Jan 25, 2016
Anza Na Ulichonacho Kupata Mafanikio.
Kisaikolojia na
kimaumbile binadamu wote ni sawa ila tunatofautiana jinsia na matumizi ya vitu
tulivyopewa na mwenyezi Mungu. Na hii ndio hupelekea tofauti kubwa kati ya
walichonacho (Matajiri) na wasionacho (maskini).
Katika kuanza na
ulichonacho leo tunaangalia vitu sita ambavyo tumepewa kama zawadi na Mungu. Na
kila mtu amepewa sawasawa na mwenzie ila tofauti ni matumizi yetu katika
kutupatia kile tunachokitaka katika maisha yetu ambacho ni Mafanikio.
Ili
kufanikiwa haijalishi upo katika hali gani, kitu kikubwa kwako ANZA NA
ULICHONACHO KUPATA MAFANIKIO. Unaweza ukajiuliza kivipi? Usipate tabu. Ungana nami
mzee wa Nyundo nikuhabarishe na kukupa nyundo za kukuzindua katika usingizi ili
upate mafanikio ya kweli.
1. Akili.
Ni ukweli kwamba kila binadamu ana akili ya kung'amua jema na
baya ila sio wote wanaojua thamani ya akili walizonazo. Wapo wanazitumia kwa
faida na malengo na kupata mafanikio ila wapo wanaozitumia vibaya na kuishia
kuishi maisha shida hadi wanakufa.
Katika kuitumia akili ndipo huonekana tofauti ya wanaojua na
wasiojua kitu. Wanaofuata mkumbo na wanatumia akili zao kufikiri na kuamua ni
nini wafanye, kivipi na wakati gani. Ili kuonyesha matumizi sahihi ya akili
kila binadamu anatakiwa kufikiri na kuwaza kabla ya kuamua kufanya jambo lolote
katika maisha yake.
Ni vyema tusiwe watu wa kuamini kirahisi tunayoona na kusikia
kwa watu na kuyafanya bila tafakari. Tuzitumie akili zetu katika kujituma na
kufikiri kwa utofauti na wanavyofiki wengine . Tuwe tayari kujifunza kwa wenye
elimu juu ya kile tunataka kufanya na sio kuiga wanavyofanya watu
wengine.
TUMIA AKILI YAKO VIZURI KUKUFANIKISHA. |
2. Muda.
Kila binadamu awaye ana muda na amepewa muda wa kuishi na
kufanya mambo yake kwa uhuru na amani . Lakini si watu wote wanaoutumia
muda wao vizuri katika kujipatia mafanikio. Wengi hutumia ujana wao katika
starehe, ulevi na kujirusha. Wengine wanatumia muda wao katika kufuatilia
maisha ya watu umbea na majivuno.
Pamoja na kutumia muda hovyo lakini kumbuka, huo ndio muda wako
wa kujitafutia maisha na mafanikio. Muda ndio rasilimali muhimu kuliko zote
ukiutumia vizuri hakika mafanikio utafanikiwa. Embu jiulize kuna tofauti gani
kati ya tajiri na masikini katika muda? Kila mtu ana masaa 24 tofauti ni
matumizi tu .
Ukafatilia utagundua, tajiri ana panga malengo na mipangilio
yake katika siku wakati maskini hana mipangilio na muda wake anaweza kushinda
asubuhi hadi jioni anaangalia
Televisheni au movie ambazo hazimsaidii kitu katika maisha yake. Jiangalie
vizuri unatumiaje muda wako ili kuyafikia mafanikio yako?
3. Watu.
Kila mtu iwe kwa kutaka
au kutotaka amezungukwa na jamii ya watu. Na kimsingi umepewa watu hao na Mungu
ili uweze kuwatumia na kupata kile unachotaka. Kuna wale wa hiyari na ambao
unalazimika kuwatafuta mwenyewe ili wakusaidie kupata kile unataka katika
maisha yako.
Kwa mfano mwalimu inabidi
umtafute ili akupe elimu, wataalamu wa afya inakulazimu uwafuate ili wakutibu. Lakini
kuna watu ambao umepewa bila kutaka au kupanga wewe kama wazazi, ndugu, wajomba
na mashangazi. Hakuna aliyepanga kuzaliwa na wazazi fulani au kuzaliwa tumbo
moja na mtu fulani bila kujali ni masikini au tajiri.
