Feb 27, 2015
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutumia Muda Wako Vizuri Na Kukuletea Mafanikio Makubwa.
Muda ni mali! Huu
ni usemi maarufu sana kwa vijana na wazee. Unaonekana ni usemi wa kawaida na
uliozoeleka kwa watu wengi, maskini na matajiri, wanawake na wanaume. Japokuwa watu
wengi tunautumia usemi huu, lakini baadhi yetu hatuelewi maana yake na wengi
wetu hatuutumii katika maisha yetu.
Muda ni mali
maana yake kila kitu, vitu vyote vinavyoonekana vidogo na vikubwa ni matokeo ya
matumizi ya muda. Hata mimi na wewe ni matokeo ya matumizi mazuri ya muda. Kila
mafanikio yaliyowahi kutokea na yanayoendelea kutokea ni matokeo ya matumizi
mazuri ya muda. Kwa hiyo kuna uhusiano mkubwa sana kati ya mafanikio na
matumizi ya muda,yaani muda ukitumika vizuri mafanikio yanapatikana na muda huo
huo usipotumika vizuri hakuna mafanikio.
Hakuna haja ya
kueleza na kufafanua maana ya muda, ila nataka ujue kuwa kuna aina za muda, ndiyo
zipo aina mbili za muda. Aina ya kwanza ya muda ni MUDA WA SAA. Muda huu
unaanzia sekunde hadi mwaka. Katika muda wa saa, tunaposema miaka miwili ni
miaka miwili, haizidi wala haipungui.Tunaposema huyu ana miaka hamsini ina
maana mtu ameishi vipindi hamsini ambapo kila kipindi kina jumla ya miezi kumi
na mbili, haizidi wala haipungui.
Aina ya aili ya
muda ni MUDA HALISI. Muda halisi unaundwa na muda wa saa na matukio. Katika
aina hii ya muda tunaangalia matukio yaliyotokea katika muda wa saa
husika.Tunalinganisha idadi ya miaka na miezi na matukio au mafanikio
yaliyopatikana katika kipindi husika. Watu wanaweza kuwa sawa katika muda wa
saa lakini wakawa tofauti katika muda halisi. Mtu anaweza kuwa na umri wa miaka
sitini(katika muda wa saa) lakini akawa kwa mafanikio ni kama mtu aliyeishi
miaka thelathini tu.
Na pia mtu
mwingine anaweza kuwa na umri wa miaka thelathini, lakini akawa na mafanikio
makubwa sana kimaisha kama mtu aliyeishi miaka mingi sana duniani, yawezekana
hata miaka sabini. Usichanganyikiwe, nalinganisha muda wa saa na mafanikio. Muda
halisi unatuambia kwamba kuna kuchelewa katika maisha. Muda halisi
unatukumbusha kuwa kuna wakati tunaweza kupoteza miaka yetu bila kujua. Unatukumbusha
kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi.
Tumejifunza aina za muda na tofauti
zake, sasa tuangalie matumizi ya muda wa
saa.Tunatumia muda huu kufanya mambo
matatu ambayo yanatuleta kwenye muda halisi, tukiwa tumewahi au
tumechelewa tunatumia muda katika kufikiri, kusema au kuzungumza na kufanya
mambo mbalimbali katika maisha yetu.
Baada ya
kuangalia matumizi ya muda wa saa, tumegundua kuwa tunautumia muda kama chombo
kutusafirisha kutoka katika ulimwengu wa namba na mahesabu kwenda kwenye
ulimwengu wa halisi,ulimwengu wa vitendo ambapo tunaweza kufanya tathmini na
kuona kuwa tumewahi au tumechelewa, tuko nyuma au tuko
mahali sahihi.
Sasa tuangalie
mambo ya kufanya ili tuweze kuutumia muda wa saa na kufikia mafanikio ambayo yataweka
uwiano sawa kati ya muda wa saa na muda halisi katika maisha yetu.Yapo mambo
mengi ambayo unapaswa kuyafanya ili uweze kutumia muda wako vizuri, baadhi ya mambo hayo ni haya yafuatayo:-
1. Weka kumbukumbu ya mambo unayofikiria, unayoyasema na kutenda.
Kumbukumbu ni
muhimu sana katika maisha ya binadamu kwa sababu ndizo zinazotusaidia kufanya
tathmini. Jitahidi kuweka kumbukumbu za mambo unayofikiri, unayosema na kutenda
japo kwa siku moja. Mwisho wa siku jitahidi kukukumbuka mambo uliyofikiria, uliyosema
na kutenda yawe mazuri au Mabaya. Hii itakusaidia kufanya tathmini ya matumizi
ya muda kwa siku hiyo.
Tathmini hiyo
itakusaidia pia kujua umetumia muda vizuri au vibaya. Mara nyingi sana siyo
rahisi kukukumbuka mambo yote uliyofikiria na kusema lakini ni rahisi
kukukumbuka matukio na mara nyingi matukio hutokana na kufikiri na kusema,kwa
hiyo kukumbuka matukio ni njia rahisi zaidi yakukuwezesha kufanya tathmini ya
siku nzima.
2. Weka ratiba ya siku nzima.
Ratiba ni muhimu
sana katika maisha ya kila siku.Usianze siku bila kujua utafanya nini siku
hiyo. Unaweza kuweka na kupanga ratiba ya siku inayofuata kabla ya kulala au
asubuhi kabla hujaanza jambo lolote. Watu wote waliofanikiwa, wamefanikiwa kwa
sababu ya matumizi mazuri ya muda, wanafanya kazi zao kwa ratiba na wana
nidhamu linapokuja swala la matumizi ya muda. Bila kuwa na ratiba muda hutumika
bila mpangilio na wakati mwingine muda hupotea bure. Unapoweka ratiba hakikisha
kila kitu ulichokiweka kina wakati na muda wake. Kinaanza saa ngapi na kuisha saa ngapi. Ni
vyema ratiba hii iwe na mambo ya msingi tu. Usisahau mapumziko. Mapumziko ni
muhimu kwa utendajibora wa akili na mwili.
3. Epuka kuwa na mipango mingi.
Katika ratiba
yako usiweke mambo mengi sana ambayo utekelezaji wake ni mgumu au
yanachosha.Weka mambo machache ambayo
yanakupa nafasi ya kupumzika na kutafakari namna ya kuianza siku inayofuata. Ukiweka
mambo mengi kuna hatari ya kuyatekeleza nusunusu na mengine yanaweza yasitekelezwe
kabisa.
4. Usiruhusu mambo yasiyo ya msingi kuingilia ratiba
yako.
Mara unapoanza
kutekeleza mipango ambayo iko kwenye ratiba yako, usiruhusu mambo yasiyo ya
msingi kuingilia na kuvuruga ratiba yako. Kuwa na nidhamu na heshimu ratiba
yako. Zipo dharura lakini si dharura zote
zinahitaji kushughulikiwa papo .Kama dharura ni ya msingi na inahitaji
kushughulikiwa papo hapo hamna tatizo.Jifunze kutambua na kutofautisha dharura
zinazohitaji kushughulikiwa papo hapo na zile zinazoweza kushughulikiwa baada
ya ratiba kukamilika.
Kuna watu ambao
wako tayari kuvuruga ratiba zao na kuacha shughuli zao kwa sababu ya mambo
yasiyo ya msingi kwa mfano kuangalia mechi na burudani zingine ambazo
haziwasaidii katika maisha yao. Narudia tena,uwe na nidhamu heshimu ratiba
yako.
5. Epuka kutumia muda mwingi kufanya mambo yasiyo ya
lazima na yasiyo na faida.
Epuka kutumia
muda mrefu kufanya mambo yasiyo ya msingi na yasiyo na faida kwa mfano kuchati
kwenye mitandao ya kijamii, kuangalia mechi na burudani zingine wakati ambapo
unatakiwa kufanya mambo ya msingi kwa ajili yako na jamii inayokuzunguka. Sina
maana mitandao ya kijamii mibaya ila nasisitiza kuwa na kiasi na kuipa nafasi
ndogo katika maisha ya kila siku. Kama
utakuwa unawasiliana kwenye mtandao
wa kijamii basi iwe kwa faida na si kupoteza muda.
