Jul 21, 2015
Kipaji Chako Ni Ajira Namba Moja.
Tunu
muhimu za mafanikio ambazo Mungu amewekeza ndani ya kila mtu ni vipawa/talanta.
Kwa bahati mbaya sana na pengine kutokujua umuhimu wa vipawa, watu wengi
hawatilii maanani vipaji walivyonavyo. Wengi wanaishi kwa kuiga maisha ya watu
wengine kana kwamba wao ni nakala ya wengine. Kipaji chako ni mtaji mkubwa kama
utaamua kukitumia vizuri ipasavyo. Kipaji chako ni fursa ya kufanikiwa
maishani. Ni daraja la maendeleo kwa binadamu yeyote yule.
Kipaji
ni umahiri wa kipekee aliouweka Mungu ndani ya akili ya mtu unaongoza usadifu
wa viungo na fikra zake kufanya jambo Fulani kwa upekee kabisa. Ni talanta
ambazo mtu anazo siyo kwa sababu kasomea bali ni ujuzi wa kuzaliwa nao, elimu
inakusaidia tu katika kumfanya atumie kipaji chake kwa ufanisi na kwa manufaa
zaidi. Kwa mfano, michezo mbalimbali, sanaa kama mziki, kuchora, kucheza mpira,
kuimba, kusanifu, kubuni program za kompyuta, mitandao, na wakati mwingine
kuchonga. Wapo watu ambao wana vipaji katika eneo mojawapo wanachotakiwa
kufanya ni kuvitumia vipaji vyao.
Watu
mashuhuri na wale waliofanikiwa sana ni wale waliotumia vipaji vyao vizuri.
Kuna mifano hai mingi kama Filbert Bayi wa Tanzania alitumia talanta yake ya
kukimbia mbio, wanamuziki kama vile Michael Jackson, Rose Muhando walitumia
sauti zao kufanikiwa. Na hata wachezaji maarufu wanatumia vipaji vyao kucheza
mipira na wanafanikiwa kuliko hata wasomi wenye shahada lukuki.
Wasanii
na wana michezo wengi ni miongoni mwa watu maarufu na matajri sana duniani,
japokuwa walio wengi hawana elimu kubwa kiasi cha kushangaza , walichofanya ni
kutumia vipawa vyao kama ipasavyo. Maana hata sukari iliyo katika chai bila
kukorogwa chai inaonekana haina sukari. Vivyo hivyo vipaji tunavyo, ili vifanye
kazi vizuri inabidi tuvikoroge.
Mungu
alituumba na vipaji na talanta nyingi tofauti ili tuvitumie kufanikiwa
maishani. Kila mtu ana talanta yake imejificha ndani ya umaizi wa akili yake.
Tunahitaji kuweza kuziibua talanta hizo
kule ziliko fichika, na kuzitumia huku tukibadili mitazamo na kasumba.
Huwa nasikitika sana kumsikia mtanzania anasimama kwenye chombo cha habari
akisema yeye ni maskini anahitaji msaada. Wakati huo kafunika talanta zake
kibindoni, na nyuma kaacha ardhi kubwa, misitu mingi na hata watoto wengi ambao
ni nguvu kazi muhimu katika kuchangia maendeleo.
Wapo
watanzania wanadiriki kusema kuwa “sisi tutaendelea kubaki maskini hivihivi” na
wengine wanadai umaskini wao ni mpango wa Mungu. Huu ni uongo na ni dhambi.
Mungu angetaka sisi tuwe maskini asingeweza kutupa ardhi kubwa, asingetupa mvua
nyingi na maji mengi, asingetupa samaki wengi, asingetupa ndege na wanyama
wengi wa mwituni. Asingutupa afya njema na nguvu. Mungu alitupatia vyote hivi ili
tuwe matajiri tuwasaidie na wale wanaoishi nchi zisizo na ardhi (mawe tu), nchi
zisizo na bahari, nchi zisizo na msitu, mto wala bwawa. Sisi siyo maskini
kamwe.
