Dec 7, 2018
Haya Ndiyo Mambo Matano Yanayofanya Maisha Yako Kuwa Magumu Kila Siku.
Mara nyingi kwa watu wenye umri mkubwa huwa
tunafikiri kwamba, tulipokuwa wadogo maisha yalikuwa rahisi, si
ndiyo? Na sasa tunaona mambo yamebadilika na kuna ugumu umeingia
katika maisha yetu ya kila siku. Naomba nikwambie kwamba,
maisha bado yapo rahisi vile vile kama tulivyokuwa tunayaona utotoni na kila
siku yataendelea kuwa hivyo milele. Tofauti iliyopo ni kuwa tumeongezeka umri na hata maumbo yetu yamebadilika, na
jinsi tunavyoongezeka umri ndivyo tunavyozidi kuyafanya yawe magumu.
Tulipokuwa wadogo kila kitu tulikangalia katika mtazamo wa
matumaini. Tulikuwa tunajua tunachohitaji na hatukuwaza tofauti juu ya mahitaji
yetu kama tunaweza kukosa kitu tunachohitaji. Tuliwapenda watu
waliokuwa wanatuonyesha tabasamu. Tuliwakimbia waliotuonyesha nyuso za
kisirani. Tulikuwa tunakula pale tunaposikia njaa, na kunywa pale tuliposikia
kiu na kulala tulipojisikia kuchoka.
Sasa tunavyozidi kuishi sana mawazo na akili zetu
zinatawaliwa na hisia hasi juu ya mahitaji yetu katika maisha kutoka katika
nguvu za nje.
Kwa namna moja ama nyingine tunaanza kusita na kuhoji nafsi zetu
juu ya mahitaji yetu. Pale kikwazo kipya au maumivu
yanapotufika tunaanguka na kukata tamaa. Jambo hili linatutokea
mara kwa mara katika maisha yetu, na mara kadhaa tumeshajiapiza kuwa hatutaki
kuanguka tena kama ilivyotokea mwanzo bila kutafuta ufumbuzi wa jambo
lililosababisha kuanguka tunaishia kukwepa tatizo.
Badala yake tunatumia vitu kama chakula na pombe kutibu
majeraha yetu na kujaza mapengo ya furaha zetu.
Wengi wetu tunafanya kazi masaa mengi mpaka usiku wa manane,
tukikimbia utatuzi wa tatizo lililotokea katika familia zetu iwe na mke au
watoto. Tunatunza hasira na visasi mioyoni mwetu,
tunafanya utapeli na udanganyifu kwetu wenyewe na kwa wenzetu ili tu tusonge
mbele. Na pale mbinu zinaposhindwa kufanya kazi,
tunaanza kuishi juu ya uwezo wetu, tunatumia uongo kuficha uongo, na kula na
kunywa zaidi ili tu tuyafanye maisha yetu yawe na nafuu.
Katika mfumo huu wa maisha tu nazidi kuyafanya maisha yetu yawe
magumu zaidi na zaidi na tunaanza kupoteza muunganiko wa nafsi zetu halisi na
mahitaji yetu halisi katika maisha tunayoishi. Kama kwa utangulizi huu
umeshaanza kukuna kichwa na kujiuliza kama na wewe upo humo, hapa nakuletea
mambo ambayo ukianza au kuendeleza kuyafanya yatafanya maisha yako kuwa magumu
bila sababu za msingi, unajua mambo hayo ni yapi?
Haya
ndiyo mambo matano yanayofanya maisha
yako kuwa magumu kila siku:-
1. Unaangalia watu wengine kukupa majibu ya maswali
ambayo ungejijibu mwenyewe.
Wakati tulipokuwa wadogo, uwezo wetu wa kujiamulia mambo yetu
ulikuwa mdogo na wakubwa zetu walibeba hilo jukumu la kutuamulia kipi cha
kufikiri,
kipi ni chema na nini maana ya kufanikiwa. Sasa ushakua, hupaswi
kuendelea kuishi utegemezi wa fikra tena katika maisha yako. Kuwa huru
jivue gamba la utegemezi ili uanze kutumia ubongo wako katika kutoa majibu ya
maswali yanayokukabili kila siku katika maisha yako.
Anza kutegemea fikra zako, isikilize nafsi yako, vunja
kichuguu cha utegemezi nje ya mlango wako. Mpaka sasa unajua jambo gani ni
sahihi katika maisha yako.