Ninasema hivi kwa
sababu hili limekuwa tatizo Kubwa sana
kwa kizazi cha sasa hasa vijana, tena wanafunzi ambao wanatakiwa wasome kwa
bidii wasipoteze muda hata kidogo. Muda wa kufanya mambo ya msingi utumike
kufanya mambo ya msingi na mambo mengine yapewe nafasi ya pili au ya mwisho.
5. Tumia sehemu Kubwa ya muda wako kufanya mambo ya
msingi.
Unashauriwa
kutumia 75% hadi 80% ya muda wako kufanya mambo yenye tija kwako na kwa
wanaokutegemea.Tumia sehemu Kubwa ya muda wako kufanya mambo yatakayokujenga na
kukuimarisha kiakili,kijamii na kiuchumi. Fanya kazi za kukuingizia kipato, soma
vitabu, magazeti, na majarida yatakayokuongezea
maarifa na kupanua ufahamu wako.Ukiingia kwenye Internet soma vitu
vinavyokujenga na siyo kufuatilia habari za watu maarufu huku hakuna cha maana
unachopata.
Wengine wanaingia
kwenye Internet kuangalia ili kuangalia
picha za ngono na utupu. Watanzania wengi watu wazima ukiwauliza walisoma
vitabu lini, hawakumbuki, wengine wanakwambia shule ya msingi na wengine
sekondari, inasikitisha. Wengine
hata wanaponunua simu, hawasomi vile vitabu vinavyoelekeza namna ya kutumia
hiyo simu. Watu walio wengi sana kama ni kusoma wanapenda kusoma vitu ambavyo
haviwasaidii sana katika maisha yao kama magazeti ya udaku.
Nakutakia kila la
kheri, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora
yatakayoboresha maisha yako.
- Makala hii imeandikwa na Deogratius Harold wa Mbeya- Tanzania.
- Mawasiliano 0718 610 022
Feb 24, 2015
FEDHA: Sababu 7 Zinazokufanya Ushindwe Kuwa Na Pesa Zakutosha Katika Maisha Yako.
Katika maisha kuna wakati
unaweza ukawa unajiuliza na pengine kushangaa kwanini umekuwa ni mtu ambaye
huna pesa za kutosha wakati ukija kuchunguza maisha ya wanaokuzunguka ni watu
wenye pesa na maisha yao wanayaendesha vizuri tu. Inawezekana ukawa unafanya
kazi ama biashara nzuri inayokuingizia kipato cha kutosha lakini kutokana na
sababu usizozijua huwa ukijikuta ni mtu wa kuishiwa na kujikuta kuwa huna pesa.
Kama umekuwa ukiishi hivi na kuwa mtu wa kuishiwa na kushindwa kuwa na pesa za
kutosha , makala hii ni muhimu sana kwako. Je, unajua ni sababu zipi
zinakufanya ushindwe kuwa na pesa ya kutosha katika maisha yako?
Hizi
Ndizo Sababu 7 Zinazokufanya Ushindwe Kuwa Na Pesa Pesa Zakutosha Katika
Maisha Yako.
1. Una
tabia mbaya zinazokuzuia kupata pesa.
Kuwa na tabia mbaya
zinazokuzuia kupata pesa, ni sababu mojawapo ambayo inasababisha wewe ushindwe
kuwa na pesa za kutosha kukosha. Kama maisha yako yametawaliwa na tabia mbaya
kama matumizi mabaya ya pesa, ulevi na kuangalia TV kwa muda mrefu, hali ambayo
inakupelekea wewe kupoteza muda mwingi sana ambao ungekusaidia katika suala
zima la uzalishaji, sahau kuwa na pesa. Hii inatokea ni kwa sababu tabia zako
hizo zinakuwa hazikusaidii kukuzalishia zaidi ya kukufanya uzidi kuishiwa na
kujikuta kukosa pesa katika maisha yako, mara kwa mara.
2. Unazungukwa na watu wengi ambao sio sahihi kwako.
Ili tuweze kufanikiwa na
kuwa na mafanikio makubwa zaidi, tunahitaji kuwa na watu sahihi na
waliofanikiwa zaidi yetu ili kuweza kutupa hamasa ya mafanikio. Katika maisha
yako unapokuwa umezungukwa na watu wengi ambao ni hasi, hawaamini katika
utajiri na mafanikio, ni lazima wewe utaanza kuwa kama wao kidogo kidogo na
mwisho wa siku utajikuta umekuwa mtu ambaye na wewe unashindwa kuwa na pesa za
kutosha kama wao. Kuzungukwa na watu wengi ambao sio sahihi kwako hii ni sababu
mojawapo inayokusababisha wewe ushindwe kumudu kupata pesa.
3. Umekuwa mwongeaji sana bila kuchukua hatua.
Unapokuwa mwongeaji sana juu
ya ndoto zako bila kuchukua hatua yoyote uwe na uhakika ni lazima mifuko yako
iwe tupu, haina kitu. Watu wengi huwa ni waongeleaji wazuri sana wa ndoto na
malengo waliyonayo, lakini linapokuja suala la vitendo inakuwa hakuna. Kama
unatabia hii uwe na uhakika lazima pesa zitakupiga chenga, kwa sababu ndoto
bila vitendo ni kazi bure. Wapo watu wengi sana hapa duniani ambao walikufa na
kuzikwa na ndoto zao nzuri walizokuwa nazo bila kuzifanyia kazi. Jifunze
kufanyia kazi ndoto zako, ili ubadili maisha yako.
4. Umekuwa hauna mipango maalumu.
Ni kitu ambacho unatakiwa
ujiulize mara kwa mara katika maisha yako kuwa unataka kuwaje baada ya miaka
michache kuanzia sasa? Unataka kuwa kama ulivyo sasa kwa kutegemea kazi ya aina
moja? Ama una mipango gani mathubuti uliyojiwekea, ambayo itakusaidia uweze
kuweza kuongeza kipato chako? Tatizo la watu wengi ambalo huwa lina sababisha moja
kwa moja kuwa watu wa kushindwa kushindwa kupata pesa za kutosha katika maisha
yao, linatokana na kuwa watu wakukosa mipango maalum itakayowaongoza kwenye
uhuru wa kifedha.
5. Umekuwa ukikata tamaa mapema.
Kuwa na tabia ya kukata
tamaa mapema kwa kile unachofanya, hiki ni kitu kingine ambacho kimekuwa
kikikufanya uendelee kushindwa sana kupata pesa za kutosha katika maisha yako. Umekuwa
ukikosa pesa kwa sababu, unakuwa unaachia fursa nyingi ambazo zingeweza kukusaidia kukupatia kipato
cha kutosha. Kwa sababu ya kukata tamaa mapema unajikuta ukiwa ni mtu ambaye unapoteza
pesa nyingi, ambazo zingeweza kukusaidia katika maisha yako.
6.
Umekuwa ni mtu wa kupoteza muda sana.
Kama unaishi na unaendelea
kuishi maisha ya kupoteza muda katika maisha yako huwezi kufanikiwa kwa
chochote, zaidi utaendelea kuwa maskini. Watu wengi bila kujijua huwa ni watu
wa kupoteza muda sana katika mambo yasiyo ya msingi kama mitandao ya kijamii,
TV na mengineyo. Kwa kupoteza muda huko hushindwa kupangilia mambo ya msingi
ambayo yangeweza kuwasaidia kuingiza kipato na matokea yake husababisha kuwa ni
watu wa kushindwa kupata pesa. Kama unaishi maisha haya ya kutumia muda hovyo,
usilaumu kama utakuwa ni mtu wa kushindwa kupata pesa za kutosha katika maisha
yako.
7.
Umekuwa huna tabia ya kujiwekea akiba.
Hili ni kosa ambalo umekuwa
ukilifanya mara kwa mara, umekuwa ukitumia kiasi chote cha pesa na kujikuta
huna akiba hata kidogo. Kama maisha yako yako hivi, suala la kushindwa kupata
pesa nyingi kwako halitakiwa jambo la kushangaza. Unaposhindwa kuweka akiba
hata kiasi kidogo basi maisha yako utazidi kuyafanya kuwa magumu siku hadi
siku.
