Sep 17, 2015
Mambo 7 Yakukusaidia Kutunza Muda Wako Vizuri.
Matumizi
mazuri ya muda ni moja kati ya changamoto kubwa sana inayotukabili wengi wetu.
Mara nyingi imekuwa ikitokea kwa wengi wetu karibu kila siku, kujikuta tuna mambo
mengi ya kufanya ukilinganisha na muda tulionao. Kutokana na mambo hayo kuwa mengi,
mipango yetu mingi pia hujikuta imekwama na kushindwa kuendelea kutokana na ukosefu
wa muda.
Lakini
hata hivyo, pamoja na changamoto zote hizo za ukosefu wa muda, kwa wengine bado
hubaki kuwa ni watu wa kupoteza muda katika maisha yao. Nikiwa na maana kuwa,
wanakuwa ni watu ambao hawajali sana kupoteza muda wao na pia hata wanakuwa wanawapotezea
wengine muda hivyohivyo. Najua umeshawahi kuwaona watu wa namna hii katika
maisha yako wasiojali thamani ya muda.
Hawa
ni watu ambao huishi maisha yasiyo na mafanikio sana kutokana na kupoteza muda
mwingi sana katika maisha yao. Kitu cha muhimu hapa kujua ni kuwa muda ni kitu
cha thamani sana kuliko kitu chochote duniani.
Mafanikio yote yanategemea muda. Unapopoteza muda wako ni sawa na kupoteza
mafanikio yako. Sasa jiulize kama wewe unapoteza muda unategemea nini katika
maisha yako?
Ili
uweze kufanikiwa na kuwa tajiri ni lazima kujifunza kutumia muda wako vizuri
tena sana. Watu wote wenye mafanikio makubwa ni watumiaji wazuri wa muda wao
kuliko unavyofikiri. Kinachowatofautisha wao na wewe ni matumizi ya muda tu na
sio kitu kingine. Hiyo yote inaonyesha siri kubwa ya mafanikio ipo kwenye muda.
Kitu kingine cha kujiuliza tena je,
unataka kutunza muda wako na kujijengea mafanikio ya kudumu? Kama jibu ni NDIYO.
Yafuatayo Ni Mambo 7 Yakukusaidia
Kutunza Muda Wako Vizuri.
1. Weka vipaumbele vya kila siku.
Ili
uweze kuepuka muingiliano wa mambo ni lazima kujifunza kuweka vipaumbele vya
kila siku. Andika mambo ya lazima ambayo unatakiwa uyafanye kwa siku hiyo
husika bila kuacha kitu. Hilo litakusaidia kutopoteza hovyo muda wako ulionao
kwa sababu kila kitu kitakuwa kwenye ratiba yake na muda wa kukifanya.
2. Jiwekee malengo.
Kama
utakuwa unajiwekea malengo hiyo itakuwa ni silaha ya kukuwezesha kutumia muda
wako vizuri pia. Kwa sababu utakuwa unajua kabisa baada ya muda fulani unatakiwa
uwe umetekeleza kitu hiki ama kile. Wengi wanaopoteza muda mara nyingi ni watu
ambao hawana malengo hata yale ya siku moja tu. Na kwa sababu hiyo kwao muda
kupotea ni kitu ambacho hakikwepeki.
3. Fanya mambo machache kwa uhakika.
Ni
rahisi sana kwako kupoteza muda kama utajikuta unataka kafanya mambo mengi kwa
wakati mmoja. Hii ni kwa sababu utashika hiki mara kile na kujikuta hakuna
ulichokifanya zaidi ya kurukaruka. Ili kufanikiwa jifunze kufanya mambo
machache kwanza ikiwezekana jambo moja tu. Hiyo itakupa ufanisi wa kutunza muda
wako vizuri sana.
4. Weka kumbukumbu ya muda wako.
Ili
uweze kujua muda wako unautumiaje, ni vizuri kujiwekea kumbukumbu ya muda wako
jinsi unavyoutumia. Unaweza ukaona ni kitu kama cha kijinga lakini ikifika siku
kitakusaidia kujua tathmini ya wapi hasa unapopoteza muda wako mwingi ili kama
ikiwezekana ujirekebishe. Kwa kujiwekea kumbukumbu ya muda wako uwe na uhakika
utaweza kumiliki na kuutawala muda wako vizuri sana kwa mafanikio.
5. Kuwa makini na mambo
yanayokupotezea muda.
Kuna
mambo ambayo wengi wetu huwa yanatupotezea muda bila sababu. Jiulize ni kitu
gani ambacho kinakupotezea muda sana. Je, ni mitandao ya kijamii, simu, mpira
au ni kitu gani? Ukishajua kitu kinachokupotezea muda sana, tafuta njia nzuri
namna ya kupunguza matumizi hayo. Acha kupoteza muda wako hovyo kwa kitu
ambacho hakikupi faida ya moja kwa moja, badala yake linda na tunza sana muda
wako kwani hapo ndipo mafanikio yako yalipo.
6. Jifunze kusema HAPANA.
Wengi
huwa wanajikuta ni watu wa kupoteza muda wao pengine kutokana na kukubali vitu
vingi bila kujiuliza kwa nini walikubali. Kabla hujasema ndiyo kwa jambo lolote
la makubaliano jiulize linawezekana? Kama hutajifunza kusemaHAPANA hii itakufanya
uzidi kupoteza muda wako mwingi wa thamani siku hadi siku bila ya wewe kujua. Kama
huelewi kitu ni bora ukasema HAPANA kuliko ukafanya na ukaacha, hiyo itakuwa ni
kupoteza muda.
7. Wape wengine majukumu.
Kama
pengine kuna jambo ambalo unataka kulifanya wewe, lakini ukagundua wapo watu
ambao wanaweza wa kakusaidia katika jambo hilo ni vizuri ukawapa wakafanya.
Hiyo itakusaidia kufanya majukumu mengine zaidi na isitoshe utakuwa umeokoa
muda wako mwingi. Acha kung’ang’ania kufanya mambo yote wewe, wape na wengine
wakusaidie majukumu hayo ili kuokoa muda wako.
Kumbuka,
muda ni kitu cha thamani sana ambapo ukijenga tabia ya kuutumia vizuri utakuwezesha
kufikia mafanikio makubwa yanajitokeza katika maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika matumizi bora ya muda wako na
endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.