Aug 31, 2015
Tabia Tatu Muhimu Ambazo Watu Wenye Mafanikio Wanazitumia Kila Siku Kufikia Mafanikio Makubwa.
Njia
pekee na ya haraka kwa wewe kufikia mafanikio makubwa ni kuhakikisha
unajijengea tabia kama walizonazo watu wenye mafanikio makubwa. Watu wenye
mafanikio makubwa katika maisha yao wana tabia za aina fulani ambazo wanazifuata
kila siku bila kuacha. Ni tabia hizo hizo ambazo zinawasaidia sana
kuwafanikisha kwa kile wanachokifanya.
Ili
uweze kufanikiwa na hatimaye kufikia viwango angalau vinavyofanana na wao, unalazimika
kujifunza kujijengea tabia kama walizonazo. Hiki ndicho kitu cha lazima ambacho
unatakiwa kufanya kila wakati. Bila kujijengea tabia hizo, suala la kuwa na
mafanikio makubwa sahau katika maisha yako, zaidi utaishia kuwa kama ulivyo sasa na maisha yako
ya kawaida tu.
Usije
ukafikiria nasema hivi kwa lengo la kukatisha tamaa au ukaona kwamba na
kudharau huwezi kitu, hapana. Ninachotaka ujue hapa huo ndio ukweli wa wazi ambao ninaotakiwa
nikwambia uujue, sitaki kukudanganya kwa chochote, ni lazima kujijengea tabia
hizo kwa faida zetu wenyewe na mafanikio yetu.
Na
pia tambua kwamba tabia hizo ndizo zilizowasadia na kuwafikisha watu kama akina
Bill Gates, Warren Buffet, Brian Tracy na wengineo wengi wenye mafanikio
makubwa pale walipo sasa. Maisha ya watu hawa siku zote wanazitenda tabia hizi na
kuzifuatilia bila kuacha. Unaweza ukawa ni mmoja watu kama hawa ikiwa utakuwa na
tabia kama zao. Je, Unajua ni tabia zipi hasa walizonazo?
1. Kupangilia siku inayofuata mapema.
Unaweza
ukafikiri ni kitu cha kitoto lakini huo ndiyo ukweli, watu wenye mafanikio siku
zote wamejijengea utaratibu wa kupangilia siku zao mapema ikiwezekana kabla.
Nakumbuka wakati ninajijengea tabia hii mwanzoni niliona ni kama kitu kinachopteza
muda na wala hakina maana yoyote ile kwangu.
Lakini
nilipouzoea utaratibu huu nilikuja kugundua unapopangilia siku yako mapema,
mambo yako mengi unakuwa unayafnya kwa urahisi na ufanisi mkubwa. Hii inakuwa hivi kwa sababu unapopangilia siku
kila kitu kinakuwa kwenye utaratibu na ratiba ya utekelezaji. Hivyo inakuwa sio
rahisi kupoteza muda kwa namna yoyote ile.
Kwa
msingi huo, matokeo chanya utayaona ikiwa utafuata tabia kama hii. Kabla
hujalala jizoeze kila siku kupanga mambo yako mapema na kujua kwa siku ya kesho
unakwenda kufanya nini?. Kwa kadri siku zinavyosonga utazoea na utaona
utaratibu ni wa kawaida. Ni muhimu sana kwako kujifunza tabia hii ya kupangilia
siku yako mapema ili kufanikiwa zaidi.
2. Kuweka vipaumbele mapema.
Watu
wenye mafanikio mbali na kuipangilia siku nzima ya kesho mapema, lakini ni watu wenye utaratibu mzuri wa kujiwekea
vipaumbele mapema kabla ya siku inayofuata haijaaanza. Wanakuwa ni watu wa
kujua kesho wataanza kufanya kazi gani na itafuatia kazi gani tena. Hakuna
ajali wala mshituko wa kiutendaji kwao. Kila kitu kimepangwa tayari katika utaratibu
ambao ni rahisi kuweza kufuatwa.
Watu
hawa wanajua bila vipaumbele hakuna kitakachoweza kufanikiwa zaidi ya kurukia
hiki au kile katika kazi na kujikuta ni mtu wa kugusa na kuacha kazi. Kwa
sababu hujiwekei vipaumbele unaweza ukawa unashangga siku nzima ya kazi
hujafanya kazi ya maana zaidi ya kuruka ruka mara huku mara kule. Hiki ni kitu
ambacho kinawatokea wengi.
Hata
ukija kuangalia mazingira mengi ya kazi nyingi zinafanywa bila ufanisi kwa sababu
ya kukosa vipumbele. Ukijifunza kuweka vipaumbele kazi zako nyingi utaweza kuzisukuma
kwa mwendo mkubwa kuliko unavyofikiri. Kwa sababu ndani yako unakuwa na kitu
kinachokwambia ni lazima nifanye kitu hiki. Ukichunguza siri kubwa mojawapo ya
watu wenye mafanikio umejificha kwenye tabia hii ambayo siyo rahisi kwako
kujua.
3. Kukamilisha kazi waliyoianza mpaka
mwisho.
Kama
unataka usifanikiwe katika maisha yako jiwekee utaratibu wa kuanza kazi
nyingine kabla hujamaliza ile ya kwanza. Kwa maisha hayo ukiamua kuyachagua
kwako, suala la kuwa na mafanikio litabaki kuwa kwako hadithi. Wapo watu ambao
maisha yao yako hivi, ni watu wa mipango mingi hivyo kujikuta wanarukia mpango
huu mara ule lakini yote ikiwa inatakiwa umaliziwaji.
Watu
wenye mafanikio ni watu wa kulenga kitu kimoja na wanahakikisha kumekamilika na
kufuata kingine tena. Hata siku moja hawarukii mambo, ni watulivu ndani ya
mioyo yao lakini pia ni watu wa kujizuia kukurupuka. Hii ni moja ya tabia
waliyojijengea na inawasidia kufikia mafanikio makubwa katika maisha yao siku
zote.
