Sep 1, 2021
Sheria Nne (4) Za Kujenga Utajiri, Hata Kama Huna Kitu Kabisa.
Kwa kiasi kikubwa idadi ya tulio wengi bila ya kujali ni maskini au tajiri tumezaliwa katika familia maskini. Hata unapoona wengine wanakuwa wamefanikiwa sana, hiyo haina maana kwamba wao wametakotea katika koo au familia za kifalme, bali ni matokeo ya nguvu na juhudi zao wenyewe.
Kwa mantiki hiyo
inamaanisha hivi, ili uweze kupata utajiri, mbali na juhudi binafsi zipo sheria
ambazo mtu anatakiwa azifuate ili kufikia lengo hilo. Na kwa kufuata sheria
hizo haitajalisha wewe umetokea katika familia gani au umetokea katika nchi au
wewe ni wa rangi ipi ni lazima utafanikiwa.
Kwa kusoma makala haya
ya leo, utajifunza sheria chache za msingi ambazo mtu unatakiwa uwe nazo au
uzifahamu ili zikusaidie kujenga utajiri hata kama umetokea familia maskini.
Uwezo wa kufikia utajiri unao tena sana, ni suala la kuamua na kuanza
kutekeleza sheria za mafanikio. Sheria hizo ni zipi? Twende pamoja katika somo.
1. Tengeneza
tabia za kukuwezesha kuwa tajiri.
Utajiri haujengwi kwa
bahati mbaya hata kidogo. Zipo tabia ambazo unatakiwa uzijenge ili zikusaidie
kutengeza msingi imara wa utajiri unaotaka kwenye maisha yako. Tabia ya
kujiwekea akiba, kutunza muda na kujenga maamuzi sahihi ya kimafanikio ni
moja ya tabia bora ambazo ukiziendeleza kwa muda zinakupa mafanikio ya wazi.
Angalia sana katika
maisha yako usije ukajuta kwa sababu ya tabia zako mbaya ambazo
zitakuangusha na kukufanya ukashindwa kufikia utajiri. Kuwa makini na
tabia hizo, jikague na jenga tabia za kukuwezesha kufanikiwa. Kwa kadri
unavyojenga tabia hizi kila siku, ndivyo utazidi kukaribia mafanikio yako kwa
sehemu kubwa.
2. Fanya kazi kwa juhudi sana.
Ikiwa ndio unaanzia
chini kabisa huna kitu, hakuna kitakachoweza kukutoa hapo ulipo zaidi ya
kufanya kazi kwa juhudi sana. Hapa inabidi ufanye kazi kwa bidii tena huku
ukiwa na nidhamu ya hali ya juu kwa kuhakikisha kila ukipatacho unakitunza
vyema na kinakusaidia kufanikiwa kwako.
Kama umeamua kujitoa
kisawasawa na kufanya kazi kweli na kuachana na maneno, utafanikiwa. Hii ni
sheria inayotumiwa na watu karibu wote wenye mafanikio makubwa duniani. Siku
zote watu hao ni wa kufanya kazi kwa bidii kubwa hali inayopelekea kuleta
mafanikio yao ya uhakika na kujenga utajiri.
3. Tengeneza vyanzo
vingi vya fedha.
Hakuna utajiri
unaojengwa kwa kutegemea chanzo kimoja cha pesa, utajiri unajengwa kwa
kujiwekea vyanzo vingi vya pesa. Kama una chanzo kimoja cha pesa na una nia ya
kuwa tajiri hauataweza kuwa hivyo. Siri au sheria ya kuwa tajiri inakutaka wewe
kutengeneza vyanzo vingi vya pesa.
Vyanzo hivyo vya pesa
vitaingiza pesa bila kujali sana wewe unafanya kazi moja kwa moja au haufanyi.
Matajiri wengi ndivyo wanavyotengeneza utajiri wao na hii ni siri mojawapo
ambayo unatakiwa uijue kwa ufasaha. Huhitaji sasa kusita sita , weka vyanzo
vingi vya pesa utengeneze utajiri wako.
4. Tambua namna ya
kutunza pesa zako.
Itakuwa ni kazi bure
kama unatafuta pesa, hujui namna ya kuzitunza vizuri. Kuna watu ambao
tatizo sio namna ya kupata pesa, bali ni jinsi ya kuzitunza pesa hizo. Utakuta
mtu anapata pesa kweli, lakini matumizi yake yapo juu sana, hicho ni kitu
ambacho ni sumu au kiziuzi cha mafanikio yake moja kwa moja.
Inabidi ufike mahali
uwe na nidhamu ya hali ya juu, juu ya pesa zako, achana na matumizi ya hovyo,
hayawezi kukufikisha popote. Kila wakati kaa chini na elewa namna ya kujifunza
juu ya kutumia pesa zako kwa busara. Pesa zako zisije zikakufanya ukawa kama mwendawazimu,
tulia ili ujenge utajiri wako.
DAIMA TUPO PAMOJA
MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Nikutakie siku njema
na kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa,
Ni wako rafiki katika
mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio,
mwandishi na mjasiriamali,
Blog,
dirayamafanikio.blogspot.com
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.