Unao uwezo wa kuishi maisha
yoyote ya kimafanikio kama utaamua kuwa hivyo kweli katika maisha yako. Kuwa na
fikra sahihi zitakazo kuongoza kwenye uhuru wa kifedha. Kwa kifupi, hizo ndizo
sababu zinazokufanya ushindwe kuwa na pesa ya kutosha katika maisha yako.
Nakutakia kila kheri,
endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku, kwa elimu na maarifa bora
yatakayoboresha maisha yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com
- dirayamafanikio.blogspot.com
Feb 20, 2015
Haya Ndiyo Maradhi Ya Utajiri Wa Ghafla. Soma Hapa Kujua Zaidi.
Siku hizi mazungumzo yanayohusu pesa, mali na utajiri kwa ujumla, yamekuwa ni jambo la msingi linalopewa kipaumbele na kila mtu katika jamii yetu. Ingawa, tamaa ya kutaka kujitajirisha kwa vyovyote vile, imejengeka na kujizatiti ndani ya mioyo ya watu kiasi cha kutufanya kuwa kama watumwa vile. Mwelekeo huu wa kupenda na kutamani sana utajiri, umewafanya baadhi ya watu wavuke mipaka ya maadili mema na kuutafuta utajiri huo kwa njia za mkato, zisizo halali.
Nakumbuka kuna jamaa yangu
mmoja kipindi cha nyuma kidogo, baada ya kumaliza shahada yake ya kwanza ya
biashara katika chuo kimojawapo hapa nchini, aliweza kubahatika kuajiriwa na
serikali katika idara moja iliyokuwa ikijihusisha na maduhuri ya serikali
kutoka kwa wafanyabishara wadogo na hata kwa wale wakubwa. Katika muda wa miaka
tu tokea aajiriwe, jamaa huyu aliweza kujitajirisha kwa kiwango kikubwa na cha kutisha sana.
Njia alizotumia katika
kujitajirisha kwake bado inabaki kuwa siri yake. Lakini kwawatu wenye kujua
kiwango chake cha mshahara na muda aliofanya kazi, hawakusita kusema kwamba,
utajiri huo ulipatikana kwa njia za mkato mkato, ikiwa ni pamoja na kuibia
serikali. Mara baada ya kuona kwamba ametajirika kiasi cha kuogofya, akawa sasa
hata mwenyewe anaonekana kutokuamini, kutokana na wingi wa pesa alizokuwa nazo.
Hivyo kutokana na hali hiyo, alianza kushitakiwa na dhamira yake.
Matokeo yake ni kwamba ,
alianza kuingiwa na hofu ya kuja kukamatwa na mwajiri wake. Hali hiyo iliendelea
kumsumbua kwa muda mrefu. Katika hali kama hii aliendelea kusumbuliwa na
maumivu makubwa ya kiakili na kihisia. Hivyo, ikawa kwamba, katika harakati za
jamaa huyu kuondokana na maumivu hayo, aliamua kutafuta mwavuli wa kumpa nafuu.
Ilibidi aanze ufujaji wa pesa hizo kwa kulewa kupita kiasi na ngono za hovyo.
Ilifika hatua ambapo jamaa
huyu akawa anashindana na mkewe katika kuzichota fedha hizo kutoka sehemu
walikokuwa wakizihifadhi ndani ya nyumba yao. Migogoro ya ugomvi kwenye ndoa
yake likawa ni jambo la kawaida. Vilevile jamaa huyu akawa anawaalika jamaa
zake aliomaliza nao masomo ya chuo kikuu, wakanywa na kufurahia maisha.
Alifanya hivyo, bila yeye
mwenyewe kujua kwamba, ilikuwa ni jitihada yake ya kutibu majeraha ya hisia
zake, kutokana na kushtakiwa na dhamira zake, kwa vitendo vyake vya ubadhirifu, rushwa na wizi wa
fedhaza ofisi yake. Hata hivyo, tiba hiyo haikufua dafu kwani hatimaye jamaa
huyu aliamua kuacha kazi yeye mwenyewe kwa hofu ya kudakwa na mwajiri wake.
Wataalamu wengi wa afya ya akili
wanadai kwamba mtu anapopata utajiri wa ghafla huwa ni ngumu sana kwake kuweza
kukabiliana nao huo utajiri wa ghafla. Wataalamu huweza kuongeza kuwa utajiri
huo huweza kusababisha familia kuvunjika na kuharibu kabisa maisha yao. Na
kwamba fedha hizo, zinakuwa haziwaletei tena amani, uraha na hata kuridhika
kama walivyokuwa wakifikiri mwanzo.
Vilevile kulingana na maoni
ya wataalamu mbalimbali wa masuala yahusuyo afya ya akili, wanaendelea kudai
kuwa watu wengi ambao hupata utajiri huu wa ghafla na wa kupindukia mara nyingi
huwa ni watu wa kuugua maradhi ambayo yamepewa jina la maradhi ya utajiri wa
ghafla, ambayo huwa yana dalili kama hizi:-
Kushtuka moyo sana, hofu za
ghafla na ya mara kwa mara, kukosa usingizi, kukosa amani na kuhisi kuwa na
hatia kwa sababu ya kuwa na pesa nyingi kupindukia ambazo tena ukiangalia sio
za halali. Pia, kuhisi kwamba hawastahili kuwa na pesa au utajiri mkubwa wa
kiasi hicho. Watu wengi wenye utajiri mkubwa na wa ghafla ndivyo walivyo na
wanaishi na maradhi ya utajiri wa ghafla, ingawa sio rahisi sana kubaini na
hawawezi pia kukwambia.
Hivyo, ni vizuri tukawa na
mtazamo chanya na unaofaa kuelekea kwenye utajiri tunaoutaka na kuumiliki baada ya kufanya kazi halali
tena pengine muda mrefu, ni sehemu tu ya jitihada za kujipatia mafanikio ya
kweli. Kwani mafanikio haya yanatutaka tuutumie utajiri huo vizuri. Kutumia
utajiri huo vizuri ni pamoja na kuutumia katika kuwatendea mema watu wengine,
kuutumia katika kazi na miradi mbalimbali ya kijamii.
Kwa kufanya hivyo, ni wazi
kabisa tutakuwa tumeigundua na kuipata siri au tiba itakayoweza kutusaidia
katika kuepukana na mashtaka hata hukumu itokanayo na utajiri wa haraka haraka.
Nakutakia kila la kheri,
endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kupata maarifa bora yatakayobadili maisha
yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com
- dirayamafanikio.blogspot.com
Feb 19, 2015
Hatua Tano Muhimu Za Kufikia Malengo Uliyojiwekea.
Habari ya leo mpenzi msomaji
wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Nimatumaini yangu ya kuwa umzima wa afya
na unaendelea vizuri na harakati za kuboresha maisha yako ya kila siku. Ninakukaribisha
sana katika siku nyingine tena, ambapo tunakutana kujadili maisha, lengo likiwa
ni kuhakikisha tunapata maarifa bora yatakayoweza kutusaidia kuweza kuboresha
maisha yetu na kuwa ya kiwango cha juu kabisa cha mafanikio kama tunavyotaka
iwe.
Katika makala yetu ya leo tutaangalia
hasa juu ya malengo na jinsi ambavyo tunaweza kufikia malengo tuliyojiwekea
bila kizuiliwa na kitu chochote. Mara nyingi wengi wetu kuna wakati huwa ni
watu wa kujiuliza, nitawezaje kufikia lengo hili ama lile katika maisha yangu.
Ni maswali ambayo huwa yanakuja pengine kutokana na mtu huyo kugundua kuwa kuna uwezekano wa
yeye kutotimiza malengo yake kwa sababu anazozijua yeye, ikiwa ni pamoja na
wasiwasi ama kushindwa kujiamini.