Hitimisho
Ikiwa
utaendeleza tabia hizi tatu katika maisha yako, uwe na uhakika ufanisi na
utendaji wako wa kazi utaongezeka na kuwa wa kiwango cha juu.
Kwa
makala nyingine nzuri zaidi endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na
kuboresha maisha yako kila siku.
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,
Aug 24, 2015
Jinsi Unavyoweza Kushinda Tatizo Ulilonalo Na Kuishi Maisha Ya Ushindi Na Furaha.
Kila mmoja wetu katika maisha yake huwa
anakabiliana na matatizo ya aina fulani, ambayo katika hali ya kawaida huwa
siyo rahisi kuyakwepa. Matatizo haya mara nyingi huwa yanajitokeza katika
biashara zetu, familia na wakati mwingine ni matatizo ya mtu binafsi ambayo
huwa nayo. Wakati mwingine matatizo haya, huwa yanaonekana ni makubwa sana
kwetu kama mlima kiasi kwamba tunaanza kufikiri tunashindwa kuyamudu.
Kutokana na matatizo haya wapo ambao hufikiri na
kujiona wanamkosi na wapo ambao hufikiri kuwa wamerithi kwa namna fulani
matatizo. Kila mtu huja na mtazamo wake kutokana na matatizo yanayomkabili.
Kitu wasichokijua kumbe ndani yao wanauwezo mkubwa wa kushinda matatizo waliyonayo
na kuishi kwa ushindi ili mradi tu waitambue siri hiyo na kuweza kuitumia
vizuri.
Katika makala hii utajifunza njia, mbinu na
mikakati ya kukusaidia kushinda tatizo ulilonalo na kuishi maisha ya ushindi.
Utatambua jinsi unavyoweza kuhamasika na kujiamini wewe mwenyewe binafsi kuwa
unaweza kutatua tatizo lako na kufanikiwa kusonga mbele bila shida yoyote.
Ieleweke kuwa kila tatizo ndani yake huwa lina njia ya kulitatua hata liwe
kubwa vipi.
Inaweza isiwe rahisi sana kwako kunielewa lakini, kwa
vyovyote vile iwavyo kama una tatizo linalokukabili huo si mwisho wa kufanikiwa
kwako. Bali ni dalili tosha ya kukupeleka kwenye mafanikio unayoyataka. Unaweza
ukajiuliza kwa nini hiyo iko hivyo? Ni kwa sababu matatizo yanakuwa yanakupa
ukomavu ambao hukuwa nao hapo mwanzo ikiwa utajifunza kupitia matatizo hayo.
Unawezaje kushinda matatizo uliyonayo na kuishi
maisha ya furaha na ushindi?
1.
Amini inawezekana kulitatua tatizo ulilonalo.
Siku zote ushindi wa mambo yote huwa unaanzia
kwenye kuamini. Kuamini ndiyo nguzo kuu ya mafanikio. Unapokuwa na imani inakusaidia
kuweza kutatua tatizo ulilonalo hata liwe kubwa vipi. Kitendo cha kuwa na imani
kinakupa ujasiri wa kukabiliana na tatizo lako bila woga. Watu wenye imani
kubwa mara nyingi huwa ni washindi katika mambo yao.
Hata ukiangalia dini nyingi duniani msingi wake
mkubwa umejikita kwenye imani. Watu mbalimbali waliopata matatizo kipindi hicho
walitumia imani kama nguzo kuu na kuamini kuwa wanaweza kufanikiwa kutoka
katika matatizo waliyonayo na ni kweli waliweza kutoka. Hivyo ili uweze kutoka
katika tatizo ulinalo ni muhimu kuwa na imani ya kukusaidia kutoka hapo.
2. Lijue
tatizo lako vizuri.
Kuamini tu peke yake hakutoshi, ili kuweza kutoka
kwenye tatizo ulinalo ni muhimu pia kulijua tatizo lako vizuri. Kwa nini
ninasema ni muhimu kulijua tatizo lako? Unapolijua tatizo lako hiyo inakusaidia
kuweza kulikabili vizuri bila woga na
hatimaye kulishinda. Kama tatizo lako hulijui vizuri itakuwa ngumu kulishinda.
Hata unapokwenda kwa daktari kwa ajili ya kutibiwa pamoja
na kuwa unajua kuwa unaumwa na umemweleza daktari kuwa pengine kichwa kinauma,
lakini daktari huyu atalazimika kukupima kabla ya kukupa dawa. Anachofanya daktari
hapa, nikuhakikisha anajua tatizo lako vizuri kabla hajakupa dawa ambazo hazihusiki.
Ili utoke kwenye tatizo ulinalo ni muhimu ulijue vizuri ili upate njia sahihi
za kulikabili.
3.
Acha kuchanganyikiwa na tatizo lako.
Hata kama ikitokea tatizo lako limekuwa kubwa kiasi
gani gani kitu cha msingi acha kuchanganyikiwa na tatizo lako. Unaweza ukasema ‘aah hili haliwezekani’, lakini ninachotaka kukwambia inawezekana. Unapokuwa unakuja
juu ama unajihisi kuchanganyikiwa mara nyingi kinachokutokea unakuwa hauna
uwezo wa kulikabili hilo tatizo na badala yake unalikuza.
Watu wengi huwa wanashindwa kukabili vizuri matatizo
yao kutokana na kuhisi kuchanganyikiwa. Linapotokea tatizo kaa chini kwanza
tulia kwa muda kisha tambua njia sahihi ya kulikabili. Mara nyingi huwa
linaonekana kubwa ni kutokana na jinsi tunavyolipokea. Tuchukulie kweli hata
kama ni kubwa hata ukija juu kiasi gani au uhisi kuchanganyikiwa utafanyaje?
ndio limeshatokea. Kitu cha msingi tuliza kwanza sana akili yako unapopata
tatizo, ili upate njia sahihi za kulitatua.
