Jan 30, 2015
Haya Ndiyo Maajabu Makubwa Yanayoweza Kufanywa Na Mawazo Yako.
Kila dakika ambayo inapita
imeshakwenda zake, hairudi tena na hii ina maana kwamba, siku zako za kuishi
zimepungua tayari. Ni ajabu hata hivyo, kwamba kila mtu anasubiri siku moja,
siku fulani atakapofanikiwa jambo fulani, ndiyo aanze kufurahia maisha. Siku
hiyo haitafika, ni leo.
Kila dakika inayopita,
sehemu Fulani ya mwili wako, nayo imeondoka, imeharibika, hairudi tena. Lakini
inasikitisha kuona kwamba, kila siku watu wanajiambia kwamba, watafanya tu,
wakiwa hawajui kwamba, wanachakaa na muda sio mrefu watakuwa wameachana na
miili yao, na kuwa kitu kingine tofauti.
Kumbuka tu kwamba, kila
dakika inayopita, seli za mwili zipitazo bilioni tatu zinazalishwa mwilini ili
kuchukua nafasi ya nyingine za idadi kama hiyo ambazo zimekufa katika dakika
hiyo moja. Hatua hizi za mabadilishano ya seli hufanyika bila wewe kujua, kwa
sababu zinaongozwa na kusimamiwa na mawazo ya kina.
Unaweza bila shaka kuona ni
kwa namna gani, mawazo yako ya kina yana nguvu. Kwa mfano, mawazo haya ya kina
hupokea kiasi cha vitu au mambo 600,000 ya kiufahaumu kwa dakika moja. Hii ina
maana kwamba, mawazo hayo yana uwezo mkubwa sana, kuliko unavyofikiri na yana
uwezo wa kufanya chochote katika maisha yako.
Ni ukweli yana uwezo mkubwa
wa kupindukia. Hadi siku za karibuni, kompyuta ambayo ilikuwa na nguvu kuliko
nyingine duniani ile ya clay, ambayo ina uwezo wa kufanya mikokoto milioni 400 kwa
sekunde. Ili kuweza kufanya kazi inayoweza kufanywa na mawazo ya kina kwa
dakika moja tu, kompyuta hii inatakiwa kufanya kazi kwa kiwango hicho kwa miaka
100.
Je, huoni kwamba, mawazo
yako ya kina yana uwezo wa kuzalisha chochote, kufanya chochote, kubuni
chochote na kubadili chochote na kubadili chochote, kutokana na uwezo wake
mkubwa sana? Mawazo ya kina ndiye mjenzi wa maisha ya kila mmoja wetu, lakini
yanaweza pia kuwa mbomoaji wa kila kitu kutegemea tu unayatumia vipi.
Mawazo ya kina ndiyo mratibu
na mdhibiti wa mawazo yetu. Kama ilivyo nyuklia, huweza kutumika vizuri na
kuzalisha makubwa au kutumika vibaya na kuangamiza mamilioni. Mawazo yakina
yana nguvu kubwa kupindukia na kama kila mmoja angejua namna ya kutumia, dunia
ingekuwa haiko hovyo kama ilivyo leo.
Katika hatua za kuanzia, mtu
anatakiwa aamini kufikiri vizuri, kufikiri kwa njia ambayo itamsaidia, badala
ya kufikiri kwa njia ambayo itamuumiza na kumkera. Kufikiri vizuri ni kuamini
kwamba, mtu anaweza, kuamini kwamba, matatizo kwenye maisha ni changamoto na
siyo mwisho wa dunia au kushindwa kwako kabisa kama wengi wanavyofikiri.
Kutumia vizuri mawazo yetu
ya kina hakuwezi kuwepo kama kufikiri kwetu katika maisha ya kawaida ya kila
siku kumeharibika. Tukiwa na hofu, wasiwasi, chuki, visasi, hisia za kushindwa,
woga wa kutokea mabaya na kuvunjika nguvu kirahisi, inaweza kuwa vigumu kwetu
kuyatumia mawazo ya kina kwa faida yetu.
Mawazo yako ya kina
yanauwezo wa kufanya maajabu au chochote unachotaka katika maisha yako kama
utaamua kuyatumia vizuri. Kama unataka utajiri au furaha ni jukumu lako kuanza
kufikiria kwa vile vitu unavyovitaka na sio vinginevyo, hiyo ndiyo nguvu kubwa
ya mawazo unayotakiwa kuitumia na ikakusaidia kukufanikisha katika maisha yako.
Nakutakia mafanikio mema,
endelea kutembelea mtandao huu wa DIRAYA MAFANIKIO kwa kujiendelea kujifunza vitu vizuri zaidi,
karibu sana.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713048035/dirayamafanikio@gmail.com
Kama Unataka Kuwa Mtaalamu Katika Shughuli Unayofanya? Soma Hapa.
Si kila anayefanya shughuli fulani huwa na utaalamu nayo, wengine
wanaifanya kwa kuwa tu nafasi ilitokea ya kuifanya. Na hautachukua muda kumgundua
mtu anayefanya kazi zake kwa utaalamu, na yule anayebangaiza njaa tu, kwa
jinsi wanavyoenenda na tabia zao. Mara nyingi
waajiri na wateja hulalamika kuwa anayewafanyia
kazi hana utaalamu.
Yawezekana humalizi kazi vizuri, umemcheleweshea au hata
kumzungusha kwa muda mrefu bila taarifa sahihi. Si mara moja tunasikia
ni jinsi gani tunatakiwa kuwa wataalamu katika shughuli
tunazofanya. Kama unataka kupata mafanikio, kuchukuliwa kama mtu
makini, kuonekana una mchango kwa unaofanya nao shuguli zako, kuzifanya
kitaalamu ndio njia pekee ya kukufikisha huko.
Lakini tujiulize waajiri ama wateja
wanatafsiri gani juu ya utaalamu? Wengi wao watakuona mtaalamu ikiwa wewe: Unafika eneo la kazi
katika muda unaotakiwa; Unaifanya kazi uliyopewa vizuri; Unamaliza kazi kwa
wakati.
Unadhani kuna matukio mengine ambayo
unahisi ukiyafanya yatakuonyesha wewe si mtaalamu? Kuna matukio ukiwa
unayafanya yanakutafsiri moja kwa moja kuwa wewe si mtaalamu wa shughuli
unayofanya.
Kwa mfano ukiwa:- Unachelewesha kazi za watu, unahudhuria vikao
ukiwa haujajiandaa, unatumia muda mwingi kuongea umbea muda wa kazi, kuwavunjia
heshima wenzako, kuwasubirisha wateja
muda mrefu bila sababu za msingi, kuiba mawazo ya watu wengine kufanyia
shughuli zako bila kuwahusisha, na kuvunja ahadi zako mara kwa mara.