Wengine kutokana na wasiwasi
ama kushindwa kujiamini kama nilivyosema, hujikuta ni watu wa kuamini kuwa
labda wanaotimiza malengo ya aina fulani ni watu wenye vipaji, wamejaaliwa na
pia ni watu wenye bahati sana katika maisha yao, kitu ambacho sio kweli hata
kidogo. Kiukweli, unaouwezo mkubwa wa kutimiza malengo yoyote unayojiwekea
katika maisha yako, kama utaamua iwe hivyo kwako. Hakuna kitu ama mtu mwenye
uwezo wa kukuzuia wala huhitaji nguvu za ziada kufanikisha hilo.
Unaweza ukawa unaanza
kujiuliza nifanye nini au ni kipi cha kufanya ili niweze kutimiza malengo yangu
muhimu niliyojiwekea? Ni vizuri kujiuliza hivyo maana hiyo nayo ni hatua ya
kuonyesha kuwa una nia na mafanikio unayoyataka na wala hutanii. Kipo kitu
muhimu ambacho wewe unatakiwa ufanye ili kutimiza malengo yako, kitu hiki
nikufatilia na kufanyia kazi hatua hizi tano za kufikia malengo yako na si
vinginevyo. Ukifanya hivyo uwe na uhakika utafikia malengo
yako bila wasiwasi. Unajua hatua hizo ni zipi?
Hizi
Ndizo Hatua Tano Muhimu Za Kufikia Malengo Uliyojiwekea.
1.
Ni lazima uwe na hamasa ya kutaka kufanikiwa.
Hautaweza kufanikiwa kama
huna njaa na kiu kubwa ya mafanikio ndani mwako. Ili uweze kufanikiwa hasa kwa
malengo uliyojiwekea ni lazima uwe na hasira kubwa ya mafanikio. Ukiwa na
hasira hii, itakusaidia wewe kupita eneo lolote, hata katikati vizuizi ama
vikwazo ambavyo huwa tunakutana navyo katika safari ya mafanikio. Watu wengi
wenye mafanikio makubwa duniani ni watu ambao walikuwa na hasira na malengo yao
waliyojiwekea.
2.
Anza kuchukua hatua mapema.
Kuongea sana juu ya mipango
na malengo mazuri uliyonayo hakutakusaidia kitu, zaidi ya kuchukua hatua muhimu
za kuelekea kwenye utekelezaji. Anza kuchukua hatua mapema za kutekeleza ndoto
zako hata kwa kidogo kidogo ipo siku utafika. Ni bora ukafanya kwa kidogo hiyo
itakusaidia sana tofauti na ambavyo ungekaa na kusubiri, hiyo ingekuwa
inakupotezea muda sana katika maisha yako.
3.
Unahitaji kujifunza zaidi.
Hii ni hatua muhimu pia ya
kufikia malengo unayoyahitaji katika maisha yako. Ni muhimu kujifunza na
ukapata maarifa yanayoendana na malengo unayoyahitaji katika maisha yako. Hiyo
itakusaidia kujua vitu vya msingi vinavyoendana na malengo uliyojiwekea. Kwa
mfano, kama malengo yako ni kuwa millionea baada ya miaka 20 kuanzia sasa ni
lazima uanze kujifunza kuishi maisha wanayoishi mamilionea kwa kujisomea kila
siku.
4.
Unahitaji kuwa na mitazamo chanya.
Mara nyingi kuna wakati huwa
tunashindwa kufikia malengo yetu tuliyojiwekea kutokana na mitazamo tuliyonayo
juu ya malengo yetu. Kama unajiona huwezi kufikia malengo yako, huo ndio ukweli
hutaweza kuyafikia. Jenga mitazamo chanya ambayo itakusaidia kufikia malengo
muhimu uliyojiwekea. Achana na fikra ama imani za kuwa huwezi kufanikiwa kwa
sababu hii na hii, jiwekee mitazamo chanya na utaweza kufikia malengo yako.
5.
Jifunze kutokana na makosa.
Kuna wakati huwa tunafikia
mafanikio kwa yale tunayoyahitaji baada ya kukosea sana hiki na kile. Hautaweza
kufikia mafanikio au malengo yako kwa urahisi kama unavyofikiri, kuna wakati ni
lazima ukosee. Unapokosea huo ndio huwa wakati muhimu kwako wa kujifunza
kutokana na makosa uliyoyafanya. Acha
kusononeka wala kulia kama kuna sehemu umekosea, hiyo hatakusadia kitu. Badala
yake, chukua hatua muhimu ya kunyanyuka pale ulipoanguka, jifunze na kisha
songa mbele.
Mwisho, unaposhindwa kufikia
malengo yako kwa namna yoyote ile acha kulaumu vitu ambavyo viko nje ya wewe kuwa
ndiyo vimesababisha ushindwe kufikia malengo uliyojiwekea. Mara nyingi sisi
wenyewe huwa ndio huwa vizuizi wa malengo yetu. Jifunze hatua hizo tano muhimu
zikusaidie kufikia malengo muhimu uliyojiwekea katika maisha yako.
Nakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio. Ansante kwa kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO na endelea kuwashirikisha wengine kujifunza mambo mazuri
yanayoendelea humu.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com
- dirayamafanikio.blogspot.com
Feb 18, 2015
Mambo 5 Yanakuzuia Wewe Kuwa Tajiri.
Watu wengi huwa ni watu
wakijirudisha nyuma katika maisha yao
pasipo kujua hasa kutokana na vitendo, mienendo, hulka na hata tabia walizonazo
kwa ujumla. Hayo ni mambo machache kati ya mengi ambayo yamekuwa yakisimamisha
ndoto za watu wengi katika safari nzima ya kuelekea kwenye utajiri. Kiuhalisia,
ili uweze kufikia ngazi kubwa ya mafanikio na hatimaye kuwa tajiri unahitaji
kujifunza vitu vingi sana vitakavyoweza kukusaidia kusonga mbele, ikiwa na
pamoja nakujua vitu vinavyokuzuia wewe kuwa tajiri. Leo katika makala hii
tutazungumzia mambo yanayokuzuia wewe kuwa tajiri katika maisha yako.
Yafuatayo
Ni Mambo 5 Yanakuzuia Wewe Kuwa Tajiri.
1. Umekuwa
ukiathiriwa sana na mazingira uliyopo.
Hii ndiyo sababu kubwa
mojawapo inayokufanya ushindwe kufikia mafanikio makubwa na hatimaye kuwa
tajiri. Hili limekuwa likitokea kwako pasipo kujua na pengine umekuwa ukiona
kama jambo la kawaida tu kwako, bila kugundua kitu. Inawezekana ukawa umekulia
katika jamii maskini ambapo muda mwingi tokea unasoma shule na mpaka sasa uko
mtaani umekuwa ukiona watu wengi wanaokuzunguka ni maskini. Picha utakayokuwa
inakujia kichwani kwako ni kuwa haiwezekani kuwa tajiri. Unaamini hivyo ni kwa
sababu ya mazingira yanayokuzunguka unaona wengi ni maskini na ni kitu ambacho
kimekuwa kikikuathiri na kukuzuia wewe kuwa tajiri.
2.
Hujaamua kuwa tajiri katika maisha yako.
Maamuzi ni kitu cha muhimu
sana katika maisha yako. Hata kama utakuwa unasoma vitabu vya mafanikio kwa
wingi, kuhudhuria warsha na semina mbalimbali za mafanikio, kama hujafanya
maamuzi mazito ya kutaka kuwa tajiri katika maisha yako, huwezi kuwa tajiri.
Mafanikio makubwa ya maisha yako yanategemea sana na maamuzi unayoyafanya leo
kila siku. Ukiamua kuwa tajiri kisha ukajitoa kulipia gharama za kuwa tajiri,
hilo linawezekana. Maamuzi utakayochukua yana nguvu ya kukutoa kwenye umaskini
na kukufanya kuwa tajiri. Mpaka sasa hujawa tajiri moja ya kitu kinachokuzuia
ni maamuzi yako mwenyewe.
3.
Umekuwa mtu wa kuahirisha sana mambo yako.
