google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Dec 8, 2018

Jambo Hili Lisiwe Kizuizi Cha Mafanikio Yako...Kila Mtu Anapitia.

No comments :
Haijalishi unafanya kitu gani na una uhakika gani wa kukamilisha kitu hicho, lakini huwezi kukipata kitu hicho moja kwa moja kwa jinsi unavyotaka wewe iwe. Yapo mambo ambayo ni lazima yataingilia malengo yako hayo kwa namna moja au nyingine.
Unapojiwekea malengo, utafika wakati malengo yako yataingiliwa tu. Itafika wakati pesa ambayo ulikuwa umeitenga kwa ajili ya malengo fulani, unaweza ukashangaa umeitumia kwa dharura na kujikuta tena unaanza upya.
Lakini pia unaweza ukawa umeamua kufanya kazi fulani inayohitaji utulivu, lakini ukashangaa simu ikaita, au ukapokea dharura ya kuitwa pengine na bosi wako na miingiliano mingi kama hiyo ambayo naweza kusema haikwepiki kirahisi.
Yanapotokea mambo kama haya ambayo yanaingilia ndoto na malengo yako isifike mahali ukajikuta unakata tamaa. Unachotakiwa kuelewa ni kwamba, mwingiliano wa vitu katika malengo, ni kitu ambacho kinamtokea kila mtu na kwa wakati wake.

Mwingiliano wa mambo ukizidi, ni sumu ya mafanikio yako.
Kama ikitokea umepoteza mwelekeo na huoni tena dalili ya kufanikiwa kutokana na mambo mengi kuingilia ndoto zako, usikate tamaa, unatakiwa kurudi haraka sana na kuendelea kuifatilia ndoto yako.
Usipoteze muda wako kulalamika au kulaumu hali ambayo imekupata, badala yake tumia muda huo, kutafuta njia ambayo itakufanya uirudie ndoto yako haraka sana na sio kuipotezea kama ambavyo unataka kufanya.
Ni kawaida sana kwa mambo ambayo yanaonekana kwa macho ya kawaida hayawezekani, kuingiliwa na vitu ambavyo hukutarajia. Lakini ukikata tamaa na kusema ndio basi, uwe na uhakika utaipoteza ndoto yako.
Weka mkazo katika akili yako wa kusahau karibu kila kitu nakuamini, unaweza kuirudia ndoto yako hadi kuifanikisha, hata kama hapa kumetokea mwingiliano mkubwa sana ambao kwa uwazi umeonekana kukuvuruga na kukuchanganya kabisa.
Kuingiliana mambo ambayo hukutegemea kunapokuja kama huelewi vizuri, unaweza ukaacha kila kitu, lakini nikwambie hivi tu, kitu hiki kidogo kisiwe kizuizi kwako cha kukuzuia kufanikiwa hata kidogo.
Maisha ya mafanikio makubwa bado yanakuja kwenye maisha yako, changamoto ndogo kama hizi kwako kutokea, anza kuzichukulia kama fundisho la kukukomaza na kukupeleka kwenye mafanikio  makubwa. Jipe moyo na inawezekana.
Tunakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio yako makubwa.
Daima tupo pamoja mpaka maisha yako yaimarike na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kujifunza kila siku maisha na mafanikio.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Dec 7, 2018

Haya Ndiyo Mambo Matano Yanayofanya Maisha Yako Kuwa Magumu Kila Siku.

No comments :
Mara nyingi kwa watu wenye umri mkubwa huwa tunafikiri kwamba,  tulipokuwa wadogo maisha yalikuwa rahisi, si ndiyo?  Na sasa  tunaona mambo yamebadilika na kuna ugumu umeingia katika maisha yetu ya kila siku. Naomba nikwambie kwamba, maisha bado yapo rahisi vile vile kama tulivyokuwa tunayaona utotoni na kila siku yataendelea kuwa hivyo milele. Tofauti iliyopo ni kuwa tumeongezeka  umri na hata maumbo yetu yamebadilika, na jinsi tunavyoongezeka umri ndivyo tunavyozidi kuyafanya yawe magumu.

