google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jun 17, 2015

Mambo 5 Unayoyapoteza Katika Maisha Yako Kwa Sababu Ya Kuwa Na Hofu.

No comments :
Kuwa na hofu ni kitu ambacho kila binadamu anacho, lakini kwa bahati mbaya hofu hizi zimekuwa zikiwatesa na kuwaumiza wengi zaidi. Hili limekuwa likitokea hivyo, kutokana na wengi wetu kuwa na hofu zilizopitiliza zaidi.

Je unajua ni madhara kiasi gani ambayo unaweza ukayapata katika maisha yako kutokana na wewe kuwa na hofu nyingi? Kwa haraka haraka naomba nikutajie mambo unayoweza kuyapoteza katika maisha yako ikiwa tu wewe utakuwa mtu wa hofu sana.  

1. Hofu inakupotezea mipango na malengo yako.
Hofu unazokuwa nazo katika maisha yako, mara nyingi huwa ni rahisi kuweza kukupotezea mipango na malengo yako uliyojiwekea. Hii huwa inatokea  kwa sababu unapokuwa una hofu zaidi unakuwa unajikuta unashindwa kufuata malengo yako uliyojiwekea kwa usahihi. Na hilo huwa linatokea pengine kwa sababu ya kuogopa ukubwa wa malengo uliyojiwekea.

Watu wengi kutokana kutawaliwa na hofu nyingi katika maisha yao, wamejikuta wakiwa ni watu wa kushindwa kutimiza karibu malengo yao muhimu ambayo wanajiwekea. Kiukweli ukiwa na hofu nyingi, tambua kabisa kuwa utaharibu mambo yako mengi katika maisha yako. Hivyo basi ni muhimu kuweza kumudu hofu ulizonazo ili kufanikiwa.

 2. Hofu inakupotezea ujasiri.
Unaweza ukawa jasiri na kuweza kusimamia maisha yako kweli, lakini unapokuwa una hofu kwa bahati mbaya huo ujasiri huwa huwa unatoweka. Hiki ndicho kitu kimojawapo ambacho hofu huweza kutupotezea katika maisha yetu. Tambua kuwa kwa kadri unavyozidi kuwa na hofu ule ujasiri na ushujaa wote hutoweka. Huwezi kuwa shujaa wa kweli kama ndani yako umejawa na hofu nyingi.

Kama haunielewi kwa hili sana, tuchukulie kwa mfano umeajiriwa iwe na serikali au kampuni fulani. Wakati huohuo kuna madai au haki fulani unazozidai kwenye eneo hilo unalolifanyia kazi. Ikiwa ndani yako utakuwa na hofu za kufikiri kuwa kwa kudai kwako haki zako unaweza kufukuzwa kazi uwe na uhakika, huwezi kufanya mabadiliko. Kwanini? Ni kwa sababu hofu inakuwa imekupotezea ule ujasiri bila ya wewe kujijua.


3. Hofu inakupotezea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.
Elewa kuwa, hakuna maamuzi yoyote ya maana ambayo unaweza ukayafanya ikiwa ndani mwako una hofu nyingi. Maamuzi yote mara nyingi utakayoyafanya wakati una hofu yatakuwa yana nia ya kukufanya uikimbie hofu hiyo inayokukabili. Hivyo kwa maana hiyo hayawezi kuwa maamuzi sahihi kwako zaidi ya kujilazimisha ili kwako upate unafuu fulani wa kutoka kwenye hofu.

Jaribu kufikiri kidogo katika maisha yako juu ya maamuzi ambayo umewahi kuyachukua ambayo yalikuwa ni ya hofu zaidi. Utakuja kugundua kuwa maamuzi uliyoyafanya hayakuwa yako na si hivyo tu pia hayakuwa sahihi kwako kwa asilimia zote. Bali ni maamuzi ambayo uliyafanya kutokana na hofu zako. Kutokana na hofu hizo ulipoteza uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.


4. Hofu inakupotezea fursa nyingi.
Ni rahisi sana kumkuta mtu akifanya kazi ileile hata kwa miaka ishirini bila kuiboresha na kwa bahati mbaya kazi hiyo inaweza kuwa haimsaidii sana hata yeye katika maisha yake. Hiki ni kitu ambacho nimekiona sana kwa maisha ya wengi wakiwa palepale bila kusogea kutokana na kuwa ving’ang’azi wa kazi ambazo hazina tija kwao eti kwa sabau ya mazoea, hivyo ni ngumu sana kwao kuweza kuzibadilisha.

Unapokuja kuchunguza kwa nini inakuwa hivyo kwao, jibu ni rahisi tu hofu walizonazo. Kutokana na hofu zao wanaogopa ikiwa wataacha kazi au watabadilsha biashara maisha yao yatakuwaje? Ni watu ambao hawana uhakika wa njia mpya, hivyo ni bora wabaki hapo walipo. Katika maisha yako hakuna kitu kibaya kama kupoteza fursa kubwa kwa sababuya hofu ulizonazo. Jifunze kuzikabili na zidi kusonga mbele.


5. Hofu inakupotezea furaha na amani ya kweli.
Hakuna utakachoweza kukifurahia katika maisha yako  ikiwa wewe umetawaliwa na hofu nyingi. Kikubwa utakachokuwa ukiwaza tu hizo hofu zako na mwisho wa siku utajikuta ile amani ya kweli ndani yako imetoweka kabisa. Unaweza ukawa shahidi kwa hili kwa kukumbuka zaidi kupitia maisha yako binafsi kuwa kipindi ambacho upo ama ulikuwa na hofu nyingi ni lazima ulikuwa ukikosa ile furaha ya kweli.

Si wewe tu jaribu angalia watu wote iwe jirani zako ama marafiki zako ambao hawana furaha sana. Ukija kuwaangalia sana watu hao kinachowafanya wawe hivyo  mara nyingi ndani mwao wanakuwa wana hofu nyingi zaidi. Hofu hizo huweza kuwapelekea washindwe kujiamini, kujiaona kama vile hawafai na zaidi ya yote furaha wanayokuwa nayo pia huweza kutoweka kabisa katika maisha yao. Hiyo yote inakuja kwa sababu ya hofu.


Kumbuka, unao uwezo wa kufanya mabadiliko katika maisha yako kila siku ikiwa utaamua hivyo. Hata hofu zako ulizonazo unaweza kuzibadilisha na kuishi maisha ya ushindi unayoyataka yawe kwako. Hayo ndiyo mambo muhimu utakayoyapoteza ikiwa utazidi kukumbatia hofu.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YAMAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,
dirayamafanikio@gmail.com

No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.