Unashindwa kufikia ndoto zao
kubwa kwa sababu ya tabia yako hii ya kuahirisha mipango yako mara kwa mara,
hali ambayo imekuwa ikisababisha uzidi kukosa fursa nyingi kila kukicha. Kama
kuna jambo umeamua kulifanya na kulitekeleza ni vizuri ukalifanya leo ili uweze
kufikia mafanikio yako unayoyataka. Kama ni kesho ambayo unasema kila siku
utafanya hutaweza kuja kuipata mpaka unazeeka. Jifunze kufanya mambo yako leo
leo na achana na kesho utapoteza muda wako bure kuisubiri na kesho haitafika.
4.
Umekuwa ukitumia pesa zako vibaya.
Hili ndilo kosa kubwa ambalo
umekuwa ukilifanya na limekuwa likikugharimu na kukuzuia kuwa tajiri. Mara
nyingi umekuwa ukitumia nguvu nyingi kutafuta pesa zako, lakini unapozipata
umekuwa ukizitumia hovyo sana hali inayosababisha ushindwe kuweka hata fedha
kidogo kwa ajili ya akiba yako. Na umekuwa ukifanya hivi kwa sababu ya kukosa
nidhamu binafsi juu ya pesa zako na umejikuta umekuwa mtumwa wa pesa. Kama
unaendelea na maisha haya ya kutumia pesa zako bila ya utaratibu maalumu, tambua
kabisa utabaki kuwa maskini siku zote na hili halina ubishi.
5.
Umekuwa ni mtu wa kupoteza muda sana.
Ni jambo ambalo nimekuwa
nikilisema mara kwa mara kuwa, kama unaishi na unaendelea kuishi maisha ya
kupoteza muda, elewa huna kabisa maisha ama kwa maneno rahisi huwezi kufanikiwa
tena katika maisha yako. Muda ni kila kitu katika maisha yako unapocheza na
muda, inakuwa ni sawa na kuchezea maisha yako mwenyewe. Ubaya wa muda
ukiupoteza ndio haurudi tena hata ufanye nini. Jifunze kutumia muda wako vizuri,
ili ukuzalishie na ukuletee mafanikio
makubwa.
Hayo ndiyo mambo yanayokuzuia
wewe kuwa tajiri katika maisha yako, nakutakia kila kheri katika safari yako ya
mafanikio. Nakusihi endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO
kujifunza na kuhamasika kila siku. Usisite pia kuwashirikisha wengine ili
tujifunze wote kwa pamoja mambo mazuri yatakayoboresha maisha yetu.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com
- dirayamafanikio.blogspot.com
Feb 17, 2015
Mambo 6 Unayotakiwa Kujua, Ili Kuboresha Biashara Yako.
Kuwa na kiu ama shauku ya
kufikia ngazi kubwa ya kimafanikio kibiashara, ni hitaji ambalo kila
mjasiriamali na mfanyabiashara wa kweli
huwa nalo ndani ya moyo wake. Pamoja na kiu hii ya kutaka kufikia
mafanikio hayo makubwa kibiashara, wajasiriamali wengi hujikuta wakikwama na kushindwa kutimiza malengo yao. Kwa kawaida, huwa yapo
mambo mengi yanayochangia kutokea kwa hali hii, ikiwemo na kufanya biashara kwa
mazoea na matokeo yake kushindwa kuboresha biashara.
Unaposhindwa kuboresha
biashara yako, sio tu kwamba itapelekea wewe kukosa wateja, bali pia
itakusababishia kushindwa kufikia mafanikio makubwa uliyojiwekea katika maisha
yako. Kwa kujua hilo, ni muhimu sana kwako kuiangalia na kuichunguza biashara
yako mara kwa mara na kufanya marekebisho muhimu na ya lazima, ili kupata
matokeo chanya unayoyahitaji na si vinginevyo. Lakini, hautaweza kufanya
chochote au marekebisho yoyote kama hujui mambo haya.
Haya
Mambo 6 Unayotakiwa Kujua, Ili Kuboresha Biashara Yako.
1. Kubali
Kuwa Kuna ushindani.
Ni muhimu kujua hili mapema
kuwa biashara unayoifanya hauko peke yako, wapo watu pia wanaofanya biashara
kama ya kwako. Kwa kujua hilo hutakiwi kubweteka, kujiachia ama kulala na
kusubiri wateja waje, utakuwa unapoteza muda na hutapata mafanikio makubwa kama
unayoyataka. Badala yake, fanya kazi kwa bidii kuweza kukabiliana na upinzani
ulionao na usiogope wala kutishwa na
chochote, hapo utakuwa umefanya kitu cha kuboresha biashara yako.
2. Kuwa
na malengo na biashara yako.
Ili uweze kufikia mafanikio
makubwa unayoyataka katika biashara yako, ni muhimu pia kujiwekea malengo
maalum ya kibiashara. Malengo hayo yatakusaidia kujua ni wapi unapotakiwa
kufika baada ya muda fulani na wapi ulipokwama. Unapokuwa na malengo juu ya
biashara yako, ni lazima nidhamu yako itakuwa juu hasa katika mambo ya pesa na
utahakikisha kufanya lolote ili biashara yako ikue. Biashara yoyote unayoifanya
kama haina malengo maalumu haiwezi kukua na kufika mbali hata iweje.
3. Jitoe
Kufanya kazi kwa bidii.
Kwa kuwa umeamua kuwa
mjasiriamali, kitu pekee ambacho kinaweza kufanya biashara yako ing’ae ni
kufanya kazi kwa bidii, kwa ubunifu na
maarifa makubwa. Nguvu nyingi, mawazo na mwelekeo mkubwa unatakiwa kuupeleka
kwenye biashara yako ili ikuletee mafanikio makubwa na si vinginevyo. Kumbuka, wewe ndiyo bosi na
mkurugenzi wa biashara yako unayoifanya, ukilala au kusinzia ujue kabisa kila
kitu kitaharibika na hutaweza kusonga mbele.
4. Ishi na watu wenye mitazamo chanya.
Itakuwa ni ngumu sana kwako
kufanikiwa kama utakuwa una watu wengi wanaokuzunguka ni wenye mitazamo hasi na
biashara unayoifanya. Watu hawa watakukatisha tamaa kwa maneno na mienendo yao
na utajikuta unashindwa kusonga mbele. Ili uweze kuboresha biashara yako na
kufikia mafanikio makubwa, ni muhimu sana kuwa na watu chanya ambao wanauwezo
wa kukusaidia kwa hali yoyote ile hata pale ambapo mambo yako yanakwenda hovyo.
5. Badili
jinsi unavyojitazama mara moja.
Kuwa na mtazamo chanya juu
ya biashara yako ni kitu cha lazima sana kwako, ili iweze kuleta mabadiliko
unayatarajia. Biashara yako haitafika popote kama utakuwa mtu wa kuitazama na
kuona kuwa haitafanikiwa sana kama unavyoziona za wengine. Kutokana na mitazamo
wako huo utaanza kufanya mambo kizembe hali itakayopelekea wewe kushindwa. Kama
unataka kuboresha biashara yako, badili
jinsi unavyojitazama wewe na biashara kwa ujumla.
6. Jifunze
zaidi kuhusu biashara.
Unatakiwa kujifunza na
kuilewa vizuri biashara unayoifanya kila siku. Hiki ni kitu ambacho hutakiwi
kukwepa kwani kitakusaidia kuiboresha biashara yako kwa sehemu kubwa sana. Kwa
kadri jinsi utakavyozidi kujifunza juu ya biashara yako, utagundua mapungufu
mengi ambayo ukija kufafanyia kazi, itakusaidia kuhama kutoka ngazi moja na
kuelekea ngazi nyingine zaidi ya mafanikio kibiashara.
Kumbuka, ili tuweze
kufanikiwa na kufikia mafanikio makubwa, tunalazimika kuboresha biashara zetu kwa sehemu kubwa kila siku.
Kama utashindwa kuboresha biashara yako, basi elewa tu hutafika mbali sana
kimafanikio kama unavyofikiri, kwani
nguvu ya ushindani itakushinda na utajikuta umebaki pembeni na kuwa mtazamaji
kwa wengine. Kwa kuanzia, hayo ndiyo mambo muhimu unayotakiwa kuyajua ili
kuboresha biashara yako.