Tulipokuwa wadogo kila kitu tulikangalia katika mtazamo wa matumaini. Tulikuwa tunajua tunachohitaji na hatukuwaza tofauti juu ya mahitaji yetu kama tunaweza kukosa kitu tunachohitaji. Tuliwapenda watu waliokuwa wanatuonyesha tabasamu. Tuliwakimbia waliotuonyesha nyuso za kisirani. Tulikuwa tunakula pale tunaposikia njaa, na kunywa pale tuliposikia kiu na kulala tulipojisikia kuchoka.
 Sasa tunavyozidi kuishi sana mawazo na akili zetu zinatawaliwa na hisia hasi juu ya mahitaji yetu katika maisha kutoka katika nguvu za nje.

Kwa namna moja ama nyingine tunaanza kusita na kuhoji nafsi zetu juu ya mahitaji yetu. Pale kikwazo kipya au maumivu yanapotufika tunaanguka na kukata tamaa. Jambo hili linatutokea mara kwa mara katika maisha yetu, na mara kadhaa tumeshajiapiza kuwa hatutaki kuanguka tena kama ilivyotokea mwanzo bila kutafuta ufumbuzi wa jambo lililosababisha kuanguka tunaishia kukwepa tatizo.
Badala yake tunatumia vitu kama chakula na pombe kutibu majeraha yetu na kujaza mapengo ya furaha zetu.

Wengi wetu tunafanya kazi masaa mengi mpaka usiku wa manane, tukikimbia utatuzi wa tatizo lililotokea katika familia zetu iwe na mke au watoto. Tunatunza hasira na visasi mioyoni mwetu, tunafanya utapeli na udanganyifu kwetu wenyewe na kwa wenzetu ili tu tusonge mbele. Na pale mbinu zinaposhindwa kufanya kazi, tunaanza kuishi juu ya uwezo wetu, tunatumia uongo kuficha uongo, na kula na kunywa zaidi ili tu tuyafanye maisha yetu yawe na nafuu.

Katika mfumo huu wa maisha tu nazidi kuyafanya maisha yetu yawe magumu zaidi na zaidi na tunaanza kupoteza muunganiko wa nafsi zetu halisi na mahitaji yetu halisi katika maisha tunayoishi. Kama kwa utangulizi huu umeshaanza kukuna kichwa na kujiuliza kama na wewe upo humo, hapa nakuletea mambo ambayo ukianza au kuendeleza kuyafanya yatafanya maisha yako kuwa magumu bila sababu za msingi, unajua mambo hayo ni yapi?

Haya ndiyo mambo  matano yanayofanya maisha yako kuwa magumu kila siku:-

1. Unaangalia watu wengine kukupa majibu ya maswali ambayo ungejijibu mwenyewe.

Wakati tulipokuwa wadogo, uwezo wetu wa kujiamulia mambo yetu ulikuwa mdogo na wakubwa zetu walibeba hilo jukumu la kutuamulia kipi cha kufikiri,
kipi ni chema na nini maana ya kufanikiwa. Sasa ushakua, hupaswi kuendelea kuishi utegemezi wa fikra  tena katika maisha yako. Kuwa huru jivue gamba la utegemezi ili uanze kutumia ubongo wako katika kutoa majibu ya maswali yanayokukabili kila siku katika maisha yako.

Anza  kutegemea fikra zako, isikilize nafsi yako, vunja kichuguu cha utegemezi nje ya mlango wako. Mpaka sasa unajua jambo gani ni sahihi katika maisha yako.
Usiache wengine wakuamulie nini cha kuchagua kwani mwisho wa siku wewe ndio mwathirika mkuu wa maamuzi yako. Pale utakapoacha kuishi kwa kadri ya maelekezo ya watu wengine na ukaanza kuishi kwa kadri ya majibu yanayotoka kichwani mwako utapata kile kitu unachohitaji katika maisha yako.


2. Unaruhusu watu wengine wakufanye ujione una hatia kwa namna unavyoishi. 
Ili mradi haumuumizi mtu kwa mambo unayofanya endelea kuishi kadri upendavyo na katika njia unazoona zinakupa furaha wewe mwenyewe. Muda mwengine tunapoteza mwelekeo pale tu tunapojaribu kuishi kwa kadri ya mtazamo wa watu wengine, kujaribu kuishi matarajio yao na mambo yanayowafurahisha wao kwetu. Chukua muda na anza kutafakari juu ya mfumo huo wa maisha.

