Aug 29, 2021
Tumia Mambo Haya Vizuri, Utafanikiwa.
Kila wakati, unatakiwa kutumia kile ulichonacho kwa uhakika na vizuri kabisa. Acha kujidanganya kwamba unataka mafanikio makubwa wakati hata ile misingi ya kutengeneza mafanikio makubwa unaiharibu hovyo hovyo.
Haiwezekani eti unasema unataka mafanikio makubwa wakati unatumia muda, pesa na nguvu zako hovyo, ambapo vitu hivyo kwa pamoja vingekusaidia kufikia mafanikio makubwa kama ungevitumia vizuri na kwa busara.
Pesa unazozipata hazijiamulii zenyewe kwamba ‘sasa mimi pesa ninakwenda kununua kitu hiki au kile.’ Wewe ndie mwenye jukumu la kupanga pesa zako zitumike wapi na kwa sababu ipi.
Sasa kama hiyo iko hivyo, kwa nini unafanya maamuzi mabovu ambayo yanakupotezea pesa nyingi na kwa kiasi kikubwa? Kuwa makini sana na matendo yako ili yasikupotezee pesa ambayo ni moja rasilimali muhimu kukusaidia kufanikiwa.
Hapo ulipo najua una pesa za kiasi fulani hata kama ni ndogo, najua una muda na nguvu fulani, sasa kwa nini hivi vitu usivitumie kwa uangalifu ili viweze kukusaidia kukupa mafanikio makubwa na badala ya kuvipoteza tu kiholela.
Watu matajiri, wanajua namna ya kutunza pesa zao vizuri, kwa nini wewe usiwe miongoni mwao? Huna pesa si kwa sababu pesa zinakukimbia bali ni kutokana na matendo yako yanayofukuza pesa.
Kitu cha kufanya jiulize, ni hatua zipi utaweza kuzichukua ili kuweza kulinda rasilimali zako za kukusaidia kufanikiwa ambazo ni pesa, muda na nguvu zako. Kama hujui tafuta watu wenye mafanikio kisha wafatilie.
ukiwafatilia watu hao utajua ni kwa jinsi gani wanavyotunza pesa zao, muda wao na nguvu zao za kuwawezesha kufanikiwa. Kaa ukijua ukitumia mambo hayo vizuri, utake au usitake yatakusaidia kufanikiwa.
Kila la kheri katika kufikia mafanikio yako.
Kama unapenda kujiunga na kundi la mafanikio ili uweze kujifunza zaidi mambo mengi ya kimafanikio. Tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER'S kwenda 0687449428 na utapewa utaratibu wa kuunganishwa.
Hakimiliki©2021 Imani Ngwangwalu. Haki zote zimehifadhiwa. Makala hizi hutolewa kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Ruksa 'kushare' na usibadili kitu chochote bila ya ruhusa ya mwandishi.
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.