Feb 2, 2016
Pale Ulipo Una Hali Gani Ya Maisha?
Na
Noel Ngowi, Moshi.
Yawezekana
wakati huu wa sasa pale mahali ulipo una wakati mgumu na umekata tamaa kwa vitu
au sehemu fulani ya maisha yako. Pale unapoangalia mambo yalivyo magumu sana na
kila jambo kwako haliendi na unadhani huwezi kutoka pale ulipo kwenda sehemu ya
maisha bora, mafanikio na furaha.
Je,
mpaka sasa umechukua hatua gani? Je, una wazo ya kwamba utapata mafanikio lini?
Amka, acha kujidanganya usiruhusu mawazo ya umaskini kukutawala. Tambua ya kwamba
hukuumbwa uwe maskini. Kwa hali yoyote uliyonayo, usijishushe wala kujiona wewe
ni wa chini hivyo, hukuumbwa uwe hivyo kama unavyofikiri.
Japokuwa
hali ya umaskini inakuwepo kwenye maisha, lakini unapaswa kutambua ya kwamba
una uwezo wa kuushinda umaskini huo. Inawezekana umezaliwa kweli maskini,
lakini sio kuja kuwa maskini. Kama ambavyo Bill Gates aliwahi kusema wakati
fulani ‘kuzaliwa maskini sio kosa lako,
bali kufa maskini ndiyo kosa lako’. Tumia uwezo na nguvu za ajabu ambazo
Mungu amekupa kuwa na mafanikio.
Tambua
wewe una thamani kubwa sana ya kuleta mafanikio makubwa yoyote unayoyataka
katika maisha yako kuliko unavyofikiri. Kila kitu unacho mkononi mwako ukiamua
iwe hivyo. Kama unaona huna kitu kwa sasa sawa, usilalamike sana jipange. Unayo
nafasi kubwa ya kubadilisha kesho yako kwa kuitumia leo vizuri.
KIZUIZI CHOCHOTE UNAWEZA KUVUKA HADI KUFANIKIWA. |
Kumbuka
kuwa na mafanikio sio kitu cha siku moja, bali inakuhitaji wewe kuchukua muda
na kuamua kupanga na kujitamkia namna utakavyopata mafanikio. Fahamu namna unavyojitazama
sivyo Mungu anavyokutazama. Inawezekana unajiona mnyonge sana, maskini wa
kutupwa lakini je, Mungu ndivyo unavyokuona?
Una
uwezo mkubwa sana ndani yako, fungua akili na macho, tafuta unachoweza kufanya
na kifanye kwa utofauti zaidi ili ufanikiwe. Hebu jaribu kujiuliza utabaki
kuomba omba na kuona wengine wakifanikiwa mpaka lini? Acha kukata tamaa mambo
yote yanawezekana kama unafikiri yanawezekana.
Hujachelewa
hata kidogo, kuchukua uamuzi wa kubadilisha maisha yako. Tambua kila siku ni
mpya na wewe ni vyema ukaanza siku mpya leo na mawazo mapya ya kubadilisha
maisha yako. Acha kulalamika na kuwalalamikia wengine ndiyo eti waliokukwamisha.
Chukua hatua juu ya maisha yako mwenyewe. Wajibika juu ya maisha yako.
Jifunze
kukataa kujiona hufai na anza kutafuta mafanikio siku zote bila kuchoka. Usingoje
dakika nyingine kupita, inuka, tafakari na ishi maisha mapya ya furaha. Hapo ulipo sio sehemu yako. Ni nini kinachokufanya
ukae na kuendelea kuridhika bila sababu. Anza kuishi maisha ya mafanikio sasa.
Ukiamua
unaweza kufikia mafanikio yako makubwa bila ubishi na hakuna mtu wa kukuzuia
katika hilo. Wewe ndiye unayetakiwa sasa kuamua maisha yako unataka yawe vipi?
Tunakutakia
siku njema na mafanikio mema yawe kwako.
Kumbuka endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila wakati, kwa ajili ya
kujifunza na kuhamasika.
Kama
makala hii imekusaidia kwa namna moja au nyingine, fanya tendo la upendo kwa kumshirikisha
na mwingine aweze kujifunza kupitia mtandao huu.
Diraya mafanikio inatoa pongezi na shukrani za pekee zimwendee Noel Ngowi kwa kuweza kutushirikisha
makala hii nzuri na bora kabisa.
Kama na wewe una makala nzuri ambayo
unaona inaweza ikawa msaada kwa watu wengine, unaweza ukatutumia kwenye e-mail
yetu ya dirayamafanikio@gmail.com
Karibu
sana na tupo pamoja siku zote.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.