Je, unafanya mambo unayoyaamini au sababu tu uwafurahishe wengine?
Anza kukumbuka matarajio yako mwenyewe ni yapi. Kuna maneno matatu yanayopendwa kutumiwa kurahisisha tafsiri ya maisha: ishi, fanya na penda ili uwe na furaha katika maisha yako sababu uhusiano waweza kufa muda wowote ila utaendelea kuishi na nafsi yako mpaka pale maisha yako yatakapoishia.

 3. Unaruhusu watu wabaya waharibu mazuri yako.

Hata siku moja usijikie hatia kuwaondoa watu wanaokurudisha nyuma katika maisha yako. Haijalishi huyo mtu ni ndugu, mpenzi, mfanyakazi mwenzako, mwanafunzi mwenzako, rafiki wa tangu utotoni au rafiki mpya. Hutakiwi kuweka chumba kwa ajili ya watu wanaokuletea maumivu katika maisha yako au wanaokufanya ujisikie mnyonge na mdogo. Labda kama watabadilisha namna yao wanavyoishi na wewe ila kama haonyeshi kujali hisia zako na anaendelea kuvuka mipaka katika maisha yako na kuendelea kukuumiza, fungua mlango watoke nje hupaswi kuendelea kuwalea.

4. Unataka kushindana na kila mtu.

Ukitaka kushindana na kila mtu utakuwa mchungu kwa watu wanaokuzunguka. Kwani utaanza kujitengenezea mazingira ya kutojifunza vitu vipya na hata kurekebishwa pale panapohitaji marekebisho. Mtu anayetaka kuwa bora hashindani na wengine ili awe bora bali anashindana kumzidi yeye wa jana ili yeye wa leo awe bora  kuliko wa jana. Na elewa hili kuwa  utakuwa bora kuliko unavyodhani, ikiwa utaachana na hiyo tabia yako ya kushindana na watu wengine katika maisha yako. Ukiendelea kushindana na wengine utakuwa unajiumiza mwenyewe katika maisha yako.

5.Unang'ang'ania kuishi na makosa yaliyopita.

Ni jambo zuri sana unapojisamehe mwenyewe kutokana na makosa uliyowahi kuyafanya siku za nyuma katika maisha yako. Unapaswa uanze kuyatumia makosa yaliyopita kama funzo na ulitumie hilo kusonga mbele katika maisha yako. Anza kutengeneza mutaskabali wako leo usiache historia ya nyuma iendelee kukutafsiri wakati majira yamebadilika. Muda mwingine malipo mazuri yanayotoka katika kujituma sio kile unachopata kwa muda huo bali kile kipya ulichojifunza ndio faida zaidi. Usijidanganye kuwa maisha ya furaha ni yale yasiyo na shida, si kweli hata kidogo bali maisha ya furaha ni kuona unavishinda vikwazo kila vinapojitokeza na kusonga mbele.

Maisha ni jinsi tunavyoyatafsiri sisi wenyewe, ikiwa tutaamua kubadili mtazamo wa namna tunavyoyachukulia au jinsi watu wanavyotaka tuyachukulie. Tunaweza kuyafikia malengo yetu. Hayo ndiyo mambo matano yanayofanya maisha yako kuwa mgumu kila siku.

Nakutakia ushindi katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,







Dec 5, 2018

Fahamu Mwezi Sahihi Wa Kuyapanga Malengo Ya Kimafanikio Kabla Haujauanza Mwaka Mpya.

No comments :
Zikiwa na siku kadhaa zimesalia ili kukamilisha mwaka na kuanza mwaka mpya ipo haja kubwa sana ya kufahamu mambo ya msingi yanayohusu malengo yako ambayo uliyapanga mwaka huu na jinsi ya kuanza vyema mwaka mpya ujao.

Fanya tafakari kuhusu malengo.

