google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jan 24, 2015

Hiki Ndicho Kitu Kinachokufanya Ushindwe Mara Kwa Mara Katika Maisha Yako.

No comments :
Habari za leo ndugu msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO, naamini umzima na unaendelea na jitihada za kuboresha maisha yako. Nakukaribisha tena kwa moyo mkunjufu katika makala hii ya leo ambayo ipo kwenye mfumo wa simulizi ambapo kupitia simulizi hii utajifunza vitu vya muhimu vinavyohusiana na  maisha yetu kwa ujumla ya mafanikio tunayotafuta kila siku. Kupitia simulizi hii utajifunza na kutambua mambo muhimu ambayo unatakiwa uyafanye na yatakayokuletea mabadiliko makubwa sana katika maisha yako.

Wakati fulani, mtu mmoja alinisimulia kisa ambacho kilinifundisha ukweli mkubwa zaidi kuhusu maisha. Mtu Yule alinisimulia kuwa kulikuwa na bwana mmoja ambaye alienda kwa kinyozi. Wakati anaendelea kunyolewa kulizuka mjadala wa masuala mbalimbali . Mjadala huo, hatimaye ulifika mahali ambapo kinyozi na mteja walijikuta wakijadili masuala ya Mungu. Kinyozi alisema, ‘mimi naamini kabisa hakuna Mungu.’ Yule mteja( Yaani Yule bwana anayenyolewa) alimuuliza, ‘ni kwa nini unaamini kwamba, hakuna Mungu?’

Kinyozi kwa kujiamini kabisa alisema, ‘naamini hivyo kwa sababu, ukienda hapo mtaani hata sasa hivi utathibitisha. Kuna mateso kibao utayaona. Naamini, kama Mungu angekuwepo kusingekuwa na watu wanaoumwa, watu maskini kila mahali, watu wanaouawa bila sababu na uovu ambao umejaa hivi sasa duniani.’ Yule mteja hakuwa anataka kubishana kuhusu masuala ya Mungu, hivyo aliamua kunyamaza. Kinyozi alimnyoa na kumaliza kazi yake, ambapo mteja alitoka nje.

Yule mteja alipofika nje alimwona mtu mmoja ambaye alikuwa na nywele chafu na ndevu nyingi zinazofanana na ukoka kwa uchafu. Kuona vile, Yule mteja alirudi hadi pale kwa kinyozi na alipoingia tu ndani alimwambia, ‘ naamini hakuna vinyozi’. Yule kinyozi alimtazama mteja wake kwa wasiwasi, kabla hajamwambia, ‘hakuna vinyozi wakati mimi unaniona hapa, na nimemaliza mara hii tu kukunyoa?’ Yule mteja alimwambia, ‘kama ingekuwa kuna vinyozi, kusingekuwa na watu wenye nywele ndefu na chafu huko mtaani.’


Yule kinyozi kwa kujiamini kabisa kwamba, ameshinda, alisema, ‘ sasa kama ni kunyolewa si hadi waje hapa ofisini, wanifuate, ndiyo watahudumiwa….’ Yule mteja alimwambia, ‘basi Mungu pia yupo, bali ni hadi wenye shida na matatizo wamfuate na kumjua na kumkubali, ndipo ambapo watapata ahueni kupitia kwake.’ Halafu alitoka nje na kuendelea na shughuli zake.

Ndivyo ilivyo, watu wengi huwa wanadhani kitu au jambo fulani halipo kwa sababu tu hawajui jambo au kitu hicho kinavyofanya kazi. Siyo lazima Mungu, kila kitu kina kanuni ya namna kinavyoweza kujidhihirisha katika hali halisi. Utakuta mtu anakwambia, haiwezekani kufanikiwa kama hujasoma, haiwezekani kufanikiwa kama huna refa, haiwezekani kufanikiwa kama huna au hujafanya kile na kile. Lakini, kati ya hao wanaosema, hakuna hata mmoja ambaye amefanya au amethibitisha nadharia yake.

Ni kwa kuona tu watu wakiwa na shida njiani, wanaamini kwamba ni majibu kwamba Mungu hayupo. Kwa kuona maskini wengi hawana hela wala mali, wanaamini kwamba, hiyo ni dalili ya kutokuwezekana. Kama ilivyo kwa Mungu, hata mafanikio yoyote yale ni lazima mtu ayafuate kule yaliko. Kwa kuyafuata mtu atakutana nayo, kwa kunyoosha miguu tu, ni kweli hatayapata. Kila kitu hapa chini ya jua kinakwenda kwa kanuni, tofauti na watu wengi wanavyofikiri na kudhani.

Kwa hiyo, kama mtu anataka kujua kitu fulani kipo au hapana, inabidi ajifunze kanuni zake. Ni hatari sana kusema haiwezekani kufanikiwa kwa kuwa wewe u maskini au umeshindwa kuyafikia mafanikio unayoyataka, haiwezekani kwa sababu njia zimezibwa. Ni hatari kwa sababu, anachokiona mtu mara nyingi ni umbumbumbu wake au udhaifu wake. Fumbua macho sasa! Ubadili maisha yako kabisa. Achana na fikra za kudhani haiwezekani, tafuta njia kwanini hufanikiwi na kisha songa mbele. Kama utakuwa mtu wa hivi tu, mtu wa kufikiria hufanikiwi kwa sababu zako binafsi zisizo na maana, basi utakuwa umeng’ang’ania kitu kinachozuia mafanikio yako na hiki ndicho kitu kinachokufanya ushindwe mara kwa mara katika maisha yako.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kupata maarifa bora, yakayokuwa msaada mkubwa kwa maisha yako.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,

0713 048 035/dirayamafanikio@gmail.com 






No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.