Sep 23, 2021
Vizuizi Katika Maisha Yako, Vipo Kwa Ajili Ya Kukuandaa Na Jambo Hili.
Vizuizi katika maisha, huwa havipo kwa ajili ya kukuzuia wewe eti ushindwe kufanikiwa. Vizuizi katika maisha huwa vipo kwa ajili ya kukuandaa uwe bora kwenye mafanikio yako.
Piga picha, ingekuwa vipi mtoto wa miaka 10 angekuwa yupo chuo Kikuu, hiyo isingekuwa na maana yoyote. Elimu yake ingeonekana bure na kukosa ule uthamani mkubwa.
Lakini, vizuizi vya miaka takribani 14 ya kupitia shule ya msingi, sekondari, kufanya majaribio, hivyo vyote vinamkomaza na kumfanya aione digrii ya chuo Kikuu ni ya thamani.
Piga picha pia, kama mafanikio unayoyataka yangekuwa rahisi tu, pasipo kupitia changomoto au vizuizi vyovyote vile, hayo mafanikio naamini yasingekuwa na raha kubwa zaidi.
Kuna wakati unaweza ukawa unalaumu sana kutokana na vizuizi unavyokutana navyo, lakini ukiangalia vinakukomaza na kukufanya ukawa bora kwenye mafanikio yako.
Unapokutana na vizuizi, ni wakati wako wa kujifunza maisha yanasema nini juu yako na si wakati wa kulaumu. Jifunze kitu kutokana na vizuizi hivyo. Usikae kizembe jifunze kitu.
Acha kuona vizuizi ni kama tatizo kwako, ona vizuizi ni kama njia ya kuweza kukukomaza wewe na kukufanya ukawa bora. Utafanikiwa sana kama vizuizi vyako utaviona kwa jicho hilo.
Kama unapitia kwenye changamoto kubwa, kaa ukijua unaandaliwa, unakomazwa hasa kwa kule unakoenda. Unajengewa misuri ya ukomavu itakayokufanya ufanikiwe.
Shukuru kama unakutana na changamoto. Shukuru kwa sababu ndio
saa ya kukomazwa. Unatakiwa kukumbuka, vizuizi havipo kwa ajili ya kukuzuia
bali kukuandaa kuwa bora.
Kila la kheri katika kufikia mafanikio yako.
Kama unapenda kujiunga na kundi la mafanikio ili uweze kujifunza zaidi mambo mengi ya kimafanikio. Tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER'S kwenda 0687449428 na utapewa utaratibu wa kuunganishwa.
Hakimiliki©2021 Imani Ngwangwalu. Haki Zote Zimehifadhiwa. Makala hizi hutolewa kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Ruksa 'kushare' na usibadili kitu chochote bila ya ruhusa ya mwandishi.
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.