Chukua walau dakika chache kutafakari juu ya malengo ambayo ulijipangia mwaka jana  ni je umeyakamilisha kwa asilimia ngapi? na kama hujakamilisha ni nini kilikuwa kikwazo kikubwa kilichofanya usikamilishe malengo hayo?

Nakusihi ufanye zoezi hili  la tafakuri juu ya maisha yako ili ujue ni wapi ulipokosea na ufanye marekebisho, ili mwaka ujao usifanye makosa hayo hayo tena ambayo yatakusababisha ushindwe tena kutimiza malengo yako Utakayopanga kuyafanya mwaka ujao.
Katika suala la upangaji wa malengo watu wengi huwa tunakosea sana ila  naomba nikukumbushe ya kwamba katika upangaji wa malengo yako ya kimafanikio mwezi wa kwanza sio mwezi wa kupanga malengo yako bali uwe ni mwezi wa kutekeleza malengo ulikwishayapanga mwezi wa  12.

Hivyo kwa maneno mengine naomba nikupe fasihi hii, mwezi wa 12 ni mwezi wa kupanga malengo yako, inapofika mwezi 1 mpaka mwezi 11 uwe ni mwezi wa kutekeleza malengo hayo.

Mpaka kufikia hapo nikutakie upangaji mwema wa malengo yako katika mwezi huu wa upangaji malengo, huku ukiweka nguvu na akili katika utekelezaji hapo mwaka ujao.

Asante kwa kusoma fasihi hii nikutakie siku njema na mafanikio mema.

Ndimi: Afisa Mipango Benson Chonya.


Dec 4, 2018

Jifunze Unavyoweza Kupanda Moyoni Yale Unayotaka Yatokee Katika Maisha Yako.

No comments :
Ipo namna ambayo unaweza ukapanda au ukatengeneza yale unayotaka na yakatokea maishani mwako. Hiki si kitu cha kushangaza tena uwezo huo wa kuumba maisha yoyote yale na uyatakayo unayo na ni jambo linalowezekana kabisa.
Kwa mfano, kama unataka usalama jishawishi moyoni mwako kwamba uko salama, kama unahitaji pesa jiambie nina pesa nyingi. Kama unataka chochote kile ukitakacho, ni zoezi tu la kukazana kujiambia kwamba unataka kitu hicho ukitakacho..
Chochote unachohitaji anza kujiambia kwamba unacho tayari. Kitu cha msingi kwako ni wewe kubadilika kuingia katika masafa unayohitaji hata kabla ya mazingira kubadilika ndipo nazingira yatafuata ya kukipata kitu hicho.
Hata kidogo usiseme sitaki magonjwa, sitaki kuumwa umwa, sitaki mwanamke mwemba mba, sitaki mwanamume maskini, maana hivyo unavyovikataa ndivyo utakavyoletewa.  Unajua kwa nini hivyo ndivyo utakavyoletewa, sikiliza. 
Mawazo ya kina yanafanyia kazi yanachopelekewa,na hayana upembuzi wowote, hayana akili kama wewe kujua kwamba hili linakataliwa au linakubaliwa. Mawazo haya yanajua kile tu unachokisema ndicho unachokitaka na yanakupa kweli.
Ndio sababu wengi sana wameletewa vile vitu walivyokuwa wakivikataa sana. Kama hauhitaji umaskini basi usiuwazie umaskini bali wazia utajiri. Jiambie mimi ni tajiri, huku ukijionesha wewe ni aina gani na kiwango gani wewe ni tajiri, jiambie wewe una pesa nyingi.
Kile mlichokuwa mnakosea ni kule kumueleza Mungu matatizo yako, mimi nateseka,mimi naonewa baba, mimi ni mgonjwa, baba mimi sina pesa. Yale mliyokuwa mkimtajia Mungu ndiyo mliyokuwa mkirudishiwa zaidi.
Akili za kina ndizo zilizokuwa zikitendea kazi mazungumzo yenu hayo na kusema ukweli hizo hazina akili ya kupambanua bali zina akili ya kuumba kinachohitajiwa. Unaona sasa kila unachokitajja ndicho kinachotokea kwenye maisha yako.
Mawazo ya kina yana nguvu mara 90 ya mawazo ya kawaida, na linapofanikiwa jambo kuumbika humo basi hufanyika mara moja, ni nguvu ya uumbaji. Kwa lugha rahisi mawazo haya ya kina ndio ynayoumba maisha yako hata kama wewe hujui.
Jambo la msingi kwako usipeleke humo vitu usivyohitaji, peleka humo vitu unavyohitaji vitokee maana kila kitakachofanikiwa kuumbika humo hutokea. Kwa sababu hii dio maana unatakiwa uwe makini sana na kile unachokiongea maana unakiumba.
Ni sababu mojawapo kwa sababu hatuna zuri na baya kwa sababu kwa kadiri unavyosema lile ndilo baya unalipa uwezo wa  kufanyika tena na tena kwa sababu chochote unachokandamiza unakivuta zaidi, kukandamiza ni kukikataa na hivyo kukilazimisha kiingie ndani ya mawazo ya kina, ni sawa na kukandamiza bomu.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA NDUGU, JOSEPH JACKSON WA MWANZA TANZANIA, MAWASILIANO 0754 688 219.

