Dec 8, 2016
Kipimo Cha Mafanikio Kabla Ya Kuanza Mwaka Mpya.
Zikiwa zimebaki siku kadhaa ili
kumaliza mwaka huu, hatuna budi kuendelea kumuomba na kumshukuru mwenyezi Mungu
azidi kutupa neema na baraka zake ili tuumalize mwaka kwa vizuri na kuanza
mwaka mpya tukiwa ni watu wenye furaha mioyoni mwetu huku tukipanga mipango thabiti ili tuweze
kuuanza mwaka mpya vyema.
Lakini kama hiyo haitoshi maisha ya mafanikio huenda sambamba na kufanya tathimini, hatuwezi kuanza mwaka mpya, bila kufanya tathmini kwa yale ambayo tumeyatekeleza kipindi cha nyuma. Endapo utashindwa kufanya tathimini utashindwa kuelewa ni wapi ambapo ulishindwa kutimiza lengo lako.
Kufanya tathimini ni muhimu sana ili kuifanya akili yako itambue ya kwamba ni muhimu kuweka uchumbuzi yakinifu kwa mambo ambayo umeyafanya katika kipindi hiki kabla ya kumaliza siku 365 na kuanza mwaka mpya.
Inawezekana bado upo kwenye mataa na bado unashangaa uelekee wapi, wala usipate tabu kwa kuwa nataka tuweke mambo bayana ambayo yatukusaidia kufanya tathimini katika mwaka huu ambao zimesaria siku kadhaa kuisha.
Ipo hivi mwanadamu katika kila kitu lazima ajue mambo aliyoyofanya hupimwa katika njia kuu mbili ambazo ndiyo kipimo tosha cha mafanikio yako.
1. Ulichokisababisha.
Jambo la kwanza ambalo litakusaidia wewe kufanya tathimini ni kuangalia ni mambo gani ambayo uliyapanga na umekwisha yatekeleza? Si kuyatekeleza tu bali kuyatekeleza kwa ufasaha bila kujali changamoto ambazo umezipitia.
Ulichokisababisha ni mkusanyiko wa mambo yote chanya ambayo umeyafanya katika kipindi chote cha mwaka huu, hata hivyo kitu hicho ambacho umekifanya ni lazima kiwe kitu ambacho ni cha kuacha alama kwa watu wengine.
Au kama kitakuwa si cha kuacha alama, kitu hicho kitakuwa ni kitu ambacho kitakuwa fundisho kwa wengine ambao wanakutazama wewe. Kama umepanda miti hongera sana, kama umeanzisha biashara hongera pia, kama umejenga nyumba hongera kama umenunua gari hongera kwako, najua fika kwa hayo ambayo umeyafanya utasababisha utengeneze kitu kinachoitwa "wivu wa maendeleo" najua fika alama hiyo wengi wao watajifunza kutoka kwako.
2.Ulichokisuluhisha.
Jambo la pili na la mwisho ambalo nilitaka kuzungumza nawe, ni kwamba tathimini ya kile ulichokifanya lazima upime katika kuyatazama mambo ambayo umeyatatua, eidha katika jamii ambayo unaishi au mambo yako binafsi. Nazungumza katika hili nikiwa na maana siri kubwa ya mafanikio yako ipo katika usuluhisho wa changamoto.
Kama ulianzisha jambo lolote ujue fika hilo jambo ni majibu ya changamoto fulani, hivyo kwa namna moja ama nyingine kama endapo ulifanya hivyo na hujaweza kufikia lengo lako, unachotakiwa kufanya ni kuangalia sababu za msingi zilizokufanya ushindwe kufikia lengo na si kukata tamaa.
Kwani kama utakuwa ni mwenyeji wa kukataa tamaa tambua fika mtu aitwaye mafanikio utakuwa ni mgeni kwako. Ili kutengeneza ukaribu wa mafanikio yako kwa mwaka ambao unataraji kuanza hivi karibuni unatakiwa kupanga malengo yako upya huku ukibuni mbinu mpya za kuzitumia ili kufikia malengo mapya. Kwani huwezi kufanikiwa daima kama utaendelea kutumia njia ile ile kama unataka matokeo tofauti.
Imeandikwa na mkeleketwa wa Mafanikio Afisa mipango Benson Chonya.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.