Mar 19, 2015
Hiki Ndicho Kitu Kinachokufanya Ushindwe Kupata Kile Unachokihitaji Katika Maisha Yako.
Kuna wakati katika maisha
yako unaweza ukajikuta ama unatamani sana uwe katika ngazi fulani ya mafanikio,
lakini ni kitu ambacho huwa hakitokei kwako. Wakati mwingine umekuwa
ukidhamiria na kuamini kwamba, lazima itakuwa, lakini huwa haiwi kama unavyofikiria.
Pamoja na juhudi nyingi ambazo umekuwa ukizifanya, zimekuwa ni kama kazi bure
kwani mara nyingi umekuwa ukishindwa kupata hasa kile unachokihitaji katika
maisha yako ambacho ni mafanikio.
Pengine umekuwa ukijitahidi
hata kufanya sala au tahajudi(Meditation) ili kuweza kubadili mwelekeo na
kuweza hata kufanikisha kile unachokihaji, lakini wapi mafanikio hayo umekuwa
huyaoni. Ni kitu ambacho kumekuwa kikikuchanganya na kushindwa kuelewa unakosea
wapi hasa na ufanye nini? Hali hii imekuwa kuna wakati inataka kukuvunja nguvu
na kukufanya uamini kuwa, suala la kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako
ni kitu ambacho hakiwezekani.
Katika hali ya kushangaza
umekuwa ukiona wengine wakijaribu kuomba mara moja na kuweza kufanikisha jambo
lile, wakati kwako inakuwa ni vigumu sana, ingawa kama ni kudhamiria, na
kuamini kwamba itakuwa ni kulekule na pengine zaidi kwa hilo linaloshindikana.
Hali ama matokeo kama hayo yamekuwa yakikutisha tamaa na kukupelekea wewe
kutaka kuamini kuwa una kitu kama mkosi au laana fulani hivi inayokuzuia
ushindwe kufanikiwa, kitu ambacho sio kweli hata kidogo.
Bila shaka kwa namna moja au
nyingine unaweza ukawa umewahi kukutana na hali hii katika maisha yako ambayo
pengine imekuwa ikikuumiza kichwa na kushindwa kuelewa kabisa ni kitu gani
kinachopelekea wewe usiweze kupata matokeo mazuri kwa kile unachokihitaji
katika maisha yako?
Ingawa ukweli ni kwamba,
kuamini kwamba inawezekana na kudhamiria kumudu, huweza kuzaa au kutozaa
matunda kwa sababu moja tu kubwa. Huwa
kunakuwa na kusigishana au kupingana kati ya kile ambacho mtu anachoamini na
kile ambacho anadhamiria au kupania kiwe katika maisha yake na hiki huwa ndicho
kitu kinachokufanya usipate kile unachokihitaji katika maisha yako.
Kama mtu kwa mfano, anadhamiria au anapania kwamba,
anataka kuona uhusiano wake na mke wake au mume wake unakwenda vizuri, huku
akiwa anaamini kwamba, wanawake hawaaminiki, au wanaume ni wakorofi, uhusiano
huo hauwezi kuwa mzuri, hata kama amepania na kusali vipi kwake uhusiano mzuri
hauwezi kutokea. Unajua ni kwa nini?
Iko hivi, mara nyingi kupania
au kuamini kwetu kwamba, inawezekana na kutaka kwetu jambo liwe kama
tunavyotaka, sala zetu na maombi yetu, vyote hivi huwa vinafanyiwa kazi na
mawazo yetu ya kina. Sasa, kama kuna kitu kingine ambacho ni kinyume na kile
tunachotaka au kupania kiwe, ni wazi tunakuwa tunayachanganya mawazo ya kina na
inakuwa ni vigumu sana kupata kile tunachokihitaji katika maisha yetu.
Kama kweli tunataka uhusiano
wetu uwe mzuri na tunaamini kwamba, inawezekana, lakini huko kwenye mawazo yetu
ya kina tunaamini kwamba, wanawake ni dhaifu, hatutaweza kupata tunachotaka kwa
sababu, mawazo yanakuwa yanapokea
taarifa au imani mbili zenye kukinzana au kupingana.
Kwa kuamini kwamba, wanawake
ni dhaifu, lile wazo la kwamba inawezekana kuwa na uhusiano mzuri na bora sana
litatupwa nje na kufanyiwa kazi lile lililokuwa hapo awali. Ni hadi ile imani
kwamba, wanawake ni dhaifu iondolewe, ndipo ambapo kudhamiria au maombi
yatafanya kazi.
Utakuta mtu anasali kila
siku na kuamini kwamba, atafanikiwa katika jambo fulani, lakini anakuwa ana
imani kwamba, rangi yake itamponza kwa sababu, anashindana na watu wenye rangi
nyingine. ‘Wenzetu wale wanajua namna
mambo haya yanavyofanywa’, atawaza. Kwa hiyo, dhamira na sala yake
vitatupwa nje na hili la ‘wenzetu’, ndilo litakalofanyiwa kazi.
Imani zetu, ambazo
tuliwekewa kwenye mawazo yetu siku za nyuma kwenye malezi au mazingira
tulimokulia, zinakwenda kwa kina kirefu hivyo zina nguvu zaidi. Tunapoleta imai
mpya zenye kukinzana na zile za zamani, hizi mpya ni lazima zitupwe nje au
tuseme haziwezi kufanyiwa kazi kabisa kwenye mawazo yetu ya kina na kujikuta
hatuwezi kupata kile tunachokihitaji katika maisha yetu.
Hebu jaribu leo kufikiria
ama kutengeneza orodha ya mambo ambayo umekuwa ukiyaomba au ukitaka
uyafanikishe katika maisha yako na umekuwa ukiamini kwamba yanawezekana na
umekuwa ukifanya kwa kupania, lakini bado hayakubali. Kama utayapitia vizuri na
kurudi nyuma, utabaini kwamba, huenda kile ulicholishwa utotoni kuhusu
kutowezekana kwa mambo hayo, bado kina nguvu kubwa kwenye mawazo yako ya kina.
Ili sasa uweze kumudu kupata
kile unachokihitaji katika maisha yako ni muhimu sana kwako, kusafisha kwanza
mawazo yako kuhusu yale mabaya yaliyowekwa humo kuhusiana na jambo ambalo
unataka kufanikiwa kwalo. Kila kitu utaweza kukifanikisha katika maisha yako
kama hakuna kukinzana ndani yako. Kumbuka na tambua kuwa kukinzana ndani mwako
ndicho kitu kinachopelekea ushindwe kupata kile unachokihitaji katika maisha
yako.
Ansante kwa kutembelea mtandao
huu wa DIRA YA MAFANIKIO na endelea kuwashirikisha wengine kwa ajili ya
kujifunza zaidi, mpaka maisha yako yaimarike.
NAKUTAKIA KILA LA KHERI
KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048035,
- dirayamafanikio@gmail.com,
- dirayamafanikio.blogspot.com.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.