4. Acha
kufikiria sana juu ya tatizo hilo.
Usipoteze muda sana kufikiria juu ya tatizo lako. Si
maanishi hapo unakuwa unalipuuza hapana, ila badala ya kulifikiria tatizo hilo sana
weka nguvu zako nyingi katika kulitatua tatizo hilo na kulishinda. Kama utaendelea
kulifikiria tatizo hilo kwa muda mrefu usishangae kama itatokea hutapata
suluhisho la kulitatua.
Weka nguvu nyingi chanya katika kutatua tatizo lako.
Ikitokea umeshindwa kwa namna moja au nyingine tafuta msaada wa kukusaidia
kutoka kwenye tatizo hilo na acha kung’ang’ania kulifikiria. Inawezekana tatizo
linalokusumbua linaweza lisiwe kubwa sana kama unavyolifikiria, zaidi
unajiumiza bure kwa kulifikiria sana.
5.
Acha kuzungumzia kushindwa.
Inaweza ikawa inaonekana kweli upo katika hali
ngumu ambayo inapelekea kushindwa hiyo ni sawa, lakini acha kuzungumia juu ya
kushindwa kwenye tatizo lako. Kwa kadri unavyokuwa unazungumzia kushindwa
ndivyo ambavyo unakuwa unakosa ujasiri wa kukabiliana na tatizo ulinalo na
mwisho wa siku unajikuta unashindwa kabisa kulitatua.
Kumbuka tatizo lolote ulinalo unaweza kukabiliana
nalo. Haijalishi ukubwa uliopo kwenye hilo tatizo, kwa vyovyote vile iwavyo mwisho
wake upo. Jipe moyo inawezekana na hakuna marefu yasiyo ya ncha, kama ni hivyo
na tatizo lako litaisha hivyohivyo bila wasiwasi.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia
mafanikio makubwa. Karibu sana kwenye mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO
kujifunza na kuhamasika kila siku na endelea kuwashirikisha wengine kuweza
kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 035,
Aug 21, 2015
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuishi Kwa Mafanikio Kazini Kwako.
Watu wenye uwezo mkubwa wa kijamii, wanaweza kuishi
karibu na kila mtu, na ikiwa unataka kufanikiwa katika fani yako, unatakiwa
kuwafanya watu wajisikie vizuri. Jaribu kuchunguza ni kitu gani kinachowaudhi,
nini kinawafurahisha na baadae utumie vifaa hivyo wakati unaposhirikana nao
kila siku.
Nguzo kuu ya kupendwa ni kuweza kujinasibisha na
hali tofauti. Hii haina maana kwamba, unalazimika kuwa mtu ambaye wewe sivyo
ulivyo. Kila mmoja wetu ana matatizo yake, anaweza kubadilika na ni mwenye
utashi tofauti. Unahitaji kujitambua wewe mwenyewe kiasi cha kutosha na
kufahamu ni kwa namna gani tofauti unaweza kujitokeza kwa kundi fulani la watu.
Fani ya saikolojia inayoelekea kwenye suala hili ni
Saikolojia ya jamii. Na kwa bahati nzuri tunazo kumbukumbu nyingi sana kutoka
kwenye tafiti za kidaktari zinazotueleza namna mawazo, hisia na tabia za watu
zinavyotawaliwa na uhalisia, fikara na matarajio ya watu wengine. Tumia utafiti
huu kuwa mtu ambaye kila mtu atapenda kufanya nawe kazi.
Lakini waweza kugundua katika nafsi yako zinazoweza kushirikiana na kila mtu, ikiwa ni mwangalifu kwa nafsi
yako na zile za wengine. Wanasaikolojia ya jamii huwaita watu wanaochunguza
hali za kijamii na kujaribu kutafuta vile watakavyoweza kuishi na jamii
kulingana na wao walivyo kuwa ni ‘ wafuatiliaji
wa juu ya nafsi’.
Wafuatiliaji wa nafsi ni mabingwa wa kutambua kile
watu watu walio mbali mbele yao wanachotarajia kwa wakati waliopo. Na watu hawa
wana hisia za juu katika ufundi na mbinu za kuvutia, hutazama watu wengine
wanavyotumia mbinu fulani, hujizoeza na baadaye kuzitumia wao.
Kwa baadhi ya watu, ujuzi huu wa kufuatilia wengine
ndani ya kundi, huja wenyewe, wao ni kama kinyonga wanaoweza kusoma hisia za
watu wengine.
Vinyonga hawa hujua nini cha kusema kwa wakubwa wao
wa kazi ili kuwafurahisha wakati pengine ng’ombe wa wakubwa hawa nyumbani
wanapokufa. Watu wengine ni wafuatiliaji wa nafsi. Watu hawa hujaribu kubadili ili kuweza kwenda
mbele kama wanavyotaka wao.
Watu hawa wanachojua ni hali moja tu ya kujiendesha
kama wanaweza kubadilika kwa kufuata hali ilivyo. Hawa ni watu unaoweza kukuta
wakifanya mizaha kwenye mkutano muhimu wa kikazi ama kuonekana wasio na mzaha
kwenye tafrija ama pikiniki ya kampuni.
Mara nyingi vinyonga huonwa kuwa wapuuzi na hawa
wafuatiliaji wa chini wa nafsi, lakini ukweli ni kwamba vinyonga huwa
hawapotezi nafasi kutokana na uwezo wao wa kufanya kazi ns watu wa kila aina.
Ikiwa utaweza kufanya kazi na watu wenye tabia
tofauti, si kwamba utapendwa zaidi kwenye nafsi yako ya kazi tu bali utaweza
kutimiza malengo yako binafsi.