Dec 3, 2018

Marafiki Ambao Hutakiwi Kuwa Nao Kama Unataka Kufika Mbali Kimafanikio.

No comments :
Upo mchango mkubwa sana wa marafiki katika kutufikisha kwenye mafanikio. Lakini hata hivyo ieleweke hivi si kila rafiki ni rafiki mwema katika kutusaidia kutufikisha kwenye mafanikio yetu. Wapo marafiki ambao hawafai kuambatana nasi hata kidogo kama tunataka kufanikiwa na kuweza kufika mbali kabisa kimafanikio.
Hapa kati makala haya nataka nikuonyeshe rafiki  ambao hutakiwi kuambatana nao katika safari yako ya kimafanikio. Kama utaamua kuambatana na marafiki hawa ujue kabisa utakuwa unafanya kazi ya ‘makitaimu’ yaani utakuwa huendi mbali sana kimafanikio. Twende sasa pamoja kujifunza aina hii ya marafiki unaotakiwa kuwaepuka.

1. Marafiki wakosoaji.
Aina hii ya marafiki watakakukosoa kila kitu unachokifanya au kile ulichonacho. Watakosoa kwamba ukifanyacho hakifai. Watakosoa utendaji wako wa kazi na hata pia wanaweza kukosoa aina ya maisha unayoishi.
Kuwa na marafiki wa namna hii ambao ni wakosoaji ni sawa na kujitafutia majanga. Hawa ni marafiki ambao unatakiwa uwakwepe sana. Kuendelea kukaa na marafiki hawa huko ni kujipotezea muda wako wewe, kwani hawatakusaidia kufanikiwa.
2. Marafiki wasio na malengo ya kimaisha.
Hawa pia ni aina ya marafiki wabaya sana kwenye maisha yako. Unapokuwa na marafiki wa aina hii unatakiwa kuelewa kwamba upo uwezekano mkubwa hata wewe ukaanza kuishi mfumo wa maisha yao yaani ukaishi bila malengo yoyote.
Marafiki hawa kwa sababu hawana malengo, basi hata muda wao wanautumia hovyo sana. Muda ambao ungetumika kufanya vitu vya msingi wao wanaoupoteza, ukifatilia sababu hasa, utagundua hawana malengo maishani mwao.
3. Marafiki watumiaji.
Hii ni aina ya marafiki ambao muda wao mwingi sana wanawaza juu ya kutumia. Marafiki hawa hawako tayari kuweka pesa kwa ajili ya kuwekeza bali ni kuzitumia. Kila ikifika ijumaa wao ni sherehe kwa kujirusha huku na kule.
Epuka sana marafiki hawa kwani watakufanya wewe ushindwe kuwekeza pesa zako kwa ajili ya kesho. Pia marafiki hawa watakufanya utumie sana pesa zako hovyo bila mpangilio. Kama ukiweza kuwaepuka marafiki hawa basi utajenga mwelekeo wa kufanikiwa.
4. Marafiki wanaopenda ushindani usio na maana.
Hawa ni marafiki ambao kila kitu ukifanya wanataka kushindana na wewe. Kwa mfano, ukinunua kitu hiki na wao wanataka kununua. Ukiwekeza kwenye mradi huu na wao wanataka kuwekeza. Kama unataka kufika mbali kimafanikio, hawa ni marafiki ambao pia hawakufai kabisa
Kuendelea kuwa na marafiki hawa, inabidi utambue wanakupotezea sana nguvu zako nyingi ambazo ungezitumia kuweza kufanikiwa. Kwa kifupi hawa ni marafiki wasumbufu kwako na hawakufai katika kukufikisha kwenye ndoto zako.
Kwa kuhitimisha makala haya, hizi ndizo aina za marafiki unaotakiwa kuwaepuka sana katika maisha yako. Ni jukumu lako sasa kuchagua marafiki waliobora kwako na kuachana na marafiki watakaokurudisha nyuma kimafanikio.
Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatimia.
Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kujifunza maisha na mafanikio.
Pia rafiki, kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu mafanikio, karibu kwenye kundi la WHATS APP LA MAFANIKIO, kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S kwenda 0713 048 035, hapo utapata utaratibu mzima wa kujiunga.
Kama wewe ni mfugaji wa kuku na unahitaji vifaranga bora, waone DM POULTRY FARM PROJECT kwa huduma ya uhakika. Hawa ni wauzaji wa vifaranga wa kuku aina ya KUROILER, SASSO, KIENYEJI ASILIA na KUCHI. Kwa mahitaji ya vifaranga wasiliana nao kwa 0767 048 035 au 0686 141097 na wote mnakaribishwa.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 713 048 035,




