Feb 22, 2016
Sababu Zinazoweza Kufanya Biashara Yako Ikafa, Hata Kama Ina Mtaji Mkubwa.
Mara
nyingi wengi wanaoingia kwenye biashara kwa mara kwanza huamini sana mtaji ndio
kila kitu. Kwa imani hiyo, hujikuta mara baada ya kuingia kwenye biashara
wanakuwa hawaweki nguvu nyingi katika maeneo mengine muhimu ili kuboresha
biashara zao. Na matokeo yake hupelekea biashara hizo kuanza kufa huku zikiwa
zina mtaji mkubwa kabisa.
Kinaweza
kuonekana ni kitu cha kushangaza lakini huo ndio ukweli. Unajua ni kwa nini ? Ni
kwa sababu waliaminishwa toka siku nyingi kwamba ukiwa na mtaji mkubwa basi,
kila kitu kimekwisha. Lakini, leo katika makala yetu tutaangalia sababu
zinazoweza kupelekea biashara yako ikafa, hata kama ina mtaji mkubwa.
Kwa
kupitia makala haya itakuonyesha na kukupa ukweli wa wazi kwamba, mtaji mkubwa peke yake sio ‘gerentii’ ya kukufanya wewe ukafanikiwa
kibiashara. Yapo mambo mengine ya ziada
ambayo unatakiwa kuyazingatia na kuyatilia mkazo kila siku, ili biashara yako
iweze kukupa yale matunda unayoyataka.
Kumbuka
haijalishi biashara yako ina mtaji kiasi gani, lakini elewa ukweli huu inaweza
ikafa usipozingatia mambo haya ya msingi. Sasa nataka twende pamoja kujifunza
na kujua mambo au sababu zinazoweza kupelekea biashara yako ikafa, hata kama
ina mtaji mkubwa vipi. Karibu sana
tujifunze pamoja.
1. Kukosa usimamizi imara.
Kama
unaona unataka kuanzisha biashara yako, halafu ukagundua huna usimamizi imara
ni bora ukaachana na hiyo biashara. Na kama ungekuja kwangu leo na kunieleza
hali hiyo ilivyo, ningekushauri hivi ‘ Chukua pesa hizo kisha nenda mjini, katafute
sehemu wanakochoma nyama nzuri kula pesa yote usibakize hata Shilingi mia moja.’
Sikutanii.
Kwa nini nakwambia hivyo, kufanya biashara yako huku ukiwa huna usimamizi wa
kutosha ni sawa na kupoteza pesa hizo. Tena unazipoteza bila kufaidi hata tone.
Hapa unaona hata kama ungekuwa na mtaji mkubwa vipi, kama huna usimamizi ni
lazima biashara hiyo itakufa tu, hakuna ubishi.
KUKOSA USIMAMIZI BORA, NI SUMU YA BIASHARA. |
2. Kukosa elimu ya biashara.
Najua
umeshawahi kusikia sana fulani alipata mkopo wa
benki milioni sitini, lakini biashara zake zimekufa. Unajua chanzo chake
kimojawapo ni nini? Ni kukosa elimu ya biashara. Wengi wanapokosa elimu hii
huwekeza kiholela sana matokeo yake kupoteza pesa nyingi bila sababu ikiwa
pamoja na mtaji.
Kwa
hiyo ili kufanikiwa kibiashara ni lazima wewe kuwa na elimu ya kutosha
kibiashara. Pengine unataka kujiuliza nitaipata wapi sasa? Sikiliza huhitaji
gharama kubwa sana kuipata. Unaweza kujifunza kupitia semina, huwezi hilo
unaweza kujifunza kupitia mitandao ya kuhamasisha au ukanunua vitabu
vinavyohusu biashara ukajifunza polepole. Lakini kikubwa usiikose elimu hii,
vinginevyo utapoteza mengi ikiwa pamoja na biashara yako.
3. Matumizi mabaya pesa.
Sio
kwa sababu biashara yako ina mtaji mkubwa na inaingiza pesa nyingi kwa siku,
basi na matumizi yako yanakuwa yako juu bila sababu. Kama unafanya hivyo kwenye
biashara yako nikupe tu uhakika huu, huwezi kufika mbali. Ni lazima uwe na
mpangilio mzuri wa matumizi yako ya pesa ili kuifanya biashara yako ikazidi
kuendelea.
Acha
kujidanganya kwa kuendelea kutumia pesa vibaya, utazipoteza zote mpaka
utashanga. Kikubwa unajua jinsi huo mtaji ulivyoupata. Kama ni hivyo kwa nini
uutumie hovyo? Kuwa makini na pesa zako. Tofauti na hapo biashara yako itakufa
tu hata kama sio leo, lakini lazima itakufa.
