Mar 12, 2015
Iheshimu Leo Isije Kukugharimu Kesho.
Hivi umewahi kufanya kitu
fulani halafu miaka ikapita ukajiuliza kama ni wewe umefanya hilo jambo, mimi
nimewahi. Kuna wakati katika maisha unaweza ukajikuta umefanya jambo fulani
halafu baadaye ukaja kujuta, ukajiona ni mjinga au hata limbukeni. Wakati
mwingine linaweza likawa fundisho kwako kiasi cha kwamba hata mtu akushawishi
vipi huwezi kurudi kufanya jambo hilo tena.
Hata hivyo tikirudi nyuma
huenda wakati unafanya hayo mambo ulikuwa unashauriwa, hivyo ukajikuta ukawa
sikio la kufa lisilosikia dawa. Au huenda hukupata nafasi ya mtu kukwambia
unachofanya siyo na kwamba kitakuja kukugharimu maishani. Tuachane na sisi
ambao tumepitia huko, tukajifunza na tukamwomba Mungu hiyo historia isije
kujirudia tena katika maisha yetu.
Leo, naongea na wale
wenzangu na mimi ambao tunaingalia leo. Kesho ni kama hatuijui vile au kama
haitakuwapo kutokana na mambo tunayoyafanya. Wengine husema ‘kesho itajijua’.
Kama ingekuwa hivyo basi tusingekuwa tunaihangaikia kesho.
Inafahamika wazi kuwa kila
mtu ana uhuru wa kufanya kile anachokisikia, lakini ukweli unabaki palepale
kwamba hata uhuru wa mtu binafsi una mipaka yake. Huwezi kufanya kila kitu bila
kuzingatia mambo muhimu hasa ya kimaadili.
Unajua kwa sisi vijana kuna
mambo mengi tunayafanya kwa sababu ndio wakati wake, ujana si maji ya moto
bwana. Ni kweli wala siyo uongo lakini wengi wetu tunafanya kwa kufuata mkumbo.
Kuiga sijui fulani kafanya hivi na mimi nifanye, mwingine kaenda huku na wewe
huyo kama kumbikumbi vile. Sasa unavyofanya hivyo unajua mwenzako kwa nini
anafanya?
Wengi hasa wasichana wanaona
fahari kumuiga fulani kafanya hivi ama vile. Kapate kile yeye atafanya kile
akiwezacho hata kama kitamgharimu maisha yake lakini bora tu awe kama fulani.
Kumbuka kuna kesho katika maisha yako, Yule unayemuiga hufahamu alivyojipanga
hadi akafanya yale unayoyaona. Mambo mengine ni siri ya mtu. Sasa wewe unaingia
kichwa kichwa utaumia.
Mwingine anaweza kuona
rafiki yake, kachora tattoo na yeye huyo. Hivi unafahamu kwamba unaweza kukatisha
ndoto za kuwa na mafanikio kuliko uliyonayo kwa sababu ya kufuata mkumbo? Kuna
vitu tunaweza kuviona ni vya kawaida lakini kuna watu hadi leo wakikumbuka
jinsi vilivyowagharimu katika maisha yao inakuwa inauma. Kuwa mtu na msimamo
wako, maisha yako ni yako. Mwisho wa siku utakuja kusimama wewe kama wewe
kwenye mambo yako ya msingi.
Nakumbuka kuna jamaa mmoja
alipata nafasi ya kazi serikalini lakini alikuwa amechora tattoo. Kila siku
akawa mtu wa kuvaa mashati yenye mikono mirefu, hata kukiwa na joto la aina
gani hata mikono hawezi kukunja.
Alipoona watu wanamuuliza
sana na kuna baadhi ya watu walianza kuhisi kwamba kuna kitu anaficha,
alilazimika kwenda india kufanyiwa upasuaji. Huko alichomwa sindano ile ngozi
ya juu iliyokuwa imechorwa ikaamuka halafu ikakatwa. Baada ya hapo aliuguza
kidonda na kurejea akiwa na kovu. Hadi leo anakovu kwenye mikono. Sasa shida
zote za nini? Iheshimu leo, isije ikakugharimu kesho.
NAKUTAKIA KILA LA KHERI
KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa
kupata elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.
- Makala hii imeandikwa na Suzan mwillo wa Gazeti La Mwananchi.
- Mawasiliano suzanmwillo@yahoo.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.