Dec 2, 2018

Aina Ya Watu Wanaoendelea Haraka Kwenye Maisha Yao.

No comments :
Kwenye maisha wapo watu ambao ukiwaangalia kwa haraka wanaonekana ni kama hawaendelei upesi yaani zile hatua za mafanikio kwao zinaonekana zinachelewa kabisa, na wapo watu ambao wanaonekana wanafanikiwa upesi sana.
Hili nafikiri umeshawahi kuliona, na kuna wakati labda ulijiuliza hawa wanaoendelea sana ni watu wa namna gani. Pia ukaendelea kujiuliza kwa nini wao waendelee upesi na wengine wasiendelee upesi? Je, kuna bahati au nini sababu?
Katika makala haya leo tutajifunza aina ya watu ambao wanaendelea sana. Watu hawa ni wa aina gani, karibu tujifunze.
1. Watu wenye mapenzi na kile wanachokifanya.
Watu hawa wenye mapenzi na kile wanachokifanya, ama ‘passionate people’ huwa ni watu wanaofanikiwa. Kwa nini kwao kufanikiwa kunakuwa nje nje ni kwa sababu watu hawa watafanya kila linawezekana hadi kuona wanafanikiwa.
Itafika mahali watu hawa watakosea, lakini kwa sababu wana mapenzi na kitu hicho watakifanya na hadi kuona wanafanikiwa tena kwa kiasi kikubwa kwenye maisha yao. Jaribu kuwatafuta  watu wa namna hii, utagundua wanaendelea kwa haraka sana.
2. Watu wenye nidhamu ya hali ya juu.
Pia kundi lingine la watu ambao wanaendelea kwa haraka ni hili la watu wenye nidhamu kubwa. Nidhamu inawafanya watu hawa wajitume kufanya kile wanachotakiwa kukifanya hata bila kujali kama wana hamasa au hawana hamasa.
Wakati watu wengine wana subiri wapate hamasa ndio wafanye kitu, watu hawa wanajituma tu, pasipo kujali hamasa hiyo. Kwa kifupi ni watu wanaofanya pasipo kujali wanajisikia au hawajisikii ila wao wanafanya, kwa sababu hiyo wanaendelea sana upesi.
3. Watu wanaojitoa mhanga.
Inasemekana pia watu wanaojitoa mhanga juu ya maisha yao, ‘risk taker’ pia ni watu wanaoendelea sana. Watu hawa kwanza hawaogopi kuchukua hatua yoyote, pia hata wakishindwa wanarudi upya tena upesi sana.
Mafanikio yoyote yanawafata watu wa namna hii bila kipingamizi. Mafanikio hayawezi kukwepeka ikiwa unajitoa kweli hata kwenye mazingira ambayo yanaonekana ni hatarishi kwa wengi. Kujitoa huko ndiko kunakowafanikisha sana watu hawa.
4. Watu wanaozingatia jambo moja.
Wale watu ambao mawazo yao wanaweka kwenye jambo moja na kulifanya kwa usahihi, watu hao wanafanikiwa moja kwa moja. Watu hawa mara nyingi hawataki kuzigawanya nguvu zao zikawa katika maeneo makubwa mawili.
Kwa sababu hiyo ya kuweka nguvu zao katika eneo moja hujikuta wakifanikisha mambo yao na kuendelea kwa upesi. Hawa ni watu ambao nasema wanazingatia sana PLAN A ya maisha yao kuliko ile PLAN B. Wanaamini mafanikio yao yapo kwenye ule mpango wa kwanza, hivyo kwa hili hufanikwa.
5. Watu wanaojua kuishi na watu vizuri.
Uzuri wa watu hawa, kwa sababu wanajua kuishi na watu vizuri, hilo linawasaidia kufanya biashara kwa ushirikiano mkubwa, hiyo haitoshi inawasaidia pia kuweza kuwajua wateja kwa wengi kila siku zinavyokwenda.
