Mar 17, 2015
Kama Unatafuta kitu Hiki Katika Maisha Yako, Utateseka sana.
Hebu fikiria, jaribu
kufikiria, halafu karibia kuamini au amini kabisa kwamba, una vitu vifuatavyo.
Una magari ya kifahari kumi, nyumba za kifahari mbili kila mkoa kwa mikoa yote
Tanzania, mashamba ya ekari elfu moja kila mkoa na fedha zipatazo shilingi
bilioni kumi benki. Hebu fikiria.
Najua unaweza kujenga
taswira, kama tunavyofanya wakati tunapoota ndoto za alinacha, hadi kufanya
hali ionekane kuwa ni kweli. Hebu fikiria tena kwamba, kwa sababu ya mali hizo
umekuwa maarufu katika nchi za afrika mashariki na kati. Hebu fikiria kwamba, unaandikwa
na kutajwa magazetini, redioni na kwenye televisheni.
Jione kwenye hizo fikra zako
kwamba, hayo ndiyo maisha yako, tajiri na maarufu. Halafu endelea kufikiria
kuhusu maisha yako. watu wanakujua, wanakuogopa, wanakushangaa na
kukunyenyekea. Kila unapoenda unajua watu wanakutazama na kutamani wangekuwa
kama wewe labda.
Endelea kufikiria kwamba,
umekuwa tajiri na maarufu tangu mwaka 1990 hadi leo. Hebu jaribu kufikiri kwa
makini zaidi, baada ya kusifiwa, kuogopwa, kunyenyekewa na kufahamika kila kona
, halafu kingefuata kitu gani? Ni kitu gani ungekuwa umekipata? Sawa, umesifiwa
na kufahamika na ukajisikia vizuri. Halafu inakuwaje baada ya kujisikia vizuri
kwa muda wote huo?
Katika kufikiri kwako,
unadhani bado utaendelea kujali kusifiwa na kunyenyekewa? Hapana, haiwezekani.
Baada ya muda fulani wa kusifiwa na kunyenyekewa, utagundua kwamba, hakuna
chochote ndani ya sifa hizo na kunyenyekewa huko. Kwanini? Kwa sababu, wewe siyo kusifiwa na kunyenyekewa, wewe ni
wewe hiki ndicho kitu hasa nataka ukijue vizuri hapa.
Lakini, hata kama utaendelea
kusifiwa na kujisikia vizuri, halafu itakuwa ni kitu gani? Hebu fikiria kwamba,
kila asubuhi ukiamka, magazeti yamendika kuhusu wewe kwa sifa zote, hata bei ya
viatu vyako, televisheni zinakuonesha
ukipanda gari lako la kifahari na kwenda uendako na redio zinazungumzia
juu ya fedha na utajiri wako sana tu. Hebu fikiria, unadhani itakusaidia kitu
gani hiyo?
Mwisho wa sifa hizo ni upi
hasa? Unaposifiwa ni wapi panajisikia vizuri, ni sehemu gani ya mwili inapata furaha au starehe? Lakini,
gharama ya kulinda sifa na kunyenyekewa huko unaijua? Huwezi kuijua kwa sababu
hujaingia kwenye sifa na kunyenyekewa na watu. Ukiingia na wale ambao tayari
wameshaingia, wanataka kutoka, hawataki tena ‘balaa’ hilo.
Mcheza soka maarufu wa siku
za nyuma kidogo, David beckam aliwahi kusema, maisha yake ni upuuzi mtupu kwa
sababu ya umaarufu, Diana aliwahi kujuta kufahamika kwake. Unapotafuta
mafanikio kaa chini ujiulize kweli unataka mafanikio hayo makubwa hasa au
unatafuta sifa tu ili watu wakujue?
Halafu jiulize tena
wakishakujua nini kinatokea? Tunawajua akina Bush, Tunawajua akina Neymer, hata
pia tunawajua akina Tyson. Halafu kuwajua kwetu kunawapa kitu gani, kinatokea
kitu gani? Wanaendelea kuwa watu walewale, wanaendelea kuwa binadamu na kama
sisi, miili yao itapotea hivi pindi.
Kuna profesa mmoja kwa jina
alipata kufahamika kama Yunus, ambaye ni raia wa Bangladesh. Huyu alikuwa ana Benki
ambayo iliweza kukopesha na kubadili hali za maisha ya familia karibu millioni
tatu(siyo watu, ni familia) nchini humo.
Lakini, pamoja na uwezo huo
aliokuwa nao yeye alipata kuishi kwenye nyumba ya kawaida tena ya kupanga. Hiyo
yote inaonyesha profesa huyu alikuwa hataki sifa wala kunyenyekewa na kuandikwa
kila mahali kwenye magazeti hilo lilikuwa sio lake, kikubwa alichokuwa
akitafuta ni mafanikio katika maisha yake na ambayo yatasaidia na wengine.
Tuna watu katika jamii yetu
tunayoishi, huwa ni watu wa kupenda sifa sana kiasi cha kujiita waheshimiwa. Si
ajabu huwezi kuwashangaa watu hawa wakilewa sana kwa lengo la kutaka kuonyesha
jeuri ya pesa kiasi cha kwamba mpaka kuweza kusahau nyumbani kwao.