Hebu leo tuangalie njia kumi utakazoweza kutumia kuwa mtaalamu
katika shughuli yoyote unayofanya. Jitahidi kufanya shughuli zako kitaalamu na
watu waweze kukuamini, kukuheshimu, na kukuona una uwezo wa kipekee. Japo
mazingira ya kila kazi yanatofautiana lakini linapokuja suala la
utaalamu huwa na tafsiri moja dunia nzima.
Hebu tuangalie sifa za kuwa mtaalamu ni zipi:-
1. Umahiri.
Lazima uwe mahiri katika kile unachofanya, ukitumia ujuzi na
maarifa ya kutosha katika kazi yako ni lazima utaonekana mtaalamu na
watu. Ni muhimu kwako kujifunza hili ili kuweza kujenga uwezo mkubwa wa kufanya
kazi kwa ufanisi ambapo itakupelekea wewe moja kwa moja kuwa mtaalamu katika
kile unachokifanya. Na utakuwa mtaalamu kutokana kujifunza kwako mara kwa mara,
hivyo ni muhimu kuwa mahiri.
2. Zingatia muda:
Watu watakuwa wanakutegemea wewe ufike katika muda
unaotakiwa ili shughuli ziende na umalize kwa wakati. Sio kuendelea
kufanya shughuli zako kwa mazoea tu bila kujali muda, kwani hakuna anayependa
kumuamini na kumpa kazi mtu asiyemaliza kwa wakati. Kama utaendelea kuwa mtu
ambaye sio wa kutunza muda na unajidanganya kuwa eti unataka kuwa mahiri kwa kile
unachokifanya sahau katika maisha yako.
3. Uaminifu.
Unatakiwa kuwa muwazi wa shughuli zako, na wale
unaofanya ama unaowafanyia kazi nao wajue nini kinachoendelea. Ukianza
kujifanya mjanja mjanja, katika
shughuli unayofanya huku huwaweki wazi watu wengine hakuna
atakayekuona mtaalamu hata kidogo. Matokeo yake utajishushia heshima hasa pale
itakapobainika kuwa mambo yako hayaendi sawa kiaminifu zaidi.
4. Uadilifu.
Utaonekana mtaalamu ikiwa utakuwa unasimamia kanuni
za shughuli yako. Hakuna anayependa kumpa kazi mtu asiyejua kufuata kanuni
za kazi yake. Jifunze kufuata kanuni za kazi yako ili uwe mtaalamu uliyebobea
vinginevyo utajikuta unakuwa ni mtu wa kubabaisha katika eneo ulilopo. Zingatia
pia misingi ya maadili kati yako na wafanyakazi wenzako hilo ni jambo la
msingi.
5. Heshima.
Kama huna heshima kwa watu wengine unaofanya nao au
unaowafanyia shughuli basi hautaonekana mtaalamu hata kidogo. Ni muhimu
sana kwako kuchunga heshima kwa wafanyakazi wenzako hata kama umewazidi cheo ni
lazima uwe na heshima kwao. Kuwa na heshima tambua kuwa hiyo ni nguzo kubwa
wewe ya kuweza kukutambulisha kuwa wewe umebobea na ni mtaalamu katika kazi
yako na wala si mbabaishaji.
6. Ongeza ujuzi.
Tafuta ujuzi wa ziada, usiendelee kung'ang'ania ujuzi ule
ule kila siku. Toka nje ya yale unayoyafahamu ili kupata mengine
mapya kuongezea katika yale unayayafahamu ili kuboresha zaidi
utendaji. Kama utaendelea kung’ang’ania kuwa na ujuzi ule ule bila ya wewe
kutaka kubadilika na kujifunza kitu
kipya, elewa kabisa utakuwa unajipunguzia sifa za kuwa mtaalamu kwa kile
unachokifanya.
7. Mtazamo chanya.
Kama wewe kila siku unaangalia makosa tu bila kuwa na mtazamo
chanya juu ya shughuli unayofanya kuwa mtaalamu itakuwa ndoto kwako. Ni lazima
uwe na mtazamo chanya ili ujue nini cha kufanya kuliko kuangalia makosa tu kila
wakati ambapo hayo makosa yanaweza yakakupunguzia na kasi ya kufanya vitu
vingine vitakavyoweza kubadili mwelekeo wako na pengine kukufanya kuwa mtaalamu
zaidi.
8. Toa msaada:
Wasaidie wenzako unaofanya nao shughuli sio kwa kuwa wewe
unafahamu kitu fulani basi hutaki wenzako wafahamu. Waonyeshe jinsi
ya kufanya kazi vizuri pale unapoweza na wasikilize pale
wanapokuuliza maswali. Unapowasaidia wenzako ambao unakuwa unafanya nao
kazi hii inakufanya kila siku utajikuta unaongeza utaalamu wako katika maisha
yako.
9. Tenganisha matukio.
Usihusishe matukio ya nyumbani au mtaani na kazi, ukiwa
katika shughuli zako weka mawazo yako yote hapo. Utakuwa mtu wa ajabu
kufika eneo la kazi na kuanza kushughulikia masuala ya nyumbani huku
ukiacha kazi haziendi. Jifunze kufanya kazi
kwa uangalifu ili usije ukajikuta unaupoteza muda wako mwingi pasipo
kujijua hiyo inaweza ikawa ni hatari sana na itapunguza utaalamu wako.
10. Kuwa msikivu.
Kila mtu ana hitaji la kusikilizwa pale anapokuwa
na jambo la kusema,
Kwa hiyo wape watu nafasi ya kukuelezea yale wanayodhani
yatasaidia katika utendaji wa kazi. Acha kuwa king’ang’azi wa kutaka
mipango yako au mambo yako ndiyo yatekelezwe na kusahau usikivu unaotakiwa kuwa
nao hata wewe ili kuleta ushirikiano utakaoleta ufanisi hata kwako na kukufanya
kuwa mtaalamu zaidi.
Kila mmoja
wetu anapenda kupata mafanikio katika shuguhuli ile anayofanya, basi tuanze sasa kufanya kazi kitaalamu ili
tuweze kufikia yale tunayoyataka. Nakutakia mafanikio mema, karibu DIRA YA MAFANIKIO uendelee kujifunza na kuhamasika kila siku.
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 035/dirayamafanikio@gmail.com.
Jan 29, 2015
Kama Hupati Matokeo Mazuri Kwa Kile Unachokifanya, Soma Hapa Kujua Nini Cha Kufanya.