Unatakiwa kuelewa hivi kwenye maisha hatufanikiwi tukiwa sisi kama sisi, ni lazima tuwe na ushirikino na watu. Kwa kuwa na ushirikiano huo inasaidia sana kuweza kukuza mahusiano yetu kibiashara na hatimaye na sisi kuweza kufanikiwa kwa haraka.
Hizi ndizo aina za watu ambao kwenye maisha huwa ni watu wa mafanikio au kuendelea sana. Kama unataka kuwa miongoni mwao unaweza ukavuta tabia mojawapo hapo na wewe ukawa ni miongoni mwa watu wenye mafanikio ya kasi katika sayari hii.
Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatimia.
Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kujifunza maisha na mafanikio.
Pia rafiki, kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu mafanikio, karibu kwenye kundi la WHATS APP LA MAFANIKIO, kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S kwenda 0713 048 035, hapo utapata utaratibu mzima wa kujiunga.
Kama wewe ni mfugaji wa kuku na unahitaji vifaranga bora, waone DM POULTRY FARM PROJECT kwa huduma ya uhakika. Hawa ni wauzaji wa vifaranga wa kuku aina ya KUROILER, SASSO, KIENYEJI ASILIA na KUCHI. Kwa mahitaji ya vifaranga wasiliana nao kwa 0767 048 035 au 0686 141097 na wote mnakaribishwa.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 713 048 035,


Dec 1, 2018

Kitu Kimoja Ambacho Unatakiwa Kukijua Kuhusu Mafanikio.

No comments :
Kila mtu anataka kufanikiwa. Kila mtu ana kiu, hamasa na nia kubwa ya kuona anafanikiwa kwenye maisha yake. Japokuwa, pamoja na kiu hiyo kipo kitu kimoja ambacho unalazimika ukijue ili uweze kufikia mafanikio hayo.
Kama hutaweza kukijua kitu hicho na huku ukitafuta mafanikio yako, kitakachotokea kwako ni kwamba utakuwa unapata tabu sana kwenye safari ya mafanikio. Kwa lugha rahisi kuna wakati utakuwa huelewi elewi jinsi mambo yanavyokwenda.
Najua safari ya mafanikio ina anza na watu wengi sana, lakini kwa bahati mbaya wengi wanakuwa ni watu wa kuishia njiani. Unajua ni kwa nini, ni kwa sababu ya wengi kushindwa kukujia kitu hicho muhimu katika mafanikio.
Kitu hicho ambacho wewe unalazimika sana kukijua kwenye safari yako ya mafanikio ni kwamba mafanikio yanatumia muda mrefu sana kuyafikia. Hiki ndicho kitu unatakiwa ukiweke kwenye akili yako na kutambua mafanikio hayafikiwi siku moja, yanahitaji muda ili uweze kuyafikia.
Kuna kipindi, wakati naanza kuandika kwenye blog hii nilikuwa nashangaa sana kwa nini inachukua muda mrefu kwa blog hii kuwa na wasomaji wengi. Kwa sababu hii niliamua kujifunza muda halisi wa mafanikio kwa watu waliofanikiwa hasa ni upi.
Nilichokuja kugundua ni kwamba mafanikio yanatumia muda mrefu na si mfupi kama unavyofikiri ili kuweza kuyafikia. Kwa chochote kile unachokifanya, inatakiwa utenge muda wa kutosha ili mpaka kuanza kuona matunda yake.