Watu wanaoweza kujenga urafiki na watu wa aina
tofauti kwa wingi, wanakuwa na uwezo kubadilikaa vile wanavyofikiri wao ndivyo
walivyo, kwa mujibu wa Profesa Tracy McLaughlin-Volpe, mhadhiri wa Saikolojia
kwenye Chuo kikuu cha Vermont.
Tofati na kuwa na marafiki wenye tabia za aina
moja, kuwa na marafiki wenye tabia tofauti kunakupa uwezo zaidi za aina moja,
kuwa na marafikki wenye tabia tofauti kunakupa uwezo zaidi wa kujijengea picha
nzuri zaidi yako, unakuwa una nafsi ya kuweza kubadilika na kuwa tu unayetaka
kuwa.
Unahitaji kuwa mtu unayebadilika pale inapobidi,
kwa sababu wanasaikolojia wa jamii pia wamegundua kwamba watu hukumbuka
kirahisi mabaya kliko mema.
Hivyo, ukimweleza mfanyakazi mwenzako mgeni kwamba
mkubwa wenu ni mtanashati , muwazi asiye na mwelekeo, ni wazi mfanyakazi huyo
mpya atamchukulia zaidi mkubwa wenu huyo kama mtu asiye na mweleko kabisa,
Kumbukumbu zako mbaya huweza kunasa zaid kwenye
akili yako kuliko kumbukumbu nzuri. Ikiwa unataka kupendwa, kubaliana na
udhaifu wako na uwa tayari kuubadili. Wale wanaojaribu kwa katia hali zao bora
wasikivu, wenye kuweza kujieleza, wanaopenda wengine bila wao wenyewe kujua
watafanya mambo mazuri ofisini mwao.
Tunakutakia
kila la kheri katika safari yako ya ujasiriamli na endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza na kuhamasika zaidi.
DAIMA
TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,
Aug 20, 2015
HIVI NDIVYO UNAVYOWEZA KUKABILIANA NA WATU WABAYA KATIKA MAISHA YAKO.
Katika maisha yako kwa vyovyote vile huwezi kukosa
watu ambao ni lazima wakuone wewe ni mbaya wao, hufai, huna maana wala lolote
na pengine wanaokupinga kwa mambo mengi ambayo unayafanya hata kama yana msaada
kwao. Unapokutana na watu hawa ambao kwako ni lazima wanakuwa wanakuumiza kwa
namna moja au nyingine huwa unajisikiaje?
Inawezekana ukawa unajisikia vibaya sana kiasi cha
kutaka kupambana nao, lakini ukija kuangalia hiyo kwako haikusaidii sana. Kitu
cha kutambua ni kwamba hawa ndiyo watu wabaya kwako ambao huwezi kuwakwepa,
lakini unao. Kama ni hivyo unawezaje kukabiliana na watu hawa ambapo wakati
mwingine wanaweza kuwa ni jamaa zako wa karibu?
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kukabiliana Na Watu Wabaya
Katika Maisha Yako.
1.
Weka mikakati ya kuongea nao.
Badala ya kuwapa nafasi ya kukuongelea wewe tu,
fanya mpango wa kuweza kuongea nao. Usifanye kosa la kuwakimbia au kuwaongelea
na wewe pembeni. Ukifanikiwa kuongea, hiyo itakusaidia kuweza kulewana nao
vizuri kwa kujua nini hasa tatizo na kulitafutia majibu yanayotakiwa. Na huo
ndiyo unaweza ukawa mwisho wa kukuongelea wewe tena vibaya katika maisha yako.
2. Tafuta
marafiki chanya.
Inaweza kabisa kwako ikawa ngumu kuongea nao na
kila kitu unaona kama kimeshindikana. Lakini kitu muhimu cha kufanya hapa fanya
mpango wa kutafuta marafiki wengine chanya ambao utakuwa nao. Marafiki hawa
watakusaidia kuona mambo kwa mtazamo chanya na kukusahaulisha na wabaya wako ambao pengine
wanakuumiza moyo.
3.
Tafuta msaada zaidi.
Ni vizuri ukatafuta msaada wa kuweza kukusaidia
kupata kile unachohitaji na ukaacha kulaumu kwa nini watu hao wanakusema
vibaya. Tafuta ushauri kwa mtu makini ambaye anaweza kukupa ushauri mzuri wa
namna gani utakavyokabiliana na wabaya wako. Kwa kubadilishana mawazo na
mwingine inaweza kuwa kukupa majibu ya upesi ni nini kifanyike.
4. Acha
kusikiliza sana maneno hayo.
Kama unaamini unasemwa kwa tabia ambayo kwako wewe
uaona ni sahihi, endelea na tabia yako hiyo bila kusikiliza kitu chochote.
Funga masikio na songa mbele kwa kile unachoona ni msaada kwako. Ukisikiliza
kila kitu utajikuta ukiumia sana na mwisho hutafanya kitu chochote cha kuweza
kukabiliana na tatizo lako la kukabiliana na wabaya wako.
5.
Achana nao.
Inaweza ikawa ni uamuzi mgumu kwako, lakini kama
mambo yote yameshindikana hakuna namna ya kufanya zaidi ya kuachana nao. Haina
haja ya kushikiria kitu ambacho kinakutesa. Kwa vyovyote vile watu hao hawana
msaada kwako ni vyema ukafanya uamuzi mgumu wa kuwatoa kwenye ubongo wako na
kuendelea na mambo mengine, vinginevyo utaumiza kichwa kufikiria mambo ambayo
huna uwezo nayo.
Zipo namna nyingi ambazo unaweza ukakabiliana na
watu wabaya maishani mwako, hizo ni baadhi ya mbinu ambazo unaweza kuzitumia
kulifanikisha hilo.
Kwa
makala nyingine nzuri zaidi endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza
kila siku na kuboresha maisha yako.
DAIMA
TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,
Aug 19, 2015
Siri 6 Za Mafanikio Ya Mjasiriamali.