Umewahi kuona ama kusikia
kuhusu watu waliojaribu bidhaa au kufanya biashara hii na ile na kupata
mafanikio makubwa lakini unapojaribu wewe hupati matokeo mazuri? Je, umekuwa
mtu anayeona hakuna kitu kinachoweza kukusaidia kupata mafanikio makubwa katika
maisha yako? Huenda umekuwa ukijaribu kutumia njia fulani za kuboresha maisha
yako, inayoonekana kuwa nzuri sana,
lakini umechoshwa sana na kukwama kila wakati.
Mara kwa mara umekuwa
ukijitahidi kufanya hiki na kile lakini umekuwa huoni matokeo hasa ya kile
unachokitaka. Kuna wakati umekuwa ukijiuliza pengine una mkosi au nini shida?
Na imekuwa ikifika wakati unaanza kujihisi kutaka kukata tamaa kwa kile
unachokifanya na kuona kuwa maisha kwako tena basi hayawezekani. Hebu tutazame
jinsi unavyoweza kuwa umefikia hatua hiyo uliyopo na sababu zinazoweza
kupelekea mambo haya kukutokea.
Kwanza, huenda kuna wakati
ulijaribu kitu ama kwa kufuata ushauri, ama maelezo uliyosoma, ama kwa kuona
mafanikio ya mtu mwingine. Kimsingi, umejaribu njia hiyo kwa kufuata uzoefu
mzuri wa mtu mwingine. Hata hivyo ulipojaribu, hukupata matokeo kama
uliyotarajia, ukaamua kuamini kuwa haikukusaidia. Lakini mawazo haya ni kweli
kiasi gani? Mara nyingi, tena mara nyingi sana, matokeo ya vitu vya aina moja
kwa watu tofauti huwa tofauti na ni kosa kujihukumu na kujilinganisha na watu
wengine. Pengine ulihitaji muda zaidi. Huenda mazingira yako ni tofauti kabisa.
Bila kujali hayo na jinsi
ulivyofikia, ulijijengea ukweli ndani ya nafsi yako na ukweli huo ni kwamba ‘jambo hili halikukusaidia’ ingawa kwa
ukweli wa ndani kabisa, ukweli wako huo uliegemea kwa juu kwenye ulinganifu wako
na mtu mwingine na ambaye hauna uhusiano wowote wa moja kwa moja nawe na kile
ambacho ni bora kwako. Ni vema ukafahamu pia kwamba matokeo na mafanikio yote
hayo unayoyaona kuhusu mtu huyo mwingine, yalikuwa kwa wakati ule
uliozungumziwa na hiyo haina maana kwamba sasa ni zamu yako kutumia njia ama
ushauri huo na kwamba matokeo mazuri kama yale yatakutokea nawe.
Kuanzia hapo, kila kitu
utakachokijaribu kitafananishwa na kuhusishwa na matokeo ya kile cha kwanza,
huku ukiwa na ukweli ndani yako ambao mwangwi wake unazidi kuunguruma wa ‘hili halikunisadia mara ya kwanza ngoja
tuone safari hii kama litaweza’ tayari unakuwa kama unajipiga vita. Inawezekana hukutarajia kushindwa kwa
njia ya moja kwa moja, lakini tayari unauona uwezekano huo na uamuzi wako
umeegemea kwenye matokeo mabaya ya mwanzo.
Kwa kadri unavyojaribu mambo
mengi ukiwa na mawazo haya, ndivyo unavyozidi kuyajenga mawazo haya ndani yako.
Hatimaye inakuwa ni dhana iliyojaa ‘hakuna
kitu kitakachosaidia.’ Kabla ya kutambua hilo, hiyo ndiyo aina ya mtu utakayokuwa.
Mtu unayejaribu kufikia malengo fulani maalumu ama kujaribu kitu hiki ama kile
ama teknolojia ile na kuwa na kauli ndani yake kwamba, ‘wengine wanafanikiwa lakini si mimi’
Sasa nini cha kufanya kama
hupati matokeo mazuri kwa kile unachokifanya ukilinganisha na wengine? Ni vipi
utaweza kijitoa kutoka kwenye mzunguuko huu? Kwanza, fahamu jinsi ulivyofikia
huko, kwa kuilinganisha nafsi yako na matokeo ya watu wengine walioko kwenye
njia tofauti kabisa nawe, ingawa huenda walikuwa wakitafuta matokeo kama
unayoyataka wewe hivi sasa.
Halafu ujijengee dhana yako.
Iruhusu nafsi yako kupata mafanikio kimtindo wake, bila kuamua kwa kuangalia
kile kilichowatokea watu wengine, au matakwa yaliyowekwa na watu wengine zaidi
yako wewe. Na ni pale utakapoamini kwamba unayo haki ya kufanikiwa, na ni kwamba,
na ni kwamba utafanikiwa, ndipo maisha yako yatakapobadilika. Kila utakachokijaribu,
kitakusaidia kwa sababu, umefahamu kwamba kinatakiwa kukusaidia wewe na si mtu
mwingine.
Subira yako ya ndani na
kutokuwa na maamuzi ya kabla ya mafanikio unayotaka, yenye kuegemea nje ya
nafsi yako, itafanya kazi kwako kwa nguvu kubwa na utarudiwa na uwezo wako na
kuweza kudhibiti mwelekeo wa mambo yako. Lakini kikubwa, jiwekee na wewe
malengo yako na kuwa tofauti na kufanya mabadiliko kwa kile unachokifanya
ukilinganisha na wengine uliwaona, hii itakusaidia kukuletea matokeo tofatuti
katika maisha yako.
Nakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa
kupata maarifa bora, yakayokuwa msaada mkubwa kwa maisha yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713048035/dirayamafanikio@gmail.com
Jan 28, 2015
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kumudu Kuishi Katikati Ya Tufani Za Kimaisha.
Ukijaribu kutafakari jinsi
binadamu anavyokumbana na matatizo magumu ya aina mbalimbali ya kimaisha,
huenda unaweza ukahisi hali fulani ya kukata tamaa na hata kujiuliza kwamba, ni
kwa jinsi gani binadamu huyu anaweza kukabiliana na hata kujikwamua kutoka
kwenye hali hizo zinazokatisha tamaa. Hebu jaribu kukumbuka matatizo ya
kiuchumi, ugaidi, magonjwa mabaya ya kuambukiza, vita na migogoro mbalimbali ya
kijamii, majanga ya asili na mengineyo.
Yote hayo kwa muda mrefu
yamekuwa ndiyo changamoto kubwa kwa binadamu. Hata hivyo, ukweli ni kwamba,
bado kuna uwezekano mkubwa kwa binadamu huyu kuendelea kustawi na kushamiri
kimaisha pamoja na kuzungukwa na matatizo hayo. Mambo yafuatayo yanaweza
kumsaidia mtu katika harakati zake za kuyaboresha na kuyaendeleza maisha yake
katikati ya changamoto hizo.
