Dec 18, 2014
Kanuni Muhimu Katika Kuendesha Biashara Yako, Ili Iwe Na Mafanikio Makubwa Unayoyataka.
Wengi wetu tumekuwa
tukibuni, tukiiga na hata kuanzisha biashara mbalimbali ambazo, zimekuwa
hazidumu wala kuendelea kwa muda mrefu kwa sababu ya kufilisika. Kukwama na
kufilisika au kutokuendelea kwa biashara zetu hizi, limekuwa ndilo tatizo sugu
au kikwazo kigumu kwa wafanyabiashara walio wengi, wakubwa kwa wadogo.
Wengi wetu tumekuwa
tukilitafutia dawa au suluhisho la kudumu tatizo hili bila mafanikio. Kuendelea
kudumu kwa tatizo hili, kumesababisha baadhi ya watu kukata tamaa kabisa ya
kuendelea kufanya biashara. Hata hivyo maelezo na mifano halisi nitakayoitoa
hapa, inaweza kutusaidia kutupatia majibu ya uhakika au suluhisho la kudumu
nini kifanyike.
Ni muhimu kwetu kufata
maelezo haya au kanuni hizi ikiwa endapo tumedhamiria kutimiza wajibu wetu wa
kufanya biashara tuzipendazo, ili kuboresha maisha yetu na jamii kwa ujumla. Kanuni
hizi ni muhimu hasa kwa watu walioamua kuanzisha biashara ndogondogo na
wanazomiliki wenyewe, pengine baada ya kuchoshwa na kazi za kuajiriwa au kwa
sababu nyingine.
Ukiweza kuzitumia
kanuni hizi ndogondogo vizuri katika biashara yako, itakuletea mafanikio
makubwa unayoyataka na hutajuta tena. Huna haja ya kulalamika tena wala kulaumu
kwa sababu ya biashara zako kwenda hovyo, ni wajibu wako sasa kuzitumia kanuni
hizi ili uone manufaa yake katika biashara yako. Unajua kanuni hizi ni zipi?
Hizi
ndizo kanuni muhimu katika kuendesha biashara yako, ili iwe na mafanikio
makubwa.
1. Ifanye
biashara yako iwe ya thamani na ubunifu kila siku.
Kushindwa kutambua
thamani ya ubunifu, ni jambo ambalo hupaswi kulifanya. Ni rahisi kuangukia
kwenye mtego wa dhana kwamba lengo la biashara ni kutengeneza fedha tu. Lakini lengo
sahihi la biashara ni kutengeneza thamani. Wakati si rahisi kutengeneza fedha
katika kipindi kifupi bila kutengeneza thamani, kutengeneza fedha bila thamani
si kitu cha kudumu.
Ni lazima biashara yako
iweze kujenga thamani kwa ajili yako na wateja wako. Kwa jinsi utakavyotambua
thamani ya kile unachotoa, ndivyo utakavyoweza kuelekeza nguvu zako zaidi. Kama
biashara yako ni ya michezo kama ya kompyuta ama mingine, basi ujue thamani
unayotengeneza hapo ni kuburudisha akili.
Ni kwa kutambua hivyo tu,
ndipo utakapoweza kujitahidi kufanya huduma yako iwe bora zaidi na kuthamini
wateja wako. Imetokea mara nyingi wamiliki wa biashara wameshindwa kutambua
thamani wanayojaribu kutoa. Hawa hubaki tu wakitarajia makubwa bila ya kujua
watayafanya vipi, kwani hawajui hata lengo la biashara yao. Ukitoa thamani kwa
huduma unayotoa, wateja utapata tu.
2. Acha
kujaribu kuuzia watu wasio sahihi.
Wakati mauzo ni kitu
muhimu ili biashara iweze kudumu, huna haja ya kuhamanika kwa hilo na kudhani
unalazimika kumlazimisha kila mtu unayekutana naye kufanya nawe biashara, ikiwa
ni pamoja na marafiki zako na watu wa familia yako. Ni kupoteza wakati kujaribu
kuwauzia watu ambao unajua wazi hawahitaji kile unachouza.
Kuuzia watu wasio
sahihi ni pamoja na kujaribu kumuuzia kila mtu unayemwona mbele yako. Wapo wateja
ambao ni rahisi kuwauzia kile ulichonacho kuliko wengine. Kwa mfano unafanya
kazi ya kutengeneza tovuti halafu unakutana na mtu asiyejua chochote kuhusu
intaneti na unaanza kumtangazia biashara yako ya tovuti, ni wazi utapoteza
wakati wako kwani huyu si mteja wako sahihi.
Unatakiwa uwe na uwezo
wa kukataa kuwapatia maelezo wateja wanaoonekana wazi kuwa na uwezekano wa
kukuletea matatizo kuliko faida katika biashara yako. Waache wapinzani wako
wafanye kazi ya kuwauzia badala yake. Kwa kufanya hivyo utajiokoa na matatizo
ya kuumia kichwa kwa kuongea na watu ambao sio sahihi katika biashara yako.
3. Acha
kutumia pesa nyingi kupita kiasi.
Kama biashara yao bado
ni changa, acha kutumia pesa nyingi kupita kiasi mpaka utakapokuwa na mtiririko
wa uhakika wa fedha zinazoingia. Usitumie fedha za kufanyia biashara hadi pale
itakapokuwa muhimu sana na kwa manufaa yaliyo wazi kwa biashara yako. Hapa itabidi
ujifunze kutokufanya matumizi yasiyo ya lazima katika biashara yako.
Ili kufanikiwa katika
suala hili la kutokutumia pesa nyingi kupita kiasi, ni muhimu kujua utumie
nini, kwa sababu ya nini, na kwa nini. Ikumbukwe pia katika malengo ya kawaida
ya biashara, biashara inatakiwa kuingiza fedha mfukoni mwako, hivyo kabla ya
kuwekeza unatakiwa ujue namna ya fedha ulizotoa mifukoni mwako kuwekeza
zitakavyorudi.
4. Acha
ugumu (ubahili) katika kutumia fedha.
Wakati kutumia pesa
nyingi bila umuhimu ni kosa katika biashara, ni kosa pia kufanya biashara yako
huku ukiweka mbele matumizi yaliyotawaliwa na ugumu katika matumizi ya fedha
zako hata pale inapokuwa muhimu. Usiruhusu ugumu au ubahili ukwamishe ufanisi
wa kazi yako.
Kama itatakiwa
kuwatumia wataalamu wazuri wenye uwezo wa kufanya kazi Fulani vizuri kuliko
utakavyofanya mwenyewe ama watakavyoweza kufanya watu wasio na uhakika, wa bei
rahisi ni vizuri ukawatumia hao. Nunua vifaa imara na vinavyofanya kazi vizuri
ikiwa una hakika fedha zako zitarudi.
Nakutakia kila la kheri
katika mafanikio ya biashara yako na endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza zaidi, karibu sana.
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 0345/dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.