Ili
uweze kufanikiwa ukiwa kama mjasiriamali unahitaji kuzijua siri ama mbinu
muhimu za kuweza kukupa mafanikio hayo. Mbinu hizi zitakusaidia kukuongezea
maarifa ambayo yatakupelekea kufanya
shughuli zako kwa ufanisi na kukupa
mafanikio unayoyahitaji.
Ni
mbinu ambazo ambazo zinatumiwa na wajasirimli wengi wenye mafanikio makubwa
duniani kote. Kwa hiyo ni muhimu hata kwako wewe kuweza kuzitimia. Na mbinu au
siri hzi zipo za aina mbalimbali ambazo mjasiriamali anatakiwa kuzitumia ili
kujipatia uhakika wa mafanikio zaidi.
Zifuatazo
Ni Siri 6 Za Mafanikio Ya Mjasiriamali.
1. Kauli nzuri za kumjali
mteja.
Moja
kati ya sumu kali katika biashara yoyote ile ni kutokumjali mteja. Kwani kwa
kauli yako unaweza kumfanya mteja wako akawa ni wa kudumu katika biashara yako
au kumfukuza kabisa mteja huyo.
Wengi
hufikiri kuwa asipomridhisha mteja mmoja haina tatizo kubwa katika biashara
yake. Lakini ukweli ni kwamba mteja huyo mmoja ana nafasi kubwa ya kukutangazia
biashara yako, kwa kadri utakavyomhudumia vizuri ndivyo atakavyoshawishi
wengine waje kwenye huduma yako.
Acha
kutumia kauli za matusi badala yake tumia maneno mazuri, yenye mvuto mbayo
yatamfanya mteja wako ashawishike kurudi kwako tena. Kujali mteja siyo lazima
uwe mwongeaji sana, bali waweza kutumia maneno machache kama ‘karibu dada, au
samahani’ na mengineyo. Hii ndiyo siri mojawapo ya mafanikio kwa mjasiriamali.
2. Uaminifu.
Uaminifu
ni moja kati ya nguzo muhimu sana kwa mjasiriamali yoyote Yule. Inabidi mjasiriamali
awe mwaminifu kwa wadau wote husika, yaani kwa wateja wake, anakochukulia
bidhaa zake, wafanyabiashara wenzake, taasisi za fedha, serikali na washirika
wake wote.
Unapokuwa
mwaminifu unakuwa unazidi kushirikishwa mambo mengi ya kijasiriamali. Hata mafanikio
ya wajasiriamali wengi wenye mafanikio yametokana na uaminfu. Uaminifu ni moja
ya kati ya mambo yanayotangaza biashara kwa kiasi kikubwa sana. Hivyo matunda
ya kesho katika ujasiriamali yanatokana na uaminifu unaounyesha kila siku.
3. Kujali muda.
Katika
karne hii ya syansi na teknolojia watu wengi huzingatia sana muda ili waweze
kukamilisha mipango yao katika muda unaohitajika. Hivyo kitendo cha kumpotezea
mtu muda wake unamuuingizia hasara kubwa sana. Pengine hujui muda huo kidogo
mtu huyo angeingiza kiasi gani cha pesa.
Kwa
hiyo kwa mjasiriamali ni vyema akawa wa kisasa zaidi kwa kuzingatia muda katika
shughuli zake za kila siku. Ni muhimu sana kuheshimu ahadi ulizopanga na wateja
wako na hata wafanyabiashara wenzako. Muda unachukua nafasi kubwa katika
maendeleo binafsi ya mjasiriamali.
4. Utafiti wa bei na masoko.
Moja
kati ya mambo yanayoweza kupunguza kasi ya mauzo ya mjasiriamali ni bei ya
bidhaa zake kutofautiana kwa kiasi kikubwa na jirani zake. Utakuta bei ni
ileile lakini kila mtu amejipangia bei yenye tofauti kubwa na jirani zake.
Wengine bila uoga hupanga bei mara mbili au tatu zaidi ya jirani zao.
Wateja
wanapoanza kukimbia mtu hufikiri anamkosi, wenzake wanamfitini au amerogwa!
Lakini kumbe sivyo. Bei zako mbaya ndizo zinaweza kuwa chanzo cha kukimbiza
wateja. Kwa hiyo unapopanga bei ni muhimu kuangalia mambo kama tafiti za jirani
zako wanauzaje au uimara wa bidhaa zako.
5. Kubana matumizi.
Ili
upate faida nzuri katika biashara yako, suala la kubana matumizi ni muhimu
sana. Yako maeneo mengi ambayo mjasiriamali anaweza kubana matumizi bila
kuathiri mwenendo wa biashara yake.
Katika
kubana matumizi hakikisha unabana matumizi bila kuharibu ubora wa bidhaa ila
jalli sana matumizi ambayo siyo ya lazima kwako kuyafanya katika biashara yako.
Na pia biashara yako ifanye isije ikabeba matumizi yako mengi binafsi, badala
yake jipangie mshahara.
6. Usafi.
Moja
kati ya vivutio muhimu kwa wateja ni usafi. Wateja hupendelea kununua bidhaa au
kupata huduma katika sehemu na wahudumu walio safi. Hivyo, inatakiwa
mjasiriamali azingatie usafi katika maeneo kama eneo la biashara, usafi binafsi
na bidhaa ziuzazwo au zizalishwazo.
Lakini
kama eneo lako la biashara litakuwa linaendelea kubaki chafu hadi kusubiri eti
Bibi afya aje akague, tayari utakuwa umeshapoteza wateja wengi. Tambua kuwa
unapoimarisha usafi katika biashara yako ndivyo unavyoongeza idadi ya wateja
wako.
Kwa
kadri mjasiamali anavyojua siri hizo, ndivyo hujikuta katika nafasi nzuri ya
kufanikiwa.