Lakini kutokana na watu hawa unaweza na unapaswa uwatumie katika
ushauri na maarifa waliyonayo ili kupata kile unachotaka ambacho si kingine ni
mafanikio. Kushindwa kwako kuwatumia watu hawa hili litakuwa ni tatizo lingine
ambapo ukishindwa kufanikiwa usimlaumu mtu.
4. Kipawa / kipaji.
Huu ni uwezo wa ndani alionao kila binadamu bila kujali kabila
lake au rangi yake ana kile anachoweza kukifanya tofauti na wenzake. Hicho
ndicho kipaji na mtu akikigundua na kukitumia vizuri hupata mafanikio kwa
haraka.Tena ndio wale ambao muda mfupi hupata utajiri wa ghafla na watu kusema
kajiunga na Freemason huyo au amemuua mama yake ili apate utajiri na maneno
mengineyo.
Siku zote tafuta ukijue kipaji chako na kitumie upate utajiri na
mafanikio katika maisha yako. Unapokuwa na kipaji na ukikitumia ipasavyo
mafanikio makubwa yanakuwa upande wako. Jaribu kuangalia watu wote ambao
walimudu kutumia vipaji vyao kwa namna moja au nyingine maisha yao yako vipi,
bila shaka ni ya mafanikio makubwa sana.
5. Nguvu.
Kila mtu amepewa nguvu na uwezo wa kufanya jambo fulani.Tunaweza
kuzitumia nguvu zetu katika kilimo, biashara na hata kazi yeyote halali na
kujipatie kile tunataka katika maisha. Tatizo watu wengi tumebweteka tunataka
maisha simple/rahisi tulale tuamke kesho
matajiri bila kufanya kazi.
Vijana wengi utakuta wanataka kufanya kazi rahisi na kupata
faida kubwa. Wanacheza mchezo wa kubeti wakiamini watatoka kimaisha, wanacheza
bahati nasibu wakiamini watapata utajiri, wengine wanauza miili yao
wakiamini ndio njia pekee ya kupata maisha mazuri na bora kumbe wanapotea na
kuharibikiwa kabisa.
6. Afya.
Kila binadamu amepewa afya ya mwili kabla ya kufikwa na maradhi.
Tunapaswa tujue uzima na afya ni majaaliwa ya mwenyezi Mungu hivyo tuzitumie
vizuri afya zetu katika kupata kile tunataka katika maisha yetu. Afya ni kitu
cha muhimu kukilinda na kukitumia vilivyo kwa faida ya maisha yetu.
Ili tufurahie maisha yetu lazima tujali afya zetu kwa kula
vyakula bora na vinywaji bora. Na sio kula ilimradi chakula. Na kunywa
ilimradi tu au kwa kuwa watu wanakula nasi tule. Tujitahidi kuzilinda na
kuzitumia vizuri afya zetu ili tuweze kutimiza malengo yetu tuliyojipangia katika
maisha. Bila afya nzuri hakuna Mafanikio. Kila mtu na azingatie mbinu hizi katika
mafanikio yake zitamsaidia na kumwongoza.
Kabla ya kuhitimisha makala hii ni vyema ukajiuliza je, unatumia
vizuri akili, watu, muda, nguvu, afya na kipawa ulichonacho kukusaidia kufikia
mafanikio yako? Tafakari juu ya hili na chukua hatua.
Asanteni kwa kunifuatilia na kuwa pamoja nami. Pia naamini
umepata mwanga na kitu cha kukusaidia kutoka hapo ulipo.
Nakutakia siku njema na endelea kujifunza mambo mengine matamu
ya kimafanikio hapa kwenye mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kila wakati.
Shukrani za pekee zimwendee SHARIFF H. KISUDA a.k.a MZEE WA
NYUNDO kwa kutushirikisha makala hii nzuri. Unaweza ukawasilina naye kwa simu
namba 0715 079993 kwa msaada zaidi wa Saikolojia ya mafanikio.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.