4. Kukosa ubunifu.
Ili
uweze kukabiliana na ushindani, ubunifu ni muhimu sana katika biashara yako. Bila
kuwa mbunifu huwezi kufanikiwa katika hiyo biashara kutokana na mazingira ya
ushindani mkubwa tulionao kwa sasa. Kwa hiyo ni lazima kuwa mbunifu na kuifanya
biashara yako ikaonekana ya tofauti na kukupa wateja wa kutosha.
Wengi
wanaoshindwa kwenye biashara ni wale walioingia kwa kiburi cha mtaji mkubwa na
kusahau ubunifu. Haijalishi unafanya biashara ndogo au kubwa weka ubunifu. Kila
wakati tafuta ni kitu gani biashara yako inakosa, kisha kiboreshe zaidi. Jitahidi
sana kuweka ubunifu ili kuifanya biashara yako iwe hai siku zote, vinginevyo utaiua.
5. Kukosa nidhamu.
Kama
unaendesha biashara yako na ukakosa nidhamu ya kuiendesha biashara hiyo, elewa
kabisa utakuwa na mchango mkubwa sana wa kuiua. Nidhamu ni msingi mkubwa sana
wa mafanikio yoyote na sio biashara tu peke yake. Jaribu kuangalia watu wote
wenye nidhamu ya kazi mafanikio yao yakoje? Bila shaka ni makubwa.
Biashara
nyingi sana zinazokufa huku zikiwa na mtaji mkubwa mara nyingi hukosa nidhamu. Tuchukulie
una duka la reja reja, huwezi kufanikiwa ikiwa unafungua na kufunga unavyotaka.
Ni lazima uwe una nidhamu ya muda, nidhamu ya kuwajali wateja au nidhamu ya
kauli nzuri. Kwa kukosa nidhamu hizi biashara itakufa tu hata iwe kubwa vipi.
6. Kukosa wateja.
Kati
ya kiungo muhimu sana kwenye biashara yako ni wateja. Bila wateja hakuna
biashara inayoweza kufanyika. Sasa kama utakuwa huna wateja hiyo inamaanisha
biashara yako kwa vyovyote vile itaenda kufa hata ufanye nini. Maana hao ndio
wawezeshaji wakubwa kwenye biashara yako kuendelea.
Sasa
huwa zipo sababu zinazopelekea biashara hii ikakosa wateja na nyingine ikawa na
watej wengi. Hivyo ni vyema ukazijua sababu hizo ili zikusaidie kuweza kujenga
biashara ya uhakika na yenye mafanikio makubwa.
7. Kukosa vipaumbele.
Biashara
yoyote iwe inanza au inaendelea ni lazima iwe na vipaumbele vya msingi ambavyo
vinatakiwa vifuatwe kila siku. Kama kipaumbele chako kimojawapo ni kutaka
kukuza mtaji ni vyema ukawa makini kuhakikisha hilo linatimia na kutekelezeka kwa
haraka sana.
Lakini
kama pia vipaumbele vyako ni kuhakikisha unadumisha mahusianao mazuri na wateja
wako, pia ni bora ukatekeleza. Unapokosa vipaumbele hata vile unavyoviona ni
vidogo ni rahisi sana kwa biashara yako kuweza kufa na kushindwa kuendelea hata
kama ina mtaji wa kutosha. Kwa sababu hapa tunasema biashara inakuwa inakosa
dira maalumu.
8. Kukosa mgawanyo wa majukumu.
Pia
biashara inaweza ikafa hata kama ina mtaji wake mkubwa, ikiwa itakosa mgawanyo
wa majukumu. Ni lazima biashara iwe na
mgawanyo wa majukumu ili iweze kusonga mbele. Kama unaona unafanya biashara
huku kila kitu umeshikilia wewe na hakuna wa kukusidia elewa upo kwenye hali
mbaya.
Ni
lazima utafute watu wa kukusaidia hata kama pale haupo mambo yaweze kwenda sawa
kabisa. Siri mojawapo kubwa ya kufikiwa mafanikio makubwa kwenye biashara yako
ni kutengeneza mgawanyo mzuri wa majukumu kwa wasaidizi wako. Kushindwa kufanya
hivyo ni lazima utaua biashara yako.
Kama nilivyoanza kwa kusema zipo sababu nyingi ambazo zinaweza kupelekea biashara yako ikafa, hata kama ina mtaji mkubwa. Kwa leo naomba niishie hapo. Tukutane wiki ijayo kwa makala nyingine nzuri ya biashara. Kumbuka kuchukua hatua. KILA LA KHERI.
Ni
wako rafiki katika kusaka mafanikio ya kweli,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 04 80 35,
E-mail; dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.