Tunakutakia
kila la kheri katika safari yako ya ujasiriamli na endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza na kuhamasika zaidi.
DAIMA
TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,
Aug 15, 2015
Njia 6 Muhimu Za Kukusaidia Kuitawala Hofu Inayokukabili Katika Maisha Yako.
Habari za leo mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRAYA MAFANIKIO, ni matarajio yangu ya kuwa umzima na upo tayari kwa siku nyingine tena kwa ajili ya kujifunza
kitu kipya cha kuweza kubadili maisha yako. Katika makala yetu ya leo
tutaangalia namna tunavyoweza kuzitawala hofu zetu zinazotukabili mara kwa mara katika maisha.
Mara nyingi katika maisha yetu hofu huwa inaonekana
ni kama kitu cha kawaida kwa binadamu kwa sababu tu, kila mtu inampata. Wengi wetu
bila kujijua huwa tuna hofu za aina mbalimbali ambazo huwa zinatukabili. Hofu
hizi huwa zinatofautiana kulingana na mtu mmoja na mwingine. Hofu hizi kwa
wengine huwa ni kubwa zaidi na kwa wengine ni za kawaida tu.
Wapo ambao huwa ni watu wa kuogopa sana juu ya
kesho yao wakiwa hawaelewi nini hatima ya maisha yao ya kesho, wapo ambao
huhofia sana kazi zao wakiwa hawana uhakika wa ajira zao na wapo pia ambao
huhofia juu ya kifo na mengineyo mengi. Ukichunguza utagundua hizi ni baadhi ya
hofu chache, kati ya nyingi ambazo wengi huweza kuwa nazo katika maisha yao.
Lakini hata hivyo ikumbukwe pia hofu hizi mara
nyingi huwa zinasababishwa ama kuzalishwa na jamii yetu tunamoishi. Kwenye
jamii ukiangalia zipo hofu nyingi ambazo
huwa tunapewa kama ‘wewe hufai katika hili,’ huwezi kufanikiwa’ na nyingine
chungu nzima na matokeo yake tunajikuta ni watu wa hofu kila kukicha.
Sasa tunawezaje kuzitawala hofu hizi na kuishi maisha
ya amani?
1. Kuwa
makini na mambo yanayokupa hofu.
Ni muhimu sana kuwa na makini na yale mambo yote
yanayokupa hofu sana. Jaribu kufakari na kujiuliza ni kipi kinachokufanya wewe
kuwa na hofu zaidi. Na pia jiulize tena ikiwa utaachana na hofu hizo nini
ambacho utakipoteza? Kwa kifupi, utagundua hofu nyingi ulizonazo ni wewe
mwenyewe umeamua kuzishikiria na zinakutesa bure.
SOMA; Mambo MuhimuYa kukusaidia Kukupa Furaha Katika Maisha Yako.
2.
Tambua kila mtu ana hofu zake.
Unaweza ukawa unahofu kwa sababu ya kuogopa
kushindwa kitu ulani . Hiyo inaweza ikawa ni sawa lakini kitu cha kutambua
kwako ni kuwa kila mtu kwa namna moja ama nyingine huwa anashindwa kwa sehemu
yake. Kama ni hivyo ni lazima kwako wewe kuweza kumudu hofu zako na kuacha
kuogopa kila kitu bila sababu ya msingi.
3.
Jifunze zaidi mambo chanya.
Hii ni njia mojawapo rahisi ya kuweza kukabiliana
na hofu kwa urahisi. Unapojifunza vitu chanya utajikuta ule woga uliokuwa nao
unapungua siku hadi siku. Unaweza kujifunza kupitia nukuu za mafanikio ama
vitabu au blog nzuri zinazohamisisha kama DIRA YA MAFANIKIO na AMKA MTANZANIA.
Kwa kufanya hivyo utajikuta hofu ulizonazo unakuwa sasa unauwezo wa kuzitawala.
SOMA; Mambo 5 Unayoyapoteza Katika Maisha Yako Kwa Sababu Ya Kuwa Na Hofu.
4. Jaribu kufanya mambo mapya.
SOMA; Mambo 5 Unayoyapoteza Katika Maisha Yako Kwa Sababu Ya Kuwa Na Hofu.
4. Jaribu kufanya mambo mapya.
Inawezekana mfumo wa maisha unaoishi nao wa kufanya
mambo yale siku hadi siku ndiyo unaokupa hofu. Jifunze kufanya mambo mengine
mapya ambayo yataweza kukuongeza ujasiri na nguvu ya kuweza kuikabili hofu uliyonayo.
Kwa kufanya hivyo utajikuta unaitawala hofu yako na kuwa na maisha ya tofauti
na ambayo unayo sasa.
5.
Sikiliza mziki unaokupa matumaini.
Ni vizuri kusikiliza muziki ambao unakupa matumaini
na faraja katika maisha yako ya kesho. Acha kusikiliza mziki tu kwa sababu upo kwenye
kifaa cha kusikilizia. Kwa kusikiliza miziki hii itakupa nguvu kubwa ya wewe
kuweza kusonga mbele pale unapokuwa na hofu na kumudu kuzitawala hofu hizo kwa
sehemu kubwa katika maisha yako.
SOMA; Hivi Ndivyo UnavyowezaKuongeza Thamani Zaidi Katika Maisha Yako.
SOMA; Hivi Ndivyo UnavyowezaKuongeza Thamani Zaidi Katika Maisha Yako.
6.
Kuwa mtu wa matumaini.
Ishi maisha kwa kuamini kuwa hofu ulizonazo unaweza
kuzishinda. Acha kuwa mwoga sana kupitiliza hiyo kwa vyovyote haitakuweza
kukusaidia wewe zaidi ya kukupotezea kwenye njia ya mafanikio. Unapokuwa
unaishi kwa matumaini inakuwa ni njia rahisi kwako ya kuweza kutawala hofu
zinazokukabili.
