufanikiwa.
5. Nguvu ya hamasa.
Hii ni nguvu ambayo huwa tunayo ndani yetu ambayo mara nyingi huweza kuipata kutokana na kuona wengine ambavyo wananya vizuri katika mambo yao ama wakati mwingine huwa tunaweza kuipata kupitia vitabu, mitandao ya kuhamasisha na kuelimisha kama huu wa DIRA YA MAFANIKIO na semina au warsha mbalimbali.
Jaribu kufikiri kidogo, bila haka unaweza ukawa shahidi mzuri wa hili hasa pale ambapo huwa unajisomea vitabu vya mafanikio. Kuna msukumo au nguvu fulani ambayo huwa unaipata kutoka ndani mwako, pengine kutokana na kile kilichoelezwa kuweza kukugusa zaidi katika maisha yako. Nguvu hiyo mbayo huwa unaipata hiyo ndiyo nguvu ya hamasa, ambayo ipo ndani mwako.
Kwa kumalizia makala hii, tambua kuwa binadamu kama binadamu anazo nguvu nyingi sana ndani yake ambazo akiweza kuzitumia zinaweza kumfanyia mambo makubwa na kumfikisha kwenye kilele cha mafanikio. Hizo ni baadhi tu ya nguvu tulizonazo ndani mwetu.
Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza zaidi.
Kama una maoni, maswali au ushauri karibu sana.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,


   





No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.