1.
Jifunze kuangalia mambo kwa mtazamo chanya.
Litazame kila jambo
linalokujia au kukupata kwa jicho lenye mtazamo mzuri na chanya. Katika suala
hili inapaswa kukumbuka kwamba ,
kunapotokea hali fulani itakayosababisha watu kusongeka, ujue kwamba, siyo
lazima kila mtu asongeke na kwamba kunapotokea maradhi mabaya ya kutisha na
yanayosababisha vifo, siyo lazima kila mtu afe. Huu ndio ukweli wenyewe, na
bila shaka huwa tunahuzunika na kujisikia vibaya, pale tunapoona wenzetu
wanateseka. Lakini hata hivyo, mateso yasiyo ya lazima yanatokana na hofu
wasiwasi wetu hayana faida kwetu zaidi ya kutuumiza na kutuacha tukiwa wagonjwa
hoi vitandani mwetu.
2. Fanya
yale unayoweza kuyatimiza, usiyoyaweza achana nayo.
Wakati wote unapaswa
kujiandaa kama vile askari wanavyofanya. Ujifunze kuzitupilia mbali hofu zako.
Kwa kufanya hivyo utajiongezea uwezo wako wa kustarehe na kuburudika na maisha
yako. Kwa kawaida, hofu iliyofika katika kiwango kikubwa na cha kudumu ni nguvu
za kukuondolea uwezo wako wa kukabiliana na kupambana na hali ngumu zozote zile
zinazokujia. Hivyo, kufanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya hali hizo za
kutisha na kukatisha tamaa, ni jambo muhimu na linalopaswa kuzingatiwa kwa
makini ili tuweze kuishi maisha yasiyotuelemea.
3. Yasawazishe
maisha yako.
Fanya kila uwezalo, ili
uweze kuyasawazisha maisha yako kwa kufanya kazi zako za kila siku kwa bidii,
maarifa na kwa kufuata utaratibu uliojiwekea. Pia unapaswa kujiwekea muda kwa
ajili ya kufanya mambo yanayokuhusu wewe binafsi, familia yako, hata jamii yako
kwa ujumla. Ukiwa unafanya hivi mara kwa mara utakuwa unajijengea uwezo mkubwa
wa kupambana na kila hali ngumu inayojitokeza katika maisha yako.
4.
Tafakari kwa kina, Sali na uwe mwenye shukrani.
Hebu tafakari, Sali au hata
ufikirie kidogo kuhusu Baraka za namna mbalimbali unazozipata ambazo zinatokana
na wewe kuwa hai. Unaweza pia ukatembea tembea kwenye maeneo yenye kuvutia na
kujiburudisha, kama vile bustanini, kwenye ufukwe wa bahari, na mbali kwingine
kotekote unakohisi kwamba, kuna mandhari ya asili. Kutafakari kwa kina ni njia
ambayo imethibitika kuwa na nguvu ya kupunguza sononi, na vilevile kuzingatia
kwa makini masuala ya kiroho huongeza kwa kiwango kikubwa ile hali ya kuwajali,
kuwathamini na kuwahurumia watu wengine.
Ukweli ni kwamba jawabu kwa
kila tatizo lipo, hata katikati ya matatizo na vurugu nyingi, bado unaweza
kulipata. Hivyo unapoamua kuutumia ushauri huo hapo juu, unaweza kujiongezea
amani yako ya akili na kuridhika na maisha yako, mambo ambayo ni muhimukutumika
kwenye maandalizi yako ya kupambana na changamoto mbalimbali za kimaisha.
Kumbuka tu kwamba, walioweza kuokoka wakati wa mauaji ya halaiki kwenye kambi
dhalili za mauaji za Hitler, wengi ni wale waliokuwa na matumaini, wale ambao
walikuwa wakijiambia kila wakati kwamba, kila penye vurugu, pana suluhu.
Nakutakia mafanikio makubwa na
endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza na
kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713048035/dirayamafanikio@gmail.com
Jan 27, 2015
Sababu Sita Zinazokufanya Ushindwe Kufikia Mafanikio Makubwa Katika Maisha Yako.
Kuna wakati katika
maisha yako unaweza ukajikuta unafanya kila kitu cha kukusaidia kukufanikisha,
lakini ukawa unashangaa mambo yako hayaendi vizuri kama unavyofikiri au kutarajia
. Mara nyingi hiki huwa ni kitu cha kuumiza ubongo na inabidi wewe mwenyewe
binafsi utulie ili kujua nini chanzo au sababu hasa inayopelekea wewe ushindwe
kufikia mafanikio unayoyata katika maisha yako.
Kiuhalisia, huo zipo sababu zinazopelekea ushindwe kufikia mafanikio
makubwa, ingawa kwa wengi huwa sio rahisi kuweza kuzijua na kuzitambua kwa
haraka. Kama unataka kufanikiwa,
hakikisha unazijua sababu hizi zinazokuzuia wewe kufanikiwa.
1.Unatumia
muda wako vibaya.
Mara nyingi umekuwa
ukiishi maisha ya kupoteza muda wako hovyo. Haya ndiyo maisha ambayo umekuwa
ukiishi kwa muda mrefu na umekuwa ukiiona ni kitu cha kawaida tu, kupoteza muda
wako bila sababu. Kitu usichokijua ni kuwa muda ni kitu muhimu sana katika
kutimiza malengo yako uliyojiwekea. Hakuna mipango wala malengo yoyote hapa
duniani, ambayo utaweza kuyatimiza kama utakuwa ni mtu wa kupoteza muda kila
mara katika maisha yako.
Ukijaribu kuchunguza
kwa makini, utagundua kuwa watu wengi wasio na mafanikio hapa duniani ni wale
ambao pia matumizi yao ya muda ni mabovu. Hawa ni watu ambao wanauwezo
wakishinda wakipiga soga kutwa nzima wakiongea hili mara lile hata kwa yale
yasiyo na maana, ni watu ambao wanauwezo wa kushinda kwenye mitandao ya kijamii
karibu kutwa nzima na ni watu pia ambao usishangae ukakutana nao kila mahali
wao wapo tu. Kama unaishi maisha haya ya kuchezea muda hivi, nakupa pole, uwe
na uhakika utakufa maskini na ndio kitu ambacho kinakufanya ushindwe kufikia
mafanikio makubwa.
2.Umekuwa ukiahirisha sana mipango na malengo yako.
Jaribu kujiuliza
mwenyewe ni mara ngapi umekuwa ukisema nitafanya hik na hiki kesho na inapofika
kesho hufanyi tena na imekuwa kwako sasa kama ni kawaida na umezoea. Kama utakuwa wewe ni mtu wa
kuahirisha mipango na malengo yako uliyojiwekea kaika maisha yako itakuwa ngumu
sana kutimiza hayo malengo yako. Kwa sababu hiyo kesho unayoisubiri na kusema
kuwa utafanya haitafika.