Usiache wengine wakuamulie nini cha kuchagua kwani mwisho wa siku
wewe ndio mwathirika mkuu wa maamuzi yako. Pale utakapoacha kuishi kwa kadri ya
maelekezo ya watu wengine na ukaanza kuishi kwa kadri ya majibu yanayotoka
kichwani mwako utapata kile kitu unachohitaji katika maisha yako.
2. Unaruhusu watu wengine wakufanye ujione una hatia kwa namna
unavyoishi.
Ili mradi haumuumizi mtu kwa mambo unayofanya endelea kuishi kadri
upendavyo na katika njia unazoona zinakupa furaha wewe mwenyewe. Muda mwengine
tunapoteza mwelekeo pale tu tunapojaribu kuishi kwa kadri ya mtazamo wa watu
wengine, kujaribu kuishi matarajio yao na mambo yanayowafurahisha wao kwetu. Chukua
muda na anza kutafakari juu ya mfumo huo wa maisha.
Je, unafanya mambo unayoyaamini au sababu tu uwafurahishe wengine?
Anza kukumbuka matarajio yako mwenyewe ni yapi. Kuna maneno matatu
yanayopendwa kutumiwa kurahisisha tafsiri ya maisha: ishi, fanya na penda ili uwe na furaha katika maisha yako sababu
uhusiano waweza kufa muda wowote ila utaendelea kuishi na nafsi yako mpaka pale
maisha yako yatakapoishia.
3. Unaruhusu watu wabaya waharibu mazuri yako.
Hata siku moja usijikie hatia kuwaondoa watu wanaokurudisha
nyuma katika maisha yako. Haijalishi huyo mtu ni ndugu, mpenzi, mfanyakazi
mwenzako, mwanafunzi mwenzako, rafiki wa tangu utotoni au rafiki mpya. Hutakiwi
kuweka chumba kwa ajili ya watu wanaokuletea maumivu katika maisha yako au
wanaokufanya ujisikie mnyonge na mdogo. Labda kama watabadilisha namna yao
wanavyoishi na wewe ila kama haonyeshi kujali hisia zako na anaendelea kuvuka
mipaka katika maisha yako na kuendelea kukuumiza, fungua mlango watoke nje
hupaswi kuendelea kuwalea.
4. Unataka kushindana na kila mtu.
Ukitaka kushindana na kila mtu utakuwa mchungu kwa watu
wanaokuzunguka. Kwani utaanza kujitengenezea mazingira ya kutojifunza vitu
vipya na hata kurekebishwa pale panapohitaji marekebisho. Mtu anayetaka kuwa
bora hashindani na wengine ili awe bora bali anashindana kumzidi yeye wa
jana ili yeye wa leo awe bora kuliko wa jana. Na elewa
hili kuwa utakuwa bora kuliko
unavyodhani, ikiwa utaachana na hiyo tabia yako ya kushindana na watu wengine
katika maisha yako. Ukiendelea kushindana na wengine utakuwa unajiumiza
mwenyewe katika maisha yako.
5.Unang'ang'ania kuishi na makosa yaliyopita.
Ni jambo zuri sana unapojisamehe mwenyewe kutokana na makosa
uliyowahi kuyafanya siku za nyuma katika maisha yako. Unapaswa uanze kuyatumia
makosa yaliyopita kama funzo na ulitumie hilo kusonga mbele katika maisha yako.
Anza kutengeneza mutaskabali wako leo usiache historia ya nyuma iendelee
kukutafsiri wakati majira yamebadilika. Muda mwingine malipo mazuri yanayotoka
katika kujituma sio kile unachopata kwa muda huo bali kile kipya ulichojifunza
ndio faida zaidi. Usijidanganye kuwa maisha ya furaha ni yale yasiyo na shida,
si kweli hata kidogo bali maisha ya furaha ni kuona unavishinda vikwazo kila
vinapojitokeza na kusonga mbele.
Maisha ni
jinsi tunavyoyatafsiri sisi wenyewe, ikiwa
tutaamua kubadili mtazamo wa namna tunavyoyachukulia au jinsi watu wanavyotaka
tuyachukulie. Tunaweza kuyafikia malengo yetu. Hayo ndiyo mambo matano yanayofanya
maisha yako kuwa mgumu kila siku.
Nakutakia ushindi
katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa
kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 0345/dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.