Jul 25, 2018
Jinsi Umaskini Unavyomaliza Maisha Yako.
Na Eryne Banda,
Dar es salaam.
Umaskini ni kutokuweza kumiliki kitu chochote katika maisha iwe
ni nyumba, gari, shamba, ardhi na kadhalika. Ni kuishi kwa kusaidiwa na watu.
Hapa mtu anakuwa hana uwezo wa kujisimamia, anaishi kwa kuombaomba.
Nikumbushe kwamba umaskini umechangia familia nyingi kutikisika
kiuchumi, zingine zikisambaratika kabisa. Umaskini umesababisha afya mbaya
katika baadhi ya familia huku wengine wakishindwa kuwapa elimu bora watoto wao.
Pamoja na hayo kabla hatujaingia kwenye somo jinsi umaskini
unavyoweza kukumaliza, naomba tuangalie kwanza, aina mbalimbali za umaskini
ambazo zimetuzunguka na zinaendelea kutesa wengi pasipo kujua chanzo chake.
Umaskini wa mawazo.
Huu ni umasikini mbaya sana. Watu wengi wana fedha lakini hawana
mawazo mapya. Umaskini wa mawazo ni mbaya kuliko umaskini wa mali. Jamaa mmoja
aliwahi kusema “mwisho wa mawazo yako ndio mwanzo wa matatizo yako”. Tatizo la
matajiri wengi ni kutokuwa na mawazo mapya japokuwa wana fedha nyingi.
Yapo mapepo yaliyofunga akili za watu ili wasiwe na mawazo
mapya. Mawazo mapya yanatoka kwa Mungu, hivyo tunapaswa kumuomba Mungu kwa
bidii ili atupe mawazo mapya. Je, jiulize hapo ulipo upo tayari kujenga mawazo
mapya kwa kiasi gani au bado unataka kuendelea na mawazo yako yaleyale?
Umaskini wa tabia.
Mtu mmoja aliwahi kusema; karama itakupeleka juu lakini tabia
itakufanya uendelee kubaki chini. Watu wengi wana karama nzuri, vipawa vizuri
lakini wameshindwa kwenye tabia. Watu wengi wamefukuzwa kazi kwa sababu ya
tabia zao mbaya huku wengine wakipewa majina mabaya sababu ya tabia zao.
Ni vema sote tukaelewa kwamba; tabia yako ndiyo
inayokutambulisha kwa watu; ndiyo itakayokupa kibali; ni wakati upo peke yako;
yale mambo unayoyafanya wakati wengine hawakuoni. Tabia yako ndiyo
itakayokufanya uendelee kuwa maskini au uwe tajiri; ndiyo inayokufanya
udharauliwe au uheshimiwe.
Ni muhimu sana kumuomba Mungu abadilishe tabia yako ili iwe
nzuri na ndipo utakapofanikiwa. Usiposhughulikia tabia yako, tabia
itakushughulikia wewe. Watu wengi watakupenda kwa sababu ya tabia yako nzuri.
Kumbuka: Utajiri wa tabia ni zaidi ya utajiri wa fedha/mali. Maisha ndivyo
Yalivyo.
Umaskini wa marafiki.
Mafanikio yanahitaji uwe na watu wazuri na hakika, huwezi
kufanikiwa peke yako. Watu wengi wamekosa kuwa na marafiki wazuri ndiyo maana
wameshindwa kufanikiwa. Umaskini wa marafiki ni kuunganishwa na marafiki wabaya
ambao ni chanzo cha kuangamiza hatma yako.
Kwa mfano, ili Daudi awe mfalme, Mungu alimuunganisha na
Yonathani ili aje kuwa mfalme. Bila ya Yonathani, Daudi asingekuwa mfalme hata
kama alikuwa amepakwa mafuta.
Alihitaji mtu wa kumshika mkono na kumfikisha kwenye kiti chake
cha ufalme. Soma andiko la Mungu katika 1Samweli 18: 3, “Nao Yonathani na Daudi
wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe.”
Mpenzi msomaji, wapo watu ambao Mungu amewaandaa ili waweze
kukufikisha kwenye hatma yako. Mungu anaweza kukuunganisha na mtu mmoja tu na
maisha yako yakabadilika.
Tazama marafiki zako ulio nao, ndipo unapoweza kufanikiwa kwani
huwezi kufanikiwa peke yako. Ni lazima uwe na watu wazuri wa kukusaidia. Muombe
Mungu akuunganishe na marafiki wazuri, watu wenye bidii kuliko wewe.
Naamini msomaji wangu umejifunza jambo hapo. Tuishie hapa hadi
wiki ijayo ambapo nitaendeleza kidogo mada hii muhimu kwa kutaja aina zaidi za
umaskini ili uweze kujijua kinachokusibu hapo ulipo.
Endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kwa ajili ya
kujifunza na kumasika kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Makala hii imeandikwa
na Eryne Banda wa Dar es salaam,
Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.