Kitakachobaki kwako
ni kila siku itakuwa kesho kesho na utajikuta ndivyo unavyozidi kupoteza muda
wako na fursa muhimu za kukupatia mafanikio katika maisha yako. Kama kweli
umemua kufanya mambo yako yafanye sasa hata kama ni kwa kidogo wewe fanya tu.
Achana na habari ya kesho, ambayo unaingoja kila mara, hiyo haitafika milele.
Kama unataka kubadili maisha yako na kuwa ya mafanikio makubwa, acha kuahirisha
mambo yako.
3.Umekuwa ukiishi maisha ya visingizio sana.
Hii ni sababu kubwa
sana inayokufanya ushindwe kusonga mbele katika maisha yako kutokana na
visingizio vingi ambavyo umekuwa navyo. Umekuwa ukitoa visingizio mara kwa mara
kila kukicha kwa nini hufanikiwi. Hebu angalia ni mara ngapi umekuwaukisema
huwezi kuanzisha biashara kwa sababu huna mtaji, ni mara ngapi umekuwa ukisema
unashindwa kutoka kwenye umaskini kwa sababu una wategemezi wengi na hujiwezi.
Umekuwa una visingizio hivyo ambavyo vyote ni kama unajitetea tu.
Lakini, sababu kubwa
inayokufanya ushindwe kufanikiwa katika maisha yako ni wewe mwenyewe. Unao uwezo
mkubwa wa kubadilisha maisha yako ukitaka na hakuna kitu cha kukuzuia. Kama
ukiamua leo hii, ukaachana na visingizio vingi ambavyo umekuwa navyo, elewa
kabisa utabadili maisha yako kwa asehemu kubwa sana na utaanza kuishi maisha
unayoyataka. Visingizio visiwe sababu yaw wewe kuzuia kufikia mafanikio yako,
jifunze kuwajibika na chukua hatua juu ya maisha yako.
4.Umekuwa ukikata tamaa sana mapema.
Haijalishi umeshindwa au umekosea mara ngapi
kwa kile unachokifanya, kitu ambacho hutakiwi kufanya katika maisha yako ni
kukata tamaa. Unapokuwa unakata tamaa unakuwa una utangazia ulimwengu kuwa
mafanikio kwako basi tena. Kukata tamaa ni sababu ya kwanza ambayo inapelekea
wewe ushindwe kwa kila kitu unachofanya katika maisha yako. Kama umeshindwa
jambo na unafikiria kuwa upo mwisho wa safari na huna sehemu nyingine ya kwenda, tambua unajidanganya nafsi
yako.
Umejifunga jela mwenyewe na mawazo yako ya kujikatisha
tamaa. Kwa kufikiria hivyo ni kujitengenezea nafasi ndogo ya kufanikiwa
katika unalolifanya,na nafsi yako itaanza kuamini wewe ni mtu wa kushindwa. Tunaishi katika ulimwengu wenye njia nyingi za kufanikiwa
katika yale tunayojishughulisha nayo. Kumbuka pia wakati mwingine ni
lazima kushindwa mara nyingi ili ufanikiwe. Na ndio maana unaposhindwa mara
moja sio mwisho wa kila kitu. Wazo lako lolote ambalo
limeshindwa kazi,linafungua njia ya wazo litakaloshinda.
5. Umekuwa ukiishi maisha
ya kuwa na mitazamo hasi sana.
Wewe ni matokeo ya
kile unachokifikiri na kukiamini katika maisha yako. Kama unaamini utafanikiwa
ni kweli utafanikiwa na kama uaamini maisha yako ni kushindwa ni ukweli
usiopingika lazima ushindwe . Ni mara nyingi umekuwa ukishindwa kufanikiwa na
kufikia malengo yako makuu kutokana na fikra hasi ambazo umekuwa ukizibeba sana
kila siku. Mara ngapi umekuwa ukiamini ya kuwa mafanikio wamejaliwa wengine na
wewe ukijitoa kabisa? Kama unataka kubadii historia ya maisha yako, jifunze
kuyaangalia mambo kwa mtazamo chanya zaidi, utafanikiwa.
6. Umekuwa mwongeleaji sana juu ya ndoto zako.
Ili uweze kufanikiwa
na kufikia malengo yako ni muhimu sana kwako wewe kuwa mtu wa kuchukua hatua
kwa vitendo mapema sana. Kama utakuwa wewe ni wa kuongea na hauchukui hatua
yoyote dhidi ya ndoto zako itachukua muda sana ama haitawezekana kabisa kufikia
malengo yako. Watu wengi wamejikuta wakiwa ni waongeleaji sana juu ya ndoto
zao. Kuongelea sana juu ya ndoto na mipango mizuri uliyonayo hakutakusaidia
kitu na ndicho kitu ambacho kimekuwa kikikuzuia ushindwe kufikia malengo yako
makubwa uliyojiwekea mara kwa mara.
Nakutakia kila la kheri katika
safari yako ya mafanikio makubwa na endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YAMAFANIKIO kila siku kujifunza zaidi, mpaka maisha yako yaimarike.
IMANI
NGWANGWALU,
0713048035/dirayamafanikio@gmail.com
Jan 24, 2015
Hiki Ndicho Kitu Kinachokufanya Ushindwe Mara Kwa Mara Katika Maisha Yako.
Habari za leo ndugu msomaji
wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO, naamini umzima na unaendelea na jitihada
za kuboresha maisha yako. Nakukaribisha tena kwa moyo mkunjufu katika makala
hii ya leo ambayo ipo kwenye mfumo wa simulizi ambapo kupitia simulizi hii
utajifunza vitu vya muhimu vinavyohusiana na maisha yetu kwa ujumla ya mafanikio
tunayotafuta kila siku. Kupitia simulizi hii utajifunza na kutambua mambo
muhimu ambayo unatakiwa uyafanye na yatakayokuletea mabadiliko makubwa sana
katika maisha yako.
Wakati fulani, mtu mmoja
alinisimulia kisa ambacho kilinifundisha ukweli mkubwa zaidi kuhusu maisha. Mtu
Yule alinisimulia kuwa kulikuwa na bwana mmoja ambaye alienda kwa kinyozi.
Wakati anaendelea kunyolewa kulizuka mjadala wa masuala mbalimbali . Mjadala
huo, hatimaye ulifika mahali ambapo kinyozi na mteja walijikuta wakijadili
masuala ya Mungu. Kinyozi alisema, ‘mimi
naamini kabisa hakuna Mungu.’ Yule mteja( Yaani Yule bwana anayenyolewa)
alimuuliza, ‘ni kwa nini unaamini kwamba,
hakuna Mungu?’
