Mar 26, 2015
Kiri Kosa, Jifunze, Jipe Nafasi Ya Kuanza Upya.
Katika safari ya maisha, ni jambo la kawaida kabisa kukutana na vikwazo vinavyoweza kukatisha tamaa. Ukubwa wa vikwazo au changamoto hizo, zinaweza kukusababishia ukaiona dunia kama imegeuka, au wakati mwingine ukatamani ipasuke uingie ndani yake.
Yapo mambo mengi yanayoweza
kukufanya ufikirie hivyo. Huenda yakawa ni makosa ya kibinadamu, matatizo,
changamoto, kukatishwa tamaa na baadhi ya watu au kujiponza mwenyewe kutokana
na hili au lile. Lakini ukikaa chini, ukatafakari utatambua kuwa hakuna binadamu
asiyeteleza kwa kufanya makosa au kupitia changamoto kwenye safari ya maisha.
Hivyo wakati mwingine
unapaswa kuelewa kuwa kwa kila linalokupata, bado unayo nafasi ya kufungua
ukurasa mpya. Kupatwa na mitihani katika maisha, mara nyingi ni darasa mojawapo
tunalotakiwa kuliangalia kwa umakini ili kupata somo au fundisho lililo ndani
yake.
Ikiwa mtihani huo umekuja
kutokana na kosa ulilofanya, ni vyema kukubali kama umekosea na kisha kujipa
nafasi ya kusonga mbele. Tunaelewa kuwa maisha ya kila mmoja wetu kwa namna
moja au nyingine yanaendeshwa na misimamo mbalimbali. Kuna wale wanaoamini kuwa
wao hawawezi kufanya jambo Fulani na
wakati mwingine kuamini kuwa hawawezi kukosea kabisa.
Ni sawa lakini tukumbuke
kwamba hakuna binadamu aliyekamilika kwa kila mmoja wetu anaweza kuteleza na
kufanya kosa bila kukusudia . Hivyo basi kwa namna yoyote ile katika maisha
yetu kutenda makosa ni sehemu ya maisha. Ni vyema kujifunza kukubali kama
umekosea na kujirekebisha.
Pili, jifunze kutokana na
lile kosa. Si dhani kama leo ukikosea jambo Fulani unaweza kulirudia kosa kama
lile siku nyingine. Hata kama ikitokea labda kwa namna nyingine tena. Nakumbuka
wakati nikiwa mdogo baba yangu aliniletea zawadi kama pongezi ya kufanya vizuri
darasani.
Siku hiyo aliponiletea
tulikuwa tumekaa na kaka zangu. Alinikaribisha tukiwa pamoja ili iwe chachu kwa
wao kufanya vizuri pia. Au pengine kuwafanya waone wivu na wao waweze kufanya
vizuri wakiwa shuleni. Basi alinipa ile zawadi. Wakati wa kupokea nilifanya
kosa kwa kupokea na mkono wa kushoto. Kwa ukali aliniambia nirudishe ile zawadi
akaondoka nayo.
Baada ya kutafakari kwa muda
nikakumbuka kumbuka kuwa nilifanya kosa kupokea na mkono wa kushoto kitendo
ambacho alishawahi kutusisitizia kuwa siyo cha heshima. Lile lilikuwa funzo
kwangu kwani mpaka leo sikuwahi kufahamu ile zawadi ilikuwa ni ya aina gani,
kwani ilikuwa imefungwa.
Baada ya kutokea kwa kadhia
ile na kuweza kugundua kosa langu, moja kwa moja nilienda kuomba msamaha kwa
baba. Tangu siku ile sikuwahi tena kumpa au kupokea kitu chochote na mkono wa
kushoto. Hata ikitokea hivyo kama nimejisahau lazima nitaomba radhi.
Ninachoamini mimi ni kwamba
kwa hali yoyote ile ni lazima tuyape nafasi maisha yaendelee. Hivyo hatuna haja
ya kuangalia nyuma pale tunapojikwaa, kwani utakachoambulia hapo ni maumivu
tena inawezekana ukaumia hapo kuliko awali.
Wapo waliofikia kufanya
maamuzi ya ajabu baada ya kukutwa na mtihani au kufanya makosa katika jamii.
Wengine hata waliweza kutengwa kutokana na makosa yao. Lakini kushindwa kwao
kukubali makosa waliyotenda, kulizaa matatizo mengine. Kwani utakuta ili
kuondoa aibu iliyo mbele yao, waliamua kukimbia miji yao na hivyo kwenda kuanza
maisha sehemu nyingine.
Suluhisho pekee la jambo
kama hili ni kuomba msamaha na kujipanga upya. Usikubali kukata tamaa kwa
kuanguka mara moja, hata ukianguka mara tatu bado unayo nafasi ya kusimama na
kuanza upya na kufanya vizuri hata pengine kuliko mwanzo. Kitu kikubwa jiamini
kisha chukua jukumu la kusonga mbele kwa kujiamini zaidi, utabadili maisha yako
na utafanikiwa.
Nakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa ajili
ya kujifunza na kuboresha maisha yako.
- Makala hii imeandikwa na Suzan Mwillo wa Gazeti la Mwananchi.
- Mawasiliano suzanmwillo@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.