Hizo ndizo njia muhimu unazoweza kuzitumia kuweza
kuiondoa hofu inayokukabili katika maisha yako. Kwa makala nyingine zaidi
endelea kufuatilia DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,
dirayamafanikio@gmail.com
0713 048035,
Aug 13, 2015
Jifunze Kilimo Bora Cha Vitunguu-2
Habari rafiki na mpenzi
msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO karibu tena katika siku nyingine
ambapo tunapata nafasi ya kujifunza juu ya fursa ya uwekezaji katika kilimo cha
vitunguu lakini ikiwa ni makala ambayo tuliianza wiki iliyopita.
Katika makala hiyo ya wiki
iliyopita tuliweza kuangalia aina za kilimo cha vitunguu, mahitaji muhimu
katika kutayarisha shamba, upandaji wa mbegu za vitunguu, matunzo ya vitunguu,
namna ya kupata mbegu bora pamoja na aina za vitunguu vinavyolimwa nchini kwa
wingi.
Leo katika makala yetu,
tutaendelea na kuangalia katika maeneo mengine muhimu yanayohusika katika suala
zima la uzalishaji wa vitunguu na kukupa faida inayotakiwa ikiwa wewe ni
mkulima uliyepania kufanikiwa. Kwa kuanza makala yetu, tutaanza na kujifunza
magonjwa na wadudu waharibifu kwa vitunguu.
SOMA; Jifunze Kilimo Bora cha Vitunguu
Magonjwa
na wadudu waharibifu kwa vitunguu.
Vitunguu vinashambuliwa na magonjwa na wadudu
mbalimbali na kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili
kudhibiti tatizo kwanza shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua hatua
za kuzuia kabla uharibifu mkubwa haujatokea.
Wadudu waharibifu.
Kuna aina tatu (3) za wadudu wanao haribu zao
hili:
1.Viroboto wa
vitunguu.
Hawa ni wadudu waharibifu namba moja wa zao la
vitunguu hapa nchini Tanzania. Husababisha upotevu mkubwa wa mavuno. Wadudu
hawa huonekana hasa wakati wa kipindi cha joto.
Dalili za kugundua.
Majani yaliyo shambuliwa na wadudu hawa huwa
na mabaka meupe yenye kung'aa. Katika hali iliyo kithiri majani yote hugeuka
kuwa na tabaka nyeupe au kijivu cheupe na baadaye majani hunyauka kabisa.
Kuzuia.
Mdudu huyu huzuiwa kwa kupiga dawa kama vile
thiodan-35, Parathion nk. Ili kupunguza uvamizi mkubwa, panga upandaji wa
vitunguu mapema ili kipindi cha joto kiingiapo zao lako liwe
limekomaa.
Epuka kupanda zao la vitunguu sehemu iliyo
kuwa na mazao aina ya vitunguu kama vile liksi, vitunguu swaumu, n.k. Wadudu
wengine waharibifu wa vitunguu ni funza anayekata miche na minyoo ya mizizi. Hawa
hupigwa vita kwa kuzingatia mzunguko wa mazao bustanini.
2. Chawa wekundu.
(Thrips)
Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa
wekundu. (Thrips) ambao wanashambulia majani, Uharibifu uletwao na wadudu chawa,
unatofautiana msimu mmoja na mwingine kutegemeana na hali ya hewa. Mvua kidogo pamoja na joto kali unasababisha
mlipuko wa wadudu.
Wanashambulia majani kwa kukwarua kwarua na
kunyonya maji hivyo kusababisha majani kuwa na rangi ya
fedha/siliver na baadaye majani yanakauka. Upungufu mkubwa wa mazao unatokea.
Njia ya kudhibiti hawa wadudu ni:-
·
Kuweka shamba katika
hali ya usafi
·
Kuondoa magugu
shambani na yanayozunguka shamba la vitunguu
·
Kupulizia dawa ya
wadudu kama karate, selecron, dursban, actellic.
3. Sota (cutworms)
Sota au viwavi wa nondo wanasababisha
uharibifu mkubwa. Viwavi wanakata mashina ya miche michanga sehemu ya chini ya shina juu ya ardhi. Sota
wanapendelea kula wakati wa usiku na mchana kujificha kwenye
ardhi karibu sana na sehemu waliokata shina. Uharibifu huu
unapunguza sana idadi ya mimea shambani na
kuleta upungufu wa mazao.
Wadudu hawa wanadhibitiwa kwa kupulizia dawa
kama; Karate Dursban na Actellic na kuweka shamba katika hali ya
usafi.
SOMA; Kilimo Bora Cha Pilipili Hoho Na Faida Zake.
4. Utitiri wekundu (Red spider mites)
Hawa ni wadudu wadogo sana, ambao wanajificha
upande wa chini wa majani. Wanafyonza maji kwenye majani na
kusababisha majani kuwa na rangi nyeupe. Wadudu hawa wanatengeneza utando mweupe kuzunguka majani na mashina. Mmea
unashindwa kutengeneza chakula na baadaye inakufa.
Njia ya kudhibiti:-
·
Kupulizia dawa za
wadudu Karate na Selecron.
·
Kuteketeza masalia ya
mazao
·
Kutumia mzunguko wa
mazao
5. Vipekecha majani (leaf miner)
Hawa ni aina ya inzi wadogo, ambao viwavi wake
wanashambulia majani, kwa kupekecha na kutengeneza mitandao
wa mitaro kwenye majani. Viwavi wanashambulia majani na kusababisha majani kukauka. Upungufu mkubwa wa mazao hutokea.
Njia ya dhibiti:
·
Kupulizia dawa ya wadudu
kama karate Selecron na Dursban
·
Kuteketeza masalia ya
mazao
·
Kutumia mzunguko wa
mazao
Magugu.