Kinyozi kwa kujiamini kabisa
alisema, ‘naamini hivyo kwa sababu, ukienda hapo mtaani hata sasa hivi
utathibitisha. Kuna mateso kibao utayaona. Naamini, kama Mungu angekuwepo
kusingekuwa na watu wanaoumwa, watu maskini kila mahali, watu wanaouawa bila
sababu na uovu ambao umejaa hivi sasa duniani.’ Yule mteja hakuwa anataka
kubishana kuhusu masuala ya Mungu, hivyo aliamua kunyamaza. Kinyozi alimnyoa na
kumaliza kazi yake, ambapo mteja alitoka nje.
Yule mteja alipofika nje
alimwona mtu mmoja ambaye alikuwa na nywele chafu na ndevu nyingi zinazofanana
na ukoka kwa uchafu. Kuona vile, Yule mteja alirudi hadi pale kwa kinyozi na
alipoingia tu ndani alimwambia, ‘ naamini hakuna vinyozi’. Yule kinyozi
alimtazama mteja wake kwa wasiwasi, kabla hajamwambia, ‘hakuna vinyozi wakati
mimi unaniona hapa, na nimemaliza mara hii tu kukunyoa?’ Yule mteja alimwambia,
‘kama ingekuwa kuna vinyozi, kusingekuwa na watu wenye nywele ndefu na chafu
huko mtaani.’
Yule kinyozi kwa kujiamini
kabisa kwamba, ameshinda, alisema, ‘ sasa kama ni kunyolewa si hadi waje hapa
ofisini, wanifuate, ndiyo watahudumiwa….’ Yule mteja alimwambia, ‘basi Mungu
pia yupo, bali ni hadi wenye shida na matatizo wamfuate na kumjua na kumkubali,
ndipo ambapo watapata ahueni kupitia kwake.’ Halafu alitoka nje na kuendelea na
shughuli zake.
Ndivyo ilivyo, watu wengi
huwa wanadhani kitu au jambo fulani halipo kwa sababu tu hawajui jambo au kitu
hicho kinavyofanya kazi. Siyo lazima Mungu, kila kitu kina kanuni ya namna
kinavyoweza kujidhihirisha katika hali halisi. Utakuta mtu anakwambia,
haiwezekani kufanikiwa kama hujasoma, haiwezekani kufanikiwa kama huna refa,
haiwezekani kufanikiwa kama huna au hujafanya kile na kile. Lakini, kati ya hao
wanaosema, hakuna hata mmoja ambaye amefanya au amethibitisha nadharia yake.
Ni kwa kuona tu watu wakiwa
na shida njiani, wanaamini kwamba ni majibu kwamba Mungu hayupo. Kwa kuona
maskini wengi hawana hela wala mali, wanaamini kwamba, hiyo ni dalili ya
kutokuwezekana. Kama ilivyo kwa Mungu, hata mafanikio yoyote yale ni lazima mtu
ayafuate kule yaliko. Kwa kuyafuata mtu atakutana nayo, kwa kunyoosha miguu tu,
ni kweli hatayapata. Kila kitu hapa chini ya jua kinakwenda kwa kanuni, tofauti
na watu wengi wanavyofikiri na kudhani.
Kwa hiyo, kama mtu
anataka kujua kitu fulani kipo au hapana, inabidi ajifunze kanuni zake. Ni
hatari sana kusema haiwezekani kufanikiwa kwa kuwa wewe u maskini au umeshindwa
kuyafikia mafanikio unayoyataka, haiwezekani kwa sababu njia zimezibwa. Ni
hatari kwa sababu, anachokiona mtu mara nyingi ni umbumbumbu wake au udhaifu
wake. Fumbua macho sasa! Ubadili maisha yako kabisa. Achana na fikra za kudhani
haiwezekani, tafuta njia kwanini hufanikiwi na kisha songa mbele. Kama utakuwa
mtu wa hivi tu, mtu wa kufikiria hufanikiwi kwa sababu zako binafsi zisizo na
maana, basi utakuwa umeng’ang’ania kitu kinachozuia mafanikio yako na hiki
ndicho kitu kinachokufanya ushindwe mara kwa mara katika maisha yako.
Nakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa
kupata maarifa bora, yakayokuwa msaada mkubwa kwa maisha yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 035/dirayamafanikio@gmail.com
Jan 22, 2015
Kama Unataka Kuwa Mjasiriamali Mwenye Mafanikio Makubwa, Acha Kufanya Mambo Haya.
Mara nyingi huwa sio kitu
kigeni kwa mtu ambaye ni mjasiriamli
wakati mwingine kufanya maamuzi yasiyo sahihi, kukosea hapa na pale na hata
wakati mwingine kufanya biashara na watu ambao sio sahihi ambao wanauwezo wa
kukurudisha nyuma, hii huwa inatokea sana bila kujua. Hiyo yote inakuja kutuonyesha kuwa
katika suala zima la ujasiriamali makosa huwa yapo na ni muhimu sana kuweza
kutusaidia kusonga mbele pale tunapochukua jukumu la kujifunza kutokana na
makosa. Hata hivyo huwa yapo makosa ambayo huwa tunaweza kuyaepuka ikiwa kweli
tuna nia ya kuwa wajasiriamali wakubwa. Kama unataka kuwa mjasiriamali mwenye
mafanikio makubwa, acha kufanya mambo haya:-
1. Acha
kuogopa sana ushindani wa kibiashara.
Ili uwe mjasiriamali mwenye
mafanikio makubwa, kitu pekee ambacho hutakiwi kuogopa sana ni ushindani wa
kibiashara. Badala ya kuogopa ushindani kaa chini na kisha ujifunze ni kitu
gani unachotakiwa ufanye katikati ya ushindani huo mkubwa unaouona. Kama una
jiamini na bidhaa zako sokoni au biashara yako huna haja ya kuogopa sana
upinzani. Wajasiamali wengi kuna wakati huwa ni waoga sana wa ushindani kiasi
cha kwamba hutumia pesa na njia nyingine mbaya kukabiliana na upinzani. Badaa
ya kuogopa upinzani, jifunze sana kutengeneza wateja wapya, kuboresha huduma
zako na kila siku mafanikio utayaona katika biashara yako na utakuwa umefukia
ushindani.
SOMA:
Kanuni Muhimu Katika Kuendesha Biashara Yako, Ili Iwe Na Mafanikio Makubwa. (Bonyeza hapa kusoma)
2.
Acha kutaka kujihusisha na kila biashara.