Na
kiongozi au mwanasiasa anayetamka Tanzania ni maskini(wakati yeye ni tajiri)
huyo ni mpotoshaji. Tusiwafundishe watoto wetu mtazamo hasi hata kama
tunachangamoto. Kuwa na matatizo ni sehemu ya changamoto za maisha, tunazipaswa
kuzikabili. Maana hakuna mtu au nchi inayojitosheleza. Ndio maana hata wao
walioendelea huko ulaya bado wanakuja kwetu kununua malighafi ili wakutumie
huko kwao.
Tena
nadhani hata walioita mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini(MKUKUTA)
walikosea sana. Ingefaa ukaitwa “mkakati wa kukuza uchumi na ustawi wa maisha
ya watu”. Kuutaja umaskini wakati tupo ndani ya utajiri mkubwa ni kujitafutia
laana ya kudumu .Maana kama tunakubali sisi ni maskini kamwe hatuwezi kuweka
mikakati ya maendeleo. Tunabaki na mikakati ya kimaskini.
Nafadhaishwa
na mtazamo unaotaka kuzoeleka hapa Tanzania miongoni mwa vijana kuwa mtu yeyote
akifanikiwa: kumiliki nyumba nzuri, shamba zuri lenye mavuno mengi, gari zuri,
kiwanda na hata kuwa na elimu nzuri anaitwa fisadi, yaani mwizi. Unakuta vijana
wenye nguvu wanapita makazi ya watu wenye nyumba nzuri wanasema “unayaona
mahekalu ya mafisadi” wakimaanisha kuwa kila nyumba nzuri, kiwanda kikubwa,
shamba kubwa ni la fisadi au mwizi. Kwao maendeleo ni wizi na siyo jitihada za
kazi. Hawa wamepotoka sana.
Umaskini
siyo mpango wa Mungu wala siyo ngozi ya kuzaliwa nayo isiyobadilika. Hata
vitabu vitakatifu kama vile bibilia na msahafa vimesema wazi kwamba umaskini
siyo mpango wa Mungu. Mungu anataka kila mtu aishi maisha mazuri yenye ustawi
huku akimpenda na kutii mwongozo wake. Kila binadamu anahitaji maisha bora. Kila
binadamu anahitaji kulala pazuri, kula vizuri, kusafri vizuri, afya bora,
kupata elimu bora, mazingira safi, kucheza pazuri na kufurahia maisha kwa
ujumla.
Watu
wanakuwa kwenye shida kama vile kuishi katika nyumba mbovu, na kula chakula
kibaya au kisichotosheleza siyo kwa sababu wao wanapenda, au kudhani kuwa
maskini ndiyo sifa ya uadilifu. La hasha ni kwa sababu hawana. Fikra za kuyaona
maendeleo yoyote ya mtu au kikundi cha watu ni ufisadi ni dalili kupoteza dira
na kukosa matumaini kuelekea ufukara wa kudumu na dhiki kuu.
Na
ukiona kijana mwenye nguvu anatamka kuwa hayo majumba ni ya mafisadi, fahamu
kuwa familia yake na jamii inayomzunguka iko msibani. Si tetei wizi ama ufisadi
na si sahihi kuwa mwizi au fisadi. Na ni dhambi hata kwa mungu wezi waadhibiwe
tena vikali.
Lakini,
pia sikubaliani na mtazamo kwamba kila anayefanikiwa ni mwizi au fisadi. Kuna
watanzania wengi tu ambao wanakesha, wanafikiri na kubuni mbinu za kufanikiwa
huku wakiongozwa na jitihada kubwa ya kufanya kazi na kuchangamkia fursa ndani
na nje ya nchi na kutumia pesa kwa kwa makini katka uwekezaji binafsi bila
ufujaji.
Hawatapanyi
mapato kwa starehe na kuulimbukia utandawazi. Kila senti yao inatumika kwa tija
na manufaa. Hawa wanastahili pongezi siyo kuitwa wezi. Kazi kubwa tliyonayo
hasa vijana ni kutambua vipaji vyetu na kuvitumia ipasavyo.Tpunguze kulalamika
tuongoze juhudi zetu katika ufanya kazi zaidi. Tutafanikiwa sana maishani.
§ MAKALA HII IMEANDIKWA NA MTEMI ZOMBWE,
DAR ES SALAAM.
§ MAWASILIANO 0713 000027
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.