google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jan 21, 2015

Tabia 8 Muhimu Unazotakiwa Kuwa Nazo, Ili Kujenga Maisha Ya Mafanikio Makubwa.

No comments :
Ni ukweli usiofichika ili uweze kubadili maisha yako na kuwa ya mafanikio ya kiwango cha juu ni lazima ubadili tabia zako ulizonazo sasa na kuwa na tabia ambazo zitakuongoza kufikia mafanikio mkubwa zaidi. Unaweza usilione hili mapema lakini huu ndio ukweli, linapokuja suala la kutafuta mafanikio vipo vitu vingi unavyotakiwa kuvifanya na kubadili kama vile matumizi mabaya ya muda na pesa, lakini likiwemo na suala la kubadili tabia ulizonazo ambazo zimekufikisha hapo ulipo. (Unaweza ukasoma pia Kama Unataka Kufanikiwa Na Kuwa Tajiri, Acha Tabia Hizi)

Unapobadili baadhi ya tabia zako unakuwa unajiweka kwenye mstari wa kufikia mafanikio yako uliyojiwekea. Kumbuka, mafanikio yanajegwa na na tabia ulizonazo, kwa kadri unavyokuwa na tabia za aina fulani, ndivyo mafanikio yanakuwa upande wako na kwa jinsi unavyokuwa na tabia za aina fulani pia utajikuta ndivyo unavyofukuza mafanikio katika maisha yako bila ya wewe kujijua. Ili kujenga maisha ya mafanikio makubwa  unayohitaji, hakikisha  unakuwa na tabia hizi katika masha yako.

1. Tabia ya kuamka asubuhi na mapema.

Unapoamka asubuhi na mapema kabla ya muda uliojiwekea, kabla ya watu        wengine, unakuwa unapata muda wa kutuliza akili yako, kujisikiliza wewe mwenyewe na kupata nafasi ya kutafakari juu ya maisha yako kwa ujumla.  Pia kwa kuamka asubuhi na mapema sio tu itakusaidia kukupa muda wa ziada wa kutafakari juu ya maisha, hiyo itakusaidia pia kukujengea tabia muhimu ya kupangilia siku yako mapema, wapi uanzie na wapi uishie, ambapo tabia hii itakuongoza kwenye mafanikio. Watu wengi wenye mafanikio wana tabia hii muhimu ambayo inawafanya wazidi kufanikiwa. Ni tabia ambayo unaweza hata wewe kuwa nayo ili ikuletee mafanikio mkubwa.


2. Tabia ya kuilisha akili yako kila mara.
Mara nyingi maisha yetu kwa wengi huwa yametawaliwa na kula vyakula vya kila aina, hilo unalijua. Lakini kuna kitu muhimu ambacho huwa haukilishi na kukisahau mara kwa mara. Kitu hiki sio kingine ni akili yako. Kama ambavyo mwili wako unahitaji kula kila siku pia  hata akili yako inahitaji kulishwa tena sana kila siku. Unahitaji kuilisha akili yako kwa kujisomea kila siku na hili ndilo hitaji la msingi unalotakiwa kuwa nalo ili uweze kufanikiwa. Usiache siku ikapita bila kwako kujifunza kitu kitakachobadili maisha yako. Tumia muda wako vizuri jifunze hata kwa dakika 20 au 30 kwa siku, baada ya muda utaona mabadiliko makubwa katika maisha yako. Hii ni tabia muhimu sana kwako ambayo hutakiwi kuiacha ili kujenga mafanikio ya kudumu.

3. Tabia ya kufanya mazoezi kila siku.

Hata kama ni kwa dakika kumi na tano tu, unahitajika kujiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi kila siku. Ili uweze kufikia mafanikio makubwa unayotaka, kumbuka unatakiwa kuwa na akili safi ndani ya mwili wenye afya ya kutosha. Unapojenga tabia ya kufanya mazoezi unakuwa unaifanya akili yako iwe nzuri kiafya na kujikuta ukifikiri vizuri zaidi. Isitoshe mazoezi yanakusaidia  wewe kupunguza magonjwa hususani ya moyo na mengineyo mengi ambayo ungeyaweza kuyapata kizembe, kama ungekaa tu bila kufanya mazoezi ya aina yoyote ile, hivyo ni kitu kizuri kwa mafanikio yako unayoyahitaji.

