Jan 10, 2015
Kama Unataka Kufanikiwa Na Kuwa Tajiri, Acha tabia Hizi.
Watu wengi mara nyingi
huwa wanafikiri kukosa mafanikio ni matokeo ya kukosa bahati au ni matokeo ya
mapungufu Fulani waliyonayo katika maisha yao, kitu ambacho siyo cha kweli.
Kutokana na kuwa na fikra hizi, huwazuia
wengi kufanikiwa na kujikuta ni watu wa kulaumu na kushindwa kujua nini
kinachowazuia wasiweze kufanikiwa wakati kila kitu cha kuwafanikisha wanacho.
Wengi hujikuta
wakitafuta vitu vingi vilivyo nje yao na kusahau kitu kimoja kikubwa kinachowazuia
mafanikio yao. Kitu hiki pekee kinachozuia sana mafanikio ya wengi ni tabia
tulizonazo. Wengi wamekwama na kushindwa kuendelea sio kwa sababu hawana mtaji
wala akili ni kwa sababu ya tabia zao. Tabia ni kikwazo kikubwa cha maendeleo
ya mtu binafsi kuliko unavyofikiri.
Kama
Unataka Kufanikiwa Na Kuwa Tajiri, Acha tabia Hizi:-
1. Acha
tabia ya kuahirisha mambo.
Kama kuna jambo au kitu
unachotakiwa kukifanya leoleo ni vizuri ukafanya kuliko kukiacha na kutegemea
utafanya kesho. Wakati wa kubadili maisha yako upo sasa na wala si kesho kama
unavyofikiri. Hiyo kesho unayoisubiri haitafika na wala hakuna kesho kama
unavyofikiri. Ni mara ngapi umesema utafanya kitu hiki kesho na hukufanya? Hii
ni moja ya tabia inayokuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa unayoyataka.
Unataka kuwa tajiri achana na tabia hii kwanza.
2. Acha
tabia ya kufikiria sana makosa uliyoyafanya.
Wengi wanakuwa
wanashindwa kusonga mbele kutokana na kufikiria sana makosa waliyoyafanya siku
za nyuma. Kama kuna sehemu ulikosea, hiyo imeshapita chukua hatua sasa za
kusonga mbele. Acha kuumia na kung’ang’ania kufikiri pale ulipokosea, hiyo
haitakusaidia sana zaidi ya kukurudisha nyuma. Kama ambavyo nimekuwa nikisema
mara kwa mara kukosea ni sehemu ya maisha ya binadamu, kitu cha msingi jifunze
kutokana na hayo makosa.
3. Acha
tabia ya kuongelea sana ndoto zako.
Watu wengi sana ni
waongeaji juu ya ndoto zao lakini sio watendaji. Kama ni kuongea umeongea sana
juu ya ndoto zako, umefika sasa wakati wa kufanya mambo yako kwa vitendo. Jifunze kuchukua hatua dhidi ya
ndoto zako kila siku, hata kama ni kwa kidogo kidogo utasogea, mwisho utajikuta
unafanikisha kile unachokitaka. Hii ni tabia ambayo imekuwa ikiwakwamisha wengi
kutokana na kuongea sana. Unataka mabadiliko achana na tabia hii.
4.
Acha tabia ya kutokujiwekea akiba.
Hii ni tabia ambayo
ukiiendeleza katika maisha yako kutojiwekea kipato itakuwa ni ngumu sana kwako
kufanikiwa. Unaposhindwa kujiwekea kipato katika pesa unayoipata
kitakachokutokea katika maisha yako, utashindwa kumudu kupata pesa ya
kuendeshea miradi yako na mwisho wa siku utakuwa ni mtu wa kulalamika tu. Kama
unataka kuwa tajiri na kuwa huru kifedha anza kujifunza kujiwekea akiba, hii
itakusaidia sana kusonga mbele katika mambo yako mengi.
5.
Acha kutumia pesa zako hovyo.
Watu wengi huwa ni
watumiaji vibaya wa pesa zao hasa pale wanapozipata. Unapotumia pesa zako hovyo
hiyo hupelekea kuweza kukosa pesa ambayo ungeweza kuipata kama akiba yako ya
baadae. Mtumizi mabaya ya pesa, ni moja ya tabia kama tabia zingine, lakini
ambayo inakukwamisha kwa kiasi kikubwa kufikia ndoto na malengo yako makubwa
uliyojiwekea. Ili uweze kusonga mbele na kuachana na majuto uliyonayo jifunze
kutunza pesa zako vizuri, utafanikiwa.
6.
Acha tabia ya kuwa na madeni mengi.
Unapokuwa na madeni
mengi hiyo itakusababishia badala ya kuendelea mbele utakuwa unarudi nyuma.
Acha kulimbikiza madeni ambayo kwako yanakuwa mzigo kwako. Kabla hujakopa
chukua hatua muhimu ya kujiuliza je, kuna ulazima wa kukopa hiyo pesa? Madeni
ni kitu ambacho kimekuwa kinawarudisha wengi nyuma bila kujua, kutokana na kuwa
na elimu ndogo inayohusiana na madeni. Unataka kuwa na mafanikio, iache tabia
hii mara moja.
7.
Acha tabia ya kusubiri sana kutekeleza ndoto zako.
Hakuna muda sahihi
ambao upo wa kuanza kutekeleza ndoto zako kama unavyofikiri. Muda wa mafanikio
na kufanya ndoto zako kuwa za kweli ni sasa na wala si kesho. Acha kuwa na
tabia au fikra za kufikiri kuwa mipango yako mingi utaiyafanya siku nyingine,
hakuna kitu kama hicho. Hii ni tabia ambayo umekuwa nayo na inakukwamisha.
Unataka kutoka hapo ulipo anza kutekeleza mipango na malengo yako iliyojiwekea
mara moja.
Kama una nia ya kweli
kutaka kuleta mabadiliko makubwa katika maisha yako, anza kujiandaa kubadilika
wewe kwanza ikiwa ni pamoja na kubadili hizo tabia ulizonazo zinakukwamisha
sana. Kwa kadiri, utakavyoweza kumudu kubadili tabia zako kwa kiasi kikubwa,
ndivyo utakavyo jikuta maisha yako yanakuwa na mafanikio makubwa kuliko
unavyofikiri. Kumbuka hili, mafanikio yanajengwa na tabia tulizonazo.
Nakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa
kupata maarifa bora, yakayokuwa msaada mkubwa kwa maisha yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 035/dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Very impressive. Nimeipenda mmno
ReplyDelete