Inadaiwa kwamba kwa watu
kama hawa, ili akupe stahili yako, hata kama ni madaraka kazini, lazima
umnyenyekee. Kama ametoka ndani, ni lazima uhakikishe unamkimbilia, kupokea
mkoba na kujidai hata kama kumfuta vumbi kidogo kwenye suti hata kama haina
vumbi.
Halafu unajiuliza, ni ya
nini yote hiyo? Ni huyuhuyu ambaye anakunywa pombe hadi anasaidiwa kuingia
garini? Kwanini anywe kiasi hicho? Pesa na umaarufu aliodhani utampa nafuu,
vimeshindwa kufanya kazi hiyo. Sasa ina maana gani, utajiri na umaarufu?
Labda utajiri kama ule wa
Profesa Yunus ndiyo utajiri tunaoutaka. Utajiri unaoangukia mikononi mwa watu
waliokamilika, kimwili, kihisia, kiakili na kiroho. Huu utajiri mwingine ni
visu vyenye kuwachanja walionao na kuwakatia wanaozunguka. Umaarufu tunaoutaka,
hauna kitu kwa sababu, hata kama ungekuwa maarufu vipi, polepole umaarufu
utafifia na maisha yako ya mwili hayazidi miaka 120.
Sasa kusifiwa kwa miaka 120
tu, kuna maana gani, kunakusadia kitu gani, wakati hata dini yako haikwambii
kuwa itaishi milele. Umebaini kwamba, hukuja duniani kutafuta sifa na umaarufu,
bali umekuja kuishi ili ufurahie maisha yako. Mara nyingi tunamtaja Bill Gates
kila siku unafikiri anajali hilo? Unafikri anajali kutajwa huko, ambao ni mtihani
mgumu kuliko kutafuta mali na utajiri alionao.
Ndiyo maana unaweza kukuta
mtu amenunua kagari na kujenga kajumba, halafu anamtukana na kumdharau kila
mtu. Anakwenda kwa wanamziki wamtaje jina lake kwenye nyimbo zao, anakwenda
kwenye televisheni kujidai anasaidia watoto yatima. Anatafuta sifa na kutaka
watu wamjue. Halafu wakishamjua ndiyo iwe nini?
Akiishiwa, anajifungia
ndani, anachanganyikiwa, anajenga uadui na kila mtu, anadai amelogwa. Anakuwa anababaika
kwa sababu amepoteza kile alichodhani ndicho yeye, mali na umaarufu. Hajui kwamba,
yeye yupo kama binadamu na ni kamili
bila chochote. Ni lini binadamu atainua macho na kuuona ukweli? Inaniuma
sana.
Kutafuta kujulikana ni
kutafuta kuinuliwa kutoka pale ambapo mtu anaamini yupo(Chini) ili ajisikievizuri.
Mtu ambaye anajua yupo anapostahili hana haja ya kutaka ainuliwe kutoka hapo
nakupelekwa mahali ambapo atahisi kustahili.
Kutaka sifa ni kutaka
kuondolewa kwenye tope, kwenye uchafu, pasipo faa na kuwekwa mahali pengine. Kwa
hiyo mpenda sifa, ni mnyonge kuliko mtu mwingine yeyote.
Wengi huwa hatujui kwamba,
sisi ni sisi na hatuwezi kuwa kitu kingine, tupande ndege, tununue merikebu, tujulikane
hadi uvunguni, tuimbwe na maredio na kuoneshwa na matelevisheni kutwa kucha,
bado ni sisi tu. Thamani yetu inaendelea kuwa ileile.
Huko ndani mwetu kunaendelea
kuwa kulekule. Ni kama kiti, hata ukikiwekea marembo gani, ukaweka miguu
mitatu, ukakitandika na dhahabu na lulu, kazi yake ni ileile ya kukaliwa,
haibadiliki. Ikishabadilika, kinakuwa siyo kiti tena.
Nasi hata tuwe vipi,
ubinadamu wetu hauwezi kubadilika, uko palepale. Msingi wa binadamu
haubadilishwi na chochote, kama ambavyo dhima ya kiti haibadilishwi na namna
kilivyotengenezwa. Kila mtu anapaswa kujua kuwa, amekuja duniani kuishi kama
yeye.
Kama ni furaha atajipa
mwenyewe, kama ni kero atajipa mwenyewe, kama ni kujishusha atafanya hivyo
mwenyewe, hali kadhalika kujipandisha. Lakini, hata kama itakuwa vipi, anabaki
kuwa binadamu.
Kama nilivyoanza awali mwa makala
haya. Nakuomba ujaribu kufikiri tena kwamba, tayari una kila kitu
kinachokuhangaisha hivi sasa. Fedha kibao, magari, majumba, umaarufu, mke au
mume mzuri kuliko wote duniani, watoto wenye akili kuliko wote. Halafu kitafuata
kitu gani?
Nataka ujiulize baada ya
hayo yote kutimia, ni kitu gani kitafuata? Kama umefikiri vizuri, utagundua
kwamba, ni upuuzi mtupu mbele. Utagundua kuwa hukuhitaji hivyo vyote hivyo,
bali ulihitaji ulivyohitaji wewe kuvihitaji.
Hivyo vingine siyo wewe
uliyevihitaji. Ni nani sasa anayekusumbua na kuhangaika na kubabaika na maisha
kuvitafuta hivyo? Nakuachia swali hilo.
NAKUTAKIA KILA LA KHERI
KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu
na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035
- dirayamafanikio@gmail.com,
- dirayamafanikio.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.