Miche ya vitunguu, huota taratibu sana, hivyo
miezi ya mwanzoni, miche husongwa sana na magugu. Palizi mbili mpaka tatu
zinashauriwa na zinatosha kuweka shamba safi. Matumizi ya dawa za magugu ni
madogo lakini dawa zinazoshauriwa ni pamoja na Alachlor na Oxyflourfen
(Goal 2E).
Hizi dawa ni nzuri kwani zina uwezo wa kuua
magugu aina mbalimbali. Dawa Inapuliziwa wiki mbili mpaka tatu baada ya
kupandikizwa miche shambani. Palizi baada ya kutumia dawa ya magugu ni muhimu
ili kuondoa magugu sugu na pia kutifulia vitunguu. Wakati wa palizi, vitunguu
na mizizi iliyowazi ifunikwe kwa udongo ili kuzuia jua lisiunguze mizizi au
kubabua vitunguu.
Magonjwa ya vitunguu.
a) Ukungu
mweupe
Ugonjwa huu hujionyesha kipindi cha baridi
iliyo ambatana na unyevunyevu mwingi hewani.
Dalili za kugundua
Ugonjwa huu
·
Utaona unga wa rangi
ya zambarau katika majani.
·
Majani hugeuka rangi
na kuwa njano na baadaye kunyauka.
·
Ugonjwa huu hupenya
hadi chini kwenye tunguu na kusababisha kuoza kwake.
Kuzuia
·
Inashauriwa kubadili
aina ya zao katika shamba lako kwa kupanda mazao mengine yasiyo jamii ya
vitunguu. Kilimo cha mzunguko wa aina mbalimbali za mazao upangwe kiasi kwamba
vitunguu visipandwe eneo moja mpaka baada ya miaka 3 kama ugonjwa ulikuwa
mwingi.
·
Tumia dawa za kuzuia
ukungu. Hii ifanyike kabla ya kuona dalili za ugonjwa kwenye vitunguu. Piga
dawa kama vile maneb, Dithane M45, zineb ya unga, n.k. Wakati unapoona hali ya
hewa inayo wezesha kuenea kwa ugonjwa huu (yaani baridi iliyo ambatana na
unyevunyevu mara kwa mara). Katika kipindi hiki piga dawa kila baada ya siku
sita ili kuzuia kuingia kwa ugonjwa. Ugonjwa ukisha ingia kwenye mimea
hauzuiliki kwani hakuna dawa ya kuponyesha.
b) Ukungu wa kahawia
Ugonjwa huu unaweza kuleta madhara makubwa
wakati vitunguu vikiwa bustanini na hata wakati vikiwa katika ghala.
Dalili
zake
Vikovu vya mbonyeo hujitokeza kwenye majani na
baadaye hutoa doa la rangi ya zambarau. Vikovu hivi hukua na kutengeneza
vidonda ambavyo hukua na kufanya mzunguko katika jani zima au shina la
kitunguu. Baada ya wiki kama tatu hivi tangu kuingia kwa ugonjwa huu, majani
yote huanguka na kukauka. Ugonjwa huu hushambulia vitunguu hata baada ya kuvuna
kwa kupitia shingo ya kitunguu au sehemu yoyote yenye kovu,
kidonda au mkwaruzo.
SOMA; Badili Maisha Yako Kwa
Kuwekeza Kwenye Kilimo Hiki Cha Vitunguu Saumu.
Namna ya kuzuia
Katika bustani, mara uonapo kitunguu chenye dalili za ugonjwa
huu, ondoa mimea na kuiteketeza kwa moto ili kuzuia au kupunguza kuenea kwa
ugonjwa.
·
Kwa kinga ya bustani,
piga dawa za Dithane M 45 na dawa zingine za kuzuia magonjwa ya ukungu. Dawa
hizi zitasaidia kupunguza kutawanyika kwa ugonjwa.
·
Tumia kilimo cha
kuzungusha au kubadilisha mazao katika eneo la bustani yako. Usipande mfululizo
jamii yoyote ya vitunguu katika shamba ulilovuna vitunguu.
·
Wakati wa kuvuna,
epuka kukata au kusababisha vidonda katika vitunguu, yaani vuna kwa kung’olea
na siyo kwa kuchimba na jembe.
·
Baada ya kuvuna anika
vitunguu juani kwa siku moja au mbili kabla ya kuviweka katika magunia au
ghala.
c) Ugonjwa wa kuoza mizizi
Huu ni ugonjwa unaotoka udongoni na
unasababishwa na vimelea vya jamii ya ukungu.
Dalili
Dalili za ugonjwa huu ni mizizi kugeuka rangi
na kuwa njano na baadaye kuwa zambarau. Baada ya muda ugonjwa huenea na mizizi
hufa kwa kunyauka. Majani nayo hugeuka kuwa na rangi ya njano na kisha shina au
mche mzima hunyauka.
Kuzuia
·
Tumia kilimo cha
kuzungusha mazao badala ya kupanda vitunguu katika eneo moja toka msimu moja
hadi mwingine.
·
Panda aina za vitunguu
zinazo vumilia ugonjwa huu kwa mfano: Excel, L 36, Granex, White Granex na red
creole.
Kumbuka tumejifunza kuanzia utayarishaji wa
shamba na aina za mashamba, pili tukaangalia aina za mbegu na jinsi ya kuchagua
mbegu bora yenye kustahimili magonjwa na hali ya hewa, pia tukalenga kwenye
maeneo na hali ya hewa, tukaangaza na katika Magonjwa yanayoweza kuathiri zao
la kitunguu pamoja na kudhibiti wake.
Tunakutakia kila la kheri katika kilimo bora
na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza zaidi.
Makala
hii imeandikwa na mtaalamu wa masuala ya
kilimo na ufugaji ndugu Mosses Shio Wa TANaGRI.blogspot.com
Subscribe to:
Posts
(
Atom
)