Mar 6, 2015
Kama Unafanya Kitu Hiki Kidogo Katika Kazi Unayoifanya, Ni lazima Ufanikiwe.
Mara nyingi unapoamua kuipenda kazi yako kiukweli kutoka moyoni kitu pekee kitakachokutokea ni kuwa na mafanikio makubwa katika maisha yako. Unapokuwa unaipenda kazi yako, inakuwa inakupa nafasi ya kuweza kubuni na pia kuwavutia wengine na hata wale unaokuwa nao ukiwa hapo kazini kwako.
Mhudumu wa hoteli kwa mfano,
anapokuwa anaipenda kazi yake, huweza kuwafanya wateja kuhisi kwamba,
wanathaminiwa sana. Siku za nyuma kidogo, mimi binafsi na rafiki yangu wakati
tupo Chuo tulikuwa tukitoka kwenda kula chakula cha jioni kila wikiendi katika
mgahawa mmoja uliokuwa eneo la barabara ya sita, mjini Dodoma, ingawa sina
uhakika kama bado upo au hapana.
Hapa kulikuwa na mhudumu
ambaye alikuwa akiitwa Pendo. Huyu mhudumu alikuwa akiwafanya wateja wengi
wajihisi vizuri, bila shaka. Alikuwa na upendo kweli kama jina lake lilivyo,
alikuwa mcheshi na mvumilivu, yaani asiye na hasira. Kutokana na ucheshi wake
huo kitu ambacho kilipelekea kuwa na wateja wengi zaidi katika eneo la kazi
yake. Kwa kifupi, aliipenda kazi yake.
Pia ikafika wakati ambapo
jamaa yangu mmoja alikuwa akitafuta mtu mwenye uwezo sana wa shughuli za
mgahawa, mcheshi na mchapa kazi, ili aweze kusimamia hotel aliyokuwa anataka
kuifungua. Alikuja kuniambia kuwa alikuwa ana wazo la kwenda kumchukua mhudumu
Yule, lakini kwa bahati mbaya alienda na akawa amemkosa mhudumu Yule na
aliambiwa amepata kazi sehemu nyingine nzuri zaidi.
Hivi karibuni pia huko
Sweden, tukio linalokaribiana na hili langu ambalo nililipata kwa njia mtandao
lilitokea. Mzee mmoja mteja katika mgahawa unaofahamika kama Njuraanger, kwenye mji wa Sundsvall, ulioko katikati ya nchi hiyo,
alishangazwa na jinsi mhudumu mmoja msichana mdogo alivyokuwa akifanya kazi
yake ya uhudumu kwa uadilifu mkubwa sana.
Mzee huyo ambaye alikuwa ni
mfanyabiashara katika siku ya tukio alikuwa akila chakula cha jioni na wenzake.
Baada ya kuhudumiwa na mhudumu msichana wa miaka 19, mzee huyu alifikiria na
kuona kuwa, bakhshishi ya kawaida isingeweza kumfaa binti Yule zaidi ya kumpa
gari moja iliyoko nyumbani kwake kama zawadi na hongera kwa kazi nzuri
anayoifanya.
Mzee huyu alitoa kutoka
kwenye lundo la funguo zake, funguo za gari lile. Alimkabidhi funguo zile
mhudumu Yule ambaye awali alidhani ni dhihaka. ‘Aliniuliza umri wangu na nilipomtajia alisema ananipa gari, alinipa
funguo. Awali nilijua ilikuwa ni mzaha’ alisema binti Yule. Kesho yake
alifatana na Yule mzee na kwenda kuichukua ile gari.
Mzee huyo alipoulizwa sababu
ya kumpa msichana huyo bakshishi ya gari, alisema aliona umalaika Fulani kwa
msichana huyo. Ni wazi uhudumiaji wake ulimvutia hadi akaona ni vyema kumpa
bakshishi za kawaida haitoshi. Huyu mzee alisema aliona umalaika ndani ya
mhudumu Yule. Umalaika tulionao hauwezi kuonekana kama tunafanya shughuli kwa
kujilazimisha, siyo rahisi.
Ni wahudumu wangapi hapa
nchini wanafanya kazi zao kwa kuzipenda? Lakini ni watumishi wangapi ambao kwa
ujumla hufanya kazi au shughuli zao kwa kujilazimisha? Ni wengi sana. Matokeo
yake ni nini? Ni maumivu yasiyoisha, majuto na kujenga uadui na watu wote
tunaokutana nao hapo kwenye shughuli zetu.
Ni muhimu sana kwetu kuweza
kujifunza kuzipenda shughuli tunazofanya. Kuzipenda kuna maana ya kuziheshimu
na kuzikubali kwamba, kwa sasa, hizo ndizo shughuli zetu. Kwa kadri jinsi
tutakavyozidi kupenda shughuli zetu ndivyo tutazidi tukijikuta tunavuta
mafanikio makubwa upande wetu kwa sababu tunakuwa tunafanya kwa moyo wote bila
kuchoka. Na kama unafanya kitu hiki kidogo katika kazi unayoifanya ni lazima
ufanikiwe.
Nakutakia mafanikio mema,
endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza zaidi.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.