google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jul 28, 2015

Mambo Muhimu Ya kukusaidia Kukupa Furaha Katika Maisha Yako.

No comments :
Mara nyingi katika maisha yetu iwe kazini au katika jamii tunayoishi huwa ni watu wa kukutana na hali tofauti tofauti ambazo wakati mwingine huwa zinatupa furaha au huzuni katika maisha yetu. Lakini, pamoja na hali zote hizo kuweza kujitokeza katika maisha yetu suala la kuwa na furaha ama huzuni huwa linabaki mikononi kwetu sisi wenyewe.
Hii huwa iko hivyo kwa sababu, sisi ndiyo huwa ni watu wa mwisho wa kuamua maisha yetu tuyape furaha au huzuni. Kama tutakuwa ni watu wa kuchagua mambo ya kutupa furaha basi ni wazi maisha yetu yatajawa na furaha, lakini pia kama tutakuwa ni watu wa kuchagua mambo yakutupa huzuni pia maisha yetu yatakuwa ya huzuni hivyohivyo.
Hivyo, mpaka hapo unaweza ukawa unaona kuwa suala la kuwa na furaha au huzuni ni suala linalolenga uchaguzi zaidi katika maisha yetu. Kitu cha msingi na cha kuzingatia ili kuwa na furaha ni kuhakikisha wewe huathiriwi sana na mazingira ya nje katika kukupa furaha yako. Sasa je, ni mambo gani ambayo wewe unatakiwa kuyajua ili yakupe furaha ya kweli katika maisha yako?
1. Badili mtazamo wako jinsi unavyo yaangalia mambo.
Mtazamo ulinao juu ya maisha yako au jinsi unavyoyatazama mambo mara nyingi huo ndio unaokupa furaha au huzuni katika maisha yako. Watu wegi huwa wanatabia ya kuangalia mambo kwa mtazamo hasi sana. Kutokana na kuyaona mambo kwa mtazamo hasi ndivyo hujikuta wakipoteza furaha katika maisha yao.
Kama unataka kujenga furaha zaidi katika maisha yako kuwa na mtazamo chaya. Kama ulikuwa unahisi na kuona fulani ni mbaya sana kwako badili mtazamo wako na anza kumwangalia katika upande wa uzuri wake. Kwa jinsi unayozidi kuyaangalia mambo mengi kwa mtazamo chanya ndivyo utakavyoweza kujikuta unafurahia zaidi maisha na kuwa na furaha.

2. Fikiria majibu ya kile unachokitaka.
Wengi wetu huwa ni watu wa kufikiria sana matatizo waliyonayo badala yakufikiria njia za kutoka kwenye matatizo hayo. Hujikuta ni watu wa kuumia na kuwaza pengine kutokana na ugumu wa maisha walionao. Kwa kuendelea kufikiria matatizo badala ya kutafuta suluhu hivyo hupotezea wengi furaha.
Furaha ya kweli katika maisha yako haiji tu kwa kufikiria sana matatizo uliyonayo, inakuja kwa kutafuta suluhisho la matatizo hayo. Unaweza ukawa unajiona una mtatizo mengi sana yanakufanya ukose furaha, hiyo ni kweli lakini kitu cha msingi tafuta njia ya kuondokana na matazo hayo. Kwa kufanya hivyo utaijenga furaha siku hadi siku.
3. Angalia mambo uliyoyafanikisha.
Inawezekana ikawa unakosa furaha kutokana na malengo yako mengi kuona kama vile hayajatimia. Kwa kuangalia hivyo hiyo itakuumiza sana. Ili iweze kuondokana na hali hiyo jifunze sana katika maisha yako kuanglia mambo yale uliyoyafanikisha. Hata kama ni kidogo lakini kama ulifanikiwa kwa namna fulani jipongeze kwa hayo kwanza.
Kwa jinsi utakavyozidi kuangalia mambo uliyofanikiwa nakuyaweka katika orodha ndivyo itajikuta unaanza kupata nguvu ya kutenda zaidi na kuwa na furaha ambayo ulikuwa unahisi pengine umeipoteza kabisa. Siku zote kumbuka hili, jifunze kuyaangalia mambo uliyoyafanikisha. Mambo haya yatakusaidia kukupa furaha zaidi kuliko unavyofikiri.
4. Fanya mambo yatakayowapa furaha wengine.
Katika maisha yako kila siku fanya jambo, hata kama ni kidogo  litakaloweza kumpa mwingine furaha na siyo huzuni. Kama utamfanya mtu mwingne awe na furaha ni wazi kabisa lazima na wewe utajikuta unafuraha. Hiyo ni kanuni rahisi kabisa ambayo unaweza ukawa unaitumia kila siku katika maisha yako kukujengea furaha.
Watu wengi huwa wanategemea kupata furaha kwa wengine wakati wao huwa hawatoi hiyo furaha. Katika dunia hii mara nyingi unapata kile unachokitoa. Kama unatoa mafanikio, tegemea kupata mafaniko. Kama unatoa furaha, tegemea kupata furaha pia katika maisha yako. Hivyo ndivyo maisha yanavyokwenda.
5. Ishi na watu wenye furaha.
Kama utakuwa ni mtu wa kutafuta marafiki ambao muda mwingi wao ni watu wa huzuni, usitegemee kuwa na furaha katika maisha yako. Furaha ya kweli utaipata katika maisha yako kama utakuwa unazungukwa na watu wenye furaha zaidi. Unaweza ukawa unaanza kushangaa kwa nini hii iko hivyo?
Mara nyingi watu hawa watakusaidia kukuambukiza furaha hiyo nawe utajikuta ni mwenye furaha kama wao. Lakini kama unaishi na watu hasi watu wa kuhuzunika mara kwa mara, tambua utakachovuna hapo ni huzuni hizohizo. Watu wanaotuzunguka wanaathari kubwa sana katika maisha yetu iwe katika suala la furaha au mafanikio kwa ujumla.
6. Kila siku fanya kitu unachokipenda.
Inaweza ikawa ni kitu kidogo tu na cha kawaida unachokipenda lakini kama unakipenda kifanye kila siku kitakuongezea furaha. Kama wewe ni mtu wa kupenda kusoma vitabu soma walau kurasa chache tu, utaweza kutimiza furaha yako. Kama umezoea kuimba na unapenda kuimba, halikadhalika fanya hivyo hiyo itakuongezea furaha pia.
Kwa kawaida yale mambo tunayoyapenda hayo ndiyo huwa yanatuongezea furaha. Haijalishi mambo hao ni madogo au mkubwa kiasi gani lakini ni muhimu sana kwetu kuyafanya kila mara kama tu yanatupa furaha katika maisha yetu ya kila siku. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunayapa maisha yetu vile tunavyovihitaji na kujikuta ni watu wa furaha.
Kwa vyovyote vile iwavyo maisha yako unayouwezo wa kuyapa furaha ukiamua iwe hivyo kwako. Kwa kutegemea na kuamini kila siku kuwa maisha yako ni lazima yawe ya furaha na kufanya mambo yatakayokupa furaha katika maisha yako, hivyo ndivyo iatakavyokuwa ni lazima utakuwa na furaha. Kwa kifupi, hayo ndiyo mambo muhimu ya kukusaidia kukupa furaha maisha yako.
Ansante kwa kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO, endelea kuwashirikisha wengine kujifunza zaidi kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,





No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.