Nakutakia ushindi katika
biashara yako iwe ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku
kujifunza na kuhamasika, mpaka maisha yako yaimarike.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com
- dirayamafanikio.blogspot.com
Feb 13, 2015
Kama Unaendeshwa Na Kitu Hiki, Maisha Yako Ni Magumu Sana.
Mtu mwenye hisia nyingi
ambaye anaongozwa na hisia, ni yule ambaye huweza kuathiriwa au kutikiswa kwa
urahisi zaidi na hisia. Ni jambo zuri kujijua sisi wenyewe na haiba zetu na
hata kutambua hisia zetu. Ninapozungumzia hisia nikiwa na maana ya hali kama
kuwa na furaha, huzuni, chuki na hata wakati mwingine kijicho hizo ni baadhi tu
ya hisia.
Baadhi ya watu ni wenye
kuongozwa sana na hisia wakati ambapo wengine hawako hivyo na kwa kuutambua ukweli huu tutaweza kuzuia na
kuepuka kuumiza vichwa vyetu na hata kupata maumivu mengine katika maisha yetu.
Hata kama hatumo katika kundi la wale wenye hisia nyingi, bado kila mmoja wetu
anazo hisia na yuko katika hatari ya kuongozwa na hisia hizo.
Tunaweza kuamka mapema sana
asubuhi siku moja, huku tukiwa tumejazwa na hisia za huzuni na kwa siku hiyo
nzima tukaongozwa na kufuata hisia hizo. Siku inayofuata tunaweza tukaamka pia
tukiwa tumechukia, huku tukihisi au kutaka kuona kila mmoja wetu pale nyumbani kwetu
aondoke machoni petu, hivyo tukajikuta tukaishia kufanya vituko vya ajabu tu.
Wakati mwingine tunaweza
kuamka na hisia za kujisikitikia sisi wenyewe na kujuta sana na hata kuamua
kukaa kwenye kona tukiugulia kwa siku nzima huku tukiwa tumeshika tama. Na
kujiuliza maswali mengi ambayo hayana majibu na huku tukiwa hatutaki kabisa
kuongea na mtu. Na inapotekea mtu akatuongelesha tunakuwa wakali sana kiasi cha
kwamba tunaweza kumjibu vibaya kama sio sisi tuliozoeleka.
Hivyo basi, iwapo tutaamua
kuziachia hisia zetu zifanye vile zinavyotaka, basi ni wazi kabisa hisia hizi
zitachochea matatizo ambayo yatasababisha tutoke nje ya makusudio yetu mema na
kutupeleka kwenye makusudio au matakwa ya kutuangusha. Hapa ndipo pale
tunapoanza kusema, ‘ilikuwa ni ibilisi tu’. Ndio maana katika maisha yako, kama
bado ni mtumwa na unaendelea kuendeshwa na hisia zako, maisha yako ni magumu
sana. Ni magumu kwa sababu kila wakati utakuwa unaishi maisha yanayokuumiza
wewe tu.
Nimetumia miaka mingi ya
maisha yangu katika kufuata vile nilivyokuwa nikijihisi. Kama niliamka asubuhi
nikiwa mwenye huzuni, basi nilihuzunika siku nzima. Kwa wakati huo sikuweza
kujua kwamba, ningeweza kuzizuia hisia za aina hiyo. Sasa nimetambua kwamba,
ninaweza kupambana kikamilifu na hisia zote mbaya na zilizo hasi ambazo
zinatamani kuniongoza siku nzima.
Ni lazima tujifunze kuwa wenye
tahadhari kuhusiana na hisia zetu mwenyewe na kuweza kuelewa jinsi
tutakavyoweza kuziongoza na kuzisimamia kwa usahihi na uhakika zaidi. Njia mojawapo
ya kufanya hivyo, ni kuzijua aina tofauti za haiba au tabia na kujua namna
zinavyoitikia kwa njia tofauti, hali au mazingira yanayofanana.
Nimejifunza kwamba,
ninapoamka asubuhi nikiwa na kisirani, sipaswi kuendelea kukilea kisirani
hicho. Ninapaswa badala yake kuamua kuwa mimi, kuamua kuwa na mkabala tofauti
wa kimaisha kwa siku hiyo. Ni mimi ninayepaswa kusema ninataka nijisikie vipi,
siyo mazingira au hali inayonizunguka.
Ninapojikuta nimenyong’onyea,
ni lazima nijiulize haraka kama ni lazima ninyong’onyee. Ni wazi wazi kwamba,
huwa ninapata jibu la hapana. Kwa hiyo, kuanzia hapo hutafuta sababu ya kunyong’onyea
kwangu. Nikishaipata hutafuta sababu iliyo kinyume na hiyo, ambapo hunisaidia
kuondokewa na kunyong’onyea huko sana.
Nakutakia maisha mema yawe
ya furaha kwako, endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na
kuhamasika kila siku, karibu sana.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713048035/dirayamafanikio@gmail.com.
Feb 12, 2015
Kama Hujui, Mabilionea Wengi Duniani Wako Hivi.
Kila kundi la kipato lina
tabia na mienendo yake. Pengine kunakuwa na ugumu wa kuikwepa mienendo hiyo kwa
wahusika, baada ya kuingia humo au mienendo hiyo ndiyo imewasaidia kufika hapo
walipofika. Tunasema, kama alivyo binadamu ambapo kila mmoja ana haiba yake,
makundi ya kipato nayo yana haiba zake, ambazo zinaweza kuwa tofauti na makundi
mengine.
Kwa mfano, ukitazama kundi
la mabilionea walio wengi duniani, utabaini kuwa wana sifa ambazo zinajitokeza
sana kwa watu hao. Kuna sifa ambazo wanakuwa nazo na wala hawazipangi, bali ni
kwa sababu ya mazingira au saikolojia ya fedha, wao wanakuwa na tabia au
mienendo hiyo zaidi kuliko watu wa makundi mengine. Kutokana na mienendo hiyo
mara nyingi ndiyo inawafanikisha sana.
Ukikagua sana, utakuja
kugundua kuwa mabilionea walio wengi ni
wale ambao wanafanya biashara zinazohusiana na fedha, kama benki ikiwa pamoja
na uwekezaji wa hisa, kuna ambao wanasughulikia mawasiliano kama simu na
mitandao ya intaneti na hata kujishughulisha na ujenzi katika kiwango cha
kimataifa au kwenye maeneo mbalimbali kama sehemu muhimu ya biashara zao.
Unaweza ukajiuliza maswali
mengi kidogo na kuanza kushangaa biashara zingine vipi? haziwezi kumpa mtu
utajiri na hatimaye kuwa bilionea? Siyo hivyo, kuwa kwamba biashara zingine
haziwezi kumpa mtu ubilionea, hapana. Hizi ndizo ambazo zimewapa wengi
ubilionea zaidi. Ukitazama kwa makini utagundua ukweli huu kuwa mabilionea
wengi wamezalishwa kutokana na biashara hizo.
Pia mabilionea walio wengi wanatabia
za kuacha mali zao kwa taasisi za kusaidia au hata kwenye nyumba za ibada au
mifuko mbalimbali ya misaada baada ya kufa kwao.Na huacha fedha kidogo sana kwa
watoto wao. Hapa kwetu, watoto wakishakuwa na baba mwenye fedha, hawataenda
shule wala kujifunza maisha. Wanasubiri baba afe ili warithi. Wakati mwingine
hurithishwa hata kabla baba hajafa. Matokeo yake ni kutapanya mali na kubaki
mikono mitupu.
Hata kuna kipindi Bill Gates alishawahi kusema kwamba,
hata iacha fedha yake kwa watoto wake, bali ataitumia kusaidia kuondoa matatizo
yenye kusumbua sana dunia. Kabla hajafa ameshaanza kufanya hivyo. Watoto wake
nao wanahangaika kivyao kujua maana ya kutafuta. Ni kwa sababu, kuwa sisi,
ikiwemo kutafuta mafanikio kwa bidii zote, ndicho hasa kilichotuleta duniani.
Hujaumbwa uwe maskini.
