Sep 22, 2015
Jinsi Unavyoweza Kuwavuta Watu Unaokutana Nao.
Kwa
nguvu zake Mungu naamini umzima wa afya na unaendelea kujifunza kupitia DIRA YAMAFANIKIO ili kuboresha maisha yako. Leo napenda nianze makala hii kwa
kukuuliza swali hili, ni kwa nini baadhi ya watu, wakikutana na mtu kwa mara ya
kwanza tu, mtu huyo waliyekutana naye ‘anaboreka’ haraka? Na ni kwa nini
wengine, wanapokelewa kirahisi na watu wapya wanaokutana nao maishani?
Najua,
unajua kuna sababu nyingi. Lakini ningependa nikutajie moja tu, ili iweze kukusaidia
kukabiliana na ‘kuwaboa’ watu wengine. Na tumia neno ‘kuboa’ kwa sababu ni neno
ambalo limezoeleka kimatumizi kwa sasa, likiwa na maana ya kumfanya mtu asiwe
na haja ya kukusikiliza au kuwepo kwako hukera, wewe ukiwa ndiyo chanzo.
Kama
umekutana na mtu kwa mara ya kwanza, usizungumze sana kuhusu wewe,
usijizungumzie kwa kujisifu na kujipandisha sana. Ingawa haina maana kwamba
usijishushe. Usitake kuonesha kwamba wewe ndiye wewe.
Watu
wasiojitosha, huwa wanakawaida ya kujisifu sana, wanataka kuwavuta
wanaozungumza nao wawaone wa maana sana, huzungumza kwa muda mwingi wao tu,
hujisifu na kujikweza. Ni mara chache sana huwaacha wengine waseme.
Hebe
fikiria, hujamjua mtu, unasema kama kinanda kuhusu mambo yako, unadhani
atakuchukulia vipi? Ni lazima utamkera tu, badala ya kumfurahisha, kama
unavyofikiria. Ni lazima utaanza kuwa na wasiwasi nawe.
Jambo
la awali unalotakiwa kulifanya unapokutana na mtu mgeni, ambaye hujawahi
kukutana naye, iwe kibiashara, kimapenzi au kwa nasibu tu, inabidi uwe
msikilizaji tu kuliko kuwa msemaji.
Kuna
watu ambao wanatatizo la kutaka kusikilizwa wao tu, amablo chimbuko lake ni
kushindwa kwao kupata watu waliowajali walipokuwa wadogo.
Kama
nawe ni mmojawapo, inabidi uwe mwepesi kujikumbusha kwamba, una tatizo la
kutaka kusikilizwa wewe tu. Kujikumbusha au kukumbuka, kutakusaidia kuamua
kumsikiliza mwingine badala ya wewe kusema.
Siku
zote wanaopenda kusikiliza badala ya kusema, hao ndiyo mara nyingi huwa
wanawavutia watu, siyo wale wanaopenda kusema sana. Wengi hawalijui sana jambo
hili.
Ni
vizuri unapokutana na mtu mgeni, ukasema kidogo uhusu wewe, yaani yale mambo ya
msingi tu yanayokuhusu. Sema tu yale ambayo ni ya lazima au muhimu. Usiwe
kasuku kwanza.
Halafu,
soma kama huyo mtu ambaye humjui, ndiyo kwanza mnakutana, anavutwa na
mazungumzo gani? Unaweza ukaanza kubwata siasa wakati hataki kusikia kabisa
mambo yanayohusiana na siasa zako hizo. Unaweza ukaanza kubwata kuhusu vifo,
wakati pengine wiki iliyopita tu kapoteza mkewe au mumewe ama mtu wake wa
karibu kabisa.
Ukijua
mtu au watu wa fulani ambao ndiyo kwanza unakutana nao wanafurahia kuungumzia
mambo gani, hutawakera. Kwako itakuwa rahisi pia kuwasikiliza, kwani huenda
watakuwa na mengi, kwani wanazungumza yale wanayoyapenda na pengine wanajua
zaidi.
Unapokutana
na mtu mgeni popote na mazingira yakakulazimisha muwasiliane, siyo vibaya
ukaanza kwa kujitambuisha kwa kujitaja jina.
Hii
humjengea mtu huyo mwingine kukuamini na kuhisi ukaribu na urafiki. Onesha kwamba, mtu huyo mgeni anapozungumza
unafurahia mazungumzo yake. Unaweza kutabasamu, kumtazama bila kukodolea macho
na kutikisa kichwa mara kwa mara.
Hata
kama ikitokea mtu huyo anaongea upuuzi, ni vema kujenga uhusiano wa karibu na
mtu huyo. Wacha mgeni aseme zaidi ili umjue zaidi kuliko wewe anavyokujua.
Kumjua
kwako zaidi kutakusaidia kujua uzungumze vipi naye na kwa sababu zipi. Lakini,
usijaribu kuwa mtu ambaye siyo wewe. Kuwa wewe kwa kujikubali, bila
kujipandisha wala kujishusha.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya mafanikio yako na endelea
kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035
kwa ushauri na msaada wa haraka.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.