Kwa mfano, ilichukua muda wa miaka 11 hadi program ya ‘Microsoft’ ya bilionea mkubwa duniani kuanza kufanya kazi na kuleta mafanikio makubwa. Mafanikio yake hayakutokea tu ghafla kuna miaka ilikataika hapa katikati.
Pia ilimchukua miaka 29 kwa Abraham Lincoln hadi kuweza kuwa Rais wa marekani. Ipo mifano mingi inayoonyesha kwamba mafanikio si kitu cha mara moja tu, unatakiwa kuwekeza muda ili uweze kufanikiwa kwenye mafanikio hayo uyatakayo.
Kama utakuwa ni mtu wa kutaka mafanikio na halafu ukategemea mafanikio hayo yakatokea ghafla ghafla kwa muda mchache ni rahisi sana kwako kuweza kukata tamaa na kuona ni kitu ambacho hakiwezekani au mafanikio ni ya watu wa aina fulani tu lakini si wewe.
Kwenye akili yako sasa weka wazi, mafanikio ni safari ya muda mrefu. Unatakiwa kabisa utenge miaka angalau kuanzia 5 hadi 15 ya kutafafuta mafanikio yako  ya kweli na ya kudumu. Ukikurupuka na kutaka mafanikio ya chapu chapu utakwama.
Watu wengi wanakata tamaa kwenye safari ya mafanikio kwa sababu ya kutokujua kwamba mafanikioo yanataka muda mrefu. Katika kipindi cha kutafuta mafanikio yako unatakiwa ujitoe hasa, kuvumilia na kutoa kila ulichonacho hadi ufanikiwe.
Nimekundikia makala haya si kukatisha tamaa bali kukupa ukweli na uhalisia ulivyo. Kama una bisha chunguza mwenyewe kwa watu waliofanikiwa, utagundua wametumia muda mrefu ili kuweza kufanikiwa kwao kwa uhakika.
Kwa kifupi, hakuna mafanikio ya ghafla, hakuna mafanikio ya chapu chapu, unatakiwa kutumia muda na nguvu kujenga mafanikio yako pasipo kukata tamaa, kila siku unatakiwa ujitume kwa kutenga miaka 5 hadi 15 ya mafanikio yako.
Unatakiwa kujua hakuna ambaye atashindwa kama ataamua kufanya kazi kwa bidiii na pasipo kukata tamaa. Kwa mtu wa namna hii ushindi upo mbele yake na unamsubiri kwa hamu kubwa na wewe unaweza kuamua ikawa hivyo kwako.
Kitu cha msingi hapa ambacho unatakiwa kuelewa kwenye makala haya ni kwamba, mafanikio yanatumia muda mrefu kuweza kuyafikia. Hiki ndicho kitu unatakiwa ukiweke akilini mwako wakati unatafuta mafanikio. Ukijua hili mapema hutakata tamaa na  kikubwa kwako endelea kupambana na utafanikiwa.
Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatimia.
Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kujifunza maisha na mafanikio.
Pia rafiki, kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu mafanikio, karibu kwenye kundi la WHATS APP LA MAFANIKIO, kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S kwenda 0713 048 035, hapo utapata utaratibu mzima wa kujiunga.
Kama wewe ni mfugaji wa kuku na unahitaji vifaranga bora, waone DM POULTRY FARM PROJECT kwa huduma ya uhakika. Hawa ni wauzaji wa vifaranga wa kuku aina ya KUROILER, SASSO, KIENYEJI ASILIA na KUCHI. Kwa mahitaji ya vifaranga wasiliana nao kwa 0767 048 035 au 0686 141097 na wote mnakaribishwa.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 713 048 035,