Ni muhimu kuzingatia na
kuweka nguvu zako zote hasa kwenye biashara yako hususani katika kipindi
ambacho biashara yako haijakuwa sawasawa. Katika kipindi ambacho unaendeleza
biashara yako ili ikue na kufikia viwangi vya juu unavyotaka acha kupenda
kujihusisha na biashara nyingine ambazo zinaweza kukupunguzia nguvu kwenye
biashara kubwa. Watu ama wajasiriamali ambao mara nyingi huwa ni watu wa tamaa
kwa kutaka kila kinachopita mikononi mwao wakifanye. Hili ni jambo la hatari,
kwa sababu mambo mengi hutaweza kufanikisha yote kwa pamoja.
3.
Acha kuwa na malengo ya muda mrefu wakati wote katika biashara yako.
Katika biashara kuna wakati
mambo huwa yanabadilika tena kwa kasi kubwa sana kuliko. Unapokuwa mjasiriamali jukumu lako kubwa ni kuhakikisha unaifikisha
biashara yako mahali ambapo ni salama hata kama kuna wakati mambo yanabadilika.
Hii ikiwa na maana kuwa kuna wakati, inabidi ujifunze kutokufikiria sana
biashara yako itakavyokuwa baadae na kujikuta umesahau majukumu yako ya sasa ya
kuifanya biashara yako ili isimame na kusonga mbele. Kumbuka si maanishi usiwe
na malengo ya muda mrefu katika biashara yako, ninacholenga hapa usifikirie
muda wako wote kwa jisi biashara yako itakavyokuwa na kusahau sasa hiyo ni hatari kwako.
4.
Acha kuwa na makadirio makubwa ya faida.
Jukumu kubwa unalotakiwa
kuwa nalo kama mjasiriamali ni kuhakikisha unakuza idadi ya wateja kwa jinsi
unavyoweza hili ndilo jukumu lako kubwa. Acha kufikiria sana juu ya faida kubwa
utakayopata kutokana na biashara hiyo unayoifanya. Kumbuka, kuwa huwezi ukapata
faida yoyote ile kubwa kama una idadi ndogo ya wateja. Jifunze mbinu na namna
jinsi ambavyo utakavyoweza kuwa na wateja wa kutosha katika biashara yako.
Ukifanikiwa hili utaweza kupata faida kubwa sana ambayo unaifikiria uwe nayo
katika biashara yako.
5.
Acha kutegemea chanzo kimoja cha fedha.
Kama una lengo la kuwa
mjasiriamali mkubwa katika maisha yako na hatimaye kuwa huru kifedha, acha
kutegemea chanzo kimoja cha fedha. Kama utafanya biashara kwa kutegemea chanzo
kimoja cha pesa elewa kabisa hutafika mbali sana kimafanikio kama unavyofikiri.
Unapokuwa na vitega uchumi vingi hivi vitakusaidia kuongeza pato lako siku hadi
siku na utajikuta mwisho wa siku una kiasi kikubwa cha pesa ulichokikusanya kwa
matumizi ya leo na baadae. Wajasiriamali wote wenye mafanikio makubwa
hawategemei chanzo kimoja cha pesa ni watu wenye vianzio vingi vya pesa. Kama na
wewe unataka kuwa mjasiriamali wa mafanikio, jiwekee vyanzo vingi vya pesa.
SOMA PIA: Huu Ndio Utajiri Mkubwa Utakaoupata, Kama Utaamua Kufanya Biashara Hii (bofya hapa kusoma)
6.
Acha kuwa na matumizi makubwa ya pesa.
Ni hatari sana kutaka kukua
kibiashara huku ukiwa ni mtu wa matumizi makubwa ya pesa zako. Kama unataka kufika
mbali kwenye safari yako ya ujasiriamali, futilia mbali matumizi mabovu ya pesa
uliyonayo. Unapokuwa na matumizi mabovu ya pesa unakuwa kama hufanyi kitu, kwa
sababu unakuwa unapoteza pesa nyingi sana ambayo ilikuwa haina sababu ya
kupotea hata kidogo. Jifunze kutumia pesa zako vizuri na kwa utaratibu maalum
unaoeleweka. Ili kufanikisha hili hakikisha unatengeneza bajeti yako,ambayo
itakuwa inakuongoza.
Kwa kumaliza naomba niseme
hivi, kuwa mjariamali mkubwa na mwenye mafanikio unahitaji kujitoa kikamilifu
na wakati mwingine kujikana kabisa na kuachana na hofu yakukabiliana na mambo.
Nakutakia kila la kheri
katika safari yako ya kibiashara na ujasiriamali kwa ujumla iwe ya mafanikio.
Kwa pamoja tunaweza, endelea
kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi na karibu sana.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 035/dirayamafanikio@gmail.com
Jan 21, 2015
Tabia 8 Muhimu Unazotakiwa Kuwa Nazo, Ili Kujenga Maisha Ya Mafanikio Makubwa.
Ni ukweli usiofichika ili
uweze kubadili maisha yako na kuwa ya mafanikio ya kiwango cha juu ni lazima
ubadili tabia zako ulizonazo sasa na kuwa na tabia ambazo zitakuongoza kufikia
mafanikio mkubwa zaidi. Unaweza usilione hili mapema lakini huu ndio ukweli,
linapokuja suala la kutafuta mafanikio vipo vitu vingi unavyotakiwa kuvifanya
na kubadili kama vile matumizi mabaya ya muda na pesa, lakini likiwemo na suala
la kubadili tabia ulizonazo ambazo zimekufikisha hapo ulipo. (Unaweza ukasoma pia Kama Unataka Kufanikiwa Na Kuwa Tajiri, Acha Tabia Hizi)
Unapobadili baadhi ya tabia
zako unakuwa unajiweka kwenye mstari wa kufikia mafanikio yako uliyojiwekea.
Kumbuka, mafanikio yanajegwa na na tabia ulizonazo, kwa kadri unavyokuwa na
tabia za aina fulani, ndivyo mafanikio yanakuwa upande wako na kwa jinsi
unavyokuwa na tabia za aina fulani pia utajikuta ndivyo unavyofukuza mafanikio
katika maisha yako bila ya wewe kujijua. Ili kujenga maisha ya mafanikio
makubwa unayohitaji, hakikisha unakuwa na tabia hizi katika masha yako.
1. Tabia
ya kuamka asubuhi na mapema.
Unapoamka asubuhi na mapema
kabla ya muda uliojiwekea, kabla ya watu
wengine, unakuwa unapata muda wa kutuliza akili yako, kujisikiliza wewe
mwenyewe na kupata nafasi ya kutafakari juu ya maisha yako kwa ujumla. Pia kwa kuamka asubuhi na mapema sio tu
itakusaidia kukupa muda wa ziada wa kutafakari juu ya maisha, hiyo itakusaidia
pia kukujengea tabia muhimu ya kupangilia siku yako mapema, wapi uanzie na wapi
uishie, ambapo tabia hii itakuongoza kwenye mafanikio. Watu wengi wenye
mafanikio wana tabia hii muhimu ambayo inawafanya wazidi kufanikiwa. Ni tabia
ambayo unaweza hata wewe kuwa nayo ili ikuletee mafanikio mkubwa.