Lakini lingine la kushangaza
zaidi ni kwamba, mabilionea wengi hawana hata digrii ya kwanza. Inawezekana
walipitia vyuo lakini wakapata cheti au stashahada au walimaliza tu elimu ya
msingi au sekondari. Kwa hiyo utakuja kugundua kuwa, fedha au utajiri hausiani
sana na kusoma sana na hii inaonyesha haviko karibu. Mawazo, yaani unachoamini
kuhusu fedha na utajiri, ndilo jambo la awali kabisa.
Mabilionea wengi pia
hawakupewa urithi au kupata bahati nasibu katika maisha yao. Walio wengi wametafuta fedha kwa juhudi zao wenyewe kwa
kuanzia chini kabisa. Wengine waliweza kusota hadi wakawa kama vituko, lakini
wakaja kusimama katika njia ambayo watu wengine wameshangaa na kubakia
kusimulia wasielewe ni kitu gani kilichofanyika.
Kuna tatizo moja kwa
mabilionea waliowengi. Kwa kufuata au kuhangaika kupata mafanikio zaidi,
hujikuta wakisahau kwamba, kuna burudani, kuna ‘hobi’ na muda wa kusahau
masuala ya shughuli. Wao ni watu wa kazi tu na ubunifu ndivyo vyenye kuwaumiza
kichwa na si vinginevyo. Kuna wakati huwa wanajikuta hata wakipunguza hata
masaa ya kulala sababu ya kufanya kazi kwa bidii zote.
Hebu jaribu basi kujikagua
ili uone kama ni kweli nawe unaweza kuwa na sifa kadhaa kama hizo za
mabilionea. Huenda nawe unatamani kuwa bilionea ila hujajua au kuamua ni kwa
njia gani. Jua sifa zao, labda utawea kupima kiwango cha ukaribu wako kwao.
Siyo lazima uwe na fedha nyingi ili kuwa bilionea, anzia hapo ulipo ukiwa umepania
kuwa, unataka kuwa bilionea, utafanikiwa.
Tunakutakia kila la kheri,
endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza na kuhamasika, mpaka
maisha yako yaimarike.
IMANI
NGWANGWALU,
0713048035/dirayamafanikio@gmail.com
Feb 9, 2015
Maisha Ni Vitendo Na Si Ndoto Pekee, Ndoto Ni Mwanzo Tu Wa Maisha…
Kwa kawaida, binadamu ana mambo matatu muhimu ambayo anaweza
kuyaendesha au yakamwendesha kichwani kwake, moja ni fikra zake au mtazamo (thoughts
you think), mbili ni taswira anazozijenga kichwani kwake (image you visualize)
na tatu ni vitendo vyake (the actions you take). Sisi binadamu tunawajibu
wakuhakikisha tunaleta maendeleo katika maeneo tunayoishi kwa juhudi zetu
binafsi. Ni kweli tumesikia na kujifunza mengi katika dunia lakini maana ya
maisha iliyo halisi na ya kweli ya mwanadamu mhusika hutoka ndani ya binadamu
mwenyewe.
Kila mwanadamu anao ukweli wa maisha yake ndani yake. Mambo yote
tunayoyaona duniani, ugunduzi, vitabu, miziki, filamu na kila kitu kilichopo
duniani kilichosababishwa na mwanadamu asili yake ni ndani ya binadamu na si
nje. Ndani yako mwanadamu kuna maajabu, ndani yako kuna hazina ya maisha,
vipaji, talanta na habari njema ya maisha yako. Kutokana na upekee ulionao
duniani, huna mshindani, mshindani wako ni wewe mwenyewe. Historia ya dunia
inaonyesha kuwa wanadamu walio wengi duniani wanafichwa mambo ya ukweli na
makubwa kuhusu uwezo wao.
Toka enzi za wajasiriamali tunaowasoma katika historia akina
Adam Smith, kipindi cha viwanda na utumwa wanadamu wengi, waliishi chini ya
viwango kwa kutumika kama mashine zinazoweza kubadilishwa wakati wowote, hii
imekuwa sababu kubwa ya binadamu wengi kutokujua ukweli wa vipawa ndani yao na
hata kutojiamini kabisa. Vilevile Kutokana na mabadiliko ya maisha, karne hii
ya 21 inatabiriwa kuwa karne ya vipawa na maajabu ya ndani ya mwanadamu kwani
imedhihirishwa na baadhi ya watu wa kawaida sana ambao wameweza kugundua mambo
mengi kwa kutumia vipawa vyao.
Tunaishi katika dunia ambayo ni rahisi kubebwa na misukumo ya
nje na wengi hawaamini ukweli huu kuwa kila mtu ana kipaji, kila mtu ana habari
njema ya ndani yake hii ni kwasababu wengi wameshawishiwa na mifumo ya dunia na
maisha ya wanadamu wengine na kujikuta kuwa wanaishi si kama wao bali kama
nakala. Watu wote wenye mafanikio duniani, ambao huonekana kana kwamba
wamebarikiwa hutafuta maana ya wao kuwa wao, uwezo wao wa kipekee na kutumia
upekee walionao na kuishi maisha yao kimafanikio watakavyo wao.
Dunia hii inayo nafasi kwa mwanadamu ambaye anatafuta maana ya
maisha yake mwenyewe, haijalishi umezaliwa katika familia ya aina gani bali
ukikubali ukweli kuwa unayo hazina ya maisha ndani yako basi maisha yako
yatapata maana. Unacho kipaji ndani yako. Hakuna mwanadamu ambaye hakuumbwa na
kitu ndani yake, Mungu hakuumba takataka duniani, Mungu aliumba mwanadamu
mwenye hazina ndani yake. Kila mwanadamu anao uwezo wa kipekee na kiasili
aliojaliwa na Mungu ambao bila yeye hakuna ukamilifu. Uliletwa duniani ili
ukamilishe upekee wako. Wewe ni ukamilifu wa dunia, kuishi kama nakala haina
tofauti na kuishi kama marehemu anayetembea.
Unaweza usiwe na uwezo kuanzisha biashara ya mgahawa au ya
daladala lakini ukawa na uwezo wa kuimba na kutunga nyimbo za kila aina hivyo
ukawa mjasiriamali katika kanda ya mziki
iwapo una uwezo wa kuchekesha basi fanya ujasiriamali katika kipengele cha
ucheshi kama jamaa wa futuhi. Wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia
icheke, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia icheze,wapo walioletwa
duniani ili kuifanya dunia itembee, wapo
walioletwa duniani ili kuifanya dunia ifikiri, wapo walioletwa duniani ili
kuifanya dunia isikilize radio,TVs na muziki, wapo walioletwa duniani ili
kuifanya dunia ing'are na mengine mengi unayoyajua na ambayo mpaka sasa
hatujayajua bado lakini yamo ndani yako. Aidha wapo walioletwa duniani ili kuifanya
dunia iwe na mitandao tunayoiona sasa hivi.
Dunia hii inakuhitaji wewe kama wewe, na mafanikio yako duniani
yanakutegemea wewe kama wewe. Hata kama usipokubali ukweli wa uwezo wako wa
ndani, haitaondoa maana ya ukweli ulio ndani yako. Kumbuka kuwa utamu wa maisha
duniani ni matumizi ya kipaji chako na kusikiliza sauti ya ndani.Ulipewa vipaji
ili uvitumie duniani katika biashara,kazi,sanaa,uongozi,ujuzi,masomo na
mengine. Bila kujionea aibu mwenyewe, na kujitafuta na kujiuliza kasoro zako
ulizonazo na jinsi ya kuzizuia au kuzipunguza, tafuta kujua mazuri ya kwako
huku ukitafuta kuongeza mengine.
Ukiona Kama kuna kitu kinakufurahisha duniani, usiogope
kujaribu, jaribu, jaribu tena ipo siku utagundua wewe ni mzuri wapi. Sikiliza
sauti za dunia lakini sikiliza sana sana sauti yako ya ndani kwani ndiko
kutokako chemchem ya uhai wa maisha yako. Jifunze kujiuliza, wewe ni nani?
