Dec 15, 2016
Ifahamu Nguvu Ya Kufikiri Na Kushukuru Katika Maisha.
Katika vitu ambavyo wanadamu tumekuwa
hatuvitilii maanani ni vitu vikubwa viwili, vitu hivyo ni kufikiri na
kushukuru. Nimesema hivyo nikiwa na ushahidi tosha kwa kile ambacho nakiamini,
na pia ni sahihi kwa asilimia zote ambazo unazifahamu wewe.
Unashangaa kwanini nasema kwa
kujiamini? Wala usishangae bali tuendelee kusonga mbele mwanzo mpaka mwisho wa
makala haya ili tuweze kwenda sawa.
Ukweli ambao upo wazi ambao hauhitaji
hata mwanga wa jua ili kuonekana kwa watu wake upo bayana kabisa, ni kwamba
tumekuwa tukilalamika kwa kutoa sauti au hata kutotoa sauti ya kwamba maisha ni
magumu.
Yote hiyo inaweza ikawa hivyo kwa sababu watu tumeshindwa kuwekeza muda wetu katika suala zima
la kufikiri, huenda nikawa nimekuacha ila nataka tusemezane bila kuoneana haya.
Ipo sababu kubwa leo kuweza kutenga muda kwa kila siku angalau masaa mawili kwa
ajili ya kufikiri, si kufikiri tu bali kufikiri vitu vipya.
Kama unafanya biashara, kilimo au
kitu chochote ni vyema ukatenga angalau masaa hayo mawili kwa ajili ya
"kuwaza". Kufanya hivyo kutakufanya uweze kuwa bora hatimaye kuonesha
utofauti na wengine.
Itumie nguvu a kufikiri vizuri ikusaidie kufanikiwa. |
Hakuna maisha bora kama utaamua
kufanya kitu kile kile, kila wakati kwa njia ambazo umezizoea. Fanya kitu cha
tofauti kwa kuwa wewe ni wa tofauti.
Na kama ilivyo kauli mbiu ya mtandao
huu ni kwamba badili maisha yako kwa kuwa na fikra sahihi, hivyo fikiri sana
kwani fikra chanya huleta mabadiliko ya kweli hakuna jambo lolote litafanikiwa
kama litakuwa katika mtazamo hasi.
Lakini tukija katika upande wa pili
ni kwamba katika vitu ambavyo havipo katika tamaduni zetu ni jambo zima la
kutoa "Shukrani" kutoa shukrani ni jambo la faraja sana mbele za
Mungu na mwanadamu ambaye amekusaidia wewe kwa namna moja ama nyingine kuweza
kufika hapo ulipo.
Elewa na tambua ya kwamba usingefika
hapo ulipo kama ungesimama peke yako. Mbele ya Mafanikio yako kuna mtu nyuma
yake. Swali la kujiuliza ni shukrani gani ambazo umezitoa kwa mtu huyo?
Ukifikiri kwa umakini utagundua ya
kwamba hakuna hata mtu mmoja ambaye umewahi kutoa shukrani kwake, hii ni kwa
sababu shukrani zetu ni za mara moja kama mla ndizi.
Naendelea kujihoji pasipo kupata
majibu ni maisha gani hayo ambayo umeyachagua? Kwanini uishi maisha hayo
yasiyokuwa na faida na chukizo mbele za Mungu?
Unafikiri ya kwamba ukitoa shukrani
kwa Mwenyezi Mungu na mtu ambaye amekusaidia kuwa hapo utapungua uzito au
utafirisika? La
hasha binafsi naona kama ukiweka
utaratibu wa kushukuru itakusaidia kuweza kufanikiwa zaidi.
Huenda ninachokisema leo kikagusa moja
kwa moja. Utajiuliza labda leo Afisa mipango kaamuka na mimi, la hasha kwa kuwa
mawazo yangu hayana ukomo wa kuwaza wacha niseme tu, huenda yakagusa kwa namna
moja ama nyingine na yakakusaidia.
Nguvu ya kushukuru huongeza baraka za
kimafanikio kila wakati, haiwezekani wewe ukawa ni mtu kuomba tu kuliko
kushukuru, kufanya hivyo ni sawa na bure hata vitabu vya dini havijakaa mbali
nasi kwani vinatukumbusha ya kwamba "kila
ajuaye kuomba lazima ajue na kushukuru".
Hivyo jiwekee utaratibu wa kufikiri
na kushukuru ili uweze kupata amani ya moyo hatimaye kufikia ile ndoto kubwa
uliyonayo. Kama umenielewa vizuri baada ya kumaliza kusoma makala hii chukua
dakika chache kuwashukuru wote ambao wamekusaidia kufika hapo ulipo.
Lakini ikumbukwe kumshukuru mtu ni lazima
umwambie mtu huyo. Pia utakuwa mchoyo wa fadhira kama utashindwa kujishukuru
mwenyewe. Endapo nimekukwaza utanisamehe sana kwani wajibu wangu kukueleza
ukweli kila nipatapo nafasi.
Ndimi :Afisa Mipango Benson Chonya,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.