2.
Tabia ya kuilisha akili yako kila mara.
Mara nyingi maisha yetu kwa
wengi huwa yametawaliwa na kula vyakula vya kila aina, hilo unalijua. Lakini
kuna kitu muhimu ambacho huwa haukilishi na kukisahau mara kwa mara. Kitu hiki
sio kingine ni akili yako. Kama ambavyo mwili wako unahitaji kula kila siku pia hata akili yako inahitaji kulishwa tena sana
kila siku. Unahitaji kuilisha akili yako kwa kujisomea kila siku na hili ndilo
hitaji la msingi unalotakiwa kuwa nalo ili uweze kufanikiwa. Usiache siku
ikapita bila kwako kujifunza kitu kitakachobadili maisha yako. Tumia muda wako
vizuri jifunze hata kwa dakika 20 au 30 kwa siku, baada ya muda utaona
mabadiliko makubwa katika maisha yako. Hii ni tabia muhimu sana kwako ambayo
hutakiwi kuiacha ili kujenga mafanikio ya kudumu.
3.
Tabia ya kufanya mazoezi kila siku.
Hata kama ni kwa dakika kumi
na tano tu, unahitajika kujiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi kila siku. Ili
uweze kufikia mafanikio makubwa unayotaka, kumbuka unatakiwa kuwa na akili safi
ndani ya mwili wenye afya ya kutosha. Unapojenga tabia ya kufanya mazoezi
unakuwa unaifanya akili yako iwe nzuri kiafya na kujikuta ukifikiri vizuri
zaidi. Isitoshe mazoezi yanakusaidia
wewe kupunguza magonjwa hususani ya moyo na mengineyo mengi ambayo
ungeyaweza kuyapata kizembe, kama ungekaa tu bila kufanya mazoezi ya aina
yoyote ile, hivyo ni kitu kizuri kwa mafanikio yako unayoyahitaji.
4.
Tabia ya kutekeleza mipango yako mapema.
Kuweza kuifanya siku yako
iwe ya mafanikio, ni muhimu sana kwako kujiwekea utaratibu wa kupanga mambo
yako mapema ikiwezekana siku moja kabla ili kuepuka kuingiliana kwa mambo
ambako kunaweza kukwamisha katika mipango yako uliyojiwekea. Utaweza kufanya hivi
kwa kuwa na ratiba yako ndogo ambayo itakuonyesha kwa uzuri ni nini ufanye
katika siku husika inayofuata. Kuwa na utaratibu huu wa kujipangia mambo yako
mapema utakusaidia wewe kufanya mambo yako kwa ufanisi na utalaam zaidi. Ukiwa
na tabia hii, itakusaidia sana kufanikisha mipango yako mingi uliyojiwekea.
5.
Tabia ya kuzingatia mambo.
Haijalishi unakumbana na
changamoto za aina gani sasa, kitu kikubwa unachotakiwa nacho wewe ni kujifunza
kutenda kwa uzingativu mkubwa unapotenda mambo yako. Acha tabia ya kuairisha na
kusema ngoja nitafanya kesho, hii ni tabia ambayo itakukwamisha na kukurudisha
nyuma kila siku. Kama kuna jambo au kitu ambacho ulitakiwa kukamilisha leo leo
hata kama ni kidogo ni vizuri ukakamilisha leo ili kesho uingie kwenye jukumu
lingine tofauti. Ili uweze kujenga mafanikio, ni muhimu kwako kuwa na tabia ya
kuzingatia kila jambo unalolifanya na unatakiwa ulifanye kwa ufanisi mkubwa.
6.
Tabia ya kuangalia malengo yako upya.
Ni kweli unaweza ukawa una
mipango na malengo mazuri uliyojiwekea, lakini ni muhimu sana kwako kuwa na
tabia ya kuangalia au kukagua malengo yako mara kwa mara. Unapokuwa na tabia ya
kukagua malengo yako mara kwa mara, nakuyapitia tena tena na kuangalia wapi
ulipokosea na wapi ulipofikia inakuwa inakusaidia wewe kusonga mbele na kuyafanya malengo yako yazidi kuwa hai.
Hakikisha kila siku unatenga muda kidogo wa kuyapitia malengo yako upya. Hii ni
tabia muhimu sana mbayo unatakiwa kujijngea ili kuweza kufikia mafanikio
makubwa yaliyoko mbele yako.
7.
Tabia ya kujiamini zaidi.
Hii ni tabia ambayo muhimu
pia unayotakiwa kuwa nayo ili kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako. Kwa
kawaida linapokuja suala zima la kujiamini kwa wengine huwa ni shida kidogo.
Unaposhindwa kujiamini elewa kabisa kwako itakuwa ni ngumu kuweza kufikia
kiwango cha mafanikio unachotaka. Kwa nini inakuwa ngumu kufikia mafanikio
unayotaka? Hii ni kwa sababu kila kitu ambacho utakuwa unataka kufanya utakuwa unahisi
au unajiona kama vile huwezi, matokeo yake utajikuta utakuwa ni mtu wa
kushindwa katika mambo mengi hata kwa yale ambayo hukustahili.
8.Tabia
ya kufanya kazi kwa bidii.
Kufanya kazi kwa bidii, kuwa
king’ang’azi katika malengo yako ni nguzo muhimu sana ya kukufikisha kwenye
mafanikio makubwa katika maisha yako.
Ikiwa utaamua kujitoa mhanga na kufanya kazi zako kwa bidii zote na kujifunza
vitu muhimu kwa kile unachokifanya, elewa kabisa mafanikio makubwa ni yako.
Kama una nia ya kweli ya kutaka mafanikio makubwa, chukua jukumu la
kujibidiisha kwa shughuli zako zote unazozifanya. Matokeo na matunda makubwa
utayaona upande wako kadiri siku zitakavyokuwa zinaenda mbele. Hata ikifika
wakati huoni matokeo mazuri wewe weka bidii hupotezi kitu.
Kwa kawaida tabia zetu ndizo
zina nguvu ya kujenga ama kubomoa maisha yetu ya kila siku. Kama unataka maisha
ya mafanikio, hakikisha unajifunza kujenga tabia zitakazo kuongoza kwenye
mafanikio ya kweli na sio kukwamisha. Chukua hatua muhimu za kubadili na
kuboresha maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika
safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na
kuhamasika kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 035/dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Posts
(
Atom
)