Umetoka wapi? Una nini cha kujivunia duniani? Unataka dunia ikukumbuke vipi? Je
uko tayari kuja duniani kama moshi na kuondoka kama moshi, usikumbukwe? Nini
unaweza zaidi ya mwingine? Ni nini madhumuni yako duniani?
Kumbuka kuwa wewe ndiye mkurugenzi mtendaji wa maisha yako,
mazingira, mifumo, familia na vikwazo vyovyote duniani visiwe sababu ya
kuutuliza utu wako. Unazo nguvu zaidi ya nguvu zilizo nje yako za kuwa
unavyotaka, kulingana na jinsi ulivyojaliwa. Vipo vitu vinavyoweza kukuzuia
hata kukumaliza lakini ni uamuzi wako kusimama kidete kwaajili ya maisha yako
na kuonyesha nguvu zilizo ndani yako au kukubali kumalizwa bila ubishi wowote. Vipo
vitu vingi vinavyoweza kukuchanganya. Lakini ni uamuzi wako kukubali
kuchanganywa na kuishi maisha ya bora liende au ili mradi kumekucha mpaka
unakufa bila maana au kuamua maisha yako na kusema ama zangu ama zao nitakuwa
vile ninavyotaka maishani.
Kumbuka kuwa dunia haina huruma kwa mwanadamu aliyekubali
kumalizwa, vumilia, jiamini, Jipende, jiendeleze, jikaze, jionyeshe, jitafute
mwenyewe, jikubali na mwisho wa siku dunia itakukubali tu hata kama kuwe na
nguvu zozote mbele yako. Kumbuka kuwa dunia hii itaendelea kuendeshwa na hata
kutengenezwa na binadamu wenye uelewa mpana wa nguvu iliyo ndani yao na si
wababaishaji na wenye maisha ya maridadi.Wanadamu wote walioweza kufanikiwa.
Kuna wakati tumekuwa tukilaumu watu wasiohusika katika maisha
yetu magumu, kuwa wanaharakati wa mambo yasiyotuhusu, kutoa maoni yasiyo na
maoni na kuchambua timu za ulaya na kuelezea mchezaji fulani analipwa kiasi
gani cha mshahara. Ni lini umewahi kaa nyumbani kwako au kwenu na ukatumia muda
wako kuchambua vipaji vyako? Ambavyo ungevitumia katika maisha yako na jamii
inayokuzunguka?Kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale ambao
wametambua sababu ya wao kuwa wao, wanajijua ni nini wanakitaka na wanajua kuwa
ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe.
Maisha ya mafanikio duniani ni haki ya kila mwanadamu. Hakuna
binadamu aliyeletwa duniani kuja kushuhudia wengine wakifanikiwa huku yeye
akiwa katika umaskini siku zote. Kila mwanadamu mwenye pumzi anayo haki,
nafasi, uwezo na uchaguzi wa kuwa anavyotaka kulingana na maana ya mafanikio
atakayotengeneza na mwenyewe. Ni kweli tunaishi katika dunia yenye utofauti
kimafanikio wapo wenye mafanikio makubwa, wapo maskini na wale wenye maisha ya
kawaida. Lakini kwa pamoja yatupasa tufahamu kuwa, kila mwanadamu anao uwezo wa
kufanikiwa. Na zaidi ni kuwa kila mtu anao uchaguzi wa kuamua maisha yake,
lakini angalizo ni kuwa mtu yeyote aliyeweza kufanikiwa ametambua kuwa , kuna
vichangizi vya mafanikio / success ingredients.
Unachopaswa kutambua ni kuwa, hali ya maisha uliyonayo sasa si
kipimo cha mafanikio yako ya baadaye, unaweza kuwa vyovyote kimafanikio
kulingana na utakavyochagua mwenyewe. Ni muhimu kuyajua maisha Kwa kujua vipaji
na vichagizi hivyo ni kama vifuatavyo: Mwanadamu anayejua dhumuni lake duniani
huishi maisha ya maana. Hatukuja duniani kuwepo tu bali kuishi kimafanikio huku
tukijua kwanini tunaishi. Ukijua ni kwanini unaishi hutakubali kuishi
kiholelaholela huku ukisubiri muda wako wa kuishi duniani kuisha.
Dhumuni la wewe kuwepo duniani ni kuishi maisha yenye madhumuni,
maisha yenye mafanikio na maisha yanayonufaisha wengine. Wanadamu wote
walioweza kufanikiwa kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale
ambao wametambua sababu ya wao kuwa wao, wananjua ni nini wanakitaka na wanajua
kuwa ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe katika hilo. Ukitaka
kutengeneza maisha yenye mafanikio duniani, tafuta kujua dhumuni lako hapa
duniani.
Wanadamu wote waliofanikiwa duniani waliamini kuwa wanaweza
kuibadili dunia. Mwanadamu anayeyarudisha maisha yako nyuma ni wewe mwenyewe,
ukitaka kufanikiwa katika lolote utakalochagua jiamini na amini kuwa unaweza.
Hakuna kitu chochote kilichowahi kutokea duniani bila kujiamini. Kila mwanadamu
anayo zawadi ndani yake, zawadi hii huja kama kitu anachokipenda na kukiweza.
Ndani ya mwanadamu vipo vipawa na uwezo wa ajabu wa kuishi maisha ya mafanikio.
Kila mtu ana kitu anachopenda, kinachoweza kutumika na kuendelezwa na kuleta
mafanikio.
Dunia ya sasa ni dunia ya wanadamu wanaojua ni kitu gani
wanaweza. Wapo wanaopenda kuwa madaktari, wapo wanaopenda kuwa waimbaji nk.
Kila mtu ana kitu anachopenda kinachomfanya acheke akiwa duniani. Tafuta kitu
unachokipenda na kiendeleze, kitakuletea mafanikio. Maisha ni vitendo na si
ndoto pekee, ndoto ni mwanzo tu wa maisha. Maisha ni kuchukua hatua na si
kufikiri pekee. Maisha ya kijasiriamali ni kusonga mbele na si kupanga peke
yake. Katika yote uliyochagua maishani kuwa mtendaji, usikubali kuyaishi maneno
ishi matendo.
Maisha bila maarifa ni sawa na gari lisilo na mafuta. Ukitaka
kutembea na kuishi kimafanikio kuwa na njaa ya maarifa kila siku. Binadamu wote
wenye mafanikio duniani hawachoki kutafuta maarifa kwa kusoma vitabu, kuuliza
na kujifunaza, na hata kuhudhuria mafunzo ya kuwaendeleza mara kwa mara. Maisha
bila maarifa hayatembei. Maisha yana mengi, muda mwingine yale tunayapanga
hayaji kama tulivyopanga lakini yote hutokea kwasababu.
Mambo yote tunayapitia katika maisha huwa ni hatua ya ukuaji
kimaisha. Ukiona biashara yako inafanya vizuri tambua kuwa ni kweli biashara
yako inakua, lakini ukiona biashara yako inafanya vibaya tambua kuwa uwezo wako
unakua zaidi. Nahitimisha kwa kusema kila mtu ana uwezo wa kuchagua kuwa
mjasiriamali wa kipekee na yale ayatakayo maishani, Dunia ina mengi ya
kuyafanya na kuna kila nafasi kwa mwanadamu yeyote anayechagua kuwa anavyotaka
maishani. Chagua maisha unayotaka kuyaishi na uyaishi kweli.
Usiogope kujaribu kitu, maisha ya kuogopa kufanya kitu ni maisha
yasiyo na maana. Usikubali maisha ya ukawaida na yenye usalama ambayo
yatakufanya usiishi maisha makubwa unayostahili. Siri kubwa ya watu wenye
mafanikio duniani, ni kuwa hawaogopi maisha, wapo tayari kuumia kwa kuchagua
maisha wayatakayo. Chagua kipengele mojawapo cha kijasiriamali unachotaka
kukifanya na ukifanye kweli kwa moyo wote. Jiendeleze kila siku katika
ulilochagua kiasi ambacho utavunja mipaka na kuweka rekodi yako. Chagua
kufanikiwa.
·
MAKALA
HII IMEANDIKWA NA MESHACK MAGANGA – IRINGA
·
MASALIANO
- 0713486636
Subscribe to:
Posts
(
Atom
)