4. Tabia ya kutekeleza mipango yako mapema.

Kuweza kuifanya siku yako iwe ya mafanikio, ni muhimu sana kwako kujiwekea utaratibu wa kupanga mambo yako mapema ikiwezekana siku moja kabla ili kuepuka kuingiliana kwa mambo ambako kunaweza kukwamisha katika mipango yako uliyojiwekea. Utaweza kufanya hivi kwa kuwa na ratiba yako ndogo ambayo itakuonyesha kwa uzuri ni nini ufanye katika siku husika inayofuata. Kuwa na utaratibu huu wa kujipangia mambo yako mapema utakusaidia wewe kufanya mambo yako kwa ufanisi na utalaam zaidi. Ukiwa na tabia hii, itakusaidia sana kufanikisha mipango yako mingi uliyojiwekea.

5. Tabia ya kuzingatia mambo.

Haijalishi unakumbana na changamoto za aina gani sasa, kitu kikubwa unachotakiwa nacho wewe ni kujifunza kutenda kwa uzingativu mkubwa unapotenda mambo yako. Acha tabia ya kuairisha na kusema ngoja nitafanya kesho, hii ni tabia ambayo itakukwamisha na kukurudisha nyuma kila siku. Kama kuna jambo au kitu ambacho ulitakiwa kukamilisha leo leo hata kama ni kidogo ni vizuri ukakamilisha leo ili kesho uingie kwenye jukumu lingine tofauti. Ili uweze kujenga mafanikio, ni muhimu kwako kuwa na tabia ya kuzingatia kila jambo unalolifanya na unatakiwa ulifanye kwa ufanisi mkubwa.

6. Tabia ya kuangalia malengo yako upya.

Ni kweli unaweza ukawa una mipango na malengo mazuri uliyojiwekea, lakini ni muhimu sana kwako kuwa na tabia ya kuangalia au kukagua malengo yako mara kwa mara. Unapokuwa na tabia ya kukagua malengo yako mara kwa mara, nakuyapitia tena tena na kuangalia wapi ulipokosea na wapi ulipofikia inakuwa inakusaidia wewe kusonga mbele na  kuyafanya malengo yako yazidi kuwa hai. Hakikisha kila siku unatenga muda kidogo wa kuyapitia malengo yako upya. Hii ni tabia muhimu sana mbayo unatakiwa kujijngea ili kuweza kufikia mafanikio makubwa yaliyoko mbele yako.

7. Tabia ya kujiamini zaidi.

Hii ni tabia ambayo muhimu pia unayotakiwa kuwa nayo ili kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako. Kwa kawaida linapokuja suala zima la kujiamini kwa wengine huwa ni shida kidogo. Unaposhindwa kujiamini elewa kabisa kwako itakuwa ni ngumu kuweza kufikia kiwango cha mafanikio unachotaka. Kwa nini inakuwa ngumu kufikia mafanikio unayotaka? Hii ni kwa sababu kila kitu ambacho utakuwa unataka kufanya utakuwa unahisi au unajiona kama vile huwezi, matokeo yake utajikuta utakuwa ni mtu wa kushindwa katika mambo mengi hata kwa yale ambayo hukustahili.

8.Tabia ya kufanya kazi kwa bidii.

Kufanya kazi kwa bidii, kuwa king’ang’azi katika malengo yako ni nguzo muhimu sana ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa  katika maisha yako. Ikiwa utaamua kujitoa mhanga na kufanya kazi zako kwa bidii zote na kujifunza vitu muhimu kwa kile unachokifanya, elewa kabisa mafanikio makubwa ni yako. Kama una nia ya kweli ya kutaka mafanikio makubwa, chukua jukumu la kujibidiisha kwa shughuli zako zote unazozifanya. Matokeo na matunda makubwa utayaona upande wako kadiri siku zitakavyokuwa zinaenda mbele. Hata ikifika wakati huoni matokeo mazuri wewe weka bidii hupotezi kitu.

Kwa kawaida tabia zetu ndizo zina nguvu ya kujenga ama kubomoa maisha yetu ya kila siku. Kama unataka maisha ya mafanikio, hakikisha unajifunza kujenga tabia zitakazo kuongoza kwenye mafanikio ya kweli na sio kukwamisha. Chukua hatua muhimu za kubadili na kuboresha maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika kila siku.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,



No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.